Wednesday, January 21, 2015

Wananchi wakodi wakili kuapisha mwenyekiti

Baada ya subira ya wiki mbili ili wenyeviti na wajumbe Mtaa wa Migombani - Segerea, Dar es Salaam waapishwe na mamlaka husika bila mafanikio, wananchi wameamua kuwaapisha viongozi hao kwa kutumia wakili binafsi.
Wakati hali hiyo ikitokea Dar es Salaam, wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro baadhi ya wenyeviti wa vijiji walioshindwa wamekataa kuwaachia ofisi viongozi wapya wakidai kuwa ofisi hizo ni mali ya CCM.
Katika tukio la Segerea lilitokea jana asubuhi Segerea Mwisho, Japhet Kembo aliapishwa kuwa ‘mwenyekiti’ pamoja na ‘wajumbe’ watatu ambao ni Rose Bernard Mhagama, Nyangeto Justin na Ramadhan Seif wote wa Chadema bila kuishirikisha Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Kembo alisema wananchi wamechoshwa na danadana wanazopigwa na Manispaa ya Ilala za kutowaapisha viongozi waliowachagua.
“Wananchi wamemtafuta wakili ambaye amekuja kusimamia suala hili kisheria na ndiyo maana zoezi limefanywa hadharani,” alisema Kembo.
Mmoja wa wananchi, John Kandeo alisema: “Uchaguzi wetu haukuwa na matatizo na ni miongoni mwa mitaa iliyotangaza matokeo muda mfupi baada ya uchaguzi,” alisema.
Kembo alisema katika nafasi ya uenyekiti alipata kura 547, Uyeka Idd wa CCM kura 273 na Erick Mchata wa NCCR-Mageuzi kura 205.

Ilivyokuwa
Ilipofika saa tano asubuhi, wakili wa kujitegemea kutoka kampuni ya mawakili ya Ame & Company, Idd Msawanga aliwasili katika ofisi za mtaa huo na kupokewa kwa shangwe na wafuasi wa Chadema wakiimba ‘Peoples… Power.’
Wakili Msawanga alianza kwa kumwapisha ‘mwenyekiti’, peke yake na baadaye ‘wajumbe’ watatu kwa pamoja na kuelezwa kuwa wajumbe wawili hawakuwapo kutokana na matatizo ya kifamilia.
“Sheria ya uchaguzi inaruhusu kufanya hivi na hata hao wajumbe wawili ambao hawapo kwa leo watakaporudi nitawaapisha, ni suala la kutaarifiana tu,” alisema Msawanga.
Alipoulizwa ni kwa namna gani amejiridhisha juu ya utata wa matokeo ambao uongozi wa manispaa unasema unashughulikia, wakili huyo alisema licha ya kupewa matokeo na wateja wake pia alipata taarifa sahihi kutoka kwa mwenyekiti wa jimbo, aliyemtaja kwa jina la Gango Fillemon Kidera kabla hajatekeleza majukumu yake ya kitaaluma.
Wajumbe ambao hawakuapishwa jana ni Angelo Machunda na Paulina Mbalale.
Tukio hilo lilishuhudiwa pia na mwenyekiti aliyepita kutoka CCM, Samwel Binaji aliyetumia nafasi hiyo kumpongeza Kembo kwa kupokea kijiti cha uongozi wa mtaa huo.
“Namtakia kazi njema. Huyu ni kijana wetu hapa mtaani ambaye wananchi wameona anafaa kuwatumikia na ndiyo maana unaona wamempa ushirikiano huu unaouona tangu harakati za uchaguzi zilipoanza mpaka leo,” alisema Binaji.
Wakati anaingia katika eneo la ofisi hiyo, Binaji alipokewa na vijana waliokuwa wakimshangilia.


Manispaa yapinga
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilala (DED), Isaya Mngurumi alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema kilichofanyika siyo sahihi huku akihoji: “Kama kila mtu angetumia wakili binafsi ingekuwaje, nadhani hilo ni suala lisilowezekana.”
Akizungumzia utata wa matokeo ya uchaguzi wa mtaa huo, Mngurumi alisema uchaguzi huo wa Desemba 14 haukuwa na dosari yoyote lakini kuna pingamizi limewekwa na CCM, jambo linalochelewesha uapishaji wa viongozi hao.
“CCM wameweka pingamizi ya matokeo, hivyo ofisi yangu inafanya uchunguzi ili kujiridhisha na ndani ya wiki hii itatoa majibu yaliyo sahihi.
Mwanasheria wa Manispaa hiyo, Mashauri Musimu alisema uongozi ulioapishwa ni batili na hauwezi kupata ushirikiano kutoka kwa mamlaka husika.
“Mwenye mamlaka ya kuapisha ni msimamizi uchaguzi kwa hiyo kama wao wameamua kufanya hivyo wamekosea. Manispaa inafanya uchunguzi na muda wowote itakapojiridhisha, itawaapisha wanaostahili,” alisema.

Rombo wagoma
Wilayani Rombo, baadhi ya wenyeviti wa vijiji walioshindwa wamekataa kukabidhi ofisi kwa viongozi wa upinzani waliochaguliwa kwa madai kuwa ofisi hizo ni mali ya CCM.
Mkanganyiko huo wa ofisi umejitokeza katika maeneo ambayo yalikuwa ngome ya CCM lakini katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba mwaka jana vijiji hivyo vilichukuliwa na Chadema.
Katika uchaguzi huo Chadema ilipata jumla ya vijiji 38 na CCM 30 kati ya 68.
Vijiji ambavyo viongozi CCM wamekataa kukabidhi ofisi ni Maharo, Makiidi, Machame Alleni na Shimbi.
Baadhi ya wenyeviti waliozuiwa kuingia ofisini, Priscus Mlingi wa Kijiji cha Maharo na Maangaisho Odemari wa Kijiji cha Machame Alleni wamedai kuwa baada ya kuchaguliwa walitangaziwa siku ya kukabidhiwa ofisi lakini siku hiyo ilipowadia viongozi waliomaliza muda wao waligoma kufanya hivyo.
“Serikali ilishatangaza siku nyingi kwamba ofisi za vyama zisitumike kwenye shughuli za kiserikali, inakuwaje hawa baada ya kuona sisi tumeshinda ndiyo wanaibuka na kusema ofisi ni mali ya chama?” alisema Mlingi.
Wenyeviti hao walidai kuwa kutokana na kukosa ofisi na mihuri ya kijiji, wamelazimika kutengeneza mihuri mingine na kufanya kazi barabarani ili kuwasaidia wananchi wenye matatizo.
“Wiki iliyopita waliitisha kikao cha makabidhiano lakini nilishangazwa na mwenyekiti wa zamani kusema kuwa hawezi kukabidhi ofisi kwa Chadema, nashindwa kuelewa kwa sababu nina imani mimi nimekuwa mwenyekiti wa wananchi na wenzetu wanapaswa kulitambua hilo,” alisema Odemari
Viongozi hao walisema wameyapeleka malalamiko yao kwa Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Rombo na iwapo hatayatafutia ufumbuzi, watawaongoza wananchi kwenda kwenye ofisi ya mkurugenzi kudai ofisi kwa kuwa kinachofanyika ni hujuma.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Makiidi, Elisonguo Massawe na Elimnata Mrosso waliitaka Serikali kumaliza tofauti hizo ili wananchi wapate huduma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rombo, Mohamed Maje pamoja na kukiri kuwapo kwa tatizo hilo, alisema wilaya hiyo ina upungufu wa ofisi na kwamba baadhi ya vijiji vilikuwa vimepanga katika nyumba za watu binafsi ambao sasa wamekataa kutoa ofisi hizo.
“Ni kweli kuna tatizo la ofisi ziko na sasa tumeanza mchakato wa kupata maeneo mapya ili
Serikali ndiyo ilipie kodi,” alisema Maje.TUJIKUMBUSHE
Wakazi wa Mtaa wa Migombani wakimzonga Afisa Mtendaji wa Kata ya Segerea ambae amekuja kutangaza kurudia uchaguzi wa Nafasi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Migombani leo ambao ulifanyika tarehe 14 Disemba 2014 ambapo mgombea wa Nafasi ya Mwenyekiti Japhet Kembo Kutoka Chadema aliibuka Mshindi kwa Kura 547. Wakazi hao wamegoma kurudia uchaguzi huo kutokana na kile ambacho Afisa Mtendaji huyo alitangaza katika uchaguzi wa Mtaa huo uliofanyika tarehe 14 Disemba 2014 kuwa Uchaguzi ni Halali na Matokeo pia yatakuwa halali.

MGOMBEA CHADEMA ASHINDA UENYEKITI MTAA WA MIGOMBANI SEGEREA DAR ES SALAAM


Mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Migombani Kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema) Bw. Japhet Kembo akifurahia huku akipongezwa na wanachama na wapenzi wa Chadema mara baada ya kuibuka mshindi wa Kiti cha Mwenyekiti kwa Kupata Kura 547 huku CCM wakiwa wamepata kura 273 na NCCR kupata kura 205

No comments:

Post a Comment