Wednesday, September 3, 2014

Vigogo Chadema wamkwepa Ndesamburo

Homa ya uchaguzi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imewatikisa baadhi ya vigogo wake mkoani Kilimanjaro baada ya mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, kusisitiza hana mpango wa kupimana nguvu na mdhamini wa chama hicho taifa, Philemon Ndesamburo, anayewania nafasi ya uenyekiti wa mkoa huo.
Ndesamburo, ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Mjini, alichukua fomu juzi baada ya kurejea nchini Jumapili akitokea Uingereza alikokwenda kwa ajili ya mapumziko.
“Wako watu wanatumia mbinu chafu kunichonganisha na Ndesamburo kwamba, nimechukua fomu ya kugombea uenyekiti wa mkoa. Mimi sina mpango wa kupimana nguvu na yeye…nimejipanga kutetea ubunge wangu na kuongeza nguvu zaidi ya kutwaa madiwani wapya, ambao watawezesha Rombo kuwa Halmashauri inayoongozwa na Chadema,” alisema Selasini.
Awali, kulikuwapo na taarifa kwamba, Selasini alikuwa na mkakati wa kutaka kumrithi Ndesamburo aliyeitumikia Chadema kwa miaka 20 sasa na amekuwa mbunge wa jimbo hilo tangu mwaka 1995.
Juzi baada ya kurejea nchini, Ndesamburo alisema atafanya uamuzi mgumu wa kuendelea kulitumikia jimbo hilo au la ifikapo mwaka 2015.
“Siwezi kukataa wito wa wananchi walionitaka niendelee kutetea uenyekiti wa mkoa, cha msingi hapa ni kukiimarisha chama na kutumia uzoefu wangu katika siasa kufanya mabadiliko makubwa ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu mwakani,” alisema Ndesamburo.
Uchaguzi wa viongozi wa Chadema ngazi ya mkoa wa Kilimanjaro, unatarajiwa kufanyika Septemba 3, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment