Friday, May 29, 2015

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHESHIMIWA MCH. PETER SIMON MSIGWA, (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016

(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
1.0       UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la 2013, naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya 2014/2015 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2015/2016.

Mheshimiwa Spika, kwanza, napenda kuchukua nafasi hii kwa kipekee kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya njema. Kwa kipekee niishukuru familia yangu hasa mke wangu na watoto wangu pamoja na wananchi wangu wa Iringa mjini kwa kunipa ushirikiano mkubwa katika majukumu yake. Zaidi, namshukuru kiongozi wa Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman A. Mbowe kwa kunikabidhi jukumu la kusimamia wizara hii toka aunde Baraza Kivuli la Mawaziri kama Msemaji Mkuu wa Wiizara ya Maliasili na Utalii. Pia, kwa wabunge wa kambi nzima ya upinzani kwa kuwa kitu kimoja.  Na pia kipekee, niwapongeze viongozi wangu ambao ni wenyeviti wa Serikali za Mitaa pamoja na viongozi wa CHADEMA wa jimbo la Iringa mjini kwa kuja kuniunga mkono.

Mheshimiwa Spika, katika maandiko Matakatifu ya Biblia tunaelezwa jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu alimtuma Musa kwenda kuwaokoa wana Misri kwa kumwambia kuwa ‘nenda ukawaambie kuwa nimeyaona mateso yao, nimekisikia kilio chao  na maumivu yao ninayajua, nami nimeshuka ili niwaokoe na Farao’
Mheshimiwa Spika, UKAWA inapenda kuwaambia watanzania KUWA Mwenyezi Mungu amesikia kilio chenu, ameyaona mateso yenu   na anayajua maumivu yenu’ hivyo UKAWA imekuja kuwaokoa kutoka kwa utawala wa kidhalimu wa Serikali ya CCM ili mnufaike na rasilimali na maliasili za nchi yenu(maliasili na utalii)!

Inaendelea.....


Mheshimiwa Spika, kwa takribani miaka mitano nimekua mstari wa mbele kuishauri Serikali kupitia Wizara hii ya Maliasili na Utalii kwenye masuala ya ujangili, misitu, vitalu vya uwindaji, utunzaji wa mazingira na maliasili pamoja na njia mbadala za kuweza kuinua ya utalii ikiwemo ukuzaji wa ajira. Lakini, Serikali ya CCM imeendelea kuwa kiziwi , kipofu na kufikia hatua ya kubeza, kupuuza na hata kukebehi juhudi zetu katika kuiinua Sekta hii muhimu kwa uchumi nchini. Ikumbukwe kuwa, Sekta ya utalii inachangia takribani dola bilioni 2 ambazo ni sawa na takribani trilioni 4 za pato la taifa.  Lakini, Serikali ya CCM imekua na kigugumizi cha kuweza kuitumia Sekta hii ipasavyo zaidi ya ilivyo sasa kama ambavyo imeshauriwa na Benki ya Dunia (WB).
Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kufanya mabadiliko ya mara kwa mara ya mawaziri wa Wizara hii, wizara bado imeendelea kukumbwa na changamoto kubwa ikiwemo kuongezea kwa vitendo vya kijangili, uwindaji haramu na utoroshaji wa wanyama na nyara za taifa.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba zetu za miaka mitano mfululizo tumezungumzia umuhimu wa kuanzisha sera ya diplomasia ya uchumi ambayo mabalozi wetu watapimwa utendaji wao kutokana na utendaji wao na ubunifu wao wa kiuchumi. Tulipendekeza mabalozi hawa wapatikane kwa kuhakikisha kuwa wanaomba nafasi za kuendesha balozi hizo kwa kuonesha mipango mikakati itakayochochea masuala ya kiuchumi ikiwemo uwekezaji, utalii, biashara na kadhalika. Lakini Serikali hii imeziba masikio. Sasa muda umefika wa Serikali hii kukaa kando na kuacha akili kubwa iweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, miaka michache iliyopita nilielezea ndani ya Bunge lako kuwa watanzania tumeruhusu akili ndogo itawale akili kubwa. Na maneno yangu haya yanajidhihirisha pale ambapo wizara nyeti katika Taifa, inapokumbwa na kashfa kubwa ikiwemo kashfa ya kulinda mtandao wa majangili, kashfa ya operesheni tokomeza ambayo bado haijafutika machoni pa watanzania; lakini matokeo ya kukabiliana na changamoto hiyo yamegeuzwa kuwa ni kuwabadili watu na wala si kubadilisha mfumo. Labda tuseme kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii haina tatizo la kupata kiongozi bora wa kuweza kukabiliana na changamoto za utalii nchini lakini inakabiliwa na changamoto ya kufanya mabadiliko ya mfumo wa kiutendaji na kiuwajibikaji ili kuiwezesha wizara kufanya kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, sera za Chama cha Mapinduzi (CCM) zimeshindwa na zimeshindwa si kwa kukosa watekelezaji wazuri bali zimeshindwa kwa sababu ni sera mbaya ambazo zimegeuka kuwa janga la kudumu la Taifa. Sera hizi katika ujumla wake ndizo chanzo, kiini, na sababu ya kudumaa kwa maendeleo nchini na ndizo chanzo kikuu cha umasikini Tanzania. Sera hizi ambazo zimejaribiwa kwa miaka 50 na zaidi sasa zimethibitisha kitu kimoja tu – kushindwa kwake. Sera ya CCM kuhusu maji imeshindwa; sera ya CCM kuhusu elimu imeshindwa ; sera ya CCM kuhusu nishati imeshindwa; sera ya CCM kuhusu madini imeshindwa; sera ya CCM kuhusu gesi imeshindwa; sera ya CCM kuhusu ulinzi wa rasilimali za asili imeshindwa; sera ya CCM kuhusu kupambana na ujangili imeshindwa, sera ya CCM kuhusu ulinzi na usalama imeshindwa; Sera ya CCM kuhusu Usalama wa Taifa imeshindwa. Kwa kila kipimo sera zote za CCM zimeshindwa na hakuna iliyofanikiwa.

Mheshimiwa Spika, mojawapo ya mambo mabaya kabisa ambayo ni matokeo ya sera hizi mbovu za CCM ni kutegemea fedha za wafadhili katika mradi mingi ya maendeleo huku Taifa likiwa limebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo zinaweza kuendesha miradi ya maendeleo pamoja na uchumi bila kutegemea miradi ya wafadhili. Kosa hili lilifanywa mara baada ya uhuru lakini Nyerere – Baba wa Taifa – alilitambua hilo mara moja na katika kutangaza Azimio la Arusha alitangaza ukweli ambao ulikuwa yakini wakati ule kama ulivyo leo hii.

Mheshimiwa Spika, azimio la Arusha lilisema hivi kuhusu kutegemea fedha kama msingi wa maendeleo:
“Lakini ni dhahiri kwamba tumefanya makosa katika kuchagua silaha; kwani silaha tuliyochagua ni fedha.  Tunataka kuondoa unyonge wetu kwa kutumia silaha ya wenye nguvu, silaha ambayo sisi wenyewe hatuna.  Katika mazungumzo yetu, mawazo yetu, na vitendo vyetu ni kama tumekata shauri kwamba bila fedha mapinduzi yetu hayawezekani.  Ni kama tumesema, “Fedha ndiyo msingi wa maendeleo.  Bila fedha hakuna maendeleo”
Mheshimiwa Spika, ni azimio la Arusha ambalo lilieleza kuwa  ;
“Viongozi wa TANU mawazo yao ni kwenye fedha.  Viongozi wa Serikali, wanasiasa na watumishi, mawazo yao na matumaini yao ni kwenye fedha.  Viongozi wa wananchi na wananchi wenyewe katika TANU, NUTA (ilikuwa chama cha wafanyakazi), Bunge, UWT.,  Vyama vya Ushirika, TAPA (kilikuwa chama cha wazazi) na makundi mengine ya wananchi, mawazo yao na maombi yao na matumaini yao ni FEDHA.  Ni kama wote tumekubaliana na tunasema kwa sauti moja, “Tukipata fedha tutaendelea, bila fedha hatutaendea.”

Mheshimiwa Spika, ndio maana kila Mbunge wa CCM akisimama hapa anawaza kuhusu fedha, fedha na wala hachangii ni jinsi gani Taifa linaweza kutumia rasilimali tulizo nazo kujitosheleza kiuchumi bila kutegemea fedha za wafadhili.  Ni maono ya baba wa Tafa ambayo yanatanguliwa kushindwa kwa Serikali ya CCM kutatua matatizo ya ujangili na kuamini kuwa jumuiya ya kimataifa ndio ina wajibu wa kuisaidia Tanzania kupambana na ujangili.

Mheshimiwa Spika, ndani ya asasi za uongozi na utawala, na katika mfumo mzima wa siasa , Serikali ya CCM imeendelea kulea uozo huo,maovu hayo yanayofanywa na watu wale wale kwa mfumo ule ule na kwa uwajibikaji ule ule. Kwa mfano ni wizara ile ile inayokabiliwa na matatizo yale yale na uwajibikaji wake ni ule ule wa kubadilisha mawaziri na kuwateua wa chama kile kile na utegemee utapata matokeo tofauti kwa kupitia watu hao hao. Hii  taratibu, inageuka kuwa saratani inayolitafuna taifa letu. Tunajua sasa kwamba pasipo na uongozi thabiti na wenye nia ya kutenda mema na makubwa, tutabakia kuwaona wenzetu hasa nchi zilizopo katika ukanda wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) wanapiga hatua na sisi tukibakia nyuma, huku tukiwa na rasilimali ambazo wenzetu hawana lakini tunashindwa kuzitumia kwa manufaa ya watanzania wenyewe.



IDARA YA MISITU
Mheshimiwa Spika, idara ya misitu au Tanzania Forest Services (TFS) imeoza nchi nzima,watendaji kila mmoja anafanya lake katika  ofisi yake na hawafanyi kazi kwa mujibu wa Sheria ya misitu ya mwaka 2002 no 14.Kumekuwa na ubadhirifu mkubwa  wa fedha kutoka kanda moja kwenda kanda nyingine .Kama tujuavyo, mazao mengi ya misitu hutoka mikoa mbali mbali na kusafirishwa kwenda kwenye miji mikubwa hasa Dar Es Salaam kwa matumizi ya ndani ya jiji hivyo Es Salaam imekuwa kitovu kikubwa cha soko la biashara ya mkaa na kulifanya jiji hilo kuwa kituo kubwa cha ukusanyaji wa ushuru wa Serikali kwa wale wanaokuwa wamekwepa kulipia ushuru kutoka huko kwenye chanzo cha mazao hayo ya mkaa.

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu meneja wa kanda ya mashariki Ndugu Salim  Bakari maarufu  kama Mwarabu badala ya kuwa  mdhibiti yeye amekuwa akiwatetea wafanyabiashara wanaokiuka kulipa kodi na ametuhumiwa kwa muda mrefu kuwa mfadhili wa wafanyabiashara  haramu kutoka Tabora, Katavi, Kibondo, Bukombe, Tunduma, Dodoma, Kilindi na Bagamoyo.  Vilevile, ili kufanikisha malengo yake ameweka watu wasio na taaluma katika vituo vya ukaguzi (checkpoints) na hali akijua hawana sifa za kukagua nyaraka wala mizigo. Kwa Mfano; Katika vituo vya Ukaguzi vya Kibaha, Vikindu pamoja na Mbagala kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu ya uwepo wa vijana waliopo chini ya mtandao wa Mwarabu  ambao wanafanya kazi  kama maafisa misitu wakati  hawana sifa lakini pia wamewekwa kimkakati ili watu waweze kupitisha biashara zao bila ukaguzi yakinifu. Majina ya vijana hawa tunayo pamoja na vituo vyao vya ukaguzi.

Mheshimiwa Spika, imekuwa kawaida ktk sekta ya misitu watu kukiuka sheria na kufanya biashara kiholela kwani mwongozo wa uvunaji endelevu wa 2007 umesema bayana kuwa ili ufanye biashara ya mazao ya misitu utatakiwa kutimiza yafuatayo:
1.    Kuwa na Usajili wa unapovuna na unapopeleka kuvuna
2.    Uwe na leseni ya biashara pamoja na nambari ya utambulisho wa mlipakodi (TIN)
3.    Awe na leseni ya uvunaji,
4.    Ulipe ushuru wa Serikali kwa kuingia na Halmashauri husika
5.    Awe na kibali cha kusafirisha mazao ya misitu (Transportation Pass)
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni imeelezwa kuwa mtandao huu wa usafirishaji wa mazao ya Misitu chini ya Bwana Mwarabu unafahamika hata kwa Mkurugenzi wa Misitu na bado mtandao huu umeendelea kuota mizizi na hivyo kulikosesha taifa mapato lakini pia kuhatarisha ustawi wa mazao ya misitu nchini kwa kuwa ukaguziwa mazao ya misitu na usafirishaji wake haufanywi kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa.



KUZOROTA KWA UWINDAJI WA KITALII
Mheshimiwa Spika, uwindaji wa kitalii ni tasnia muhimu sana kwa mapato ya taifa letu na ukuzaji wa uchumi, ambayo imekua ikiingiza kiasi cha shilingi billion 34 kwa mwaka. Jambo la kushangaza ni jinsi ambavyo Serikali ya CCM imekuwa ikipuuza mambo ya msingi ambayo yanaweza kuangamiza kabisa tasnia hii. Sheria ya wanyamapori ina mapungufu makubwa ambayo yamekua kikwazo kikubwa kwa wawekezaji na hivyo Kambi ya Upinzani inaamini kuwa ikichukua nchi, itafanya mabadiliko kwa kurekebisha Sheria hii ili iwe na tija hivyo kufanya uwindaji wa kitalii kuwa endelevu na kuongeza pato la taifa.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni karibu vitalu 28 vya uwindaji vilirudishwa na Wizara tayari imeshatangaza ili kutafuta wawekezaji.  Kadhia kubwa ambayo imesababisha kurudishwa kwa vitalu hivi ni pamoja na kuwa wawekezaji hawana imani kuwa wataendelea kufanya uwindaji katika vitalu ambavyo muda wa uwekezaji kwenye vitalu hicyo ni miaka mitano tu. Ikumbukwe kuwa mwekezaji hupewa miaka mitano tu ya kuweza kuendeleza kitalu.

Mheshimiwa Spika,  kwa mfano ili Simba avunwe sheria inataka awe na umri wa miaka kuanzia miaka mitano, kama mwekezaji atapewa kitalu wakati Simba ana chini ya mwaka mmoja   maana yake hataweza kumvuna ifikapo ukomo wa miaka mitano ya umiliki wa kitalu na hivyo kupoteza gharama ambazo ametumia. Msumbiji , ambao ni jirani zetu; wameweka ukomo wa umiliki wa kitalu kuwa miako kumi. Pamoja na miaka hii kuonekana kuwa ni mingi , inasaidia mwekezaji kuwa na uhakika wa kuvuna wanyama anaowagharamia.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inaamini kuwa, uwepo wa Sheria na Kanuni bora za wanyamapori ndio utakaostawisha uwindaji wa kitalii na kuliongeza taifa mapato. Hii pia itavutia wawekezaji kuwekeza kwa kufuata na kuzingatia sheria na  taratibu zilizowekwa kama vile , kulipa ada , tozo ,uhifadhi na uwindaji endelevu.

KUPOTEA KWA MAPATO KUTOKANA NA WAGENI KUTOLIPIA TOZO  WANAPOINGIA HIFADHINI MARA YA PILI.
Mheshimiwa Spika, toka kuanza kazi kwa Waziri Nyalandu, Waziri atakumbukwa kwa kufanya maamuzi yasiyo na tija nay a kukurupuka ikiwemo; swala la ulipaji wa single entry na kuchelewesha utekelezaji wa amri ya mahakama ya  tozo kwa mahoteli ya kitalii; kutaka kutoa sehemu ya hifadhi ya taifa ya saadani; mgogoro wa hifadhi ya taifa ya Ruaha (Ihefu); pamoja na kutangaza muda wa kurefusha uwindaji kutoka miezi sita mpaka tisa.
Mheshimiwa Spika, uingiaji wa wageni hifadhini zaidi ya mara moja bila kulipa tozo stahiki wanapoingia mara ya pili (yaani Double Entry) umeendelea kuikosesha TANAPA na taifa mapato. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, katika kipindi cha Juni, 2013 hadi Machi, 2015 kupitia Hifadhi za Serengeti na Ziwa Manyara, TANAPA ilipoteza mapato zaidi ya Shilingi Bilioni 1.3, hii yote ikiwa ni maamuzi ya Waziri Nyalandu.
Aidha, baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mgeni kulipa tozo kila anapoingia hifadhini kwa kipindi cha siku 16 kwa lango moja tu la Ikoma katika Hifadhi ya Serengeti, TANAPA iliweza kukusanya zaidi ya Shilingi Milioni 17 ambazo zingepotea endapo wageni wangeruhusiwa kuingia zaidi ya mara moja bila kulipa tena.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa wizara ya maliasili na utalii imeendelea kutengeneza mianya ya kupoteza mapato na hivyo kulisababishia Taifa hasara. UKAWA imejiandaa kuhakikisha kuwa wageni wanaoingia katika maeneo ya Hifadhi za Taifa zaidi ya mara mbili bila kulipa tozo stahiki wanadhibitiwa na hivyo  kuchangia ukusanyaji wa mapato.

KUPOTEA KWA MAPATO KUTOKANA NA KUCHELEWA KUTEKELEZA AMRI YA MAHAKAMA KUU YA TOZO YA PANGO (CONCESSION FEE)
Mheshimiwa Spika, kuchelewa kwa makusudi kwa Wizara hii kutekeleza amri ya Mahakama Kuu iliyotolewa Septemba, 2014 kumelifanya Shirika la Hifadhi za Taifa kupoteza kiasi cha Shilingi Bilioni 3 katika kipindi cha kuanzia Oktoba, 2014 hadi Machi, 2015. Fedha hizi zilizopotezwa kwa uzembe wa Waziri Nyalandu zingeweza kununulia madawati ya watoto wanaokaa mashuleni, ama kununua vitanda vya wajawazito wanaozalia chini ama pia kupunguza deni la MSD .  Leo hii, Waziri Nyalandu anaposimama kusoma mafanikio ya Wizara yake aeleze ni kwa nini amelisababishia hasara taifa! Halafu leo hii anakuwa mmoja ya watu wanaojitokeza kuwania uraisi, anapata wapi nguvu hiyo?

Mheshimiwa Spika, leo hii waziri anapolikosesha Taifa mapato, anajua kuwa hawezi kuwajibishwa na ndio maana UKAWA inaamini kuwa itakapopewa ridhaa ya kuliongoza Taifa hili, haitovumilia uzembe wowote utakaolisababishia Taifa ukosefu wa mapato kama huu uliofanywa na Waziri Nyalandu.

KUMEGWA KWA MAENEO YA HIFADHI ZA RUAHA NA SAADANI
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Waziri Nyalandu ilitoa tamko la kubadili Tangazo la Serikali lilioanzisha Hifadhi za Taifa za Ruaha na Saadani  kwa kumega baadhi ya maeneo ya hifadhi hizo kinyume cha Taratibu na Matangazo ya Serikali. Sababu za kumegwa kwa maeneo hayo ni kutokana na migorogoro ya ardhi na wananchi na/au wadau wengine katika maeneo husika.  Maeneo yanayopendekzwa kumegwa kwa mujibu wa Tangazo hilo ni pamoja na  maeneo muhimu ya kiiokolojia na kwa maendeleo ya uchumi na maisha ya wananchi wake. Kwa mfano eneo la vijiji 21 ambayo Mhe. Waziri amesema limegwe kutoka eneo la Ihefu/Usangu kwenye hifadhi ya Ruaha ni maeneo  muhimu ya Ardhi oevu kwa Bonde, ambalo ndio chanzo kikuu na pekee cha maji ya mto Ruaha.  Ikumbukwe kuwa mto Ruaha ni tegemeo pekee kwa ajili uzalishaji wa umeme kwa ajili bwawa la Mtera, maji kwa ajili ya viumbe hai ndani ya hifadhi ya Ruaha na  kwa ajili matumizi ya wananchi wanaoishi mwisho wa mto (Downstream) nje ya Hifadhi ya Ruaha.

Mheshimiwa Spika, Kambi  ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuacha eneo hili liendelee kuwa sehemu ya ardhi oevu na hivyo kufanya mto Ruaha kutiririka kwa kipindi kirefu cha mwaka. Aidha,  lazima eneo lilotengwa kama sehemu ya hifadhi katika eneo la Usangu-ihefu libakie hivyo na kwamba Serikali ya CCM ijue kuwa kutoa sehemu ya hifadhi kwa wananchi sio suluhisho endelevu kwa mustakabali wa maendeleo mapana ya nchi yetu na uhifadhi. 

Mheshimiwa Spika, kwa hifadhi ya saadani; Waziri alitangaza kumega eneo kubwa la hifadhi kwa ajili ya kilimo kikubwa cha miwa, na kulitoa kwa kampuni iitwayo eco-energy. Eneo hilo ni muhimu sana kwa maisha ya viumbe mbali mbali wakiwemo  wanyama na miti aina ya mikoko, kwenye mto wami ambalo ni muhimu kwa mazalio ya samaki. Eneo hilo ni muhimu sana kama mapito ya wanyama na kwa uwepo wa hifadhi ya saadani.  Umegaji wa namna hii wa hifadhi zetu tena ndani ya muda mfupi unaweka rehani uwepo wa hifadhi zetu. Swali la kujiuliza hapa ni kwamba kama inaweza kuwa rahisi hivi kwa hifadhi za Saadani na Ruaha kwanini lisiwezekane katika hifadhi nyingine za hapa nchini?

Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu hifadhi za Taifa ni maeneo yanayotengwa kwa mahitaji muhimu ya kiikolojia na maendeleo ya kiuchumi kwa nchi yetu. Aidha nchi yetu imepata umaarufu na heshima kubwa ya kuwa na vivutio vingi vya aina mbali mbali kutokana na maeneo yaliyohifadhiwa. Umegaji wa hifadhi za Taifa na maeneo mengine yaliyohifadhiwa sio suluhisho la utatuzi wa migogoro ya ardhi. Kutokana na kuongezeka kwa migogoro baina ya wananchi na TANAPA , UKAWA inawaahidi watanzania kuwa tutatengeneza mpango wa muda mrefu wa matumizi bora na endelevu wa ardhi (land use plans) utakaowekewa sheria na kanuni zitakosimamiwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kufanya maamuzi ya kukurupuka na yasiyozingatia ushauri wa Kamati wa Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa Waziri Nyalandu ndipo kulipokulisababishia hasara ambazo zingeweza kuepukika ina ikumbukwe kuwa maamuzi haya ndiyo yaliyosababisha hata kamati na wadau kuigomea bajeti yake kwenye vikao vya Kamati Dar Es Salaam na hivyo kusababisha hasara nyingine ya kuleta wataalamu wa wizara hapa Dodoma kwa siku mbili , gharama ambazo zingeweza kuepukwa , kama angesikiliza ushauri wa kamati. Je, Waziri anaweza kuliambia bunge hili ni kwa nini alifanya maamuzi makubwa kama haya kwa kukurupuka na kutokuzingatia ushauri wa kamati kwa maslahi ya nani,?  Kwa nini waziri alikuwa na kigugumizi kutekeleza maamuzi ya mahakama?

VITA DHIDI YA UJANGILI NCHINI
Mheshimiwa Spika, mwaka 2010 Novemba ziliibuka tuhuma za kutoroshwa kwa wanyama kwa kutumia ndege ya jeshi la Qatar, baada ya bunge kupokea  taarifa husika na ikiwa imepita miaka tatu  toka kuwasilishwa kwa taarifa hiyo kuna haja ya kujiuliza mambo  yafuatayo kuhusu kutoroshwa kwa wanyama wetu;
1.    wakati taarifa ya kamati inawasilishwa bungeni kulikuwa na kesi mahakamani kuhusu utoroshaji wa wanyamapori hai na hivyo Bunge kutopata nafasi ya kujadili jambo hilo, kwa sasa kesi hiyo imekwisha, je Waziri Nyalandu anatoa majibu gani?
2.    Mhusika mkuu katika utoroshwaji wa wanyama hao hai Bwana Kamran alitoroka kwenda nje ya nchi na kwa kuwa Serikali ya CCM inajidai kuwa na mtandao mkubwa wa intelijensia, je Bwana Kamran yupo nchi gani na ni hatua gani zinachukuliwa na Serikali kumrudisha nchini kukabiliana na mashtaka dhidi yake?
3.    Inawezekanaje ndege ya jeshi kutoka nchi nyingine kutua na kupakia wanyama katika viwanja vyetu bila vyombo vya usalama kufahamu?
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kuwa Qatar inadai kuwa hawakuiba wanyama bali waliwachukua wanyama hao kihalali na ndio maana Serikali yao ilikataa kutoa visa kwa wale maafisa wa Serikali waliokuwa waende huko kuchunguza sakata hilo kwa kuwa Serikali ya CCM iliwauza kihalali wanyama ambao leo inadai kuwa waliibwa. Maelezo ya serikali, ushahidi, wa mazingira ya utoroshaji wa wanyama pori hai una viashiria vyote kuhusu uhusika wa badhi ya watumishi, usalama wa taifa, jeshi la polisi  na viongozi wa Serikali na CCM  kuhusu kuhusika moja kwa moja kwao katika masuala ya ujangili kwa kuwa hata Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM anawajua majangili hao, je ni kwa nini hawafikishwi mbele ya Sheria?
Mheshimiwa Spika, Mwezi Machi mwaka 2014 Jumuiya ya kimataifa iliadhimisha kwa mara ya kwanza Siku ya Wanyamapori Duniani ambayo iliasisiwa na Umoja wa Mataifa (UN) kwa lengo la kuyahamasisha mataifa yote duniani kutambua na kuthamini umuhimu wa wanyamapori kwa maisha ya binadamu ili kuweka mikakati na mbinu za kulinda wanyamapori Kwa namna moja ama nyingine, hatua hiyo ya UN imeonekana katika macho ya wengi duniani kama inalenga kuishawishi dunia kupambana na vitendo vya ujangili katika sehemu mbalimbali duniani, hasa Tanzania na nchi nyingine kadhaa ambazo zimeshindwa kabisa kudhibiti vitendo vya ujangili na kusababisha mauaji makubwa ya wanyamapori ambao wako hatarini kutoweka, wakiwamo tembo na faru.
Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha kuona kwamba jina la Tanzania kwa muda mrefu sasa limetawala vichwa vya habari katika vyombo vingi vya habari duniani kutokana na Serikali kushindwa kukomesha vitendo vya ujangili dhidi ya wanyamapori hao walio katika hatari ya kutoweka, ingawa imekiri wazi kwamba inayajua vizuri majangili hayo. Siyo siri tena kwamba linapozungumziwa tatizo la ujangili, dunia inajielekeza moja kwa moja kwa Tanzania kama marejeo. Kama tulivyoeleza kwa miaka mingi kuwa Tanzania inaonekana mbele ya jumuiya ya kimataifa kama taifa ambalo halitambui kwamba kushamiri kwa vitendo vya kuangamiza wanyamapori kutalifanya kuwa maskini milele na pia Serikali ya CCM imeshindwa kabisa kukabiliana na ujangili na hivyo kuzua maswali juu ya tuhuma za muda mrefu kuwa Chama hiki kinafadhiliwa na majangili kwa kuwa baadhi ya watuhumiwa wa ujangili ni makada nambari moja wa CCM.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kushutumiwa na kusutwa kila kona ya dunia kutokana na kutopambana na ujangili unaosababisha mauaji ya tembo 11,000 kila mwaka, Serikali bado imeshikwa na kigugumizi kutekeleza ahadi yake ya kuteketeza tani zipatazo 90 za shehena ya meno ya tembo yaliyohifadhiwa katika maghala yake baada ya kuzikamata kutoka kwa wahalifu sehemu tofauti. Badala yake imekuwa ikifanya juhudi kwa muda mrefu ikitaka ipewe kibali cha kuuza shehena hiyo, lakini juhudi hizo zimegonga mwamba.
Mheshimiwa Spika, pengine ni vyema tukakumbuka kwamba hadi miaka ya hivi karibuni, Serikali imekuwa na mkakati wa kuzishawishi nchi zilizosaini Mkataba wa Kimataifa Dhidi ya Biashara ya Wanyamapori na Mimea Iliyo Katika Hatari ya Kuangamia (CITES), ili iuze shehena hiyo katika soko la kimataifa. Pamoja na msimamo wake kwamba fedha hizo zingesaidia katika vita yake dhidi ya ujangili, nchi hizo ikiwamo Kenya zilipinga vikali ombi hilo. Hali ya nchi kushutumiwa na kuaibishwa kimataifa ilijitokeza pia jijini London wakati wa kongamano lililoitishwa na Serikali ya Uingereza kujadili mbinu za kulinda wanyamapori dhidi ya ujangili. Kongamano hilo lilihudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 46, wakiwamo marais wanne kutoka Afrika na wakuu wa mashirika 11 ya kimataifa. Tanzania ndiyo iliyoonekana kuwa katikati ya masikitiko na shauku za wajumbe wa kongamano hilo kutokana na ukubwa wa tatizo la ujangili hapa nchini. Ni wakati wa kongamano hilo, ndipo ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Rais Jakaya Kikwete ulipotangaza kwamba umefuta mpango wake wa kuuza shehena ya meno ya tembo, pengine ikiwa ni hatua ya kuonyesha kwamba Tanzania sasa inayo dhamira ya kupambana na ujangili na biashara ya meno ya tembo. Na hatua hii ilisabbabishwa na vikwazo ambavyo nchi wahisani walionesha iwapo ingeendelea kupigania kuuza shehena ya pembe za ndovu ilhali ikijua biashara hiyo ni haramu duniani kote.
Mheshimiwa Spika, ni muda mrefu umepita sasa tangu ahadi ya kuteketeza shehena ya meno ya tembo ilipotolewa. Sisi tunauliza: Kama kweli Serikali imedhamiria kupambana na ujangili na kuionyesha dunia kuwa ina dhamira ya kweli, ni sababu zipi zinazokwamisha utekelezaji wa ahadi hiyo? Kigugumizi cha Serikali ya CCM ambayo yenyewe ndiyo yenye dhamana ya kulinda shehena hiyo, inatupa wasiwasi kuwa; haitoweza kutetekeza shehena hii haramu kama inavyofanya kuteketeza madawa ya kulevvya kwa kuwa bado ina nia ya kuuza shehena hiyo kwenye black market yaani soko haramu kwa njia za siri na kutumia fedha hizo kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.
Mheshimiwa Spika, huku taifa likiwa limegubigwa na taswira ya kuhalalisha ujangili mbele ya jumuia ya kimataifa, Rais Kikwete na Waziri Lazaro Nyalandu wakitumia fedha za walipakodi waliamua kujisafisha duniani kupitia CNN na BBC dhidi ya madai kwamba haijachukua hatua za kutosha kupambana na tatizo la ujangili nchini. Vyovyote vile, yeyote aliyeishauri Serikali itafute kampuni ya Uingereza ya masuala ya PR kumuunganisha Rais Kikwete na Christian Amanpour, na baadaye kumuunganisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Stephen Sackur wa kipindi cha Hard Talk cha BBC, kujisafisha huku wakijua kabisa Serikali ya CCM haina nia ya dhati ya kupambana na ujangili kwa kuwa Serikali hii hii imekua ikiwalea majangili alisababaisha taifa lipate aibu kubwa. Hatua ya Serikali ya CCM kukimbilia London kujisafisha kimataifa; ilhali nyumbani bado kuchafu ni hatua ya kuonesha kuwa Serikali hii inawaogopa majangili.
Mheshimiwa Spika, swali kubwa ambalo tunajiuliza ni iwapo Rais Kikwete ‘alifanikiwa’ kuisafisha Tanzania dhidi ya tuhuma hizo kwa kuiambia BBC kwamba anawafahamu vigogo 40 wa biashara ya ujangili nchini, lakini hajawakamata? Kwa kauli yake hiyo, ameichafua zaidi nchi kuliko kuisafisha. Rais hawezi kuwafahamu vigogo 40 wa biashara haramu ya ujangili pamoja na kiongozi wao na asiwakamate, na badala yake anakwenda London kutangaza kuwa anawajua japo hajawakamata, na kisha tuamini kuwa ‘ameisafisha’ nchi dhidi ya tuhuma hizo! Hii ni dhihaka kwa watanzania wote.  Vilevile ni  dhahiri kuwa BBC inatazamwa na kusikilizwa na wengi duniani , swali kubwa ambalo mamilioni ya watazamaji duniani watakua wanajiuliza ni Rais wa namna gani anayewafahamu kwa majina vinara 40 wa uhalifu nchini mwake lakini hawakamati? Iwapo taasisi kubwa inawafahamu vinara wa ujangili iweje ishindwe kupambana nao? Kauli hii ni kithibitisho kuwa ikulu na usalama wa taifa kwa kiasi kikubwa wanahusika na mtandao wa ujangili.
Mheshimiwa Spika, kauli za Rais Kikwete zimeendeelea kuushangaza umma hasa wananchi anaowaongoza kwa kuwa alishawahi pia kutamka hadharani kuwa anayo orodha ya vigogo wa biashara haramu ya madawa ya kulevya, na hata ya magogo; lakini kauli zake hizo hazikufuatiwa na kamata kamata yoyote mpaka leo. Hata hiyo orodha ya vigogo 40 wa ujangili amebaki nayo mwenyewe mpaka sasa anapokaribia kukabidhi madaraka kwa Serikali ya UKAWA. Tunamtaka Rais Kikwete kuhakikisha kuwa siku ya kutukabidhi Ikulu hasahau majina 40 ya majangili nchini.
Mheshimiwa Spika, Mafanikio ya operesheni dhidi ya ujangili hayapimwi kwa idadi ya pembe za ndovu zilizokamatwa (seizures), na wala hayapimwi kwa idadi ya waliokamatwa (arrests); bali hupimwa kwa idadi ya waliohukumiwa (convictions). Serikali ituambie , katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ni watu wangapi mpaka sasa wanatumikia vifungo jela baada ya kutiwa hatiani kwa ujangili? Na kati ya hao, Wachina ni wangapi na vigogo wangapi? Na ni watuhumiwa wangapi waliotajwa na Rais wameshatiwa hatiani mpaka sasa?
UDHIBITI WA BIASHARA YA MENO YA TEMBO
Mheshimiwa Spika, ikiwa  ni moja ya nchi wanachama waliozindua  Mpango wa Kulinda Tembo Duniani  uliosainiwa huko London mwezi Februari, 2014 na kuhudhuria makongamano na mikutano mbalimbali iliyofuata, Tanzania  imejiwekea maazimio kadhaa ambayo yanahitaji kutekelezwa:
§  Kufanya ukaguzi wa wazi kujua ni kiasi gani cha meno ya tembo kilichopo;
§  Ni kiasi gani cha meno ya tembo yaliyopatikana kihalali (legally acquired);
§  Ni kiasi gani cha meno ya tembo yamepatikana kinyume cha sheria;
§  Kuteketeza meno yote ya tembo yaliyopatikana kinyume cha sheria  katika hali ya uwazi kama nchi nyingine za China, Hong Kong, Ufilipino na Marekani zilivyofanya;
§  Kufanya jitihada za kuwaelimisha wale wale wawindaji haramu ili kupunguza biashara ya meno ya tembo.
Mheshimiwa Spika, kwa kiwango kikubwa mapendekezo hayo hayajetekelezwa ikiwemo kuteketeza shehena ya meno ya tembo pamoja na nyara nyengine zilizopatikana kinyume na Sheria yaani kwa njia haramu.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Kambi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikpendekeza kuwa ni lazima kufanya jitihada zaidi ili kuongeza kiwango cha utambuzi na uelewa wa kujua watanzania wanashiriki vipi katika biashara haramu ya meno ya tembo ambayo bado inaendelea kufanyika. Mwaka 2013 kulikuwa na matukio mawili makubwa  ya kukamatwa kwa meno ya tembo Dar es Salaam na Zanzibar. 
Mojawapo ya mambo ambayo tumekua tukishauri kwa muda mrefu ni pamoja na kuitaka Serikali kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba shehena kubwa za pembe za ndovu zinazokamatwa (zaidi ya kilogramu 500) zinachunguzwa kwa kupima DNA. Jambo hili bado halijafanyika. Aidha, tulielezea umuhimu wa  kufanya uchunguzi kama huu ili kuongeza weledi katika kubainisha maeneo ambayo uwindaji haramu unafanyika kwa viwango vya juu kwa kuwa Tanzania imepoteza sehemu kubwa ya urithi wake wa asili na mapato endelevu. Kama tembo wakiondoka, basi na watalii wataondoka vilevile na hivyo kuhatarisha ustawi na ukuaji wa sekta utalii.
Kambi ya Upinzani Bungeni natambua kuwa kuna hitaji kubwa la kutekeleza kwa ukamilifu na kwa wakati sheria ya wanyamapori ili hatua madhubuti za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wahalifu wote waliopo katika mtandao wa biashara hii haramu. Hii ina maana kwamba watakaoshtakiwa si wale tu wanaojihusisha na uwindaji haramu, bali pia washiriki wakubwa katika kuchakata, kuuza nje ya nchi, kununua kutoka nje ya nchi, kusambaza, kupokea, na kumiliki meno ya tembo kinyume cha sheria pamoja na wale wanaofadhili kifedha biashara ya meno ya tembo na kughushi nyaraka, matumizi ya fedha chafu (money loundering), ukwepaji wa kodi na ufisadi wowote kuhusiana na biashara haramu ya meno ya tembo.
Mheshimiwa Spika, wakati nchini Kenya, watetezi wa hifadhi waliishinikiza serikali kuanzisha sheria kali dhidi ya ujangili ili kuwepo na adhabu stahiki, pili idara ya wanyamapori ya kenya (KWS) na wahifadhi maliasili kutangaza teknolojia mpya ambayo itasaidia kupambana na ujangili kama ilivyotangazwa na Daily Nations ya tarehe 26 Machi 2013, na tatu serikali ya Kenya kuongeza askari zaidi ya 1,000 ili kukabiliana na ujangili, haya yote yakifanyika Kenya kukabiliana na ujangili, Serikali ya Tanzania inaendelea kujikita  kupiga vijembe kwa UKAWA na kuendelea kulinda majangili ambao taarifa zao zimekuwa zikizifikia mamlaka zilizo chini ya serikali.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitahadharisha CCM kuwa pamoja na kejeli na udhalilishaji kwa kambi yetu ya kuashiria kuwa na chuki ya wazi na UKAWA, UKAWA imejipanga kimkakati kuhakikisha kuwa inakabiliana na aina zote za ujangili ulioozesha taifa letu hasa mbele ya jumuia ya kimataifa.
UHARIBIFU WA MAZINGIRA KATIKA MLIMA KILIMANJARO
Mheshimiwa Spika, Mlima Kilimanjaro ni urithi wa dunia unaoteketea kutokana na uharibifu wa mazingira unaochangiwa na shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi hiyo muhimu katika sekta ya utalii. Hadi sasa wataalamu wa mazingira wamethibitisha kwamba barafu katika Mlima kilimanjaro imepungua kwa asilimia 82 ya theluji yote iliyopo tangu mwaka 1912 na kwa asilimia 52 ya theluji iliyopo sasa tangu mwaka 1962. Hali hiyo imechangiwa na vitendo vya kupungua kwa uoto wa asili hasa ukanda wa misitu ya asili ya mlima huo, ambao umekuwa ukiliingizia taifa mapato makubwa kutokana na utalii unaofanywa kila mwaka hapa nchini. Hali hii inatishia theluji hiyo kupotea kabisa na kufanya kizazi kijacho kuiona theluji hiyo kupitia picha za kitalii au vitabu vya hadithi tu.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro na Bwana Lonnie Thomson, mtaalamu wa Sayansi ya Theluji (Glaciologist) unaonyesha kwamba kuyeyuka kwa theluji ya Mlima Kilimanjaro unaendelea kwa kasi kubwa. Utafiti huo umebaini kuwa zaidi ya robo ya kiwango cha theluji kilichoufunika Mlima Kilimanjaro mwaka 2000 kilipotea ilipofika mwisho wa mwaka 2007. Bwana Thompson na washirika wake walitoa ripoti hiyo tarehe 2 Novemba 2009, katika mhadhara uliondaliwa na Chuo cha Kitaifa cha Sayansi cha Marekani (National Academy of Science). Takwimu hizo zinaonyesha kwamba uyeyukaji wa theluji katika Mlima Kilimanjaro uliongezeka kwa kiasi kikubwa miongo ya hivi karibuni, anasema Bwana Thompson. Inasemekana kuwa kuanzia mwaka 1912 hadi 1953 theluji inayofunika Mlima Kilimanjaro ilipungua kwa kiwango cha 1.1% kwa mwaka. Vivyo hivyo, kati ya mwaka 1953 na 1989 wastani wa kiwango cha kupungua kwa theluji kwa mwaka kiliongezeka na kufikia 1.4%.
Mheshimiwa Spika, inakadiriwa kuwa zaidi ya mito 20 na vyanzo vya maji vipatavyo 70 vilivyokuwa vikitiririsha maji yake kutoka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) katika wilaya za Rombo, Hai na Moshi Vijijini, vimekauka na kusababisha upatikanaji mdogo wa maji. Lakini hoja ni je, nani atamfunga paka kengele, kama wanaopaswa kutekeleza maagizo mbalimbali ya utunzaji wa Mlima Kilimanjaro ndi wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo vinavyouweka mkoa wa Kilimanjaro katika mikoa inayokabiliwa na uharibifu wa mazingira kwa kiwango cha juu kabisa? Kasi ya ongezeko wa uharibifu wa mazingira ni dalili kuwa utekelezaji wa sera, sheria na kanuni za mazingira una mapungufu na ni lazima Serikali ya CCM ikae kando ili Serikali itakayoundwa na UKAWA ichukue hatua madhubuti na za haraka katika kuulinda Mlima Kilimanjaro.
UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA UTALII NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa eneo kubwa la ardhi lililofunikwa na wingi wa misitu pamoja na aina mbalimbali za maua na viumbe, Tanzania  ni mojawapo ya vivutio vikubwa vya utalii barani Afrika. Nchi yetu ina raslimali nyingi asilia ikiwemo pamoja na maeneo mengi ya nyika za mapori yenye aina nyingi za banoai.
Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa vivutio vya utalii ni pamoja na Mbuga za wanyama , hifadhi za taifa, hifadhi zilizozuiliwa na  maeneo ya kihistoria. Hata hivyo kwa sababu ya ongezeko la joto, baadhi ya hivi vivutio ikiwemo theluji katika kilele cha mlima Kilimanjaro iko katika hatari ya kupotea. Na baadhi ya wanyama katika mbunga zenye ukame mkubwa wameanza kupungua na kuathirika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, kwa muda mrefu , imeshauri Serikali ya CCM kuwekeza katika njia mbadala ya nishati ya umeme ili kuinua sekta ya utalii hasa wa mbugani. Mojawapo ya vipaumbele vya Serikali itakayoundwa na UKAWA ni pamoja na kuhakikisha kuwa nishati ya jua (solar energy) inatumika kama chanzo kikubwa cha umeme ili kuweza kukabiliana na tatizo la umeme katika maeneo yanaongoza kwa kutembelewa na watalii hasa mbuga za wanyama, maeneo ya kihistoria na majengo ya kale.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji katika Sekta ya Utalii ni suala lenye tija kubwa katika uchumi wetu kwa kuwa sekta hiyo imekuwa ikichangia katika uchumi wa Taifa licha ya uwekezaji mdogo uliofanyika katika sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika, takwimu zilizopo zinaonyesha  kuwa katika maeneo yote  ya hifadhi zetu kwa sasa kuna  kuna hoteli zenye uwezo wa kutoa huduma za malazi (carrying capacity)  kwa watu 6,681 ambapo kwa miaka mitano ijayo idadi hii itafikia uwezo wa kulaza watu 8,421. Hiki ni kwango kidogo sana cha huduma za malazi kiasi kwamba tunapoteza fursa ya kunufaika katika sekta ya utalii.
Mheshimiwa Spika, miundombinu ya usafiri na usafirishaji ya ndani ya nchi, uwekezaji katika ujenzi wa hoteli kwenye maeneo muhimu ya utalii kama vile kwenye hifadhi, mikoa inayozunguka mlima Kilimanjaro kutasaidia sana kuvutia watalii. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kuwa uboreshaji wa miundombinu ya usafiri hasa wa anga ilini kipaumbele kikubwa cha kuinua sekta ya utalii nchini na kujenga hoteli za viwango vya Kimataifa katika maeneo yenye vivutio vya watalii ili kuvutia mashirika ya mengi ya ndege toka nje kuja hapa.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu tumekua tukileta mapendekezo kwa Serikali kuhusu umuhimu wa kufufua shirika letu la Ndege la Taifa ili tuweze kumudu ushindani katika usafiri wa anga na hapohapo kuongeza idadi ya watalii katika nchi yetu. Aidha, tumeshauri umuhimu wa kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro na ule wa Julius Nyerere Dar es Salaam ili kuwa kitovu cha usafiri wa anga na kuyafanya mashirika mengi ya kimataifa kutumia viwanja hivyo vya ndege na kuongeza idadi ya watalii wa nje wanaotembelea nchini.
Mheshimiwa Spika, watalii toka nje wanapenda sana kupanda ndege za nchi wanazotembelea zaidi kuliko kupanda ndege za kuunganisha ili kupunguza gharama za usafiri. Mfano mzuri ni miaka ya themanini wakati Air-Tanzania ilipokuwa inafanya safari zake nchi za Ulaya, watalii wengi walikuwa wanakuja kwa ndege zetu. Hoja ni kwamba Serikali imeshindwa kabisa kufufua Shirika la Ndege la Taifa (ATC). Pamoja na kuwa  Kambi Rasmi ya Upinzani ilipendekeza umuhimu Serikali kuingia ubia na makampuni binafsi kupitia mpango wa Private Public Pertnership – ( PPP) ili kuboresha na kuinua huduma za usafiri wa anga hapa nchini , Serikali imeshindwa kutekeleza mapendekezo yetu.
Mheshimiwa Spika ,  ikumbukwe kuwa sekta ya utalii nchini inaongoza kwa kuingiza fedha za kigeni nchini ikifuatiwa na madini. Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwaka 2014 sekta ya utalii iliingiza Dola 2 bilioni za Marekani na kuizidi sekta ya madini ambayo ilikusanya Dola 1.7 bilioni.
Mheshimiwa Spika, mgogoro ulioibuka baina ya Kenya na Tanzania unapaswa kuwa somo tosha katika kuhakikisha sekta ya utalii nchini inakuza uchumi na kuimarika ili kuliongezea taifa mapato. Mgogoro huo uliibuka baada ya nchi ztu kuwekeana masharti ikiwemo Kenya kuzuia magari yenye usajili wa Tanzania kubeba au kushusha watalii katika maeneo ya vivutio vya watalii na Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA). Kwa upande wa Tanzania sharti lililokuwapo ni kupunguza kupunguza safari za Shirika la Ndege la Kenya (KQ) kuingia nchini, kutoka 42 hadi 14 kwa wiki.
Mheshimiwa Spika, kwa kumbukumbu za Bunge lako , mgogoro huu ulianza Desemba 22, mwaka jana, baada ya Kenya kuzuia magari yenye usajili wa Tanzania kupakia au kuteremsha watalii kwenye vivutio vya utalii na viwanja vya ndege nchini humo. Baadaye mwezi huohuo, Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki, Biashara na Utalii wa Kenya, Phyllis Kandie alikutana na Waziri wa Utalii wa Tanzania, Lazaro Nyalandu na walipeana wiki tatu za kulitafutia ufumbuzi suala hilo. Baada ya muda huo kwisha bila muafaka, Februari 6, mwaka huu, Kandie alirejesha marufuku ya awali kwa madai kuwa Tanzania imeshindwa kuchukua hatua.
Mheshimiwa Spika, katika hali iliyoonekana ni kulipiza kisasi, Machi 18, mwaka huu, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA) ilipunguza safari za Shirika la Ndege la Kenya kutoka 42 hadi 14 kwa wiki, ambayo ni karibu na asilimia 60. Mpango huo ulitekelezwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa kati ya shirika na Serikali ya Tanzania ambayo ni safari 14 kwa wiki. Kuongezeka hadi safari 42 ilikuwa ni kinyume na makubaliano.
Mheshimiwa Spika, mgogoro huu ulikuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Tanzania kwa kuwa sekta ya utalii nchini, imeendelea kuwa chanzo cha mapato kwa wananchi wa mikoa ya kaskazini hasa vijana ambao wanaotegemea shughuli za utalii kujipatia kipato ili kuendesha maisha yao ya kilasiku.
Mheshimiwa Spika, watalii wanapitia Kenya kwa sababu ya usafiri. Shirika la Ndege la Kenya (KQ) linafika katika nchi nyingi ambako watalii wanatoka. Namna pekee ya kukabiliana na hali ni kuwa na Shirika la Ndege la Taifa kama ilivyokuwa ATC zamani. Tayari Tanzania imetajwa kama mojawapo ya nchi saba duniani zinazovutia watalii kwa wingi. Kwa sababu ya ushindani, ni wazi kuwa majirani watafanya kila jitihada kuhakikisha wanashindana nasi. Ni Shirika la Ndege la Taifa pekee ndilo litakuwa suluhisho la kudumu. Kuna wanaolikataa kwa madai kuwa litaingiza hasara. Ukweli ni kwamba, shirika la ndege mara nyingi huchochea ukuaji wa sekta nyingine. Shirika la Ndege la Taifa litachochea watalii wengi kuja nchini moja kwa moja na hivyo kukuza utalii. Litasaidia wafanyabiashara wa kilimo cha maua na mbogamboga kusafirisha bidhaa zao haraka kwenda ughaibuni.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kuwa ina uwezo wa kuiinua sekta ya utalii nchini kwa viwango vya kimataifa zaidi na kuifanya ichangie pato la taifa kwa asilimia kubwa zaidi ya sasa kutoana na mipango mikakati ambayo tuemjidhatiti kuisimamia.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana, miaka 35 mfululizo ya CCM kuliongoza hili taifa sio tu kwamba imeshindwa kulisaidia hili Taifa kuwashinda na kuwatokomeza maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini bali wamezidi kuimarika kwa njia tofauti-tofauti. Ahadi nyingi za CCM nyakati za uchaguzi na katika hotuba mbalimbali zimekuwa zikionesha kwamba CCM inatambua changamoto zilizopo na inajua ni nini kinaweza kufanyika ili kukabiliana na changamoto hizo.  Tatizo limekuwa katika uwezo mdogo wa CCM kuweka mifumo sahihi ya utekelezaji wa mipango na mikakati inayowekwa na kuisimamia ili kuhakikisha kuwa mipango na mikakati hiyo inazaa matunda yanayotakiwa. matokeo yake maadui hao wameendelea kuimarika na kwa Upande wa CCM, Chama kimeendelea kujiimarisha katika kubadilisha ahadi, kauli mbiu na ngonjera za kuhalalisha kuendelea kuwepo kwa matatizo hayo!






HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, wakati wa utawala wa Rais wa Mareani Jimmy Carte , Ronald Reagan ambaye alimshinda Jimmy Varter akiwa madarakani aliwahi kusema yafuatayo;
‘in this current crisis, the government is not the solution to our problem, the government is the problem’
Kwa kifupi maneno ya Ronald Reagan, yalimaanisha kuwa;
‘Katika kadhia hii, Serikali hii siyo suluhisho la tatizo letu, Serikali yenyewe ndiyo tatizo’.
Mheshimiwa Spika, sasa umefika wakati wa watanzania kutambua kuwa Serikali ya CCM haiwezi kutatua matatizo yao kwa kuwa Serikali hii hii ya CCM ndio Tatizo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.



..................................................
Mch. Peter S. Msigwa (MB)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA MALIASILI NA UTALII.

28.05.2015

No comments:

Post a Comment