Friday, June 27, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katika kutekeleza kazi ya mbunge ya kuisimamia Serikali itakumbukwa kwamba tarehe 12 Mei 2014 nilichukua hatua bungeni ya kutaka Serikali kutatua kwa dharura matatizo katika mtambo wa maji wa Ruvu Juu yenye kukosesha maji kwa wananchi wa Mkoa wa Dar Es Salaam na Pwani.
Nilitaka kwa mujibu wa Kanuni ya 49 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la mwaka 2013, Waziri wa Maji Prof Jumanne Maghembe atoe kauli bungeni juu ya matatizo ya maji katika maeneo yanayohudumiwa na mabomba kutoka katika mtambo kwa kuweka bayana iwapo kuna hujuma na kurejesha kwa haraka huduma kwa wananchi.
Kufuatia hatua hiyo hali ya upatikanaji wa maji iliongezeka katika maeneo machache ndani ya siku chache lakini kwa sasa katika maeneo mengi yanayohudumiwa na mabomba kutoka katika mtambo wa Ruvu Juu katika kata za Kwembe, Kibamba, Mbezi Lois, Msigani, Kimara, Saranga, Ubungo na Makuburi matatizo ya maji yamejirudia.
Katika kuendelea kutekeleza wajibu wa kibunge wa kuishauri na kuisimamia Serikali natoa mwito wa wazi kwa wenyeviti wa bodi za Wakurugenzi na Maafisa Watendaji Wakuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka  Dar Es Salaam (DAWASA) na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) ndani ya siku tatu kusimamia kazi ya dharura kuhusu matatizo ya mtambo wa maji wa Ruvu Juu yanayoendelea mpaka hivi sasa.
Aidha, ndani ya siku hizo tatu wajitokeze mbele ya vyombo vya habari kutoa maelezo kwa umma kueleza kwanini mpaka sasa huduma ya maji katika maeneo mengi katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar Es Salaam  kwa ujumla yanayohudumiwa na mabomba yanayotoka katika mtambo wa Ruvu Juu hayapati huduma ya maji inavyostahili na lini matatizo yaliyopo yatapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande mwingine, ndani ya muda huo huo wa siku tatu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ajitokeze mbele ya vyombo vya habari na kueleza umma matokeo ya uchunguzi uliopaswa kufanyika ndani ya mwezi mmoja kubaini kama matatizo ya mara kwa mara ya Mtambo wa maji wa Ruvu Juu yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji  au makosa mengine ya kibinadamu.
DAWASA, DAWASCO na Wizara ya Maji wasipojitokeza ndani ya siku tatu mbele ya vyombo vya habari kutoa maelezo kwa umma nitachukua hatua za kibunge nitakazoona zinafaa dhidi ya Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kwa kulidanganya Bunge kupitia kauli ya Serikali aliyotoa Bungeni mwezi Mei 2014.
Ikumbukwe kwamba tarehe 12 Mei 2014 ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu wa mbunge wa kuwawakilisha wananchi nilieleza Bunge kwamba matatizo katika mtambo wa Ruvu Juu yamekuwa yakijirudiarudia kwa nyakati mbalimbali kwa kipindi cha takribani miezi mitatu kati ya Januari mpaka Mei 2014 katika maeneo ambayo awali yalikuwa yakipata mgawo wa maji.
Nilichukua hatua hiyo kwa niaba ya wananchi  wanaohudumiwa na mtambo huo katika kata za Kwembe, Kibamba, Mbezi Lois, Msigani, Kimara, Saranga, Ubungo na Makuburi  kwenye Jimbo la Ubungo; na kata mbalimbali za majimbo ya Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini, Segerea nk.
Kufuatia hatua hiyo, Mwezi Mei 2014 Waziri wa Maji Prof. Maghembe alitoa kauli ya Serikali ya kueleza matatizo yanayoukabili mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu kwa ajili ya Jiji la Dar es salaam na maeneo ya DAWASA katika mkoa wa Pwani.
Katika kauli yake Waziri Maghembe alikiri kwamba kwa takribani siku 67 (kati ya tarehe 01.03.2014 na tarehe 06.05.2014) mtambo ulizalisha maji chini ya kiwango na kufikia kati ya lita milioni 8.2 na lita milioni 57.4 ikilinganishwa na lita milioni 82 kwa siku, ambazo ndio uwezo halisi wa mtambo huo.
Katika kauli yake bungeni, Waziri Maghembe aliorodhesha matatizo ya mtambo wa Ruvu Juu kuwa ni: Kuharibika kwa pampu mara kwa mara kunakosababishwa na uchakavu  unaosababishwa na umri kua mkubwa miaka (60), kukatika kwa Umeme mara kwa mara, maji kuwa na tope jingi sana (turbidity) wakati wa mvua na mafuriko hali inayopunguza uwezo wa pampu za kusukuma maji na husababisha kusagika kwa vifaa vya pampu na ugumu wa upatikanaji wa vipuri halisi (genuine parts).
Hata hivyo, Waziri Maghembe hakukiri wala kukanusha juu ya madai ya kuwepo kwa udhaifu, uzembe, ufisadi na hujuma katika mitambo ya vyanzo vya maji na mitandao ya mabomba ya maji.
Waziri Maghembe alieleza Bunge kwamba Wizara imechukua hatua za kutatua matatizo yaiyopo kwa kuchonga vipuri na vifaa vya pampu katika karakana zilizopo hapa nchini kwa kuwatumia wataalamu wa jeshi, kuagiza vipuri nje ya nchi na kutoa matangazo kwa wananchi kuhusu upungufu wa maji pale uzalishaji unapopungua/kusimama.
Waziri Maghembe alilieleza bunge kwamba baada ya hatua hizo uzalishaji wa Maji wa Mtambo wa Ruvu Juu unaendelea kurudi katika hali yake ya kawaida na kutoa mfano wa kwamba tarehe 17 Mei, 2014 uzalishaji wa maji ulikua lita milioni 80.3 kwa siku.
Aidha, Waziri Maghembe alitoa kauli Bungeni kwamba Wizara ya Maji imeunda Kamati Maalum ambayo imeanza kufanya tathmini ya kina juu ya chanzo cha matatizo ya mara kwa mara katika mtambo wa kusafisha maji wa Ruvu Juu.
Waziri Maghembe alieleza kwamba kamati hiyo itafanya uchunguzi kubaini kama matatizo hayo yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au makosa ya binadamu na kuahidi kwamba kamati itatoa taarifa yake katika kipindi cha mwezi mmoja.
Mwezi mmoja umepita tangu nilipohoji bungeni tarehe 12 Mei 2014, hivyo ni wakati muafaka kwa mamlaka zote zinazohusika kuweza kutoa mrejesho juu ya uchunguzi huo na hatua nyingine za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi kama nilivyozieleza katika hoja binafsi niliyoiwasilisha bungeni kwa niaba ya wananchi tarehe 4 Februari 2013.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
22 Juni 2014



No comments:

Post a Comment