Friday, April 17, 2015

Ndesamburo amtangaza mrithi wake Moshi Mjini

Mbunge wa Moshi mjini, Philemon Ndesamburo, juzi alifanya tukio la aina yake pale alipomtangaza Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael kuwa ndiye atakayerithi mikoba yake.

Tangazo hilo sasa linavunja minong’ono iliyokuwa imezagaa kwamba Ndesamburo hatagombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao, baada ya kuliwakilisha jimbo hilo kwa miaka 15 kuanzia 2000.

Ndesamburo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Kilimanjaro alimtangaza Michael katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Manyema kuwa ndiye anatamani awe mrithi wake.

“Niwatafutieni mbunge nisiwatafutie? Niwatafutieni mrithi wangu niache? Nimtaje nisimtaje?”, hayo ndiyo maneno aliyoyatumia Ndesamburo kuwauliza wananchi kama amtaje mrithi wake au la.

“Mtaniunga mkono kwamba nitakayemtaja ndiye mtakayemsaidia? Jaffar njoo hapa bwana (akimwita Meya). Sasa nawaambia wakati ukifika ndio huyu nitakayemfanyia kampeni,” alisema Ndesamburo.

Huku akiwa amemnyanyua mkono, Ndesamburo alisema muda ukifika atamleta Michael mbele ya wananchi ili wamfanyie kampeni. Kauli hiyo ilifanya umati uliohudhuria mkutano huo kulipuka kwa furaha.

“Nimefanya hivi kwa ajili ya kuondoa majungu, kwa ajili ya kuondoa makundi na kwa ajili ya kujenga umoja wa chama chetu,” alisema huku akimsifia kuwa ni mtu msafi na anayewajibika kwa wananchi.

Hata hivyo, katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alipoulizwa jana kuhusu uamuzi huo wa Ndesamburo alisema haikuwa sahihi kumtangaza mrithi akisema ni kinyume cha Katiba yao.

“Ninakubali maoni yake binafsi kama binadamu, lakini kama mwenyekiti wa mkoa haikuwa sahihi kwa sababu hiyo ni kinyume cha Katiba. Akifanya hivyo anaminya demokrasia ndani ya chama,” alisema.

Mkazi wa Pasua Relini, Charles Mboya alipoulizwa na gazeti hili amechukuliaje uamuzi huo wa Ndesamburo alisema Meya huyo anakubalika na ndio maana hata Rais Jakaya Kikwete alimfagilia.


“Kama Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa taifa wa CCM alimfagilia Meya huoni hilo ni jembe? Kwa kweli mimi namkubali kwa sababu ni mtu mwenye msimamo thabiti,” alisema Mboya.

Februari 10, wakati Rais Kikwete akizindua jengo la kitega uchumi la Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF), alimsifu Meya kwa kutekeleza vizuri ilani ya ‘CCM’ na kuahidi kuiongezea pesa Halmashauri.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Manispaa ya Moshi, Priscus Tarimo alisema jana ameshangazwa na uamuzi huo wa Ndesamburo badala ya kuacha demokrasia ifuate mkondo wake.

Ndesamburo alianza safari ya Ubunge Jimbo la Moshi Mjini katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, lakini akaangushwa na Joseph Mtui aliyegombea kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi.

Mwaka 2000 akajitosa tena safari hiyo akipata upinzani kutoka kwa hasimu wake wa karibu wakati huo, Elizabeth Minde wa CCM ingawa aliibuka na ushindi wa asilimia 62.

Minde, ambaye ni wakili wa kujitegemea mjini Moshi alijitosa tena kuchuana na Ndesamburo mwaka 2005, lakini alishindwa tena baada ya Ndesamburo kupata kura 32,035 dhidi ya 23,773 za Minde.

Mwaka 2010, Ndesamburo alijitosa kutetea kiti chake na kuibuka na ushindi kwa kupata kura 28,697 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Justine Salakana wa CCM aliyepata kura 16,972.

No comments:

Post a Comment