Saturday, May 23, 2015

CHASO wataka kutambuliwa kikatiba Chadema

UMOJA wa Wanachama wa Chadema ambao ni Wanafunzi wa Vyuo (CHASO) wamekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwaingia kwenye katiba ya chama hicho ili watambulike kisheria ndani ya chama hicho. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Wakizungumza kwenye mahafari ya tatu ya CHASO yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Landmark, Ubungo jijini Dar es Salaam wanafunzi hao waliuomba uongozi wa Chadema kuwaingiza kwenye katiba ya chama hicho ili wawe sehemu ya chama kama walivyo BAVICHA.

Akisoma risala ya mahafali hayo yaliyojumuisha wanafunzi 411 kutoka katika vyuo 15 vilivyopo Dar es Salaam, Katibu wa CHASO, Japhet Maganga alisema wanakutana na changamoto nyingi wanapokuwa kwenye harakati za chama wakiwa vyuoni.

Maganga amesema wamekuwa wakikutana na mambo mengi wanapojulikana wao ni wanachama wa Chadema, hivyo anawaomba viongozi wa Chadema kuwaingia kwenye katiba, lakini wawe mstari wa mbele katika kutatua matatizo yao wanayokutana wakiwa vyuoni.

“Tunakutana na mambo mengi sana tunapojulikana kuwa ni wanachama wa Chadema. Wapo waliofukuzwa chuo, kusimamishwa na kunyimwa haki nyingine kama wanafunzi. Sababu kubwa sisi ni Chadema,” amesema Maganga.

Katibu huyo amesema changamoyo nyingine ni kutengwa na uongozi Chadema katika vikao mbalimbali vya maamuzi ya chama, pamoja na kutopata vifaa vya chama kwa shughuli zao za chuoni.

Maganga aliongeza: “Tukitambulika kikatiba tutakuwa na wawakilishi kwenye mikutano ya juu ya chama. Faida nyingine tutakayopata ni kupata vifaa kama bendera, kadi na vinginevyo kwa shughuli za chuoni.”

Kwa Upande wake Mjumbe Kamati Kuu Taifa (CC) ya CHADEMA, Mabere Marando ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafari hayo, amesema amebeba changamoto hizo na ameahidi kuzifikisha kwenye sehemu husika na zitapatiwa ufumbuzi, haraka iwezekanavyo.

Marando amewataka CHASO wasife moyo na vikwazo wanavyokutana navyo kwani safari ya mapindzui siku zote huwa na changamoto nyingi. “Hata mimi nimepitia huko mlipopitia nyinyi lakini nilivumilia na nimefika hapa nilipo.

Mjumbe huo amewataka CHASO wawe chachu ya kutoa elimu kwa vijana wenzao, kujiandikisha, kupiga kura na kulinda kura zao ili kuhakikisha wanaitoa madarakani CCM.

Chanzo: Mwanahalisi Online

No comments:

Post a Comment