Tuesday, February 24, 2015

YANAYOJIRI NJOMBE - BVR



CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO -CHADEMA

YANAYOJIRI NJOMBE - BVR

1. Ikiwa zoezi la uandikishaji limeanza leo tarehe 23 Feb na likitarajiwa kuzinduliwa rasmi kesho tarehe 24 Feb na Waziri Mkuu Pinda, Naibu Katibu wa CHADEMA upande wa Tanganyika ameanza Operesheni R2R BVR ambapo asubuhi mpaka mchana alikuwa katika Mji wa Makambako akipitia mitaani pamoja na msafara wa viongozi wa chama hicho ngazi mbalimbali kuhamasisha wananchi kujiandikisha.

Aidha, Operesheni hiyo imehusisha kukagua utaratibu wa uboreshaji kwa kutumia BVR kwenye vituo mbalimbali ambapo imebainika kwamba udhaifu uliokuwepo wakati wa majaribio na mwingine mpya umebainika katika sehemu kubwa ya vituo vilivyotembelewa.

Baada ya kubaini udhaifu huo Mnyika na timu ya maafisa wa CHADEMA iliyoweka kambi katika mkoa wa Njombe ikihusisha wataalamu wa TEHAMA (ICT) wamekutana na Mkurugenzi wa NEC Mallaba na kueleza kuhusu udhaifu huo.

Mfano katika kituo cha Malombwe mpaka saa 6 mchana mashine zilikuwa hazifanyi kazi. Hali kama hiyo imejitokeza katika kituo kituo cha Liamkena ambapo uandikishaji ni taratibu kwa kiwango mpaka saa 4 waliandikishwa watu watano tu.

2. Aidha, pamekuwepo na tatizo la watu wenye mikono yenye vidole sugu kutokana na kufanya kazi ngumu mashine kugoma kuwatambua na hivyo kukataliwa kujiandikisha.

Hali kama hiyo imejitokeza mfano katika kituo cha Sigfrid, Malombwe na vituo mbalimbali. Kufuatia hali hiyo ambapo Operesheni R2R BVR iliamua kutembelea vituo zaidi na kubaini kwamba vipo ambapo mashine hazikuwa zikifanya kazi kabisa mathalani Lumumba.

Kwa ujumla katika vituo vingi ukiondoa matatizo ya mashine upo pia udhaifu wa waandikishaji na waendeshaji wa vifaa vya BVR (Kit Operators) ambao wanashindwa kutumia mashine hizo na walipohojiwa baadhi walikiri kwamba wamepewa mafunzo siku moja kabla ya kuanza uandikishaji huku wakiwa hawajawahi kutumia kompyuta wala kuwa na ujuzi wa ICT.

Wapo waandikishaji ambao walionyesha kutokuwa na ufahamu wa upigaji picha na hivyo kufanya zoezi kwenda taratibu na pia kupiga picha zinazoonekana vibaya.

Kasi ndogo ya uandikishaji huku siku zikiwa saba na kwa kituo inaashiria bayana kwamba wapo wananchi ambapo mwishowe watakosa fursa ya kujiandikisha.

Operesheni R2R BVR imebaini mpaka sasa kuwa pamoja na kutumia alama za vidole mfumo umeacha mianya mpiga kura kujiandikisha zaidi ya mara moja katika vituo tofauti tofauti kwa kuwa hakuna mawasiliano ya kimfumo kati ya kituo kimoja na kingine.

Mfumo unategemea kwamba taarifa zikitumwa kanzidata kuu (central databank) ya tume ndiyo itakayochambua wakati ambapo hakutakuwa na mawakala katika hatua hiyo kuthibitisha uondoaji wa wapiga kura waliojiandikisha zaidi ya mara moja kwa kuzingatia kwamba katika kipindi cha uhakiki wa daftari la awali napo hakuna mwingiliano baina ya daftari la eneo kwa eneo wakati wa ukaguzi.

Aidha, CHADEMA imeweka mawakala katika vituo vyote lakini wanapata vikwazo vya namna vya kudhibiti uchakachuaji katika hatua ya usafirishaji wa takwimu ambapo mifumo miwili inatumika kwa wakati mmoja; wa kutumia simu na ule wa kuhamisha kwa kutumia kifaa cha kuhifadhi taarifa (flash drive) bila uhakiki wa mawakala.

Operesheni R2R BVR katika mazingira hayo haitaishia tu kuwa na mawakala kwenye vituo bali kukagua mfumo mzima.

4. Naibu Katibu Mkuu Mnyika ametaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika uzinduzi wa BVR Makambako tarehe 24 Feb aeleze namna Serikali ilivyoiwezesha tume kushughulikia udhaifu huo kwa kuzingatia kwamba mabilioni yametumika kwenye zabuni ambayo imeleta vifaa vibofu hali inahitaji uchunguzi kufanyika kubaini iwapo hali hiyo imetokana na ufisadi au imefanywa makusudi kuachia mianya ya uchakachuaji katika uchaguzi.

Mara baada ufuatiliaji huo jioni ya leo patafanyika Mkutano wa uzinduzi wa Operesheni R2R BVR jukwaani katika Jimbo la Njombe Kusini na kesho kutwa tarehe 25 Operesheni R2R inahamia wilaya ya Wang'ing'ombe kwenda kuhamasisha wananchi kujiandaa kujiandikisha.

Tumaini Makene


Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano -CHADEMA

No comments:

Post a Comment