Wednesday, June 10, 2015

Chadema wawashukia watangaza nia urais CCM.


Chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) kimesema watangaza nia ya urais nchini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuacha kuwadanganya wananchi kwamba wakipewa ridhaa ya kuongoza wataleta elimu bure kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, wakati akihutubia wakazi wa mji wa Iringa, kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na wanafunzi wa vyuo vikuu (CHASO) mjini Iringa uliofanyika kwenye Uwanja wa Mwembetogwa uliopo mjini hapa.

Aidha, Mwalimu aliwashangaa makada hao wa CCM ambao wameonyesha nia ya kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu kwamba wao walikuwa hawana lengo la kuleta maendeleo kwa vijana, mfano kuleta elimu bure na kwamba jambo hilo la kuleta elimu bure hawana uwezo nalo bali waliiba ajenda ya Chadema ya kuleta elimu bure.

Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, alisema kuwa CCM kimeshindwa kuboresha maisha ya Watanzania sekta zote nchini na kuwataka wananchi kwenye sekta zote kuikataa CCM kwani haiwathamini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana la (chadema) Bavicha, Julius Mwita alisema kuwa wasomi wengi nchini wafanyabiashara, wanafanyakazi wa umma, wakulima, pamoja na makundi mengine nchini kuungana kwa pamoja kuiondoa serikali ya CCM madarakani kwa kuwa kimeshindwa kuleta maendeleo kwa watanzania huku wakiacha watoto wakimasikini wakiteseka bila kupata elimu bora.

No comments:

Post a Comment