Saturday, August 9, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU WABUNGE WA CHADEMA KUONEKANA DODOMA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU WABUNGE WA CHADEMA KUONEKANA DODOMA

Kumekuwepo na madai yanayosambazwa kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari kuhusu baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuonekana mjini Dodoma au kujisajili kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini humo.

Chama kupitia Idara ya Habari kingependa kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo;

1. Uamuzi wa kuwataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na CHADEMA kushirikiana na wenzao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutoshiriki vikao vya bunge hilo ili kuepuka kunajisi mchakato wa Katiba Mpya, ulitokana na maazimio ya kikao cha Kamati Kuu iliyoketi Julai 18-19 na kuazimia kwamba;

Wajumbe wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA, kama sehemu ya UKAWA, watarudi kwenye vikao vya Bunge Maalum endapo tu mamlaka ya Bunge hilo yatafafanuliwa kuwa ni ya kuboresha, na sio kuibomoa au kuifuta, misingi mikuu (basic features) ya Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi na kuandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoteuliwa na Rais kwa ajili hiyo;

Wajumbe wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA, kama sehemu ya UKAWA, watarudi kwenye vikao vya Bunge Maalum endapo tu, na baada ya, ufafanuzi uliotajwa katika aya ya 2 utahusisha marekebisho ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, inayohusu mamlaka ya Bunge Maalum, pamoja na Kanuni husika za Bunge Maalum;

Wajumbe wote wa CHADEMA katika Bunge Maalum hawatashiriki katika kikao chochote cha Bunge Maalum au Kamati zake hadi hapo ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge Maalum uliotajwa katika aya za 2 na 3 utakapofanyika kwa mujibu wa maazimjo ya Kamati Kuu;

Hadi wakati huu, hakuna jambo hata moja kati ya hayo lililofanyika, huku mazungumzo yaliyotarajiwa kuokoa mchakato yakiwa yamevunjika, kwa sababu CCM na Serikali yake wameamua kudharau na kupuuza maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba badala yake kuweka maslahi ya chama hicho kwenye katiba.

2. Iwapo kuna mjumbe/wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na CHADEMA wameonekana wakijisajili kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma au watashiriki vikao vya bunge hilo au kamati zake, wataandikiwa barua ya kujieleza kisha chama kitachukua hatua kwa mujibu wa taratibu zake kupitia vikao.

3. Tunapenda pia kuwakumbusha wanachama wa CHADEMA na umma mkubwa wa Watanzania kuwa, mji wa Dodoma mbali ya kuwa Makao Makuu ya Nchi pia inapatikana Ofisi Kuu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba ambako hakujaridhiwa na Watanzania wengi, hakujazuia shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanyika ikiwemo kutoa huduma kwa watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wabunge. Suala hilo linakwenda sambamba na ukweli kwamba sehemu kubwa ya watumishi wa Bunge Maalum la Katiba ni wale wale ambao wanatakiwa kuwahudumia wabunge wa Bunge Maalum la Katiba.
Hivyo kuonekana kwa mbunge yeyote wa CHADEMA mjini Dodoma au kwenye viwanja au Ofisi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakuwezi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa mbunge husika amehudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba, kinyume na msimamo wa UKAWA.

Imetolewa leo Alhamis Agosti 7, 2014 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari- CHADEMA



No comments:

Post a Comment