Friday, May 1, 2015

Dk Slaa: Tutawarejeshea wananchi majimbo tata

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema endapo vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitashindwa kuafikiana katika kuachiana baadhi ya majimbo kabla ya Uchaguzi Mkuu, watawaeleza wananchi kwa kuwa ndiyo kiini cha kuanzishwa kwa umoja huo.

Dk Slaa alisema hayo jana kabla ya kumalizika kwa vikao vya wakuu wa Ukawa ambao wamekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani na kwa siku mbili kuanzia juzi, walikuwa wakijadili ufanikishwaji wa azimio hilo.

Dk Slaa alisema hadi sasa wameshakubaliana kuachiana asilimia 95 ya majimbo yote na kwamba ana matumaini watafanikisha, lakini akaonya kuwa ikishindikana, hawatasita kuwaeleza wananchi.

Mkoani Dar es Salaam, Ukawa imeshafikia muafaka katika majimbo mawili ya Kawe na Ubungo na kubakiza majimbo sita, wakati majimbo matano ya mikoa mingine bado yanaupasua kichwa umoja huo wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.

“(Kuanzishwa kwa) Ukawa ilikuwa ni ombi la Watanzania, ni sauti yao kwa hivyo taarifa zinazoendelea kutolewa siyo sahihi,” alisema akirejea habari kuwa Ukawa, iliyoanzishwa wakati wa Bunge la Katiba inaelekea kusambaratika kutokana na kushindwa kuafikiana kwenye baadhi ya majimbo.

“Kama ikitokea tumeshindwa kufikia makubaliano mwisho wa safari yetu, hakuna kitakachokuwa siri, tutawaeleza Watanzania,” alisema Dk Slaa.

Hata hivyo, alisema mpaka sasa hakuna dalili zozote za umoja huo kushindwa kuafikiana kwa sababu ya mvutano wa majimbo hayo, kwani mpaka sasa wameshafanikiwa kuyagawana kwa asilimia 95 nchini kote.

Alipoulizwa itakuwaje kama hawatafikia muafaka kwenye vikao hivyo vya siku mbili, Dk Slaa alisema bado kutakuwa na nafasi ya kuendelea na majadiliano katika vikao vingine.

“Aliyekwambia tuna ratiba ya kumaliza leo (jana) juu ya mgwanyo wa majimbo hayo ni nani? Hatuna ratiba maalumu kwa kuwa tunapanga ratiba wenyewe,” alisema Dk Slaa, ambaye ni mmoja wa watu wanaotajwa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa.

“Kuna mtu mwingine ambaye majadiliano yanapokuwa kwenye hali ya kuvutana, yeye anaona ni mpasuko. Sasa hilo ni tatizo kubwa.”

Habari za ndani kutoka katika vikao hivyo zinaeleza kuwa uliibuka mvutano mkali kuhusu mgawanyo wa majimbo 17 yaliyobaki mpaka sasa.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia alisema haoni dalili zozote za Ukawa kutofanikiwa katika asilimia tano zilizobakia.

“Kama tumeshakubaliana kwa asilimia 95, iweje tushindwe kuafikiana kwenye asilimia tano? Katika meza yoyote ya maridhiano, mvutano hauepukiki. Tunachoangalia ni ‘give and take’. Ikishindikana tutafuta tiba kwa sababu tunaijua,” alisema Mbatia ambaye anatajwa kutaka kuwania ubunge wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro.

Kikao hicho kilianza juzi wakati wajumbe walipopokea taarifa ya kamati mbili zilizokuwa zikifanya uchunguzi kwenye majimbo sita ya Dar es Salaam na majimbo kumi na moja ya mikoani.

Juzi, wajumbe hao walifanikiwa kugawana majimbo sita tu kati ya kumi na moja ya mikoani huku mengine yakibakia kwenye mvutano kabla ya kuanza mjadala wa majimbo sita ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Kikao hicho kilihusisha wenyeviti, makatibu, wajumbe wa sekretarieti za vyama hivyo.

Chanzo hicho kilieleza kuwa moja ya majimbo ambayo yalikuwa yanawakuna vichwa ni Serengeti ambako kigogo wa moja ya vyama hivyo anataka kuwania ubunge wakati chama chake hakina nguvu. Mkoani Dar es Salaam, mvutano katika majimbo sita unatokana na kila chama ndani ya Ukawa kuamini kuwa kwa kutumia nguvu ya umoja huo, mgombea wake anaweza kushinda.

“Kila chama kinahitaji kupata majimbo yaliyobakia bila hata kujali vigezo, kwa mfano, NLD ilikuwa inahitaji majimbo mengi lakini inaonekana kuwa na nguvu kwenye majimbo mawili tu ya Masasi na Lulindi ya Mtwara,” alisema mpashaji habari wetu.

Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema katika mipango ya chama chake, waliomba kupewa majimbo 35 wanayoamini kuwa wanaweza kufanya vizuri kwenye Uchaguzi Mkuu, lakini vyanzo vya ndani vinaeleza kuwa chama hicho kimepangiwa majimbo mawili tu mpaka sasa.

Alipoulizwa endapo hataweza kupata hata nusu ya majimbo hayo, Dk Makaidi alisema, bado haiwezi kuwa sababu ya kujiondoa ndani ya umoja huo.

“Siwezi kuondoka Ukawa nikikosa na pia siamini kama nitakosa majimbo, lazima yatapatikana tu,” alisema.

Kuhusu taarifa za kukabidhiwa majimbo mawili ya Lulindi na Masasi, Dk Makaidi alisema pamoja na majimbo hayo, leo (jana), walitarajia kuona hatima ya mgawo wa majimbo yote.

Mke wa Makaidi, Modesta Ponela ambaye mwaka 2010 aligombea ubunge wa Jimbo la Lulindi na kuibuka mshindi wa pili, alisema jana kwamba yuko tayari kugombea tena jimbo hilo endapo Ukawa itampitisha.




No comments:

Post a Comment