Tuesday, May 26, 2015

Mnyika atoka nje mkutano wa kugawa majimbo ya Kinondoni.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, juzi alitoka nje ya ukumbi wa mikutano wa Kinondoni katika mkutano ulioandaliwa na Halmashauri ya Manispaa hiyo kujadili mapendekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) yaliyotaka majimbo mawili yaongezwe katika wilaya hiyo.

Alitoka nje baada ya Meya wa Mansipaa hiyo, Yusuph Mwenda, kusoma taarifa iliyotolewa na Nec ikipendekeza majimbo mawili yaongezwe ili kufika majimbo matano.

Mnyika alipinga taarifa hiyo na kudai kuwa kuongezwa majimbo ni sawa ila fedha nyingi zitatumika katika kuendesha majimbo hayo.

“Mnataka kuongeza majimbo fedha nyingi zitatumika katika majimbo hayo, kwa nini katika Bunge la Katiba mlikataa kuongezwa muundo wa serikali tatu kwa madai kuwa gharama zitakuwa ni kubwa, je, kwa hayo majimbo, hamuoni kama gharama nazo zitakuwa ni kubwa?” alihoji Mnyika.

Alisema hakubaliani na mpango huo na hawezi kuendelea kukaa ndani ya ukumbi wa mkutano, hivyo akatoka nje.

Nje ya ukumbi alizungumza na vyombo mbalimbali vya habari na kusisitiza kuwa hakubaliani na suala hilo kuhoji kuhusu baadhi ya mambo ambayo hayajapatiwa majibu.

Alisema miongoni mwa masuala aliyohitaji kupatiwa majibu ni suala la mipaka ambayo alisema ni muhimu kuliko kugawa majimbo.

Naye mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema hana pingamizi katika kuongezwa majimbo, isipokuwa anasikitishwa na kutopata barua ambayo inaonyesha imetoka Nec.

“Meya unasoma barua peke yako unasema imetoka Nec, je, kama umejiandikia wewe na kuisoma hapa inatakiwa hata sisi tuisome na tujue nini kilichoandikwa, pia huu mkutano taarifa mbona hamkutupa sisi wabunge mpaka tunazipata kupitia kwa watu kuwa kuna ugawaji wa majimbo katika Manispaa ya Kinondoni?” alihoji.

Mwenda alisema taarifa zipo na yeye hakujiandikia na kusoma ila atatoa barua kwa kila mbunge na diwani ambazo zinaonyesha mapendekezo hayo kutoka Nec.

Pamoja na Mnyika kura zilipigwa ana madiwani 20, walikubali kuwapo kwa majimbo mapya huku 10 wakisema hawataki majimbo mapya.

Mwenda alisema mapendekezo hayo yatapelekwa Nec na hao ndio watakaorejesha nini kifanyike.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, Kinondoni itakuwa na majimbo matano ambayo ni Kawe, Ubungo, Kibamba, Mabwepande na Kinondoni.

No comments:

Post a Comment