Safu mpya ya Baraza la Wazee Taifa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imetangazwa ambayo Mwenyekiti wake ni mkazi wa Zanzibar, Hashim Juma Issa.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Uchaguzi wa chama hicho, Benson Kigaila, alisema nafasi ya Makamu Mwenyekiti katika baraza hilo ni Susan Lyimo na Katibu Mkuu ni Rodrick Lutembeka.
Nafasi ya Mwenyekiti wa baraza hilo la wazee, ilikuwa ikishikiliwa na Nyangaki Shulungashela, mkazi wa Shinyanga na nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilikuwa inashikiliwa na mkazi wa Kigoma, Erasto Shija.
Waliojitokeza kuwania nafasi ya mwenyekiti katika baraza hilo ni Arcado Ntagazwa, Issa, Jacob Koyi na Kayaga Kayaga. Awamu ya kwanza, Issa alipata kura 36 akifuatiwa na Ntagazwa aliyepata kura 23.
“Hata hivyo kwa mujibu wa Katiba ya chama chetu, ili mgombea atangazwe mshindi lazima apate asilimia zaidi ya 50 ya kura, hivyo katika nafasi hii, uchaguzi ulirudiwa kwa kuwashindanisha tena Ntagazwa na Issa, ambapo Issa aliibuka na ushindi wa kura 47 huku Ntagazwa akiambulia kura 22,” alisema Kigaila.
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Susan alipata kura 51 na kuwabwaga wa Clavery Ntigicha aliyepata kura tano, Omar Mkama 13 na Othman Haule kura tano.
Kwa upande wa Makamu mwenyekiti Zanzibar, Kigaila alisema Omar Masoud Omar aliibuka mshindi kwa kupata kura 42 na kumbwaga mpinzani wake, Bikwao Hamad Hamis aliyepata kura 32. Katibu Mkuu wa baraza, Lutembeka aliibuka mshindi kwa kura 69.
No comments:
Post a Comment