Sunday, September 7, 2014

Dk. Slaa: Rais ahusishe viongozi wa siasa mazungumzo na wazee

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemuomba Rais Jakaya Kikwete, anapopanga kuzungumza na wazee ahusishe na wa vyama vyote vya siasa badala ya kuongea na wa CCM pekee kwa kuwa wote wanamahitaji tofauti.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee wa Chadema ambao utachagua viongozi wapya.
Dk. Slaa alisema anashangaa Rais Kikwete anayesema anaongea na wazee wakati ni makada wa CCM.
“Kumbe nchi hii kuna wazee zaidi ya wale wa CCM ambao Kikwete amekuwa akizungumza nao, wazee wa nchi hii wanamahitaji yao ambayo yanahitaji kutatuliwa,” alisema na kuongeza:
“Laana itaendelea katika nchi hii ikiwa hawa wazee wataendelea kufa bila kupata haki zao wanazodai, wazee ni hazina mfano ni wale wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao wengine wamefariki hawajapata kile walichokuwa wakikidai,” alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa amemtaka Kikwete kuingilia kati suala la kuzuiliwa kwao kufungua matawi katika mikoa ya Mtwara na Lindi.
Alisema baada ya zuio hilo, Chadema ilipoenda kwa OCD, Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC), Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) na waziri kuhoji ni nani ametoa zuio hilo wote hawakuwa na majibu.
“Juzi tulipokutana na Kikwete Dodoma, tulimuuliza swali hilo naye ameshangaa.., hii ni nchi ya ajabu haipo duniani, tulimuomba Rais aliangalie na kuingilia kati kwa kuwa wana Mtwara na Lindi wanakoseshwa haki yao kikatiba,” alisema.
Pia aliwataka wazee kujiandaa kuhamasisha wenzao kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura huku akiutaka mkutano huo upitishe azimio la kuitaka Tume ya Uchaguzi (NEC) kutangaza ratiba ya uandikishaji wa wapiga kura kama ilivyoahidi itaanza mwezi huu.
Kadhalika, ameutaka mkutano huo kupitisha azimio la kulaani hatua ya wazee wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samuel Sitta na Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kushindwa kunusuru fedha za umma zinazoendelea kutumiwa na bunge hilo huku kukiwa hakuna muafaka wa kitaifa kwenye mchakato.
Kaimu Katibu wa baraza hilo, Erasto Gwota, alisema idadi ya wajumbe waliotakiwa kuwapo ilikuwa ni 101 lakini waliofika ni 85 hivyo akidi ya kufanikisha uchaguzi huo imetimia.

1 comment: