Sunday, March 1, 2015

Mbowe: Polisi mnashindwa kubaini wauaji albino, mnabaini maandamano

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameilaumu intelijinsia ya jeshi la polisi nchini kwa kugundua maandamano yanayopangwa na vyama vya siasa vya upinzani na kushindwa kugundua mipango ya wauaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).

Akifungua mkutano wa siku tatu wa wadau, kamati tendaji na baraza la uongozi wa kanda ya Ziwa Victoria jijini Mwanza jana ukijumuisha mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza, Mbowe alisema ni aibu ya ndani na nje ya nchi kwa matukio yanayotokea hivi sasa ya mauaji ya albino.

“Hawa polisi kwanini intelijinsia yao inafanya kazi kwenye mipango ya maandamano ya Chadema na vyama vingine vya upinzani…yale machozi ya waziri mkuu Mizengo Pinda bungeni yameenda wapi,” alihoji Mbowe.

Alisema ni wajibu wa jeshi la polisi kugundua mipango yote inayofanywa na watu wanaojihusisha na utekaji na mauaji ya albino kuliko kutumia gharama kubwa kujishughulisha kuzuia mikutano ama maandamano ya Chadema.

Hata hivyo, Mbowe alisema Rais Jakaya Kikwete, ameshindwa kuwalinda raia na mali zao hususan watu wenye ulemavu wa ngozi, na kusababisha kuwaacha watendaji wasiowajibika tangu mauaji ya albino yaanze miaka tisa iliyopita.

“Viongozi wetu baada ya kusimamia ulinzi wa maalbino, wanakuwa mstari wa mbele kutoa machozi pale mauaji yanapotokea…huku jeshi la polisi likishindwa kuzuia matukio hayo yasitokee,” alisema.

Akizungumzia mfumo mpya wa Biometric Voters Registration (BVR), alisema mpango huo umekuwa na gharama kubwa kwa serikali kutokana na mashine hizo kununuliwa kwa bei ‘mbaya’ zaidi.

Hata hivyo, Mbowe alisema kutokana na wingi wa watu, Tume ya Uchaguzi inatakiwa kuongeza muda wa uandikishaji katika daftari hilo ili kutoacha mtu yeyote kutojiandikisha.

“Kati ya mashine 800 zinazohitajika nchini, ni 80 tu ndizo zilizoingizwa ili kukidhi mahitaji ya watanzania zaidi ya milioni 40…kweli zoezi hilo litakuwa gumu kwa Tume,” alisema Mbowe.

Aidha, kabla ya ufunguzi wa mkutano huo, Mbowe alizindua mafunzo ya uzalendo kwa vijana wa chama hicho, Red Brigedi, kaika ofisi za kanda ya chama hicho Kona ya Bwiru jijini Mwanza.

No comments:

Post a Comment