Wednesday, May 6, 2015

Chadema yafungua milango kwa wagombea

HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefungua milango kwa wanachama wake wenye sifa za uongozi kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea wa udiwani, ubunge na urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa amesema, mwanachama aliye tayari ajitokeze kuchukua fomu hizo.

Kwa kuzingatia makubaliano ya ushirikiano wao na vyama vinavyounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, ratiba ya Chadema imejikita zaidi katika kata na majimbo ambayo hawana wawakilishi.

Dk. Slaa amesema kuwa Mei 18 hadi Juni 6 mwaka huu, wanachama watachukua na kurejesha fomu za udiwani katika kata ambazo hawana madiwani kutoka kwa makatibu kata/ jimbo na wilaya.

Julai mosi hadi 10, watachukua na kurejesha fomu wagombea katika kata ambazo kuna madiwani wa Chadema na kati ya Julai 15 hadi 20 itakuwa ni uteuzi wa mwisho wagombea udiwani wa kata pamoja na wale wa Viti maalumu chini ya kamati tendaji za majimbo.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Mei 18 hadi 25, watachukua fomu wagombea ubunge katika majimbo ambayo Chadme haina wabunge kwa sasa, pamoja na fomu za ubunge wa viti maalum kutoka kwa makatibu wa majimbo, wilaya, mikoa,mikoa na makao makuu.

Julai 6 hadi 10, watachukua na kurejesha fomu za ubunge wagombe katika majimbo ambayo yana wabunge wa Chadema kwa sasa huku Julai 20 hadi 25, itakuwa uteuzi wa awali kwa wagombe hao.

Dk. Slaa ameongeza kuwa kuanzia tarehe hiyo ya Julai 20 hadi 25, milango ya wanachama wa Chadema wanaotaka kuwania kiti cha urais itafunguliwa rasmi makao makuu, huku uteuzi wa mwisho wa wagombea ubunge ukifanyika kati ya Agosti mosi hadi 8 mwaka huu chini ya Kamati Kuu.

“Tarehe 3 Agosti Baraza Kuu Taifa litakutana na Mkutano Mkuu utafanyika siku inayofuata, lakini uteuzi wa mgombea wetu wa urais utazingatia makubaliano ya Ukawa,” amesema Dk. Slaa

No comments:

Post a Comment