CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuanguka kwa uchumi na kukithiri kwa vitendo vya kifisadi nchini, unasababishwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushindwa kusimamia sera za uwajibikaji, uadilifu na uaminifu kwa Taifa.
Kauli hiyo imetolewa juzi na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalim alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Sengerema mjini hapa Mkoa wa Mwanza.
Mwalim ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, alisema kuwa anguko la uchumi na kuongezeka maradufu kwa umasikini hapa nchini unachangiwa na utawala mbovu wa Serikali ya Chama Cha Mapinuzi.
Alisema CCM na Serikali yake imetelekeza misingi imara na thabiti ya kujenga na kuinua uchumi wa viwanda na kilimo iliyoachwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hivyo haipaswi kuchaguliwa tena katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu 2015.
“Nchi hii imegeuzwa na CCM kuwa kama bwawa la kambare kila mmoja wakiwemo watoto wadogo nao wanasharubu. Yaani CCM imewafikisha sehemu mbaya zaidi wananchi kwa umasikini na huduma mbovu za kijamii ikiwemo ile ya afya, elimu, maji na barabara.
“Leo mnasikia akina William Ngeleja wanahusishwa na ufisadi wa fedha za Escrow. Naomba niwaambie kwamba Ngeleja ni mtu mwadilifu sana, sema tu kwamba na yeye yumo kwenye ukoo wa sawa na panya wa CCM inayotafuna hela za umma bila kuwahurumieni ninyi wananchi mliopigika na umasikini,” alisema Mwalim.
Huku akishangiliwa na umati wa watu, Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema Zanzibar, alisema ili Watanzania wajinusuru na ugumu wa maisha walionao kwa miaka mingi sasa wanapaswa kuchagua Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) katika UchaguzI Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Alisema ugumu wa maisha unaowaelemea Watanzania licha ya Taifa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali duniani, ni fundisho kwa wananchi kufanya mabadiliko ya kiuongozi na utawala, kwa kuitoa Serikali ya CCM madarakani na kuweka utawala wa UKAWA 2015.
Alimshtumu Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi na utawala wa Rais Jakaya Kikwete, kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo katika kuwasaidia wananchi kuondokana na adha ya umasikini na uduni wa huduma za kijamii.
“Pamoja na kwamba UKAWA tukifanikiwa kuunda Serikali Oktoba 2015, tutahakikisha tunaanzisha mchakato wa kuunda Katiba Mpya kwa kuyaingiza maoni ya wananchi yaliyokataliwa na CCM ambayo yamo kwenye Rasimu ya Jaji Joseph Warioba,” alisisitiza Mwalim.
Aidha aliwasihi wananchi kutoipigia kura Katiba Mpya Inayopendekezwa, kwani imeandaliwa kwa ajili ya kulinda mafisadi, badala yake wajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili Oktoba waiangamize CCM katika sanduku la kura kwa kuichagua UKAWA kuingia Ikulu.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment