Wanachama wawili zaidi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamejitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti wa taifa wa chama hicho inayotetewa na mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda, Benson Kigaila, aliwataja wanachama hao kuwa ni Daniel Ruvanga na Garambenela Frank.
Kabla ya kufungwa kwa zoezi la kuchukua na kurejesha fomu katika siku ya mwisho jana, mwanachama pekee aliyekuwa amechukua fomu kuchuana na Mbowe alikuwa ni mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Tabora, Kanza Mbarouk.
Wakati akitangaza kutetea nafasi yake Alhamisi baada ya kuchukuliwa fomu na wazee wa chama hicho kutoka mikoa mbalimbali ikiwamo ya Kigoma, Rukwa na Njombe, Mbowe aliwahamasisha wanachama wenzake wa Chadema kwa kuwaambia kuwa wajitokeze kuchuana naye katika kuwania nafasi hiyo.
"Nimefanya kazi yangu kwa kujiamini sana, bila ya usalama wala ulinzi wa yeyote bali ulinzi wa Mungu, nawaheshimu wote wakubwa kwa wadogo, ila katu simuogopi yeyote na ndiyo maana nimekifikisha chama hapa," alisema Mbowe baada ya kupokea fomu ya kutetea nafasi yake aliyokabidhiwa jijini Dar es Salaam na mmoja wa wazee hao, Yassin Mzinga kutoka Kigoma.
Kigaila hakueleza kwa kina wasifu wa Ruvanga na Frank ambao walijitokeza katika siku ya mwisho jana kuchuana na mwenyekiti wao Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai na Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Kigaila alisema kabla ya zoezi la kurejesha fomu kufungwa katika siku ya mwisho jana, tayari wanachama 284 walikuwa wamesharejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.
Alisema katika nafasi nane za ujumbe wa Kamati Kuu, wanachama 58 walikuwa wameshajitokeza, miongoni mwao wakiwa ni Profesa Mwesiga Baregu, Mabere Marando, Chiku Abwao, Ansbert Ngurumo, Fredy Mpendazoe, Suzan Kiwanga na Mathayo Torongey.
Alisema kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, walioomba ni Profesa Abdallah Safari, Mussa Mabao, Martha Noah, Humprey Sambo, Winston Kulinda, Fredy Mpendazoe na Yeremiah Maganja.
Kigaila aliwataja walioomba kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar kuwa ni Said Mohamed Issa, Hamad Mussa Yusuf na Zainabu Mussa.
Alisema wanachama walioomba kugombea nafasi za makundi ya Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) ni 98, Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) ni 81, kundi la wazee 42 na wenye umri kati ya miaka 36 hadi 49 ni 63.
Kigaila aliwatahadharisha wanachama watakaoteuliwa kugombea nafasi walizoomba kutojihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa kampeni. Uchaguzi Mkuu wa Chadema unatarajiwa kufanyika Septemba
No comments:
Post a Comment