Saturday, May 30, 2015

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA MHE. EZEKIA DIBOGO WENJE (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA HIYO KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016

Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanununi za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013
_________________________

1.   UTANGULIZI.
 Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunilinda na kunijalia afya njema kwa miaka yote mitano ya utumishi wangu kwa wananchi wa Jimbo la Nyamagana kama Mbunge wao. Napenda pia kuwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Nyamagana kwa imani kubwa waliyo nayo kwangu na ushirikiano wanaoendelea kunipatia katika kazi zangu za kibunge. Ombi langu kwao ni kwamba; wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura, na waendelee kuunga mkono mageuzi kwa kumchagua mgombea atakayependekezwa na UKAWA katika ngazi ya Udiwani, Ubunge na Urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu wa 2015.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuishukuru familia yangu kwa kuendelea kunifariji na kunitia moyo pindi ninapokutana na changamoto mbalimbali za kisiasa.
Mheshimiwa Spika, napenda kutambua na kupongeza kazi na  juhudi za viongozi wetu wakuu wa  UKAWA za kuendelea kuuelimisha umma wa Watanzania juu ya umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika michakato ya kidemokrasia na mageuzi ya kisiasa katika nchi yetu. Kwa heshima kubwa naomba kutambua mchango uliotukuka wa fikra na uongozi wa Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe (Mb), Mwenyekiti wa UKAWA, na  Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Wenyeviti wenza wa UKAWA, Waheshimiwa Prof. Ibrahim Lipumba (CUF), Dr. Emmanuel Makaidi (NLD) na James Mbatia (NCCR – Mageuzi). Aidha,  pongezi hizi ziwafikie pia Makatibu wakuu wa vyama vinavyounda UKAWA, itifaki ikiwa imezingatiwa.
Mheshimiwa Spika, katika Bunge hili la kumi, hii itakuwa ni hotuba yangu ya mwisho kama Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kuwa maisha ya Bunge hili yanaelekea ukingoni. Ninaamini niliitumikia nafasi hii kwa weledi mkubwa na hata Waziri mwenye dhamana anatambua mchango mkubwa wa Kambi ya Upinzani Bungeni katika kuiboresha Wizara yake. Nawatakia wabunge wote maisha mema uraiani  baada ya bunge hili kuvunjwa, lakini niwatakie heri na ushindi wa kishindo wabunge wote wa UKAWA na watia nia wote wa Udiwani, Ubunge, na Urais watakaopendekezwa kugombea nafasi hizo kupitia UKAWA katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu wa 2015. Ni imani yangu na ni maombi ya wananchi kwamba; safari hii asilimia 80 wa wabunge wakaoapishwa katika bunge la kumi na moja watatokana na vyama vya UKAWA.

Inaendelea....


2.   HALI YA SIASA NA MWENENDO WA DEMOKRASIA   KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda, kwa dhati kabisa, kuipongeza Serikali ya Uingereza na wananchi wote wa Uingereza kwa kufanya uchaguzi huru, wa haki na wa kidemokrasia uliomwezesha Ndugu David Cameroon wa chama cha Conservative kuwa tena  Waziri Mkuu wa Uingereza kwa mhula wa pili.  Tunampongeza sana David Cameroon kwa ushindi usio na shaka alioupata, na tunamwomba asichoke kuwaelimisha marais wa nchi za Kiafrika kuheshimu na kulinda demokrasia   katika nchi zao.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda pia kuipongeza Serikali ya Nigeria na Wananchi wote wa Nigeria kwa kufanya uchaguzi wa kihistoria ambapo kwa mara ya kwanza katika Bara la Afrika, Rais aliyepo madarakani amekubali kushindwa katika uchaguzi huo na kukiachia chama cha Upinzani kuingia Ikulu kwa amani. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inampongeza sana aliyekuwa Rais wa Nigeria, Ndugu Goodluck Jonathan kwa busara zake na ukomavu wake wa kisiasa;  kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa na hivyo kuliepusha taifa hilo na umwagaji wa damu. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kujifunza kutokana na uchaguzi mkuu wa Nigeria ili chama cha Upinzani kitakaposhinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu wa 2015, Serikali isije ikagoma kutoka Madarakani kama alivyofanya Laurent Gbagbo, Rais wa Zamani wa Cote d’ivoire, ambaye hatimaye hakuweza kuukwepa mkono wa sheria wa The Hague kwa makosa ya uhalifu wa kivita.
Mheshimiwa Spika, tunatoa angalizo hilo kwa sababu tayari kuna kila dalili kwamba Serikali hii ya CCM  haiko tayari kutoa madaraka kwa chama cha Upinzani, na ushahidi wa jambo hili ni kitendo cha Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete kuruhusu Kambi za Jeshi za Chukwani na 672 KJ huko Zanzibar  kutumika kutengeneza vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi (ZAN ID) kwa wageni ili kuisaidia CCM kushinda uchaguzi kwa kutumia mamluki  jambo ambalo ni kinyume kabisa na sheria na liweza kuhatarisha amani ya Zanzibar na Tanzania nzima kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, tunampongeza Rais Mpya wa Nigeria Ndugu Muhammadu Buhari kwa ushindi wa kishindo alioupata na tunamshauri kuendelea kudumisha demokrasia ya nchi hiyo kwa kufuata nyayo za mtangulizi wake ya kukubaliana na uamuzi wa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  inapenda pia kuchukua nafasi hii   kuwapongeza wananchi wa Tunisia kwa kutumia vema haki yao ya kidemokrasia kwa kufanya uchaguzi wa Rais wao mwaka jana 2014  – uchaguzi ambao ni wa kihistoria kwani ulikuwa ni uchaguzi wa kwanza huru na wa haki tangu nchi hiyo ipate uhuru wake mwaka 1956. Ulikuwa pia ni uchaguzi wa kwanza wa kawaida wa Rais baada ya Mapinduzi ya Tunisia ya mwaka 2011, na ulikuwa uchaguzi wa kwanza tangu taifa hilo lipate Katiba Mpya mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kujifunza kutoka katika uchaguzi mkuu wa  Tunisia wa mwaka jana 2014, kwani ni uchaguzi ambao Ndugu Beji Caid Essebsi wa chama cha Upinzani alimshinda Rais aliyekuwako madarakani Ndugu Moncef Marzouki, na rais huyo kukubali matokeo ya kushindwa. Tunampongeza aliyekuwa Rais wa Tunisia Ndugu Moncef Marzouki kwa ukomavu wake wa kisiasa wa kukubali matokeo ambao umeliepusha taifa hilo kuingia katika machafuko. Aidha, tunampongeza Rais Mpya wa Tunisia, Ndugu Beji Caid Essebsi kwa ushindi alioupata, na tunamwomba aendelee kudumisha demokrasia nchini humo kama mtangulizi wake alivyofanya.
Mheshimiwa Spika, Tanzania sasa ina mifano mingi ya kuiga katika kukuza demokrasia hapa nchini. Kama taifa tuna kila sababu ya kujifunza kutoka kwa majirani zetu wa Malawi na Zambia ambapo ambapo vyama vya Upinzani vimetwaa madaraka ya dola bila kumwaga damu. Kambi Rasmi ya Upinzani inawapongeza marais Peter Mutharika wa Malawi na Edgar Lungu wa Zambia kwa ushindi wa kishindo walioupata. Aidha, tunawashauri waendelee kulinda na kudumisha demokrasia katika nchi zao.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Malawi tuna cha ziada cha kujifunza kwani awali aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Joyce Banda  kwani alikataa matokeo na kufanya jitihada za kuyabatilisha ili uchaguzi urudiwe, lakini Tume ya Uchaguzi ya Nchi hiyo ilisimama kidete na Mahakama Kuu ya Nchi hiyo nayo ilisimama kidete kuhakikisha kuwa haki ya wananchi inalindwa na uamuzi wao unaheshimiwa. Kwa funzo hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutenda haki kuanzia wakati huu wa uandikishaji wapiga kura, na mchakato mzima wa upigaji kura na kutoa matokeo ya uchaguzi ili kuliepusha taifa na machafuko yasiyo ya lazima.
Mheshimiwa Spika, la mwisho katika sehemu hii ni hali ya kisiasa kwa majirani zetu wa Burundi. Sote tunafahamu kwamba hali ya kisiasa nchini Burundi si shwari. Hali hiyo imesababishwa na Rais wa Nchi hiyo Pierre Nkurunzinza kukiuka makubaliano ya Arusha na kutangaza kugombea tena urais kwa muhula wa tatu jambo ambalo linapingwa na wananchi wa Burundi.  Kutokana na vurugu katika nchi hiyo, mamia ya warundi wamekimbilia Tanzania kutafuta hifadhi. Jaribio la kupindua Serikali ya Pierre Nkurunzinza lililoshindwa nalo limeongeza kiwango cha machafuko nchini humo.
Mheshimiwa Spika, katika mwendelezo wa machafuko nchini Burundi, tarehe 23 Mei, 2015 Kiongozi wa chama cha Upinzani  cha Union for Peace and Development (UPD) Zedi Feruz,  aliuwawa yeye na mlinzi wake kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani kwake mjini Bujumbura.
Mheshimiwa Spika, kuuawa kwa kiongozi huyo wa upinzani tayari kumevunja mazungumzo ya kutafuta   amani kati ya Serikali na vyama vya Upinzani yaliyokuwa yakiendelea nchini humo na hali ya usalama na amani nchini humo inazidi kuwa tete. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaungana na wananchi wa Burundi kulaani mauaji hayo, na inatumia fursa hii kumshauri Rais wa Burundi kuheshimu makubaliano ya Arusha ili kurejesha hali ya utulivu na amani nchini humo. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaiasa Serikali hii ya CCM kuheshimu na kuilinda Katiba inayotoa ukomo wa mihula miwili ya kugombea urais, na kuheshimu uamuzi wa wananchi watakapochagua chama cha Upinzani kushika madaraka ya dola katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015.

3.   TATHMINI YA KAZI ZA UPINZANI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika, kwa miaka yote mitano ya uhai wa Bunge hili, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itakumbukwa kwa kutoa  ushauri mzuri kwa Serikali  uliolenga kuiboresha wizara hii ili iwe katika viwango vya kimataifa lakini kwa masikitiko makubwa Serikali hii ya CCM inayojiita sikivu haikuwahi kusikia na kuyafanyia  kazi mapendekezo hayo, ndio maana tunawasihi wananchi waipumzishe katika uchaguzi wa Oktoba, 2015 na kuipa UKAWA ridhaa ya kuunda Serikali.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya masuala muhimu ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani ilipendekeza kwa miaka yote mitano ya uhai wa Bunge hili na Serikali kuendelea kuziba masikio ni kama ifuatavyo:
                                i.            Tuliitaka Serikali kuzielekeza balozi zetu kutekeleza diplomasia ya uchumi na kutoa taarifa ya namna kila ubalozi ulivyotekeleza sera ya diplomasia ya uchumi. Tulipendekeza hivi kwa kuwa ilionekana kuwa balozi zetu ziko kwa maslahi ya  kisiasa zaidi kuliko maslahi ya kiuchumi kiuchumi
                              ii.            Tuliishauri Serikali kuongeza bajeti ya maendeleo kwa balozi zetu nje ya nchi ambazo zilikuwa hoi sana kifedha ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi. Msingi wa pendekezo hili ulitokana na ukweli kwamba balozi zetu nje hazikuwa na hazina bajeti ya kutosha hadi sasa. Ilifikia wakati magari ya mabalozi yakawa chakavu na kukosa mafuta jambo ambalo liliifedhehesha sana nchi yetu. Tulitaka balozi ziwezeshwe ili kuwawezesha hata mabalozi kusafiri kwa ajili ya kutafuta fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwa ni mojawapo ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.
                            iii.            Tuliitaka Serikali kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma za balozi zetu nchini China, na Uingereza kwa kutoa hati za kusafiria kwa mataifa mengine hasa ya Afrika Magharibi ili kubaini ukweli na kuliondolea taifa aibu kutokana na tuhuma hizi.
                          iv.            Kwa miaka yote ya utawala wa Serikali hii ya awamu ya nne, tumekuwa tukiitaka Serikali kupeleka mwambata wa kiuchumi (economic attaché)  nchini China na nchi nyingine ambazo tuna balozi  ili kufuatilia fursa mbalimbali za kiuchumi katika kutekeleza diplomasia ya uchumi kutokana na mahusiano makubwa ya kibiashara  kati ya nchi yetu  na China, na kutokana kubadilika kwa zama  (paradigm shift) kutoka kwenye diplomasia ya kisiasa kwenda kwenye diplomasia ya kiuchumi.
                            v.            Kwa miaka yote mitano ya uhai wa Bunge hili, tumekuwa tukiishauri Serikali Kuwawekea zuio wahusika wa kashfa ya rada kuwa viongozi wa shughuli za kiserekali ili kuonesha uwajibikaji wa kimaadili (moral accountability) baada ya kushindwa kuwawajibisha kisheria, ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kwamba dola imetekwa na mafisadi.
                          vi.            Tuliitaka Serikali pia Kueleza bayana faida za kiuchumi tunazopata kama taifa kwa kushirikiana na jumuiya mbalimbali za kimataifa ili kuthibitisha kwamba mashirikiano hayo hayatumiki kupora rasilimali za nchi yetu kwa hila ya “uwekezaji”
                        vii.            Tuliitaka Serikali Kutoa idadi ya majengo ya balozi zetu nje (nyumba za mabalozi, nyumba za maafisa wa balozi na ofisi za balozi) kwa mchanganuo wa idadi ya nyumba katika nchi na kama nyumba hizo zina hati miliki au la ili kuweka kumbukumbu ya mali yetu iliyopo nje ya nchi.
                      viii.            Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliitaka Serikali kudhibiti matumizi ya fedha kwa ajili ya safari za viongozi wakuu nje ya nchi (state visits) kwa kuziwekea ukomo (ceiling) ili kuziba mianya ya wizi mkubwa wa fedha uliokuwa unafanyika kupitia kasma hiyo.
                           ix.            Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka Serikali kueleza mkakati ilio nao kwa ajili ya kuratibu michango ya kiuchumi ya watanzania wanaoishi na wanofanya kazi nje ya nchi (Diaspora remittance) kama nchi nyingine zinavyofanya.
                             x.            Tuliitaka pia Serikali  kuwateua mabalozi kuwa  maafisa masululi katika balozi zao ili fedha zao za bajeti zilipwe moja kwa moja kwenye balozi ili kuondoa urasimu uliopo ambapo fedha za balozi zinatoka hazina, zinakwenda wizara ya mambo ya nje ndipo zifike ubalozini jambo ambalo linachelewesha bajeti za balozi kufika kwa wakati na hivyo kuzifanya zishindwe kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, mambo ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani imefanya katika wizara hii ni mengi na siwezi kuyataja yote hapa. Itoshe kusema kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani imeshauri kwa kadiri iwezekanavyo, lakini kwa kuwa haina mamlaka ya kukusanya kodi kama Serikali, haiwezi kuyatekeleza kwa vitendo. Lakini kwa kuwa Serikali hii imeendelea kuwa kiziwi kwa mambo mazuri tunayoishauri, tunawaomba wananchi watupime kwa hoja zetu na waamue kutuchagua kama UKAWA ili tukamilishe ndoto zao zilizodumu kwa zaidi ya miaka 50 bila ufumbuzi.
4.   MATUMIZI MABAYA YA MAHUSIANO YA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika, mahusiano makubwa yaliyoibuka ghafla  hivi karibuni kati ya Tanzania na Msumbiji kiasi cha kuondoa masharti ya viza kwa raia wa nchi hizi kunatia mashaka  kwamba kuna  jambo lililojificha nyuma ya pazia ambalo halina nia njema.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba chama cha FRELIMO nchini Msumbiji ni chama rafiki na CCM. Imebainika kwamba, vyama hivi vimeamua kutengeneza mkakati wa kusaidiana kushinda chaguzi baada ya kuona dalili za kuzidiwa na nguvu ya upinzani katika nchi zao.  Mbinu wanazotumia ni kutumia Serikali za vyama vyao zilizopo madarakani kuanzisha mashirikiano ya “fasta-fasta” hadi kufikia uamuzi wa kuacha mipaka huru!!!!!
Mheshimiwa Spika, mbinu hiyo chafu tayari imeshtukiwa huko Zanzibar ambapo inasadikiwa kwamba raia wa Msumbiji wanaandikishwa katika kambi za jeshi na kupewa vitambulisho vya mzanzibari mkazi ili waweze kupiga kura katika uchaguzi wa Zanzibar. Hofu hii pia imetanda katika mikoa ya kusini mwa Tanzania ambapo zoezi la uandikishaji wapiga kura linaendelea.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa angalizo kwa Serikali kwamba haitavumilia kuona mchezo huu mchafu ukiendelea hapa nchini. Tunaitaka Serikali kulieleza Bunge hili kuna fursa gani za kiuchumi zilizogundulika Msumbiji sasa hivi hadi kuondoa masharti ya viza ambazo hazikuwepo tangu enzi za utawala wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere? Kama ni kigezo cha ujirani, Je Serikali iko tayari kufungua mipaka kwa nchi zote jirani bila masharti ya hati za kusafiria?

5.   UNYANYAPAA DHIDI YA RAIA WA KIGENI NCHINI  AFRIKA YA KUSINI
Mheshimiwa Spika, licha ya kukoma kwa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini kipindi cha utawala wa makaburu, Afrika ya kusini sasa imeingia katika rekodi ya dunia kwa kuwabagua waafrika wenzao wanaofanya kazi nchini humo.
Mheshimiwa Spika, katika sakata hilo, watanzania waliokuwa wakifanya kazi Afrika ya Kusini waliathirika sana na hivyo kulazimika kurudi nyumbani kwa hofu ya usalama wao.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba Tanzania ilisifika sana duniani kwa kupigania uhuru wan chi za SADC ikiwemo Afrika ya Kusini. Tuliwahi kuhoji katika hotuba zetu kwamba Taifa lilinufaika kiasi gani kwa kujitoa mhanga na kuingia umaskini wa kudumu kwa ajili ya  kuwasaidia wengine. Msingi wa hoja hiyo ulitokana na ukweli kwamba baadhi ya nchi hizo zilizosaidiwa na Tanzania hazitambui tena mchango wa nchi yetu katika harakati za ukombozi wa nchi zao, ndio maana watanzania sasa wanawindwa kama digidigi na kufukuzwa kwa kisingizio kwamba wanapoka ajira za wazawa wa nchi hizo.
Mheshimiwa Spika, kama tulisaidia nchi hizo kupata uhuru bila mkataba wowote wa manufaa ya kiuchumi kwa nchi yetu kutokana na siasa yetu ya wakati huo ya ujamaa, basi sasa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali kutoanzisha mahusiano ya burebure na nchi yoyote bila kufanya “Cost -Benefit Analysis” ya kutosha na kuona taifa linanufaika vipi. Aidha, tunaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ina mpango gani wa kisera wa kulinda ajira kwa wazawa kutochukuliwa na wageni?

6.   DIPLOMASIA YA UCHUMI NA MGAWANYO WA BALOZI ZA TANZANIA KATIKA MATAIFA MBALIMBALI
Mheshimiwa Spika, kwa miaka yote kumi ya utawala wa Serikali hii ya CCM, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiishauri Serikali kutazama upya mgawanyo wa balozi za Tanzania katika mataifa mbalimbali ili ulenge maslahi ya kiuchumi zaidi kuliko ya kisiasa.
Mheshimiwa Spika, msingi wa ushauri huu ni kutokana na ukweli kwamba kumekuwa na mabadiliko ya zama “paradigm shift” ambapo dunia imehama kutoka katika zama za diplomasia ya kisiasa na kwenda katika zama za diplomasia ya uchumi. Kutokana na hali hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliishauri Serikali   kwamba Serikali inapoteua mabalozi kwenda nchi mbalimbali duniani, ifanye hivyo kimkakati;   na mkakati namba moja, uwe ni mkakati wa kukuza na kuedeleza diplomasia ya uchumi ndipo zaidi kuliko mambo mengine. Kambi Rasmi ya Upinzani ilishauri kwamba ikiwa hakuna fursa za kiuchumi tutakazopata kama taifa kwa kuwa na ubalozi katika nchi fulani, ni bora ubalozi huo usianzishwe.
Mheshimiwa Spika, ni katika muktadha huo, tuliishauri Serikali hii ya CCM  kufanya tathmini juu ya  faida halisi  za kiuchumi tunazopata kutoka kila nchi tuliyoweka Ubalozi. Taarifa ya tathmini hiyo itumike kama dira ya kufanya uamuzi kama bado kuna haja ya kuendelea na ubalozi huo au kuufunga. Aidha, ni katika muktadha huohuo tuliishauri Serikali kuachana na fikra za kizamani za kurundika balozi nyingi katika ukanda mmoja kwa maslahi ya kisiasa zaidi kuliko ya kiuchumi.
Kwa mfano, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikuona mantiki ya kuwa na balozi katika  nchi zote mbili za  Rwanda na Burundi. Hii ni kwa sababu  Kijiografia, nchi hizi ni ndogo na zinapakana;  hivyo ingekuwa nafuu zaidi, kwa maana ya gharama za uendeshaji;  kuwa na balozi mmoja katika nchi mojawapo atakayehudumia nchi zote mbili. Aidha, hatukuona ulazima wa kuwa na utitiri wa balozi katika nchi za Zimbabwe, Msumbiji, Zambia, Malawi, Congo DRC na Afrika ya Kusini kwa pamoja . Tulidhani, ingetosha kuwa na mabalozi wawili ambao wangehudumia nchi zote sita kwa kuwa ziko katka ukanda mmoja.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliishauri Serikali kutumia mfano wa ubalozi wetu nchini sweden ambao unahudumia nchi nyingine za Scandinavia kama vile Denmark, Norway na Finland. Ushauri huu ulitokana na ukweli kwamba tunapata faida za kiuchumi zaidi kutoka katika nchi hizo kupitia fursa mbalimbali ikiwemo misaada ya kibajeti licha ya kuwa na ubalozi mmoja tu katika ukanda huo.
Mheshimiwa Spika,  kwa kuwa Serikali hii ya CCM imeshindwa kutekeleza diplomasia ya uchumi jambo linalodhihirisha kwamba imepitwa na wakati na hivyo kushindwa kuendana na mabadiliko ya zama, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawaahidi wananchi kwamba Upinzani utakapochukua dola baada ya ushindi katika uchaguzi wa Oktoba, 2015, Balozi zote za Tanzania nje ya nchi zitapangwa katika mkakati wa kukuza diplomasia ya uchumi.

7.   MASUALA AMBAYO SERIKALI IMESHINDWA KUTEKELEZA
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya awamu ya nne inaondoka madarakani ikiwa imeshindwa kutekeleza masuala mengi katika Wizara hii ya mambo ya nne.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii imeshindwa kutekeleza bajeti ya maendeleo kwenye wizara hii.  Kwa miaka yote ya utawala wa serikali  hii ya awamu ya nne;  Kambi Rasmi ya Upinzani ilieleza jinsi balozi zetu katika mataifa mbalimbali zilivyo na hali mbaya kutokana na kukosa fedha za kuziwezesha kufanya kazi kwa ufanisi. Hali ya balozi hizo bado ni duni, na Serikali hii inaondoka madarakani  ikiziacha katika hali mbaya.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaahidi kutekeleza bajeti ya maendeleo katika wizara hii kwa asilimia 100 baada ya kuchukua dola kupitia UKAWA katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu 2015.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii imeshindwa kupeleka mwambata wa kiuchumi (economic attaché) nchini China ili kufuatilia fursa mbalimbali za kiuchumi katika kutekeleza diplomasia ya uchumi kutokana na mahusiano makubwa ya kibiashara  kati ya nchi yetu  na China kama tulivyoishauri kwani mpaka sasa hakuna taarifa rasmi za utekelezaji wa pendekezo hilo.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii pia ilishindwa kuwawekea zuio wahusika wa kashfa ya rada kuwa viongozi wa shughuli za kiserikali ili kuonesha uwajibikaji wa kimaadili (moral accountability) baada ya kushindwa kuwawajibisha kisheria, ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kwamba dola imetekwa na mafisadi. Msingi wa pendekezo hili ni kwamba raia wa Uingereza waliohusika katika kashfa hiyo waliwajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi yao. Yalikuwa ni matarajio ya Kambi ya Upinzani kwamba Serikali ya Tanzania ambayo kimsingi ndiyo iliyopata hasara ingeunga mkono hatua zilizochukuliwa na Uingereza kwa kwawajibisha wahusika wa kashfa hiyo hapa nchini.

8.   MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2014/15 MA UCHAMBUZI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2015/16
Mheshimwa Spika, fedha iliyotengwa na Bunge kwa ajili ya bajeti ya maendeleo katika wizara hii kwa mwaka wa fedha 2014/15 ilikuwa ni shilingi bilioni 30. Hata hivyo, hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2015 fedha zilizotolewa na hazina kwa ajili ya maendeleo ni shilingi bilioni 16.6 sawa na asilimia 55.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba fedha hizi ndizo zinatumika kukarabati balozi zetu ambazo tumeshaeleza kuwa zipo katika hali mbaya. Aidha, fedha hizi hutumika kulipia pango katika majengo ya balozi tuliyokodisha na kununua magari ya mabalozi, kuendesha warsha mbalimbali na matangazo kwa ajili ya kuitangaza nchi yetu nje ya nchi. Kitendo cha kutekeleza bajeti ya maendeleo kwa asilimia 55 tu kunaleta mashaka kama balozi zetu zinaendeshwa kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/16, Wizara hii inaomba kuidhinishiwa shilingi bilioni 12 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kiasi hicho ni pungufu kwa shilingi bilioni 18 sawa na anguko la asilimia 60 ukilinganisha na shilingi bilioni 30 iliyotengwa mwaka wa fedha 2014/15. Hata hivyo
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla bajeti nzima  ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (fungu 34) kwa mwaka wa fedha 2015/16 imeporomoka kwa asilimia 19 kutoka shilingi bilioni 190.29 kwa mwaka huu wa fedha unaomalizika   2014/15  hadi shilingi bilioni 154.87 kwa mwaka mpya wa fedha 2015/16
Mheshimiwa Spika, kwa tukio hili la kupunguza bajeti ya Wizara hii ni kwamba ufanisi wa wizara hii utaendelea kudorora, na miradi mingi ya maendeleo katika wizara hii itakwama. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo ya kutosha ni kwa nini bajeti ya Wizara hii imepungua. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza itatua vipi matatizo ya balozi zetu ikiwa bajeti ya maendeleo imeporomoka kwa asilimia 60 ukilinganisha na bajeti ya maendeleo ya 2014/15
9.   HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia hotuba yangu kwa kuyapongeza tena mataifa mbalimbali duniani yaliyotumia vema haki yao ya kidemokrasia kufanya chaguzi huru, za haki na amani. Aidha kwa namna ya pekee, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawapongeza waliokuwa marais wa nchi za kiafrika walioshindwa uchaguzi wakiwa madarakani na kukubali kushindwa na hivyo kuwezesha Upinzani kuchukua madaraka ya Dola bila kumwaga damu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kujifunza kutoka katika nchi hizo na kujiandaa kisaikolojia kupokea mabadiliko pindi yatakapotokea ifikapo Oktoba mwaka huu 2015. Aidha, tunaionya Serikali kutotumia vibaya mahusiano ya Kimataifa katika kuingilia demokrasia ya ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Serikali hii imeshindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yaliyopo chini ya Wizara hii kikamilifu; kwa kuwa Serikali hii haitakuwepo madarakani wakati wa utekelezaji wa bajeti hii, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuwaomba wananchi wote wauunge mkono UKAWA katika uchaguzi wa Oktoba, 2015 ili kuwa na Serikali makini ya UKAWA itakayotekeleza majukumu ya Wizara hii kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo; kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani   naomba kuwasilisha.

Ezekia Dibogo Wenje (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA WAZIRI KIVULI WAMAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA


29 Mei, 2015

No comments:

Post a Comment