Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema kuporomoka kwa Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani kunakoshuhudiwa hivi sasa, kunaiweka nchi katika shaka kubwa ya maendeleo kiuchumi.
Amesema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, kuporomoka kwa Shilingi kutaendelea kuathiri uwekezaji mkubwa nchini.
Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema hayo wakati akifungua kikao cha Kamati Kuu ya Chadema cha siku mbili, kilichoanza jijini Dar es Salaam jana.
Alisema hali hiyo inatokana na wawekezaji kuwa na wasiwasi kuhusu hali ya kisiasa na hatima ya uchaguzi mkuu.
“Kwa hiyo, uchumi utazidi kuathirika zaidi kwa siku zijazo iwapo kitendawili hicho hakitatatuliwa,” alisema Mbowe.
Alisema anashangazwa kuona namna Rais Jakaya Kikwete anavyoendelea kukaa kimya, huku akishuhudia jinsi uchumi unavyoyumba, uwekezaji unavyozidi kuzorota na sarafu ya Tanzania inavyozidi kuporomoka kwa sasa.
UCHAGUZI MKUU
Mbowe alisema taifa liko njia panda kutokana na wakuu wa serikali, akiwamo Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kukimbia kuzungumza ukweli kwamba uchaguzi mkuu uko shakani.
Alisema ni wazi kwamba, mazingira ya nchi kuelekea uchaguzi huo hayako sawa kutokana na kuwapo ishara zote zinazoonyesha unaweza usifanyike.
Aliwashauri viongozi wakuu wa Taifa kuwa na utashi wa kuwa wakweli kuhusu suala la uchaguzi mkuu na kura ya maoni kuliko kuendelea kulidanganya Taifa.
“Ili nchi iwe na utulivu na usalama, lazima iwepo hali ya kutabirika. Angalau ijulikane nini kinafuata ndani ya miezi mitatu au mwaka mmoja ujao. Lakini kwa sasa hali hiyo haipo. Suala hilo linaleta mashaka makubwa kuhusu taifa linakoelekea,” alisema Mbowe.
Alisema serikali inastahili kulaumiwa kwa sasa kwa sababu imeshindwa kuwaandaa wananchi kuelekea katika uchaguzi huo, huku wengi wao wakiwa njia panda, hawajui kama uchaguzi upo au haupo.
Mbowe alisema hadi wakati huu hakuna mwelekeo wa kujua lini uandikishaji wa wapiga kura katika mfumo mpya wa BVR utafanyika.
Hata hivyo, alisema Rais Kikwete amekuwa akiendelea kusisitiza kwamba, kura ya maoni lazima iwepo na uchaguzi mkuu lazima utafanyika kwa wakati, wakati suala hilo linaloonekana kuwa ni ndoto.
“Kimsingi ni kwamba tunaona mazingira yote ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu hayapo. Hata kama wanataka kulazimisha kwa kauli zao kwamba ufatanyika,” alisema Mbowe.
MREMA: UMAKINI WA SERIKALI UNATIA MASHAKA
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, ameitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuokoa Shilingi ya Tanzania, ambayo imeporomoka kwa zaidi ya asilimia 20 dhidi ya dola ya Marekani ili kunusuru uchumi wa nchi.
Alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuporomoka kwa Shilingi ya Tanzania na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na serikali.
Mrema, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, alisema kwa hali ilivyo, serikali bado haijachukua hatua za kutosha kukabiliana na tatizo hilo na hivyo kutia shaka umakini wake katika kushughulikia mambo muhimu yanayowagusa wananchi.
“Ninachokiona ni kwamba, serikali inachukua suala la kuporomoka kwa Shilingi ya Tanzania kama ni jambo la kawaida. Na ndiyo maana imeshindwa kuweka mkazo katika kushughulikia tatizo hilo,” alisema Mrema.
Alisema kama tatizo hilo litataendelea kuwapo hata baada ya uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu, hali ya maisha ya Watanzania itazidi kuwa mbaya. Mrema alisema viongozi waandamizi wa serikali wanalichukulia suala hilo kirahisi kwa sababu wana fedha nyingi na kwamba wakati wa mkutano wa 20 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unaotarajia kuanza Mei 12 mwaka huu, atahakikisha anaibana serikali itoe majibu ya namna itakavyokuwa imeshughulikia tatizo hilo. Kuhusu uchaguzi mkuu, aliwataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Alisema ili kufanya mabadiliko ya uongozi na kukiondoa chama tawala (CCM) madarakani, wananchi wanahitajika kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu na kwamba, chama chake kitahakikisha kinaibana serikali ili kazi ya uandikishaji wapigakura ikamilike kwa wakati.
“Kinana (Katibu Mkuu wa CCM ), anang’ang’ana kupambana na Mrema kumhujumu jimboni wakati serikali ya chama chake imeshindwa kuyapatia ufumbuzi matatizo ya msingi yanayowagusa wananchi,” alisema.
No comments:
Post a Comment