Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeamua kutumia mabaraza yake kufanya mashambulizi ya kisiasa kujiimarisha miongoni mwa makundi maalum katika jamii.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka ndani ya chama hicho, chama hicho sasa kitayatumia mabaraza yake ya Vijana (Bavicha), Wanawake (Bawacha) na (Bazecha) kama mkakati wa kulenga makundi mahsusi ya wapiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Habari hizo zilisema kuwa chama hicho kiliyaagiza mabaraza hayo tangu mwaka jana kuhakikisha yanahamasisha makundi maalum katika jamii na kuwa mstari wa mbele kwenye mapambano ya kisiasa ya chama hicho.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene, alipoulizwa juu ya taarifa hizo, hakukubali ama kukanusha.
Makene alisema anachofahamu viongozi wakuu wa chama hicho wametawanyika sehemu mbalimbali nchini kwenye shughuli za kukijenga chama.
“Kama unavyojua, hatujawahi kupumzika tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, tumekuwa tukibadili gia na kuongeza umakini kadiri ya matakwa ya safari ya kisiasa ambayo inazidi kushuhudia Chadema na upinzani kwa ujumla ikizidi kuungwa mkono huku Chama Cha Mapinduzi (CCM), nacho kikijaribu kupambana na sisi kwa kutafuta mlango wa kutokea,” alisema Makene na kuongeza:
“Lengo la viongozi hao wakuu kutawanyika nchi nzima ni maandalizi mahususi kwa ajili kuwapatia fursa viongozi hao kushughulika na masuala makubwa ya kukiandaa chama ili kishinde na kushika dola kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.” Makene alisema mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alikuwa Shinyanga kufunga mafunzo ya uzalendo na ukakamavu kwa vijana na kufanya mkutano wa hadhara Solwa pamoja na kuendesha vikao vya kuimarisha mikoa ya Kanda ya Ziwa Mashariki.
No comments:
Post a Comment