Friday, March 6, 2015

CCM iache kuweweseka mafunzo ya uzalendo vijana wa CHADEMA.



CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

CCM iache kuweweseka mafunzo ya uzalendo vijana wa CHADEMA.


Kwa mara nyingine tena Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimerudia kutoa kauli kuhusu mafunzo yanayotolewa kwa vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwa ajili ya kuwafunza maadili ya uzalendo kwa nchi, ukakamavu na kuwandaa vijana wa chama katika misingi ya uongozi.

Kupitia Idara ya Habari na Mawasiliano, CHADEMA tunatumia fursa hii; kwanza kufafanua dhana ya mafunzo hayo wanayopewa vijana wa CHADEMA, pili kuwasaidia CCM kujua adui yao halisi atakayewaondoa madarakani mwaka huu, tatu kuendelea kuwatia shime Watanzania kusimamia masuala ya msingi yanayolikabili taifa kwa kuelewa malengo ya propaganda za Abdulrahman Kinana na Nape Nnauye wanazofanya kupitia mikutano ya hadhara.

Mafunzo ya vijana yanayofanyika nchi nzima

Kama inavyojulikana, msingi wa mafunzo kwa vijana wa CHADEMA yanayoendelea nchi nzima kupitia njia ya makongamano ya wazi uko katika Katiba ya Chama iliyosajiliwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ibara ya 7.7.5 inayosema;

“Kutakuwa na mfumo wa ulinzi na usalama wa mali, viongozi na maslahi ya chama utakaotambulika kama Brigedia Nyekundu (Red Brigade).”

Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwapatia Vijana hao wa CHADEMA maarifa juu ya maadili ya uzalendo kwa nchi yetu (kama vile kulinda rasilimali za nchi, kupiga vita ufisadi na rushwa), wanafundishwa ukakamavu na kuwandaa katika misingi ya uongozi ndani ya jamii.

Makongamano ya mafunzo hayo yanafanyika kwa wazi. Vyombo vya habari vinakaribishwa kwa ajili ya kuuhabarisha umma. Maofisa wa Serikali wanakaribishwa kutoa mada. Mathalani wakati wa kongamano la namna hiyo Jimbo la Solwa, uongozi wa chama katika eneo hilo ulipeleka mwaliko Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga ili atoe mada ya ulinzi shirikishi kwa vijana wale.

Katika hotuba zote za uzinduzi wa makongamano hayo au kufunga, Mwenyekiti wa Chama (T), Freeman Mbowe amesisitiza kuwa CHADEMA kama taasisi ya kisiasa daima inaendesha shughuli zake kwa kuzingatia mipaka ya sheria na taratibu za nchi. Amekuwa akiwaelekeza vijana hao kuwa watiifu kwa jamii, wakitumia maarifa yao waliyoyapata katika mafunzo kusimamia haki bila kujali tofauti za itikadi za kisiasa, dini wala kabila.

Mbali ya mafunzo ya Nyanja ya kisiasa, vijana pia wanafunzwa namna ya kuwa wajasiriamali ikiwa ni nyenzo ya kujitafutia maendeleo ya kiuchumi na masuala ya mahusiano katika jamii, elimu inayowasaidia namna ya kulinda afya zao dhidi ya magonjwa mbalimbali na miili yao kuwa imara.

Yote haya yamekuwa yakizungumzwa mbele ya hadhara, vyombo vya habari vimeripoti. Sasa jambo la kushangaza ni kwanini CCM wanapata kiwewe kwa vijana kufundishwa maadili ya uzalendo, kupiga vita ufisadi na rushwa, kusimamia haki katika jamii, kuwa wakakamavu na kujifunza njia za kujipatia vipato kwa ajili ya uchumi wa mtu mmoja mmoja?

Jibu lake liko wazi, CCM chama kilichogeuka kuwa mwamvuli wa mafisadi na mbolea inayomea ufisadi, hakiwezi kufurahia kuona vijana wakipewa mafunzo ya uzalendo kwa nchi yao.

Chama kilichohakikisha kinaondoa uadilifu, uwazi na uzalendo kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya, hakiwezi kukubali vijana ambao ni moja ya nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa letu na ujenzi wa demokrasia imara, wapewe mafunzo yatakayowasaidia kusimamia haki na kupinga dhuluma katika nchi.

Ni wazi kuwa chama kilichopoteza ushawishi na uhalali wa kisiasa katika jamii, kikitegemea kushinda uchaguzi kwa hila mbalimbali kama rushwa na kuchakachua kura, hakiwezi kufurahia kuona vijana wakipewa elimu ya madhara ya rushwa na kupiga vita.

Adui wa CCM si Red Brigade ni kushindwa kwa chama hicho;

Kila Mtanzania makini kwa sasa anajua kuwa tishio la kwanza litaloiangusha CCM kutoka madarakani hasa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni kupoteza ushawishi na uhalali wa kisiasa kwa Watanzania ambako kumesababishwa na masuala kadhaa ikiwemo kushindwa kwa sera za chama hicho kuwapatia Watanzania haki na matumaini katika nchi yao, kwa ajili ya amani na utulivu wa kweli.

Adui mkubwa atakayeiondoa CCM kwenye utawala wa nchi hii mwaka huu si Red Brigade. Ni CCM yenyewe ambayo imelewa madaraka kiasi cha kushindwa kusikiliza na kutekeleza matakwa na maslahi ya wananchi. Ushahidi wa hilo ni namna chama hicho kilivyotumia njia haramu na kufanya uharamia kuharibu mchakato wa kuwapatia Watanzania Katiba Mpya na bora kwa ajili ya msutakabali mweka wa taifa letu.

Wananchi wamekiona kibri hicho cha CCM kujiweka juu ya wananchi na tayari wameanza kuiadhibu, wakionesha utayari wa kuiondoa madarakani mwaka huu. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umedhihirisha hasira za wananchi na kwamba wameiva kwa mabadiliko, wakijiandaa kuchagua chama kingine kuchukua dola. Adui wa CCM ni kushindwa kwake kuwatumikia Watanzania.

Mkusanyiko huu utaiondoa CCM;sera mbovu, mipango dhaifu, kukosa utashi wa kisiasa kuwatumikia watu, kuacha misingi yake kama chama cha siasa, kushindwa kujisafisha (mf; kujivua gamba), kutoa ahadi za uongo kwa wananchi wakati wa uchaguzi (mf; maisha bora kwa kila Mtanzania), kushindwa kuondoa maonevu, manyanyaso na ukatili (mf; katika migogoro ya ardhi, vyombo vya dola), kukumbatia ufisadi, kushindwa kusimamia Serikali kuwatumikia wananchi katika kutoa huduma za msingi kama vile elimu, afya, maji.

Kushindwa kwa sera zake katika kusimamia rasilimali za taifa ili zitumike kwa manufaa na maendeleo ya Watanzania, badala yake wananchi wengi wanazidi kutopea kwenye lindi la umaskini katikati ya utajiri mkubwa unaowanufaisha watu wachache ambao sasa baada ya kushiba wameanza kutoa lugha za kejeli na dharau kwa maskini wasiokuwa na uhakika wa mlo wa kila siku. Kushindwa huko ndiyo tishio kubwa la CCM.

Vijana wa CHADEMA hawapewi mafunzo ya siri, hawafundishwi kudhuru watu, hawafundishwi kutumia silaha. Lakini hayo ndiyo wanayofundishwa vijana wa CCM kwenye kile kikosi cha Green Guard.

Walichojadili Kamati Kuu

Katika kikao Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika hivi karibuni, mojawapo ya mambo waliyokubaliana ni kutumia mikakati mbalimbali ya propaganda kupitia mikutano ya hadhara ya Kinana na Nape na wengine ili kuwatia hofu Watanzania na kuibua mijadala mingine ili kuwasahaulisha Watanzania kujadili masuala ya msingi yanayoamua hatma ya taifa letu.

Chama hicho hakipendi kuona Watanzania wakihoji udhaifu unaoendelea katika uandikishaji wa daftari la wapiga kura. Hakiko tayari kuona wananchi wakijikita kujadili na kuhoji hatma ya nchi yao kama ufisadi unazidi kutamalaki kiasi cha mafisadi kutamba kama vile wameiweka Serikali ya CCM mifukoni mwao.

Ili kuwafanya wananchi wasijadili mambo makubwa ambayo CCM haina majibu (kushindwa), wakaamua kurudi na propaganda dhidi ya mafunzo ya vijana wa CHADEMA.

Kama kweli ‘vikosi’ vya ulinzi ni tishio kwa nchi, CCM ndiyo ilipaswa kuwa ya kwanza kuacha kuwapatia vijana wake wa Green Guard mafunzo kwenye makambi ya siri, yanayohusisha matumizi ya silaha huku kikituhumiwa kuwatumia watumishi wa serikali katika kutoa mafunzo hayo.

Chama hiki kilipaswa kuwa cha kwanza kuacha kuwafundisha kwa siri vijana wake mafunzo ya namna ya kuteka, kutesa na hata kuua, kisha kinawatuma kwenda kufanya utekelezaji kwa vitendo dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vya upinzani, kipekee wakikilenga CHADEMA au baadhi ya watu wanaotimiza wajibu kwa jamii kama waandishi wa habari.

Green Guard ni kikosi pekee cha ulinzi kinachotokana na chama cha siasa ambacho kimekuwa kikifanya matukio ya kushambulia, kuteka na kutesa wakati mwingine mbele ya Askari wa Jeshi la Polisi. Kimefanya hivyo mara nyingi hususan wakati wa uchaguzi. Ushahidi wa matukio upo. Hakuna hatua yoyote imewahi kuchukuliwa.

Tunaweza kutaja mifano michache kwa sasa. Mwaka 2012 wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kirumba ni vijana hao wakiwa na kila aina ya silaha waliwateka na kuwashambulia kwa nia ya kuwaua wabunge Salvatory Machemli na Highness Kiwia. Wakawakata mapanga na shoka mbele ya askari polisi wenye silaha.

Wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kalenga, mwaka jana; ni kikosi hiki kilichomteka na kumtesa Mbunge Rose Kamili na kumtia ulemavu wa maisha. Kitendo kilichofanyika mbele ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msabatavangu. Kama hiyo haitoshi wakawateka na kuwapeleka msitu wa Nduli vijana wawili wa CHADEMA kwa nia ya kwenda kuwachoma moto. Ni miujiza ya Mungu tu iliwaponya vijana wale kutoka mikononi mwa Green Guard waliokuwa na silaha na zana za kutekeleza mauaji.

Kikosi hiki cha CCM kimewahi kuteka, kupiga na kujeruhi waandishi wa habari wakiwa kazini. Baadhi ya waathirika wa matukio hayo ni mwandishi wa habari Frederick Katulanda, Munir Zacharia na Musa Mkama.

Mfano wa hivi karibuni ni matukio yaliyofanyika wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambapo siku mbili kabla baada ya Nape Nnauye kukaririwa kwenye Gazeti la Mtanzania akizungumza kwenye mkutano wa hadhara kuwa chama chake kimejipanga kuwaagiza vijana wa Green Guard kupiga watu, kweli siku ya uchaguzi vijana wale wakafanya kazi hiyo hiyo. Matukio ya uchaguzi ule kuvurugwa yalichangiwa pia na vitendo vya vijana wa Green Guard kwa maelekezo na baraka za chama hicho.

Matendo ya kikosi cha Green Guard yanajulikana kwa wakubwa wa chama hicho na serikali yake. Hakuna hatua imechukuliwa. Kimekuwa kikifanya ‘shows’ za kijeshi mchana kweupe kikiwa na silaha huku Mwenyekiti wa CCM Taifa akipita kukagua. Kama mchana wanaweza kuonesha mifano ya matumizi ya silaha, huko kwenye kambi za siri wanafundishwa kufanyaje?

Watanzania wameshaichoka CCM. Chama hicho kinajua hilo. Kinatambua hakina tena uhalali wa kisiasa wala ushawishi wa hoja. Hakina tena majibu kwa maswali na hoja za Watanzania. Tunatoa raia kwa Watanzania kuzisikiliza na kuzipuuza propaganda za akina Kinana na Nape juu ya uvunjifu wa amani katika nchi hii.

Amani ya Tanzania imewekwa rehani na mafisadi wanaominya haki na matumaini ya wanyonge. Kila mmoja anajua wanaotishia utulivu wa nchi hii ni walioko madarakani leo ambao wameshindwa kuongoza lakini wanataka kutumia hila na nguvu za dola kutawala.

Watanzania waendelee kujipanga kuonesha nguvu ya umma hasa kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ajili ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, ambayo itakuwa njia rahisi ya kuachana na madhira ya CCM.

Imetolewa leo March 6, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano- CHADEMA

No comments:

Post a Comment