Thursday, April 23, 2015

Slaa: Utoaji zabuni vifaa vya BVR ufisadi, usanii.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amerejea kutoka Marekani huku akieleza kuwa utoaji wa zabuni ya kuingiza nchini vifaa vya uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura (BVR kits), ulikubikwa na ufisadi na usanii katika utoaji wa zabuni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Njerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, baada ya kuwasili, alisema Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ilikataa zabuni ya kwanza ya uletaji wa vifaa hivyo nchini, lakini serikali ikachomeka suala hilo bila kutangaza zabuni kama taratibu na sheria zinavyoelekeza.

“BVR ni ufisadi na usanii na ndiyo maana hakuna anayejua na hawataki kutoka hadharani kueleza mzabuni alipatikanaje, PPRA walipokataa zabuni ya kwanza serikali ikaenda kuchomeka bila kutangaza zabuni,” alisema.

Dk. Slaa alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imekuwa ikilalamikiwa kuhusiana na kuchelewa kuletwa kwa BVR, lakini dosari ya msingi katika suala la BVR ni serikali kushindwa kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivy0.

Alisema Agosti 30 na Septemba 8, mwaka jana, viongozi wa vyama vya siasa nchini walikutana na Rais Jakaya Kikwete

kujadiliana masuala kadhaa likiwamo la uandikishaji wa daftari la wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR na kukubaliana kuwa mambo ambayo siyo ya kikatiba na yasiyo ya lazima yasifanyike kwanza katika kipindi hiki ili kupunguza gharama.

Alisema miongoni mwa mambo waliyoyaomba yasifanyike kwanza ni kura maoni kwa ajili ya Katiba inayopendekezwa kwa kuwa siyo jambo la kikatiba, lakini katika hali ya kushangaza serikali ikatangaza tarehe ya kufanyika kura ya maoni licha ya kuwapo makubaliano hayo.

“Rais Kikwete alikubali na kupendekeza kuahirishwa kura ya maoni hadi baada ya uchaguzi mkuu ili kuokoa fedha ili zitumike kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, lakini hilo halikuzingatiwa,” alisema.

Aliongeza kuwa hadi sasa serikali imetumia fedha nyingi sana kufanya kampeni kwa ajili ya kura ya maoni na cha kushangaza ni kuwa serikali ndiyo inayofanya kampeni badala ya wananchi.

Dk. Slaa alisema wamebaini kuwa kuandikisha wapiga kura kwa kutumia BVR ni mbinu inayofanywa na serikali kwa sababu kuna maeneo ambayo wananchi hawataandikishwa na ndiyo maana wameanza maeneo ambayo ni ngome za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Tunataka kuwaambia kuwa tumeshtukia na tunatoa rai kwa Rais Kikwete nchi hii ni muhimu kuliko yeye, nchi ni muhimu kuliko CCM na kuliko Chadema, hata siku moja upinzani hauwezi kuleta vurugu utaletwa na serikali yenyewe inayotaka kulazimisha mambo yake,” alisema.

Hata hivyo, alisema kukwama kuandikisha wananchi katika daftari kwa kutumia BVR Chadema haiwezi kukimbilia mahakamani kwa sababu zipo kesi nyingi za Chadema ambazo hazijaanza kusikilizwa.

MAJIBU YA TUME
Alipoulizwa kuhusiana na madai hayo, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, alisema mchakato wa kumpata mzabuni ulifuata taratibu zote za kisheria na kama kuna ambaye hakuridhika, alipaswa kukata rufaa kwa mujibu wa sheria.

Alipoulizwa kuhusu kampuni zilizoomba zabuni ya kuleta BVR, alisema aulizwe Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba.Hata hivyo, Malaba, alipoulizwa, simu yake ilikuwa ikiita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu.

Kuhusu madai kuwa uandikishaji unapendelea CCM, Jaji Lubuva alisema uandaaji wa ratiba hauangalii vyama bali waliangalia mikoa jirani na Mkoa wa Njombe ambao ulikuwa wa kwanza kuandikisha wapigakura.

AONYA UCHAGUZI MKUU
Dk. Slaa akizungumzia suala la uchaguzi mkuu unaoatarajia kufanyika Oktoba mwaka huu, alisema serikali isithubutu kuuahirisha kwa kuwa upo kwa mujibu wa katiba na kama inataka kufanya hivyo ijifunze katika nchi nyingine ambazo zimekumbwa na machafuko kwa sababu watawala wake wamekuwa ving’ang’anizi wa madaraka.

“Tunataka kumwambia Kikwete muda wake unaisha Oktoba 28, mwaka huu mpaka pale atakapoapishwa rais mpya,” alisema.

Alimtaka Rais Kikwete apunguze ziara za nchi na badala yake atumie fedha kwenye daftari la kudumu la wapigakura ili wananchi wengi wapate fursa ya kupigakura.

ACT HAWANA UBAVU KWA CHADEMA
Akizungumzia Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT) Wazalendo , alisema hakiwezi kuitisha Chadema hata kidogo.

“Chadema tumeijenga kuanzia ngazi za chini kwa miaka mingi, hatumuogopi yeyote. Dk. Slaa, Mbowe na timu nzima tumezunguka Tanzania nzima kijiji kwa kijiji, hivyo hakuna mtu yeyote atakayekuwa tishio kwetu,” alisema.

AUPINGA MUSWADA WA MAKOSA YA MTANDAO
Kuhusu Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, alisema sheria hiyo haifai na kwamba atakuwa tayari kuwa mtu wa kwanza kufungwa kwa sababu haiwezekani mtu atumiwe ujumbe mfupi wa maneno katika simu yake halafu anakamatwa na kushitakiwa.

“Hatuogopi kufungwa, mimi nitakuwa wa kwanza kwenda kupelekwa gerezani kwa sababu ninaamini kama nitaletewa meseji au jambo lolote litakalohusiana na hiyo sheria na nikapelekwa mahakamani ndiyo utakuwa ukombozi wa Taifa hili utaanzia hapo hapo,” alisema.

Alisema ni kitu ambacho hakiwezekani kwenda kumshtaki mtu kwa kuandika mawazo yake, fikra zake kwenye mtandao bila kueleza ni fikra hizo zinakiuka vipi fikra za mwingine kwani kosa ni kukiuka haki ya mtu mwingine, lakini siyo kuandika fikra kwenye mtandao.

VURUGU AFRIKA KUSINI
Alisema vurugu nchini Afrika Kusini wanazofanyiwa raia wa kigeni zimetokana na serikali ya chama cha ANC kushindwa kuwahudumia vijana wake na kwamba hilo bomu linaweza kutokea hata Tanzania.

“Kuna vijana wengi hawana ajira, na ndiyo maana yanazaliwa makundi kama Panya road, Mbwa mwitu chanzo ni kukosa ajira,” alisema.

Dk. Slaa alisema: “Ifike mahali Waafrika wawe watu wa demokrasia, mwenzao akikosea akavuruga demokrasia, unamwambia kwamba amekosea bila kuoneana aibu.”

Alisema msingi wa ziara yake ni kwenda kujenga mahusiano Marekani na kwamba amejifunza mambo mengi.

ZIARA YAKE MAREKANI
Dk. Slaa alifanya ziara hiyo kufuatia mwaliko wa Gavana wa Jimbo la Indiana, Mike Pence, pamoja na taasisi mbalimbali za Marekani vikiwamo vyuo vikuu kutokana na kutambua mchango wake na chama chake kisiasa na kijamii katika maendeleo ya Bara la Afrika.

Akiwa nchini humo alishiriki mijadala mbalimbali inayohusu uwekezaji, elimu na uongozi iliyoandaliwa kwa ajili yake ambayo lengo lake kuu ni kuitangaza Tanzania na mihadhara kwenye vyuo vikuu vya Purdue, Indiana na Marion.

No comments:

Post a Comment