Wednesday, May 27, 2015

Lissu: Watanzania tuondokane na unyonge.

Unyonge na umaskini uliopo nchini kwa sasa umechangia kusababisha Watanzania wengi kuendelea kuonewa na kunyanyasika na wengi wao wakijazana magerezani kwa kukosa fedha za kuwahonga wenye mamlaka mbalimbali ili wasionewe.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu (pichani), alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara juzi katika viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

Lissu alisema unyonge ulioambatana na umaskini wa Watanzania, ndiyo unaowasababishia maumivu makubwa katika maisha yao na kufanya Taifa lililokosa mwelekeo.

Alisema mbali na kukabiliwa na unyonge huo, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania waliojaa magerezani ni wale maskini walioshindwa kutoa rushwa kwa askari polisi, wakuu wa vituo na mahakama pindi walipokamatwa kwa kutenda kosa au kusingiziwa.

Lissu alifafanua asilimia hiyo 80 ya waliopo gerezani ni wale ambao walishindwa kutoa rushwa kutokana na hali walizokuwa nazo za kukosa fedha ili kesi zao zifutwe na zisifikishwe mahakamani.

Hata hivyo, alisema chanzo cha hayo yote ni nchi kuongozwa na viongozi wasiojali maslahi ya wananchi.

Aliongeza kuwa nchi imebadilika na kuwa ya unyonyaji, uonevu na yenye kupuuzia mawazo na maamuzi ya Watanzania.

“Ninapozungumzia nchi imebadilika, namaanisha nchi inaongozwa na baadhi ya wanaoiba fedha za wananchi katika mbolea, pembejeo, dawa, karo za watoto wa Watanzania, barabara na maji… kwa hali hii tunataka mapinduzi ili tuondokane na haya," alisisitiza.

Pia Lissu aliwataka Watanzania hasa waliofikisha umri wa miaka 18, kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha katika daftari la kupiga kura ili utakapowadia uchaguzi mkuu wachagua viongozi wanaowahitaji.

No comments:

Post a Comment