TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
ZIARA YA KATIBU MKUU DK. WILLIBROAD SLAA
Kupitia taarifa hii
kwa vyombo vya habari Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapenda kuujulisha
umma wa Watanzania kuwa Katibu Mkuu, Dk. Willibroad Slaa atafanya ziara ya
kikazi katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Mbeya, Rukwa na Katavi, ambapo atakuwa
na shughuli kadhaa, ikiwemo kukagua mwenendo wa uandikishaji wa wapiga kura
unaofanyika kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR).
Katika ziara hiyo ya
siku 6 kuanzia Jumamosi ya Mei 30, 2015, Katibu Mkuu Dk. Slaa mbali ya kujionea
zoezi hilo la BVR katika vituo vya uandikishaji, atafanya mikutano ya hadhara kwenye
maeneo yote atakayozuru ambapo atazungumza na wananchi juu ya masuala
yanayowahusu katika maeneo yao pamoja na mengine ya kitaifa.
Kupitia shughuli
hizo atakazofanya, Katibu Mkuu ataendelea kuwahamasisha Watanzania wenye sifa
za kupiga kura, kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
(DKWK) linalofanyika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia mfumo wa BVR.
Aidha, Katibu Mkuu
Dk. Slaa atatumia fursa hiyo kukagua shughuli mbalimbali za chama zinazofanywa
na viongozi na watendaji wa CHADEMA katika kanda za chama; Kanda ya Nyanda za
Juu Kusini ambayo inajumuisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma Rukwa pia Kanda
ya Magharibi yenye mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi.
Katibu Mkuu pia
atapata fursa ya kukutana na viongozi na watendaji wa chama wa ngazi za chini
katika kanda hizo na kusikia kutoka kwao namna wanavyoendelea kutekeleza
programu na mikakati waliyojipangia katika maeneo yao au kuelekezwa na vikao
vya chama, ikiwa ni sehemu ya kuzidi kukiandaa chama na UKAWA yaani vyama vinne
(NLD, NCCR-Mageuzi, CUF na CHADEMA), kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Ratiba ya ziara ya Katibu Mkuu Dk. Slaa itakuwa kama
ifuatavyo;
1. Jumamosi Mei 30,
2015 - Mbozi (Vwawa) atafanya mkutano wa hadhara Uwanja wa Ichenjezya.
2. Jumapili Mei 31,
2015 – Tunduma- Mbeya, atafanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Shule ya
Msingi Tunduma.
3. Jumatatu Juni 1,
2015 – Sumbawanga- Rukwa, atafanya mkutano wa hadhara Uwanja wa Stendi ya
Chanji, mjini Sumbawanga.
4. Jumanne Juni 2,
2015 – Mpanda Mjini- Katavi, atafanya mkutano katika Uwanja wa Kashaulili.
Itakumbukwa kuwa Katibu
Mkuu Dk. Slaa alifanya ziara ya siku 3 hivi karibuni katika maeneo mbalimbali
ya Mkoa wa Kagera ambako alishuhudia udhaifu na mapungufu makubwa katika
uandikishaji wa BVR, ikiwemo wananchi kutishwa, kupigwa, kuzuiwa kujiandikisha
na viongozi wa CCM wakiwa vituoni, mashine kutofanya kazi, siku za kuandikishwa
kutojulikana na uandikishaji kufanyika ‘electronically na manually’ bila
maelezo yoyote kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Imetolewa leo Ijumaa, Mei
29, 2015 na;
Tumaini
Makene
Mkuu
wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
No comments:
Post a Comment