Friday, May 29, 2015

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA JOSEPH O. MBILINYI (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016

(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya kanuni za Bunge toleo la mwaka 2013)
1.0       UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu. Namshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mhe. Freeman A. Mbowe kwa kuniamini kwa miaka mitano kwenye nafasi hii ya uwaziri kivuli ili kusimamia mausala ya habari, vijana, utamaduni na michezo. Pia nawapongeza wenyeviti wenza wa UKAWA, Mhe. Prof Ibrahim Lipumba  , Mwenyekiti wa CUF, Mheshimiwa James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi pamoja na Mwenyekiti wa NLD Mheshimiwa Dr. Emmanuel Makaidi kwa kazi nzuri nzuri wanayoifanya ya kuwaunganisha  watanzania mpaka hivi sasa wako tayari kukiondoa Chama Cha Mapinduzi madarakani kwa ushindi wa kishindo ifikapo Oktoba 2015 .
Aidha, nasisitiza kuwa shukrani zangu za dhati kwa wana Mbeya wenzangu nitakuja kuzitoa mkoani Mbeya baada ya kuhitimisha majukumu yangu ya Bunge hili la 10 kwa kuwa agano letu lilifanyika katika ardhi ya Mbeya hivyo sina budi kurudi tena kwenye ardhi hiyo kuwashukuru watu wangu wa nguvu, kwa nafasi na heshima kubwa mliyonipa kwa miaka hii mitano na nawaahidi uwakilishi wa kiwango kile kile kwa miaka mitano ijayo.
UHURU WA HABARI
Mheshimiwa Spika, Taswira nzuri ya Tanzania kimataifa kama nchi inayofuata utawala bora na demokrasia inazidi kupotea kutokana na ubabe wa Serikali ya CCM katika kuminya uhuru wa habari nchini. Kushindwa kwa hila za Serikali ya CCM mbali na kufungia magazeti na hata kuwateka, kuwatesa na kuwaua wanahabari wanaotimiza wajibu wao sasa kumehamia katika kutunga sheria kandamizi ambazo zina malengo ya kuwafunga midomo wanahabari. Ni hivi karibuni, vyombo vya kimataifa ikiwemo gazeti kongwe Washington Post la Marekani,  lilianika ubabe wa Serikali ya CCM na kushinikiza wafadhili na wahisani hasa Serikali ya Marekani na Benki ya Dunia kusitisha kuipa Tanzania misaada ili kuishinikiza Serikali ya CCM kuzirekebisha Sheria hizo kandamizi ambazo zilisainiwa na Rais Kikwete hivi karibuni kwa kuwa zinaminya uhuru wa habari.  

Inaendelea......


Mheshimiwa Spika, Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya  Makosa ya Mitandao ambayo inalenga kuua uhuru wa habari hata baina ya mtu na mtu ambapo mtu anaweza kwenda jela kwa kosa la kufowadi ujumbe, taarifa ama picha ambayo ameipokea kutoka kwa mtu mwengine( yaani spams). Lakini pia, vyombo vya kimataifa vinaeleza kuwa kupitishwa kwa Sheria ya Takwimu kutatia hatiani watu hasa wanahabari kwa kigezo kuwa wametoa takwimu ambazo Serikali itaona si za kweli n a bila kupata kibali cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Mheshimiwa Spika, inashangaza kuona kuwa Taifa linapelekwa gizani kwa Sheria hizi za kibabe zisizozingatia dhana ya uwazi ambayo Serikali inajidai kuitekeleza. Sote ni mashahidi kuwa mara nyingi Serikali imekua haitoi takwimu sahihi za mambo mbalimbali na kwa nyakati tofauti Serikali pia imekiri kuwa haina takwimu kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo taarifa za ajira na ukosefu wa ajira. Ikumbukwe kuwa, wakati wa ajali ya Meli ya MV Spice Islander, Serikali haikutoa idadi sahihi ya watu waliokuwepo kwenye meli ile kwa kuwa haikua na takwimu. Ni vyombo vya habari ambavyo vilifichua idadi sahihi ya wahanga wa ajali ile kwa kuwa vilikuwepo eneo la uokoaji, leo hii unapowanyima watu uhuru wa kutoa taarifa zinazoambatana na takwimu za masuala husika mpaka kupata kibali cha Ofisi ya Takwimu, tunalenga kuficha ukweli gani?
Mheshimiwa Spika, kuelekea uchaguzi Mkuu ambapo mara nyingi matukio ya udanganyifu juu ya takwimu za matokeo ya uchaguzi zimekua zikichakachuliwa na Serikali , Sheria hii ya Takwimu inalenga kwa namna yoyote ile kuminya haki ya watanzania kupata takwimu sahihi ambazo zinaweza kutolewa kwa usahihi na wadau wengine ambao wanashiriki katika mchakato wa uchaguzi Mkuu. Hii inalenga kupotosha umma wa Tanzania katika kupata taairfa sahihi.

Mheshimiwa Spika , muendelezo wa malalamiko dhidi ya Sheria hizo kandamizi pamoja na muswada wa Habari ambao unaelezwa kuwa katika mkakati wa kuletwa ndani ya Bunge hili, umepingwa vikali pia na wadau wengi nchini ikiwemo Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Nchini (MOAT) ambao walifanya kikao tarehe 26 Mei mwaka huu  jijiji Dar es Salaam, walielezea kuwa muswada huu kandamizi ni tishio kwa demokrasia na amani nchini. Kambi ya Upinzani Bungeni, inaungana na wadau wote wanaoupinga muswada huu kandamizi na tunaitahadharisha Serikali ya CCM kutouleta muswada huu bila ya kuurudisha kwa wadau wake wakubwa na kufanya nao madhiriano na kurekebisha vifungu ambavyo vinaendeleza ubabe  wa Serikali hii kuminya uhuru wa habari nchini hasa kuelekea uchaguzi Mkuu wa 2015.
Aidha, Kambi ya Upinzani Bungeni inalaani taarifa za kutishiwa maisha kwa mmiliki wa kituo cha televisheni cha ITV, Dr. Reginald Mengi eti kwa madai kwamba kituo chake kimekua kikitoa habari za kiuchochezi zinazosababisha kuyumba kwa Serikali ya Rais Kikwete ikiwemo habari za kashfa ya ufisadi wa Mabilioni ya Akaunti ya Tegeta ESCROW.
MAENDELEO YA VIJANA
Mheshimiwa Spika, Serikali ya CCM haijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kushughulikia changamoto na matatizo ya vijana wa taifa hili hasa ukosefu wa ajira. Mara nyingi Serikali hii imekuwa ikiyatumia makundi mbalimbali ya wananchi ikiwemo vijana pale inapowahitaji hasa nyakati za uchaguzi. Mfano halisi ni namna ambavyo ilipora Muswada wa uanzishwaji wa Baraza la Vijana kwa kuhisi kuwa endapo muswada Binafsi wa Mbunge wa Upinzani Mheshimiwa John Mnyika ungepita, CCM ingepoteza kura za vijana. Kwa kuwa Serikali ya CCM iliingilia mchakato huu bila kujiandaa matokeo yake ni kuvuruga mchakato mzima wa uendeshaji wa Baraza hilo. Ikumbukwe kuwa, kwenye mchakato huu wa Baraza la Vijana Bungeni, Kambi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza uanzishwaji wa Baraza la Vijana uende sambamba na uanzishwaji wa Mfuko wa Vijana ambao ungewezesha Baraza hilo kujiendesha kwa uhuru. Kwa kuwa Serikali haikua na dhamira wala nia ya dhati ya kuanzisha Baraza la Vijana lakini waliutumia mchakato huo kisiasa ili kuwalaghai vijana wa Taifa hili; Serikali ilipinga kwa nguvu zote kuanzishwa kwa Mfuko wa Vijana ili Baraza hilo liwe tegemezi kwa Serikali kama njia mojawapo ya kulidhibiti. Serikali hii ya CCM pia haina nia ya dhati ya kutatua changamoto za vijana za kiuchumi na ndio maana imeshindwa kutekeleza agizo la kuzitaka halmashauri zote nchini kutenga asilimia 5 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vijana.
Kambi ya Upinzani Bungeni, inawaahidi vijana wote nchini kuwa, UKAWA itakaposhika madaraka itahakikisha kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaanzishwa sambamba na utekelezaji wa agizo la kuzitaka halmashauri zote kutenga fedha kwa ajili yao.


BARAZA LA KISWAHILI TANZANIA
Mheshimiwa Spika, suala la kukuza na kukiendeleza Kiswahili ni kipaumbele cha Baraza la Kiswahili Tanzania. Kwa muda mrefu , Serikali hii si tu kuwa imeshindwa kuwawezesha BAKITA kibajeti bali hata viongozi wakuu wa Serikali ya CCM wameshindwa kuunga mkono juhudi za BAKITA katika kueneza Kiswahili. Ni kama  Viongozi wetu wanaona aibu kutumia lugha ya Kiswahili kwenye majukwaa ya kimataifa ili kukitangaza Kiswahili. Katika hili, Rais Kikwete amekua kinara wa kutumia Kiingereza badala ya kutumia lugha yetu ya Taifa kwenye shughuli mbalimbali za kimataifa wakati viongozi wa mataifa mengine wakitumia lugha za mataifa yao; kwa mfano alipokuja Rais wa China, Rais wa Marekani Obama na hata kwenye mkutano wa  Usuluhishi wa Burundi hivi karibuni.  Lakini, Rais Nyussi wa Msumbiji alipolihutubia Bunge lako hivi karibuni alitumia lugha ya taifa lake ambayo ni kireno japokuwa ana uwezo wa kuzungumza lugha ya Kiswahili kwa ufasaha.
KUZOROTA KWA SEKTA YA MICHEZO NCHINI
A.  Viwanja Vya Michezo
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeendelea kuona umuhimu wa taifa kuwekeza katika viwanja vya michezo ili kuweza kupanua wigo wa taifa kujitangaza na kukusanya mapato yanayotokana na viwanja vya michezo nchini. Labda, wizara mpaka sasa haijaweza kujua hasara ambazo kama taifa tunapata kutokana na kutotumia nafasi zinazotokea na kutowekeza vya kutosha katika kuboresha michezo nchini.
Mheshimiwa Spika, enzi za chama kimoja, majengo na maeneo yote ya umma yalikuwa chini ya Serikali. Ujenzi na uendelezaji wa maeneo hayo ulisimamiwa na Serikali kupitia kodi za wananchi, michango, fedha za wafadhili na wahisani mbalimbali na hasa wananchi kujitolea nguvukazi. Baada ya Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, mambo yote yaliyokuwa yakisimamiwa na Serikali ya CCM yalirudishwa kwa umma isipokuwa viwanja mbalimbali vya michezo  ikiwemo uwanja wa CCM Kirumba (Mwanza), Samora (Iringa), Sokoine (Mbeya), Sheikh Amri Abeid (Arusha), Majimaji (Songea), Kaitaba (Kagera) n.k. ambavyo CCM ilivipora na kuvihodhi.
Mheshimiwa Spika, leo hii pamoja na CCM kuendelea kuhodhi viwanja hivi imeshindwa kuviendeleza na matokeo yake kuwanyima fursa wananchi wa maeneo husika kushuhudia michezo mbalimbali kwa kuwa viwanja hivyo huwa havikidhi viwango vya ubora vya michezo hali inayofanya michezo mingi mikubwa ikiwemo ya kimataifa kufanyika Dar Es Salaam pekee. UKAWA inawaahidi watanzania kuwa pamoja na kujenga viwanja vipya vya kisasa pia tutavirudisha viwanja hivyi vyote kuwa mali ya umma chini ya halmashauri za miji ili vitunzwe na vilete tija zaidi kwenye maendeleo ya michezo.

B.   Kushuka kwa Viwango vya Michezo
Mheshimiwa Spika, pamoja na tatizo la ukosefu na usimamizi wa viwanja vya michezo nchini (stadiums), Serikali ya CCM inamaliza awamu ya nne huku ikiwa imeua sekta ya michezo kabisa. Leo Tanzania inaendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu kuanzia kwenye riadha, ngumi, netiboli, mpira wa kikapu na kwa kiwango kikubwa kwenye mchezo wa soka ambao Serikali imeshindwa  hata kwenda sambamba na juhudi za makampuni binafsi na wadau mbalimbali katika kuendeleza michezo. Mara nyingi tumeishauri Serikali kuwapa kipaumbele na kuwaendeleza makocha wazawa badala yake imekuwa ikiendekeza makocha wa kigeni ambao mpaka leo hawajatusaidia wakati historia inaonesha kuwa makocha wazalendo kama Joel Bendera, Marehemu Zakaria Kinanda na wengineo walifanya kazi nzuri kwenye timu yetu na kuipa sifa nchi. Lakini leo hii tunafungwa na timu kama Lesotho tukiwa chini ya kocha wa kigeni ambaye analipwa fedha nyingi za walipa kodi. Na ndio maana si ajabu leo Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) Jamal Malinzi anapoulizwa mafanikio yake toka apokee kijiti cha uongozi kutoka kwa Leonard Edgar Tenga, anajibu kuwa ni kufanikiwa kuonesha mechi 12 za kimataifa laivu kwenye luninga.
MAPATO YA VIINGILIO VYA VIWANJA VYA MICHEZO
Mheshimiwa Spika, katika miaka ya karibuni tumeshuhudia kukua kwa viwango vya  michezo  mbalimbali ikiwemo riadha, soka, mpira wa pete na mpira wa kikapu kunakokwenda sanjari na ongezeko la wapenzi wa michezo huo katika miji mbalimbali. Hata hivyo, ongezeko hilo linaonekana wazi kutokwenda sambamba na ujenzi wa viwanja vipya, upanuzi na uboreshaji wa viwanja vya soka vilivyopo.
Mbali na Uwanja wa Taifa, kwa takribani miaka thelathini hapajakuwa na maendeleo yoyote ya ujenzi wa viwanja vipya au ukarabati wa vilivyopo ili kukidhi matakwa ya ongezeko la wapenzi wa michezo hiyo pamoka  na maendeleo ya michezo kwa ujumla. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita FIFA imeisaidia Tanzania kukarabati viwanja kadhaa, lakini jitihada hizo zimekuwa zikikwamishwa na serikali kwa kutoza kodi kubwa vifaa vya ujenzi na ukarabati wa viwanja hivyo. Ukarabati wa Uwanja wa Kaitaba unaoendelea mjini Bukoba umekumbwa na changamoto hiyo ya kodi.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati Maalum ya Kudhibiti na Kuboresha Mapato ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyotolewa Mei 2011, viwanja vingi vinavyotumika katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) vilijengwa miaka ya 1970 na 1980 na havina miundombinu inayokidhi masharti ya ulinzi, usalama na burudani.
Ukurasa wa 10 wa ripoti hiyo yenye jumla ya kurasa 95 na viambatanisho tisa unasema: “Viwanja vyetu vingi havitoi fursa kwa watazamaji kuingia uwanjani bila bughudha, kukaa kwa raha na starehe na urahisi wa kutoka uwanjani baada ya mechi.”
“Pia havitoa fursa ya watazamaji kupata viburudisho kama vinywaji na vitafunwa, sehemu ya kuuzia kumbukumbu kama picha na machapisho mbalimbali ya michezo mfano ratiba za ligi na kalenda. Haviwakingi watazamaji dhidi ya jua kali au mvua na havina huduma nzuri ya vyoo kwa ajili ya wachezaji na watazamaji,” inaongeza ripoti hiyo.
Mheshimiwa Spika, mojawapo wa vyanzo vya mapato vya wizara hii ni mapato ya viingilio vya uwanjani. Lakini leo Serikali hii iambayo imehodhi viwanja vya mali ya wanatanganyika, inawezje kujipatia mapato ikiwa inashindwa kuendelea viwanja vya watanganyika na badala yake imevihodhi kiujanja ujanja tu?
Mheshimiwa Spika, Katikati mwa msimu wa 2013/14 wa VPL, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilivifungia viwanja vyote vya soka vinavyomilikiwa na CCM pamoja na Uwanja wa Kaitaba, kutumika kwa mechi za ligi kuu na Ligi Daraja la Kwanza kutokana na dosari mbalimbali. Mbali na mfumo wa tiketi za elektroniki (ETS) uliosimikwa na CRDB kwenye baadhi ya viwanja kisha kusitishwa kibabe siku nne kabla ya mechi ya mzunguko wa pili wa VPL msimu huu ya Simba dhidi ya Yanga, viwanja vya soka nchini havina vifaa vya ukaguzi, uthibiti wa tiketi na uingiaji viwanjani (ticketing and access control facilities).
Mheshimiwa Spika, leo hii kuna mazingira makubwa ya ubadhirifu wa mapato ya viwanja vya michezo na badala yake, kusitishwa kwa mfumo wa tiketi za kieletroniki kumepelekea watu wachache kunufaika na fedha za mapato huku sekta ya michezo ikidorora. Tunaishangaa serikali ya CCM kuanzisha mambo ambayo kimsingi utekelezaji wake kwao ni mzigo na bado wanadhani watapewa ridhaa ya kutumikia watanzania. Inawezekanaje uwanja wa mpira ujae kwa kiwango cha level seats lakini watazamaji wazidi kiwango cha uwezo wa uwanja kubeba watazamaji? Je Serikali hii chovu inasubiri yatokee maafa uwanjani ndio wajue kuwa kuna umuhimu wa kufuata utaratibu ambao wanashindwa kuutekeleza?
Mheshimiwa Spika, wakati serikali ikitangaza kusitisha matumizi ya mfumo wa tiketi za elektroniki (ETS) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ni mojawapo wa mikakati ya Serikali ya CCM kuhalalisha ‘madudu’ ya ulaji kwa watendaji wa shirikisho na serikali kupitia matumizi ya tiketi za vishina. Uamuzi wa kusitisha matumizi ya ETS umelenga kurudisha ulaji wa mapato ya milangoni kupitia mauzo ya tiketi za ziada na bandia za mfumo wa kizamani wa vishina. Ikumbukwe kuwa, tiketi za elektroniki zilifuta ubebaji wa fedha za mapato kwenye viroba. Zimekuwa chungu kwa maofisa wa TFF na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambao walikuwa wameshazoea kujineemesha kwa kubeba fedha kwenye viroba na rumbesa.
Mheshimiwa Spika, toka kutangazwa kufutwa kwa mfumo hhuo wa ukataji wa tiketi kwa njia ya kieletronki kuna taarifa kuwa wakati  baadhi ya klabu zikidai kwamba hakuna uwazi kwa maofisa wa CRDB katika kutengeneza na kuuza tiketi, taairafa hzio ni za uongo kwa kuwa zimelanga kuweka Milano ya ubadhirifu wa mapato ya viingilio kwa kuwa  TFF walipewa Nyila (password) na  CRDB inayowawezesha maofisa wa shirikisho kuona moja kwa moja pesa inayoingia kupitia mauzo ya tiketi. Pia kuna makubaliano ya kuonyesha idadi ya watu waliokata tiketi dakika 10 kabla ya mechi kumalizika.
Mheshimiwa Spika, aidha mpaka sasa si TFF wala wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na michezo ambazo zimeeleza ni nani anayetengeneza tiketi kwa sasa? Huu uvunjaji wa katiba ya shirikisho. Ni aibu kwa Wizara hii kutoka kwenye mfumo wa kisasa wenye manufaa na kurudi kwenye mfumo wa kizamani ambako nchi nyingi zimeshauacha ili kuweza kuwanufaisha watu wachache huku Serikali iikosa mapato ambayo yangetumika kuimarisha viwanja ambavyo vimepokwa na CCM.
MCHAKATO WA VAZI LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa serikali ya CCM imetumia fedha nyingi  za walipa kodi kuendesha mchakato wa kutafuta vazi la taifa kama vile vazi la Taifa lingeweza kutatua matatizo ya watanzania endapo lingepatikana. Leo ikiwa imepita miaka mitatu toka kamati iliyokua ikisimamia mchakato wa vazi la taifa kukabidhi ripoti yake, ripoti hiyo haijawekwa hadahrani na hakuna anayejua azma ya fedha za walipa kodi zilizohalalishwa kutumika kwa ajili ya vazi la taifa na tena kwa kufanya mchakato huo mara mbili.
Mheshimiwa Spika, mavazi ya nchi hii yanafahamika, kama khanga, kitenge, lubega, kaniki, kibwebwe na mengineyo mengi. Kitendo cha Serikali ya CCM kuwaaminisha wananchi kuna ulazima wa kuwa na vazi la Taifa huku viongozi wa Kitaifa wakiwa wanaendelea na maisha yao ya kila siku bila uwepo wa vazi hilo ni dhahiri haujatatua matatizo yao ikiwemo ukoefu wa huduma za afya, elimu duni, ukosefu wa maji safi na salama na ongezeko la gharama za maisha.
MBIO ZA MWENGE
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekua ikipingana na utumiaji wa fedha za walipa kodi na kitendo cha Serikali kuendelea kuwatoza wananchi kwa mashinikizo bila ridhaa zao kuchangia shughuli za mbio za Mwenge wa Uhuru. Ni kweli kuwa Mwenge wa uhuru ni hazina kwa taifa letu jambo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana nalo na kwa muda mrefu tumependekeza Mwenge wa uhuru uwekwe katika makumbusho ya taifa ili kuweza kuwapatia fursa wananchi kuweza kujifunza hapo.
Mheshimiwa Spika, Suala la kuenzi historia ya Taifa ni la lazima lakini kuendelea kutumia gharama kubwa kwa jambo hili wakati Watanzania wengi hawana huduma muhimu ni dharau kubwa. Aidha, katika kipindi hiki ambacho mwenge wa uhuru unapitishwa katika sehemu mbalimbali za nchi, chama tawala nacho kinapita katika maeneo mbalimbali ya nchi kuangalia utekelezaji wa ilani yake pamoja na kuzindua miradi ya maendeleo ya wananchi. Huu ni usanii mkubwa unaofanywa na Serikali ya CCM kwa dhumuni la kuwanyonya watanzania masikini kwa kigezo cha kuwa wanachangia shughuli za maendeleo wakati ukweli ni kuwa watanzania wanachangishwa mpaka fedha kwa ajili ya malazi na chakula kwa wakimbiza mwenge kama alivyojibu Waziri Mkuu. Na kwa kuwa kumekua na malalamiko kutoka wa wafanyabiashara, wafanyakazi wa Serikali na hasa walimu sehemu mbalimbali nchini kuwa wanalazimishwa kuchangia mwenge bila ridhaa yao. Na kama CCM inataka bado mambo ya mbio za mwenge basi wagharamie wenyewe kwa asilimia 100 na si kuwalazimisha wananchi kuchangia hasa ukizingatia kuwa Waziri Mkuu alitoa kauli wiki hii kuwa kuchangia mbio za mwenge wa uhuru ni hiyari. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kusisitiza kuwa sasa ni wakati muafaka mwenge wa uhuru kupelekwa jumba la Makumbusho ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa pamoja na Serikali kusema kuwa mwenge huu unahamasisha ushiriki wa shughuli za miradi ya maendelepo, leo hii halmashauri na mikoa mingi nchi zimepokea takribani asilimia kati ya 15-25 tu ya miradi ya maendeleo, ni maendeleo gani ambayo CCM inayahamasisha huku Serikali ikiwa haifikishi fedha za maendeleo na matukio ya ngono zembe na maambukizo ya UKIMWI yakishamiri?
HITIMISHO
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawataka vijana, wana utamaduni, wanamichezo na wadau wa habari wote kufanya maamuzi sahihi itakapofika Otoba mwaka huu. Pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na wawe tayari kuiondoa Serikali hii ya CCM inayopenda kuanzisha migogoro na wananchi kila siku kitu ambacho ni hatari kwa amani ya nchi hii. Serikali hii tayari ina migogoro na wafanyakazi, walimu, wanafunzi, vijana, wazee, viongozi wa dini, wafanyabiashara, madereva na sasa bila sababu za msingi inazidisha vita na wadau wa habari.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

…………………………..
JOSEPH O. MBILINYI (MB)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI-WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO.

28.05.2015

No comments:

Post a Comment