Friday, February 27, 2015

Ukawa wawasha moto BVR.

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umesema hauna imani na uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa Biometric Voters Registration (BVR), kutokana na kugubikwa na kasoro nyingi katika siku za mwanzo za uandikishaji huo unaoendelea mjini Makambako, mkoani Njombe.

Pia umesema serikali haina sababu ya kuwekeza fedha na muda kwenye kupiga kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa, kwani uandikishaji wa wapigakura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu unasuasua.

Badala yake, umeishauri serikali kutumia fedha hizo kutoa elimu na kuhamasisha Watanzania kujiandikisha kwenye daftari hilo.

Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Prof. Ibrahim Lipumba, alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) inadanganya umma kuwa uandikishaji unaendelea vyema, wakati changamoto zilizojitokeza ni nyingi.

Alitaja kasoro zilizojitokeza kuwa ni alama za vidole sugu kutokusomeka kwenye mashine za BVR, mashine kubagua baadhi ya rangi za nguo na wafanyakazi kuchelewesha kazi hiyo kutokana na kukosa uelewa wa matumizi sahihi wa mashine hizo.

“Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), chini ya Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu, Damian Lubuva, waache kutudang’anya Watanzania kwamba zoezi linaenda vizuri na kutuaminisha kuwa litakamilika ifikapo Aprili 16, wakati kuna changamoto lukuki, ikiwamo kubwa ya ukosefu wa fedha,” alisema Prof. Lipumba.

Aliitaka Nec kuweka hadharani ripoti ya mshauri mwelekezi, Darall, kwa ajili ya Watanzania kuisoma na kujua mfumo mzima unavyoweza kufanya kazi.

“Licha ya mshauri mwelekezi kuitahadharisha tume kutotumia mfumo wa BVR kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwamo kukosa fedha za kuendeshea, uhaba wa wataalamu, pia mashine kukosa uwezo wa kutunza siri, kwani unaweza kuingiliwa wakati wowote, alishauri wadau washirikishwe kwenye kila hatua,” alisema Prof. Lipumba.

“Chakushangaza wanasiasa tunahamasisha watu wajitokeze, lakini hakuna ratiba yoyote inayoelezea maeneo mengine wataanza lini kujiandikisha.”

Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, alisema ni makubaliano ya viongozi wote wa umoja huo kuwa uandikishaji wa wananchi kwenye daftari hilo hauendi vizuri.

Alisema hakuna haja ya Rais Jakaya Kikwete kutaka kukamilisha kazi ya upigaji kura ya maoni kwenye daftari hilo wakati Watanzania hawajaandikishwa na wala serikali haina uwezo wa kumaliza kazi hiyo kwa wakati na kwamba, haina fedha za kuendeshea.

“Kwa mujibu wa watafiti wetu walioko huko Makambako, jumla ya mashine 82 tu ndizo zinafanya kazi kati ya mashine 250, ambazo tume inazo kati ya mashine 8,000 zinazotakiwa nchini. Na taarifa za ndani zimebaini kuwa mashine nyingine 68 zimepelekwa mikoa mingine kutoa elimu ya matumizi,” alisema Mbowe.

Alisema kulazimisha kura ya maoni wakati uandikishaji unakwama kutokana na sababu mbalimbali, ni wazi kuwa serikali inaandaa hatari ya taifa kuingia kwenye machafuko.

“Nec haitaki kukubali kasoro. Watanzania wamejiandaa kujiandikisha. Nec haitoi ratiba. Hapo hapo serikali inaharakisha kazi ya kuandikisha imalizike haraka ili waingie kwenye kura ya maoni. Hili hatutalikubali. Fedha za kura ya maoni zitumike kutoa elimu ya watu kujiandikisha kwa wingi,” alisema Mbowe.

Alisema matatizo yaliyojitokeza kwenye uandikishaji huo ni wazi kuwa umaliziaji hautakamilika kwa wakati na kwamba, pia utachelewesha kuanza kwa kura ya maoni, hivyo ni vyema ikasitishwa ili rais ajaye amalizie kazi hiyo.

Mbali na Prof. Lipumba na Mbowe, wengine waliohudhuria mkutano huo ni Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Mosena Nyambabe na Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk. Emmanuel Makaidi.

No comments:

Post a Comment