Wednesday, March 4, 2015

Chadema Kilosa wamjia juu Pinda.

Na Bryceson Mathias, Morogoro.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemjia juu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kikidai, Mauaji na Maafa ya Wakulima na Wafugaji, Mbigili na Mabwegere, yametokana na Serikali kupitia kwa Pinda, kutomsikiliza aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Jaji Fredrick Werema.

Akihojiwa na Tanzania Daima Jumatano, Mwenyekiti wa Tawi la Chadema Mbigili, Maftaha Hamis, alisema, Chadema kimejifunza kwa masikitiko, kuona Mauaji na Maafa ya Wakulima na Wafugaji, Mbigili na Mabwegere, yametokana na Pinda, kutomsikliza Jaji Werema.
Ndani ya barua ya Werema aliyomwandikia Pinda gazeti limefanikiwa kuona alisema, amebaini Uhalali wa Kijiji kinachojiita ‘Mabwegere’ (Usajili Na. 32758 wa 8.12.198), una shaka kwa sababu, kilipata Hati ya kumiliki Ardhi miaka 10 kabla ya kuanzishwa, Hati Na. MG/KJJ.522 ya Juni 16, 1999.

Hamis alidai, “Katika barua ya AG Kumb. AGC/G.20/19/162 ya 1.8. 2014, siku chache kabla ya Maafa ya kuchomwa Moto Nyumba 40, ikifuatiwa na Vifo vya wakulima wawili na Mfugaji mmoja, Werema alimwandikia Pinda akisema, ‘Ninashauri hatua hizo zichukuliwe haraka’”.

Ushauri wa Werema ulitokana na barua ya Waziri Mkuu Kumb. PM/P/1/569/29 ya Mei 8, 2014 kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, na kunakiliwa kwa AG kwa lengo la kujadiliwa, ambapo Werema na Bendera, walikutana mara Mbili kwenye Ofisi zao.

Kwenye uchambuzi wa Kesi za Hukumu ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa kuhusu Mgogoro wa Ardhi kati ya Kijiji cha Mabwegere na Vijiji Jirani, AG alitaja, “Mambo muhimu aliyogundua juu ya hukumu hizo, zilisababisha damu za watu kumwagika na mali kupotea.

“(i)Mahakama haikutoa uamuzi wowote kuhusu uhalali wa kuanzishwa kwa Kijiji cha Mabwegere; (ii) Mahakama haikuilekeza Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, kuipa hadhi ya Kijiji, Kijiji cha Mabwegere, Jukumu hilo si lake;

“(iii) Mahakama iliamua kwamba, Hati ya kumiliki Ardhi iliyotolewa kwa kinachoitwa Kijiji cha Mabwegere ni Hati halali; na (iv) Mahakama iliamuru kwamba, haukutolewa ushahidi wa kuthibitisha kwamba, Hamis Msabaa na wenzake 37, walivamia kijiji cha Mabwegere”.ilisema sehemu hiyo ya barua ya AG kwa Pinda.

Aidha Werema alisema, kumbukumbu zinatoa tafsiri kwamba, Kijiji cha Mabwegere kilimilikishwa Ardhi miaka 10 kabla ya kuanzishwa kwake. Kisheria Kijiji au Mtu asiyekuwepo, hawezi kumiliki Mali ikiwa ni pamoja na Ardhi; Hivyo Kijiji cha Mabwegere kumilikishwa Ardhi kabla ya kuanzishwa kwake, kunatia shaka.

No comments:

Post a Comment