Tuesday, June 17, 2014

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. JAMES FRANCIS MBATIA (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015


(Inatolewa Chini ya Kanuni ya 105(8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Mwaka 2013)

     I.        UTANGULIZI
1.   Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na siha  njema ya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili niweze kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
2.   Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, napenda kumshukuru kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe (Mb), kwa kuniteua mimi kuwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha pamoja na Mhe. Christina Lissu Mughwai (Mb) kuwa Naibu Waziri Kivuli katika Wizara hii.

Aidha, shukrani za dhati kwa Mhe. Christina Lissu Mughwai (Mb) Naibu Waziri Kivuli, waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri vivuli kutoka katika Kambi Rasmi ya Upinzani na viongozi wengine kutoka vyama vya siasa hususan CHADEMA, CUF na NCCR - Mageuzi kwa ushauri na maoni yao yaliyofanikisha kuandaa hotuba hii.

   II.        UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA MWAKA 2013/2014
Sera ya Mapato

3.   Mheshimiwa Spika, Serikali ilikusudia kukusanya mapato ya jumla ya shilingi trilioni 18.249 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje. Hadi tarehe 30 Aprili, 2014 Serikali imekusanya mapato halisi yenye jumla ya shilingi bilioni 12,882. Makusanyo hayo yanadhihirisha nakisi ya shilingi bilioni 5,475 ambayo ni asilimia 30 ya bajeti ya mwaka 2013/14. Kwa miezi 2 iliyobaki ni dhahiri Nakisi hii haitawezwa kufikiwa.  Huu ni uthibitisho wa kushindwa kwa serikali kusimamia vizuri makusanyo ya mapato kwa mujibu wa bajeti.

4.   Mheshimiwa Spika, serikali katika bajeti ya mwaka 2013/14 ilikusudia kutumia shilingi bilioni 5,645 kwenye matumizi ya maendeleo na shilingi bilioni 12,604 kwa ajili ya matumizi ya kawaida.  Hadi kufikia Aprili 2014, jumla ya shilingi bilioni 3,115 ziliidhinishwa na kutolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 5,645. Kiasi hiki ni sawa na wastani wa asilimia 55 tu ya bajeti. Hata hivyo, matumizi ya kawaida yaliidhinishwa jumla ya shilingi bilioni 13,034.7 sawa na asilimia 71 ya makadirio ya mwaka.

5.   Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizi zilizowasilishwa bungeni, kipaumbele cha serikali kinaonekana kuwekwa zaidi kwenye matumizi ya kawaida ya serikali kuliko matumizi ya maendeleo. Hali hii imekuwa ikijirudia mara kwa mara kwa serikali yetu kuweka kipaumbele kwenye matumizi ya kawaida na kushindwa kuweka kipaumbele kwenye miradi ya maendeleo.
Endelea.......



Mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Kuhusu Bajeti ya Mwaka 2013/2014

6.   Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitoa mapendekezo yafuatayo:
a)   Kwamba kufuatia shilingi bilioni 619.8  kuongezwa kwenye deni la taifa bila maelezo wala vielelezo vyovyote, Serikali ilitakiwa kutoa maelezo yaliyonyooka mbele ya Bunge hili Tukufu kuhusu sababu za matumizi hayo. Mpaka sasa, maelezo hayo hayajatolewa mbele ya Bunge lako tukufu. 
b)   Kwamba mfumo wa utoaji ripoti ya deni la Taifa mbele ya Bunge lako  Tukufu umekuwa wa kulundika masuala mengi kwenye kapu moja. Masuala hayo ni mkopo halisi, riba ya mkopo, kiasi kilicholipwa kwa mkopo huo, deni lililosalia kwenye mkopo husika pamoja na mikopo mipya iliyochukuliwa na serikali. Aidha ilitakiwa kubainisha mikopo ya ndani na ile ya nje ya nchi. Kubainisha kila jambo peke yake kwenye ripoti ya mapato na matumizi ndiyo njia pekee ya kudhibiti uwezekano wa kulipwa mkopo mmoja zaidi ya mara moja. Hata hivyo, bajeti haijaonesha kwa ufasaha kiasi cha riba kinachodaiwa na viwango vya riba katika mikopo mipya.
c)   Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alitakiwa kufanya ukaguzi maalum (special audit) katika kitengo cha Deni la Taifa (fungu 22) ili kujua mikopo inayochukuliwa kila wakati inatumika kufanyia nini, na miradi iliyotekelezwa kama ni miradi ya kipaumbele kwa mujibu wa bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Bado ukaguzi maalum haujafanyika hadi sasa.

d)   Serikali ilishauriwa kutenganisha deni halisi la Taifa na matumizi mengine yanayohusu Mfuko Mkuu wa Hazina (Consolidated Fund Services – Others) ili kuziba mianya ya ubadhirifu au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kisingizio cha Deni la Taifa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza Fungu namba 22 liwe la Deni la Taifa pekee na Fungu lingine litengenezwe kwa ajili ya Mfuko Mkuu wa Hazina (CFS). Mpaka sasa Serikali haijatoa taarifa rasmi ya utekelezaji wa mapendekezo hayo.

e)   Ilipendekezwa kiwango cha Kodi ya Mapato kwa Wafanyakazi (PAYE) kishuke kutoka asilimia 14 iliyokuwapo kufikia asilimia 9 na kuwa kodi hiyo itozwe kwa mtu anayepata mshahara unaozidi Sh 250,000 kwa mwezi. Pendekezo hilo lilifanyiwa kazi kwa kushusha kiwango hicho kufikia asilimia 12 kwa mujibu wa Bajeti ya mwaka 2014/15. Pendekezo la Kambi rasmi ya Upinzani halijatekelezwa kwa ukamilifu.  

f)    Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kwamba utaratibu wa vitambulisho vya Taifa uoanishwe na mfumo wa kutoa namba ya utambulisho kwa mlipa kodi (TIN Number) ili kila mwananchi awajibike kujaza fomu za taarifa za kodi  ‘tax returns’ bila kujali kipato chake. Suala hili lingewezesha kupanua wigo wa kodi kwa kuongeza idadi ya walipa kodi nchini na kupunguza mianya ya ukwepaji kodi. Pendekezo hili bado halijatekelezwa na serikali.


g)   Ilipendekezwa kwamba misamaha yote ya kodi iwekwe wazi na ikaguliwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Bajeti ya mwaka 2014/2015 imeridhia pendekezo hili na kuahidi kuwa misamaha ya kodi itawekwa wazi. Ni rai ya Kambi ya Upinzani Bungeni, serikali iwe inaweka bayana na kupongeza pale inapotekeleza kwa vitendo mawazo mazuri yanayotolewa na Upinzani kwa masilahi mapana ya Taifa letu.

h)   Ilipendekezwa na Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba ufanisi wa Bandari uimarishwe ili kuongeza mapato ya ndani kufikia kiasi cha shilingi trilioni 1.46 kwa mwaka.  Ufanisi wa bandari bado uko chini na Serikali bado haijatekeleza lengo hilo.

i)     Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kuwa Serikali iache kuchukua mikopo yenye masharti ya kibiashara. Badala yake vyanzo mbadala vya mapato vilipendekezwa ili kuondokana na adha ya madeni. Pendekezo hili halijazingatiwa kwa sababu bajeti ya mwaka 2014/2015 imeendelea kuonesha dira ya serikali kukopa fedha kwa viwango vya riba vya kibiashara.

j)     Ilipendekezwa kupunguza mzigo wa matumizi ya magari ya Serikali kwa kupiga mnada baadhi ya ‘mashangingi’ na kuweka mfumo wa kuwakopesha magari watumishi wote wa umma wanaostahili magari kama ilivyo kwa watumishi wa Benki Kuu ya Tanzania. Serikali iliahidi kwamba katika mwaka wa fedha 2014/15 ingeanza kutekeleza pendekezo hili. Hivyo ni matumaini ya Kambi Rasmi ya Upinzani kusikia “Commitment” ya Serikali kuhusu kuwakopesha watumishi wake magari. Kukosekana kwa sera rasmi inayoratibu ununuzi na matumizi ya magari ya umma unachangia udhaifu huu sambamba na kutokuwepo na dhamira ya kweli katika kubana matumizi yasiyo ya lazima ya viongozi wa kada ya juu katika Serikali

k)   Ilipendekezwa kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara (Mtwara University for Petroleum Studies) ili kutayarisha wataalam wa kutosha wa sekta ya Mafuta na Gesi na kuliandaa Taifa kuwa na wataalam katika maeneo hayo na hivyo Taifa kuweza kutumia utajiri wa Mafuta na Gesi uliopo nchini kwetu.

l)     Kuanzisha pensheni ya uzeeni kwa wazee wote nchini wenye umri wa zaidi ya miaka 60. Serikali ipo kimya kuhusu suala hili muhimu sana kwa wazee nchini
m) Ilipendekezwa kuifanyia marekebisho ya sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 kwa kufuta sehemu ya Kodi ya Mapato inayotoa fursa kwa kampuni za madini kutumia sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 1973 iliyofutwa (grandfathering). Pendekezo letu lilikuwa na lengo la kutaka kuweka mfumo wa ‘straightline method of depreciation’ ya asilimia 20 badala ya sasa ambapo kampuni za madini huruhusiwa kuondoa asilimia 100 ‘100 percent depreciation’ kwenye mitambo yao mwaka wa kwanza na hivyo kuchelewesha kulipa ‘Corporate Tax’. Pendekezo hili ambalo lingeipatia Serikali mapato mengi na kwa sasa bado halijatekelezwa kwa Kampuni za madini zenye mikataba.

n)   Kambi ya Upinzani vilevile ilipendekeza kushushwa kwa tozo ya kuendeleza stadi (Skills Development Levy – SDL) kutoka asilimia sita (6%) ya sasa mpaka asilimia nne (4%). Katika pendekezo hilo tulishauri kuwa waajiri wote walipe kodi hii ikiwemo Serikali na Mashirika ya Umma. Serikali ilichukua pendekezo hili kwenye mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2013/14 lakini bila kuhusisha mwajiri Mkuu, Serikali. Ni vema kodi hii ilipwe na waajiri wote nchini na ishuke kuwa asilimia 4.

DENI LA TAIFA
7.   Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa limeongezeka kwa kasi kubwa sana, hali ambayo inatishia ustawi wa taifa kama halitasimamiwa kwa umakini na haraka. Hotuba ya Waziri wa Fedha inaonesha kwamba hadi kufikia Machi 2014, Deni la Taifa lilifikia shilingi trilioni 30.563 ikilinganishwa na shilingi trilioni 23.674 la Machi 2013. Hili ni ongezeko la takribani trilioni 7 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 29 kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.

8.   Mheshimiwa Spika, hili ongezeko la mikopo ya takribani shilingi trilioni 7 kwa mwaka mmoja tu, halijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu. Ongezeko hili la takribani trilioni 7 ni sawa na bajeti nzima (full budget) ya mwaka 2008/9 ambayo ilikuwa ni shilingi trilioni 6.839. Ikumbukwe kuwa mwaka 2008/9 ni miaka mitano tu iliyopita.  Ukopaji wa namna hii unatishia uchumi  na usalama wa nchi.

9.   Mheshimiwa Spika,   kwa  mujibu wa ripoti za Benki Kuu na hotuba za bajeti za miaka iliyopita za Mawaziri wa Fedha, deni la Taifa limeongezeka kwa kasi kutoka shilingi trilioni 9.3 mwaka 2007/8 hadi shilingi trilioni 30.6 mwaka 2013/14. Hii ni wazi kuwa deni liliongezeka kwa kiasi cha shilingi trilioni 21.3. Serikali imelipa shilingi trilioni 4 na kufanya fedha zilizokopwa kuwa jumla ya shilingi trilioni 25.3 katika kipindi hicho cha miaka saba tu. Huu ni ukopaji hatarishi kwa uchumi wa taifa letu.

10.               Mheshimiwa Spika,  licha ya deni hili kuwa hatarishi kwa uchumi wa Taifa, Serikali bado inatajaria kuongeza deni hilo kwa kukopa shilingi trilioni 4.3 kama ilivyoainishwa katika bajeti ya mwaka 2014/15.

11.               Mheshimiwa Spika, Serikali imeonesha kushindwa kulipa deni hilo kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato, badala yake imekuwa ikikopa ili kulipa deni. Mfano hotuba ya bajeti ya mwaka 2014/15 imeonesha kuwa  katika shilingi trilioni 1.8 zilizokopwa katika soko la ndani, zaidi ya shilingi trilioni 1.1 zilitumika kulipa madeni ya hati fungani wakati shilingi trilioni 0.69 tu ziliwekwa kwenye miradi ya maendeleo.  Hiki ni kiashiria cha karibu sana kwa serikali kufilisika. Kukopa mikopo ya kibiashara yenye riba kubwa ili kulipa mikopo yenye riba ndogo au kwa uendeshaji wa kawaida wa serikali au taasisi zake ni kiashiria cha kutosha kuainisha maamuzi yasiyo na uelewa wa kawaida sana wa utawala na usimamizi wa fedha. (basic business and economic sense). Mikopo ya kibiashara hutafutwa kwa matumizi ya uwekezaji wenye lengo la uzalishaji.

12.               Mheshimiwa Spika, katika uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia kati 6.5 na 7 kwa mwaka, ni vigumu sana kuweza kulipa deni la Taifa linalokua kwa wastani wa asilimia kati ya 15 na 30 kwa mwaka. Bila kuwa na vyanzo vipya vya mapato  au kusamehewa deni hili itakuwa vigumu sana kuweza kulipa deni hilo kikamilifu. Hii ni kwa sababu uwiano wa ukuaji wa uchumi hauendani na kasi ya ukuaji wa deni hata kidogo. Pamoja na upungufu wote huu, Serikali imeendelea kujitapa kuwa inakopesheka, na hivyo kuashiria kutokuwepo na hofu yeyote ya kukopa huku holela.

13.               Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha zaidi ni kuwa sehemu kubwa  ya mikopo hii inakopwa katika soko la ndani. Hali hii imekuwa ikileta ushindani mkubwa kwa wananchi na wajasiriamali wanaotaka kukopa ili kukuza mitaji. Hali hii hufanya riba za mabenki kushindwa kushuka na hivyo kuwaathiri wakopaji na uchumi wa nchi kwa ujumla. Kwa maneno mengine, serikali imekuwa inazuia wajasiriamali wasikope kwa riba za bei nafuu, hivyo kufanya baadhi ya wanaokopa kwa riba zilizopo, ambazo ni kubwa kufilisiwa. Hali hii hurudisha biashara nyuma na inainyima serikali fursa ya kukuza uchumi na kukusanya mapato zaidi.

14.               Mheshimiwa Spika, mataifa mengi duniani yanakopa na yana madeni makubwa. Suala la msingi la kutofautisha nchi  moja na nyingine ni kasi ya kukua kwa deni husika na matumizi ya mkopo huo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inauliza na kutaka majibu kutoka kwa Serikali matumizi ya fedha zilizokopwa na nchi yetu ndani ya miaka 7 ni yapi na yameleta maendeleo kiasi gani kwa Taifa ( value for money).

15.               Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa bei za soko kuhusu Trekta ambazo serikali imeziidhinisha kuwa ziuzwe hapa nchini kwa ajili ya kilimo kupitia mradi wa Taifa wa Kilimo Kwanza, ni wastani wa shilingi milioni 30 kwa trekta moja lenye ubora wa hali ya juu. Endapo fedha zilizokopwa kwa miaka saba, shilingi Trilioni 25.3, zingetumika kuweka kipaumbele katika kilimo na kununua matrekta ya kisasa yenye ubora wa hali ya juu, ni dhahiri serikali ilikuwa na uwezo wa kununua matrekta 843,333. Kwa kuzingatia Kata tulizonazo hapa nchini (3000), Matrekta hayo yangeweza kugawiwa kwa kila kata kupata trekta 281. Hakika kama hili lingetendeka, Taifa letu lingekuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuzalisha chakula duniani.

16.               Mheshimiwa Spika, endapo fedha zilizokopwa kwa kipindi cha miaka saba zingetumiwa katika sekta ya elimu, kila mwanafunzi anayesoma kuanzia shule ya msingi hadi Chuo kikuu, angeweza kutengewa milioni mbili na laki tatu (sh. milioni 2.318) kwa ajili ya shule. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za sasa kuwa kuna jumla ya wanafunzi wanaokadiriwa asilimia 23 ya Watanzania wote, ambao ni  takriban wanafunzi 10,350,000 katika shule zote za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi, vyuo vya ualimu na vyuo vyote vya elimu ya juu hapa nchini. 

17.               Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa masikitiko makubwa tunauliza fedha hizi zilizokopwa na ambazo zitaendelea kukopwa na kuleta mzigo mkubwa kwa Watanzania zimefanya nini? Kumekuwa na ukosefu wa taarifa za wazi kuhusu mikopo kwa serikali yetu. Kuendelea kukosa taarifa hizi ni kubariki mianya ya ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma na kuendelea kubebesha watanzania mzigo wa kulipa bila kufahamu fedha hizo zimefanya kazi gani za maendeleo.

18.                Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwa Bunge lako tukufu litunge sheria ya bajeti haraka iwezekanavyo, pamoja na mambo mengine ili iweze  kudhibiti ukopaji na matumizi ya mikopo ya serikali. Vile vile tunapendekeza katika sheria hiyo iwe lazima kwa serikali kupata kibali kutoka katika Bunge lako tukufu kabla ya kuweza kukopa. Hii inafanyika katika nchi nyingi  duniani kama vile Marekani na Uingereza.

  III.        BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA 2014/2015
                                            Matarajio

19.               Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni   ilitarajia kuona kwenye bajeti hii ya mwaka 2014/15 yafuatayo:-

(i)           Sera ya mapato na matumizi ya serikali (fiscal policy) ambayo inalenga kukidhi mahitaji ya muda mfupi, wa kati  na yale ya muda mrefu,  na yenye mikakati  mahususi  ya kukuza uchumi wetu.
(ii)          Bajeti inayotoa kipaumbele kwa sekta ambazo ndio kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi, ajira na hatimaye kupunguza umaskini.  Sekta kama vile elimu, kilimo, nishati, miundominu na utalii .
(iii)        Bajeti inayoainisha bayana  mikakati madhubuti ya kuzuia matumizi ya anasa , ubadhrifu na  rushwa katika manunuzi ya umma .
(iv)        Mikakati maalumu ya kuongeza wigo wa walipa kodi (tax base) kutoka idadi ndogo iliyopo hivi sasa.
(v)         Bajeti ambayo inahimiza utekelezaji  kwa vitendo,  Mpango wa Maendeleo wa Taifa .
(vi)        Mikakati endelevu wa  kuratibu na kupunguza ukuaji wa sekta isiyo rasmi.


Sera za Mapato  mwaka  2014/15
       
20.               Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya mabadiliko katika sera kwa nia ya kuongeza vyanzo vya mapatao na kuondoa baadhi ya mikakati ya mwaka uliopita ikiwemo ile ambayo iliyoanza  kutumika mwaka wa fedha wa 2013/14. Kwa mfano:-

(i)           Kuongeza kiwango cha kutozwa kodi kwa wafanyabishara wadogo wadogo, ambao wengi ni wale wasio rasmi kutoka aslimia 1 hadi aslimia 2 ya mapato ghafi ya kati ya shilingi 4,000,000/= hadi 7,500,000/= kwa mwaka. Hatua hii ya serikali itasababisha wafanyabishara wadogo wadogo, kukwepa kulipa kodi na hivyo kudumaza  ukuaji wa biashara ndogo ndogo ambazo  ni  chanzo  kimojawapo cha uhakika cha  ajira nchini.

(ii)          Kufuta msamaha wa kodi ya zuio kwa ukodishaji wa ndege kwa walipa kodi wasio wakazi. Ni hoja ya  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba  misamaha ya kodi isiyo na tija ya ukuaji wa uchumi ifutwe, lakini utekelezaji wake lazima uangalie sekta na sekta.  Kufuta msamaha wa kodi ya zuio kwa wanaokodisha ndege kutaathiri sana sekta ya usafiri wa anga na utalii kwa pamoja.  Sekta hii bado  iko chini kibiashara, ikilinganishwa na baadhi ya nchi za wenzetu katika kanda ya Afrika Mashariki na Umoja wa Kiuchumi wa nchi za Kusini mwa Afrika – SADC; (Mfano,  Kenya,  Rwanda, Afrika Kusini nk).  Hakuna shirika la ndege hapa Tanzania lenye uwezo wa kununua ndege mpya za kisasa. Ndege zilizo nyingi ni za kukodisha.   Kuondoa msamaha huu itabidi nauli za ndege zipande na hivyo  kuathiri ukuaji wa sekta hii, wakati kwa upande mwingine serikali inaendelea kwa kasi kubwa ya kujenga viwanja vya ndege hapa nchini. Mfano mwezi uliopita, jirani zetu wa  Kenya wametangaza mikakati madhubuti ya kukuza utalii wa ndani na wa nje, ukiwemo wa kupunguza ushuru wa kutua uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta kwa asilimia 40.  Hii ni hatua kubwa ya ushindani katika sekta ya Utali, ukizingatia kwamba Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa vivutio vya utalii.

(iii)        Ushuru wa bidhaa wa asilimia 0.15 kwenye money transfer ulianza kutumika mwaka jana sasa umefutwa.  
(iv)        Mabadiliko ya sera ambayo hayazingatii ukuaji wa biashara. Kwa mfano, tangu tumepata uhuru kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, bajeti yetu imekuwa ikitegemea mapato ya Soda, Bia, Sigara na sasa Juisi na  Chibuku. Ni vema hatua hii ikaangaliwa kwa mapana yake kwani inaongeza athari kwenye afya za Watanzania, hasa wale wa kipato cha chini.
(v)         Kwa mara nyingine tena Serikali inadhamiria kutoza ada ya leseni.  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tumekuwa tukipendekeza  kwamba ada ya leseni itumike tu kwa ajili ya kutambua biashara na si kwa ajili ya kupata mapato. Tulipendekeza kodi hiyo ilipwe mara moja kila baada ya miaka mitano. Athari zake ni kufanya watu kuamua kufanya biashara bila leseni na kusababisha usumbufu kwa wananchi. Serikali haijatamka kama sheria ya Business Activities Registration Act (BARA) imefutwa au la.
(vi)        Badiliko linalopendekezwa na aya 102 ya kuhusu ulipaji wa kodi wakati wa kuingiza  mafuta (Upfront). Tunataka kujua kwa undani kusudio la hatua hii, kwani utaratibu uliopo sasa wa bulk procurement umekuwa ukisifiwa sana na serikali kwani umepunguza kwa kiasi kikubwa mianya ya rushwa na ufanisi wake ni mzuri. Kulikoni !
(vii)      Hakuna msisitizo wa dhati (affirmative action) wa kufufua viwanda vya nguo (textiles) na ngozi (leather) ambavyo vingelipewa unafuu wa kodi katika nyanja mbalimbali za uwezekezaji katika sekta hizi.
(viii)     Badiliko linalopendekezwa katika aya ya 95 kwamba (iii). ‘Taasisi za kidini kwa waajiriwa wake ambao ni mahsusi kwa kuendesha ibada tu’. Tunaomba ufafanuzi wa kina wa kusudio hili , kwani taasisi za kidini zilizo nyingi   zimekuwa zikifanya kazi nzuri ya kutoa huduma muhimu za kukuza Utu wa Binadamu katika nchi yetu.




21.               Mheshimiwa Spika, Inaonesha kwamba makadirio ya mapato ya mwaka unaoshia Juni 30, 2014 hayatafikiwa kwa kiasi cha asilmia 10. Inakadiriwa kiasi kitakachopatikana ni takriban Shilingi trilion 17  badala ya Shilingi trilioni 18.249.  Hivyo lengo la la mapato ya Shilingi trilioni 19.853 katika bajeti ya mwaka 2014/15  haliendani na hali halisi (unrealistic) na hivyo itasababisha  ukopaji zaidi ya ule uliowekwa kwenye bajeti. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inapendekeza mfumo wa ukadiriaji wa mapato ya serikali uwe wa uhalisi (realsitic) kuliko ilivyo sasa.


Sera za Matumizi ya Serikali

22.               Mheshimiwa Spika, ili bajeti iweze kutekelezwa kwa ufanisi ni lazima ionyeshe madeni yatakayoingia mwaka mpya wa fedha (kama yapo) na namna ambavyo madeni hayo yatalipwa.

Katika hotuba ya bajeti kwa mwaka 2014/15 serikali imelieleza Bunge lako Tukufu namna ambavyo sekta mbalimbali za maendeleo zitagawiwa fedha lakini hatujaelezwa juu ya madeni ya kila sekta yenye jumla ya takribani shilingi trilioni mbili ambayo hayakulipwa katika bajeti ya 2013/14 yatakavyolipwa.


23.               Mheshimiwa Spika, kutokuonesha madeni hayo katika bajeti kutaifanya bajeti hii mpya isitekelezeke kama zingine zilizotangulia kwani tunajua kuwa fedha zitakazokusanywa zitalipia kwanza madeni hayo. Tunaitaka Serikali itoe ufafanuzi wa jambo hili, kwamba madeni haya ni kiasi gani na namna ambavyo yatalipwa.

24.               Mheshimiwa Spika, matumizi ya magari ya anasa yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kubwa. Karibu viongozi wote wa ngazi za Wakurungezi,  Makamishna, Makatibu Wakuu, na Mawaziri wananunua na kutumia magari aina ya Toyota Landcruiser V8  (Mashangingi), licha ya kuwa thamani ya  kila gari moja la aina hiyo ni zaidi ya shilingi milioni 280, pia gharama ya kuyaendesha ni ya ghali sana.
 
25.               Mheshimiwa Spika, mikakati iliyotajwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika bajeti ya mwaka huu, kama vile Bulk procurement inaweza kusaidia. Hatua  kali zinatakiwa kuchukuliwa  kwa wale watumishi wa umma watakaobainika kufanya ubathirifu au kujihusisha na rushwa wakati wa kufanya manunuzi ya umma.  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kila mwaka hutoa taarifa za ubadhirifu lakini hakuna hatua zinazotangazwa kuchukuliwa na Serikali kuwawajibisha wahusika.  Tabia hii inawavunja moyo walipa kodi waaminifu.

BAJETI NA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA MIAKA MITANO.
26.       Mheshimiwa Spika, katika  Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano ambao sasa umefikia miaka minne ya utekelezaji wake,  malengo muhimu ya mpango huu  ni kukuza uchumi   wa nchi, ambao kama taifa tulijiwekea malengo ya kukua hadi kufikia asilimia nane   kwa mwaka (8% GDP growth per annum) ya pato la taifa. 
27.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha malengo ya mpango wa miaka mitano yaani mwaka  2011/2012 mpaka 2015/2016  Lengo ni kufikia asilimia kumi  (10%) ya pato la taifa  kwa kila mwaka, kuanzia mwaka  2016 mpaka mwaka 2025  - Dira ya Maendeleo ya Taifa (Vision 2025).  Ukisoma mipango ya serikali utaona upo uwezekano wa kufikia lengo,  lakini ukisoma utekelezaji wake ni tofauti na malengo ya mipango. 
28.       Mheshimiwa Spika, katika mpango wa maendeleo ya miaka mitano umeweka kikomo cha fedha za kibajeti kuelekezwa katika miradi ya maendeleo kwa asilimia 35. Utekelezaji wa bajeti kwa miaka takribani 4 sasa,  serikali imeshindwa kufikia lengo kwa kutenga fedha za maendeleo chini ya asilimia 30.  Pamoja na kutenga fedha kidogo katika maendeleo, pia serikali imeshindwa kugharimia bajeti ya matumizi ya kawaida.
29.       Mheshimiwa Spika, hali  hii imesababishwa  na kuwa na mipango ambayo haiendani na sera ya bajeti ya matumizi, ambayo itaweka msisitizo wa kupunguza matumizi ya kawaida kama ilivyoelezwa katika mpango wa miaka mitano katika ibara ya 4.5.1. Aidha, hakuna mkakati wa makusudi wa kufanya maboresho kutokana na makosa makubwa ambayo yameainishwa na Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kwa kipindi kirefu sasa.
30.       Mheshimiwa Spika, Tukiwa wazalendo wa nchi yetu, sote tunatakiwa  kujiuliza maswali kwa nini hatutafikia malengo? ni wazi majibu yatakuwa hatuna sera ya kuwezesha utekelezaji wa mpango, pili hatuna sera ya kupunguza matumizi yasio ya lazima. Aidha, mpaka sasa  hakuna utashi ulio bayana wa  serikali  kufanyia kazi maswali haya.
31.       Mheshimiwa Spika, ni jambo lililo dhahiri kwa viongozi walio wengi, hufanya matumizi ya anasa na kulipana posho kubwa, wakati wananchi  walio wengi hawapati  huduma muhimu? Tunatakiwa kujiuliza, je kwa mwenendo tunaokwenda nao malengo haya yatafikiwa? Swali hili ni la msingi tukizingatia kwamba Mpango huu wa miaka mitano ni sehemu ya Dira ya Taifa ya 2025, ambayo inalenga kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye kipato cha  uchumi wa kati (middle-income country). Dira ya Taifa ya 2025, inalenga kuiwezesha Tanzania kuwa na wastani wa kipato cha mwananchi (per capita income) cha Dola za Marekani 3,000 ifikapo 2025.
32.       Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  inaitaka Serikali iweke wazi ni hatua gani hadi sasa zimefikiwa katika; kwanza kutekeleza mpango wa miaka mitano, pili kutekeleza  Dira ya Taifa ya 2025  na tatu, nini mategemeo au matarajio ya nchi kiuchumi pindi muda huo utakapofika? 
33.               Mheshimiwa Spika, Ilani ya CCM ya mwaka 2005 inasema “Kukuza uchumi kwa kiwango cha zaidi ya asilimia kumi (10%) kwa mwaka ifikapo 2010 kutoka ukuaji wa sasa wa asilimia sita nukta saba (6.7%) PiaKuanza kupunguza umaskini wa watu wetu kwa namna iliyo dhahiri”, haya yalikuwa ni malengo ya kufikia mwaka 2010,  ambapo hadi sasa uchumi huijafikia asilimia 10. Aidha, asilimia 28.1 ya Watazania wote wanaishi chini ya mstari wa umaskini (below poverty line kwa takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2012), hii ni sawa na Watanzania milioni 12. Je bajeti ya taifa inawezaje kutumika katika kupunguza umaskini?

34.               Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 50  cha utekelezaji wa bajeti  serikali, inayoongozwa na CCM,  haijafanikiwa kuwa na bajeti yenye uhalisia wa kupunguza umaskini wa Watanzania, kwani Bajeti inayolenga kupunguza umaskini:
Ø Ni ile ambayo inayolenga kupunguza mzigo wa kodi kwa wananchi,
Ø Ni ile ambayo inatengeneza ajira nyingi kwa wananchi wake,
Ø Ni ile ambayo inakuza uwekezaji hasa wa ndani,
Ø Ni ile inayomfanya Mtanzania aweze kuweka akiba (savings),
Ø Ni ile ambayo inalenga kuinua maisha ya walio wengi ambao wako Vijijini,
Ø Ni ile inayolenga uchumi wa nchi umilikiwe kwa asilimia iliyo kubwa  na wananchi wake,
Ø Ni ile inayolenga kukuza ujasiriamali na,
Ø Ni ile inayokuza ulaji (increased consumption).

35.               Mheshimiwa Spika, Wataalamu tunao, rasilimali tunazo, nia tunayo, ni kwa vipi tunashindwa? Ni vema sasa Serikali iliambie Bunge lako Tukufu nini kikwazo cha kuteleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano? Au ni hila za serikali iliyoko madarakani, kuwafanya Watanzania waendelee kuwa maskini kwa maslahi yao kisiasa?
36.               Mheshimiwa Spika, ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuwaomba Watanzania wote wenye nia njema, tuuungane  pamoja kwa masilahi mapana ya nchi yetu ya kuwatoa Watanzania katika lindi hili la ufukara. Kwani Mwenyezi Mungu ametujali utajiri mkubwa wa rasilimali za kila aina , ili Tanzania pawe mahali salama pa kuishi na kukuza Utu wa Binadamu.

SEKTA BINAFSI NA AJIRA KWA VIJANA.

37.               Mheshimiwa Spika, Kwa muda mrefu sasa swala la ajira kwa vijana limejadiliwa katika Bunge hili tukufu, lakini halijapatiwa bajeti ya kutosha. Ni jambo lililo   wazi kwamba litaendelea kuwa ni tatizo kwa la Taifa na hatimae kuwa ni bomu linalosubiriwa kulipuka  wakati wowote. Upo  umuhimu wa kulitafutia ufumbuzi wa kibajeti kwani vijana ndiyo rasilimali kazi kuu kwa  maendeleo ya taifa.

38.               Mheshimiwa Spika,  inakadiriwa kwamba ajira kwenye sekta rasmi ni 1,352,559 na kati ya hizo asilimia 68.1 ni ajira katika sekta binafsi isiyo rasmi.  Tafsiri yake ni  kwamba ukichukua idadi ya watu millioni 24 wenye uwezo wa kufanya kazi, idadi yao kubwa wako kwenye sekta isiyo rasmi na wengine wengi hawana ajira. Swali je, Bajeti hii inawezaje kutumika katika kutengeneza ajira?

39.               Mheshimiwa Spika , Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka  serikali ishirikiane na sekta binafsi, ili kuweka mikakati ya  kuwa na  bajeti ambayo itaifanya sekta binafsi ipanuke na iweze kuongeza uwezo wake wa kuajiri. 

40.               Mheshimiwa Spika, swala la mazingira bora kwa uwekezaji ni la muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote duniani, hususani kwa nchi zenye nia ya kukuza uchumi wake. Utekelezaji wa dhana hii unatakiwa uanzie serikalini na kwa  mtu mmoja mmoja.
41.               Mheshimiwa Spika, ni vema Serikali ikatoa motisha na  mazingira rafiki  kuiwezesha sekta binafsi iweze kukua kwani ndiyo injini ya kukuza uchumi wetu na kuzalisha ajira nyingi kwa vijana wetu.  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi ifanye upembuzi wa kina unaolenga miaka mitano au hata kumi ijayo ya namna ya kuweka sera (macroecnomic policies) ambazo zitakuwa ni kivutio kwa makampuni yaliyopo kuweza kukuza uwekezaji.





VIPAUMBELE VYA TAIFA

42.               Mheshimiwa Spika, ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa ni lazima taifa letu kuainisha masuala yenye vipaumbele kwa ajili ya kuleta maendeleo ya dhati na kufanikisha kuwa na bajeti inayotekelezeka.

43.               Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inapendekeza kuwa masuala yafuatayo yatambuliwe na kupewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka 2014/15 na miaka ijayo. Masuala hayo ni Utawala bora, Elimu, Kilimo, Afya, Miundombinu, Nyumba na Makaazi, Michezo na Sanaa, Ajira (Kukuza uchumi Vijijini) na Ulinzi wa Rasilimali za Taifa – Wanyamapori, Misitu, Ardhi, Uoto wa Asili, Maziwa, mito, Bahari pamoja na mazao yake. Tunapenda kufafanua umuhimu wa  baadhii ya vipaumbele hivi kama ifuatavyo. 
(i)                   Utawala Bora
44.               Mheshimiwa Spika, Taifa lolote lenye kutaka maendeleo ya kiuchumi hutegemea mhimili wa utawala bora (good governance). Utawala bora ni maneno yanayojumuisha mfumo mzima wa uendeshaji wa shughuli za serikali na taasisi zake katika ngazi zote kwa kuzingatia sheria, kanuni, miiko na miongozo inayowekwa.
45.               Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia kwa mara kadhaa ndani na nje ya Bunge lako tukufu, kuwa watanzania, wakiwamo viongozi, hukiuka kwa uwazi misingi mikuu ya utawala bora. Ukiukwaji huo hujidhihirisha pale ambapo viongozi wanashindwa kutekeleza kwa ufasaha sheria zilizotungwa, kushindwa kufuata maelekezo, kujichukulia sheria mkononi katika kufanya maamuzi badala ya kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa na kukosa uadilifu katika uwajibikaji.

46.               Mheshimiwa Spika, Ulinzi na usalama wa taifa, ulinzi wa Rasilimali za Taifa kama vile wanyamapori, misitu, ardhi, uoto wa asili, maziwa, mito, Bahari pamoja na mazao yake na masuala mengine mengi ya utendaji wa kila siku wa serikali yanategemea utawala bora.
47.               Mheshimiwa Spika, mapambano dhidi ya makosa ya jinai yanaweza kufanikiwa kwa kuweka misingi na bajeti ya kutosha kwa idara husika. Ni vyema idara kama Mahakama, ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Attorney Generals Chambers), Polisi, TAKUKURU, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mamlaka za Zabuni za Serikali, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Vyombo vya Habari zinastahiki kupewa kipaumbele.    

48.               Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza, utawala bora kama kipaumbele cha taifa na kutenga bajeti ya kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya vyombo vyote vinavyosimamia haki na utawala.
(ii)                 Elimu
49.               Mheshimiwa Spika, hakuna maendeleo yoyote ya kweli yanaweza kufanyika katika sekta yoyote (ikiwemo kilimo, miundombinu, viwanda, afya, utalii nk) pasipo kujenga mfumo wetu wa elimu vizuri ili kuwa na taifa lenye watu walioelimika, wanaojitambua na wenye utaalam ili kuwezesha sekta ya elimu na elimu ya watanzania kwa ujumla kufikia malengo yaliyotajwa.

50.               Mheshimiwa Spika, ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa elimu ipewe kipaumbele kwa Taifa letu. Bajeti ioneshe ni kwa namna gani Mtanzania anaweza kupata elimu ya kumuwezesha kumudu staha za maisha na kushiriki katika shughuli za kijamii na uchumi akiwa na weledi.

Elimu ya Msingi ipewe kipaumbele kwa kila Mtanzania. Uboreshwaji wa shule za msingi na sekondari za Kata ufanywe kwa kuzipatia vifaa vya kufundishia na kujifunzia na walimu wenye weledi wa kutosha.

51.               Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza mishahara ya walimu iboreshwe na Serikali itoe misamaha ya kodi ya mapato (PAYE) kwenye mishahara ya walimu kama motisha ya kuwavutia wote wenye uwezo na sifa za kufundisha kuweza kufanya kazi zao kwa weledi na uadilifu. Swala hili linawezekana kwa Taifa letu. Kama tunaweza kutoa misamaha mikubwa kwa wawekezaji wanaovuna rasilimali za taifa letu, ni suala la kawaida na linalowezekana kutoa misamaha ya kodi kwa walimu wanaowekeza katika nguvu kazi ya taifa kwa kutumia nguvu, akili na maisha yao yote kumuelimisha Mtanzania.

(iii)               Kilimo
Chakula ndilo hitaji la msingi kwa uhai wa kila binadamu. Chakula ndicho  hufanya binadamu apate afya na nguvu za kuishi.

52.               Mheshimiwa Spika, taarifa za ulimwengu ambazo hutolewa na Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa njaa imekuwa chanzo kikuu cha vifo katika mataifa mbalimbali duniani kwa kukosa chakula. Haki ya kuishi inatekelezwa vyema kwa haki ya kila mtu kupata chakula. 
53.               Mheshimiwa  Spika, ustawi wa taifa letu unategemea uwepo wa watu wenye afya njema na wanaoshiriki katika shughuli za kujenga taifa.  Ustawi huu, unategemea uwepo wa chakula cha kutosha.   Ni kwa msingi huu kuwa taifa letu linatakiwa kutekelea kwa vitendo  sera ya Kilimo kwanza ili kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.

54.               Mheshimiwa Spika, Watanzania walio wengi vijijini wameendelea kutegemea kilimo cha mkono na kutegemea mvua za msimu. Uchumi unaotegemea kilimo cha mkono ni dhahiri kuwa hauwezi kumudu kuendesha maisha ya kila siku ya binadamu. Endapo mabadiliko hayo yatachelewa au kutokupewa kipaumbele, taifa letu halitaweza kuepuka baa la njaa.

55.               Mheshimiwa Spika, ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuwa kipaumbele kiwekwe na taifa katika kuwajengea wakulima wadogo wadogo uwezo wa kuzalisha chakula kingi na cha kutosha kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo. Pamoja na hayo, ni vyema taifa letu likahimiza kilimo cha umwagiliaji na kinachotumia zana bora za kilimo kama vile matrekta. Wakulima wakubwa na wenye uwezo, wahimizwe kujenga maghala na kuwekeza katika miradi ya kilimo ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula cha kutosha kwa watanzania na kufungua fursa za viwanda vya kusindika chakula hapa nchini. Hatua hiyo itasaidia kuokoa mazao ambayo yamekuwa yakiharibikia mashambani kwa kukosa maghala au miundombinu ya kuyasafirisha hadi sokoni. 

56.               Mheshimiwa Spika, asilimia 28.1, sawa na Watanzania milioni 12, wanaishi chini ya mstari wa umaskini (below poverty line) kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2012.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitika kuona kwamba bajeti hii haijajikita katika kuwatoa watanzania hawa katika lindi la umasikini na badala yake imekuwa ni bajeti yenye mrengo ule ule wa kila wakati ambao tumeuona katika bajeti za miaka iliyopita. Asilimia 22 ya watoto walio na umri wa  chini ya miaka mitano wana utapia mlo. Asilimia 38 ya watoto walio na umri wa  chini ya miaka mitano wamedumaa. Haya yote yanasababishwa na ukosefu wa lishe bora na ya kutosha. 

57.               Mheshimiwa Spika, kilimo hutegemewa na takriban asilimia 80 ya Watanzania kimaisha na huchangia kwa kiasi kikubwa  pato la Taifa. Lakini hili haliwezekani kama hatutaweka kipaumbele cha dhati katika kusaidia sekta ya viwanda ambayo ndiyo inayotumia (consume) / kununua kinacho zalishwa kutoka katika sekta hiyo ya kilimo. Bajeti ambayo hailengi kwa vitendo hizi sekta mbili kwa ujumla wake, ni bajeti ambayo haitawakomboa watanzania na kuwatoa kutoka kwenye lindi la umaskini.

(iv)               Afya
58.               Mheshimiwa Spika, huduma  za afya kwa watanzania zimeendelea kusambazwa ili kuhakikisha zinamfikia kila mtanzania. Hata hivyo, kuna changamoto nyingi ambazo zimesababisha kuendelea kuwapo kwa matatizo katika sekta ya afya.

59.               Mheshimiwa Spika, kuna haja ya taifa letu kuweka kipaumbele kwenye hospitali za Serikali na kuhakikisha zinatoa huduma bora kwa kila Mtanzania bila kujali hadhi, cheo, rangi, kabila wala nafasi ya mtu katika jamii.

60.               Mheshimiwa Spika, imekuwa kawaida kwa viongozi wa taifa letu pamoja na raia wengine kupenda kutibiwa nje ya nchi na kuacha hospitali zetu hapa nchini. Suala hili linatokana na ukweli kwamba hospitali zetu zina upungufu wa waganga wenye weledi wa kutosha kwa baadhi ya magonjwa, vifaa vya kisasa vya tiba na madawa. Uwepo wa magonjwa ya mlipuko, madawa yasiyo na ubora wa kutosha na kukosa vifaa vya matibabu zimeendelea kuwa sababu za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Huduma za muhimu za afya kama uzazi wa mpango, afya ya wazazi, elimu ya magonjwa ambukizi pamoja na mambo mengine ya afya ni lazima yapewe kipaumbele. Ulinzi wa afya ya mama na mtoto, vijana, wazee na watu wenye mahitaji maalum ya kiafya ni jambo la kupewa kipaumbele. Afya ndiyo itakayosaidia kuongeza muda wa kuishi wa watanzania  na kuongeza ufanisi katika kazi  za ujenzi wa Taifa.

(v)                 Miundombinu: Bandari, Reli, Barabara, Viwanja vya Ndege na Mawasiliano
61.               Mheshimiwa Spika, Watanzania hatuna budi kuendelea kuwekeza katika miundombinu. Mifumo ya miundombinu ya usafirishaji kama vile barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari na sekta ya mawasiliano ni vyema vikapewa kipaumbele cha taifa.

62.               Mheshimiwa Spika, Watanzania ni lazima tuendelee kuimarisha miundombinu ili kuendelea kunufaika na mapato yatokanayo na huduma za usafirishaji na mawasiliano. Ni dhahiri kuwa endapo miundombinu itaboreshwa, Tanzania itaendelea kuhudumia raia wake pamoja na nchi jirani zisizo na bandari wala reli. Ushuru na tozo mbalimbali zitakazopatikana zitasaidia kukuza uchumi wa Taifa letu.

(vi)               Viwanda na Biashara
63.               Mheshimiwa Spika, Watanzania hatuna budi kuwekeza kwenye viwanda ili kuweza kuinua uchumi wa Taifa kwa kutumia malighafi zitokanazo na mazao yanayolimwa hapa nchini. Ukurasa wa 2 wa ripoti ya benki kuu ya Tanzania ya Mwaka 2012/13 inaonesha kuwa sekta ya biashara (uchuuzi) ndiyo inaongoza katika kuchangia katika pato la taifa ikifuatiwa na kilimo na viwanda.

64.               Mheshimiwa Spika, hatuwezi kukubali nchi yetu iwe ni nchi ya kichuuzi. Hakuna taifa lililoweza kuendelea vizuri bila kuwa na viwanda. Serikali imekuwa inatoa vipaumbele kwa uwekezaji lakini imekuwa haitoi vipaumbele kwa viwanda ambavyo vimeshawekezwa hapa ndani ili viendelee kukua na kusaidia ajira na kukuza pato la taifa. Hali hii ndiyo imeviua viwanda vyetu vingi ambavyo tulikuwa navyo hapa nchi kama viwanda vya Mwatex, Sungura tex, General Tyre na kadhalika.

65.               Mheshimiwa Spika, Wakati nchi nyingine kama za SADC zinatoa vipaumbele katika kulinda viwanda vyao wakati mwingine kwa kuondoa kodi za bidhaa (excise duty), serikali yetu imekuwa iking’ang’ania kuongeza kodi kila mwaka na kufanya wale ambao wameshawekeza kushindwa kukua na kuongeza ajira na mapato kwa serikali.  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  inaitaka serikali ipitie upya sera za kikodi za kimkakati zitakayosaidia kufanya viwanda vilivyoko hapa nchini vistawi, viongeze ajira badala ya kuwa na hali mbaya na kufikia hali kufilisika.

 IV.        BAJETI MBADALA YA UPINZANI MWAKA 2014/2015

66.               Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua uwepo wa vyanzo vingi vya mapato kwa Taifa kama vile kodi, gharama za leseni na vibali mbalimbali, tozo na ushuru kwenye huduma mbalimbali zitolewazo na serikali pamoja na asasi zake. Katika mapato yatokanayo na kodi, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza yafuatayo:
(i)           Asasi zote zinazokusanya mapato ya serikali ziongezewe uwezo kwa kuweka mfumo wa kisasa utakaosaidia fedha zote zinazokusanywa kuwekwa kwenye mfuko mkuu wa serikali. Mfumo huu unaweza kufanyika kwa kutumia mtandao wa kompyuta. Uwajibikaji wa watumishi wa umma katika asasi hizo uongezwe kwa serikali kuhakikisha watumishi wasio na uadilifu wanaondolewa au kuwajibishwa ili kuhakikisha mapato yanaongezeka.
(ii)          Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iboreshwe katika kukusanya na kusimamia mapato ya serikali. Watumishi wa TRA wapewe ujuzi wa namna ya kukabiliana na watu wenye nia ya kukwepa kodi. Vifaa mahsusi vya kisasa vipatikane ili kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unakuwa wa gharama nafuu lakini wenye mafanikio makubwa. Gharama za ukusanyaji kodi zipungue na kuhimiza mfumo wa ukusanyaji kodi usiohitaji gharama kubwa.
(iii)        Bodi ya Rufaa za Kodi pamoja na Baraza la Rufaa za Kodi nchini ziboreshwe na kuhakikisha kuwa zinafanya kazi kwa ufanisi katika kudhibiti upotevu wa mapato kwenye kesi zinazowasilishwa mbele yake. Hata hivyo, vyombo hivi viongezewe uwezo kwa kuajiri watumishi wenye weledi wa kutosha kuhusu masuala ya kodi na waadilifu.

67.               Mheshimiwa Spika, kuhusu mapato yasiyotokana na kodi, Kambi Rasmi ya Upinzani  inapendekeza maboresho yafuatayo:
(i)                   Ukanda wa Uwekezaji kwa ajili ya kuzalisha bidhaa za kuuzwa nje ya nchi (Export Processing Zone) uboreshwe kwa kudhibiti mapato na uwezekano wa kukwepa kodi hususani kodi ya mauzo, ushuru wa stampu, nk.
(ii)                 Kuboresha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na wamiliki wa majengo na ardhi nchini.
(iii)                Kuboresha makusanyo ya mapato katika maliasili za taifa kama vile madini, misitu na bahari kuu.
(iv)               Kuboresha ufanisi wa bandari ili bandari itumike kama kituo kikuu cha kuingizia bidhaa kwa wafanyabiashara na wasafirishaji wa hapa nchini na nchi jirani ambazo hazina bandari.
68.               Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa taarifa zinaonesha kuwa Serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali kuongeza mapato, bado zipo fursa nyingi za kuongeza mapato ya Serikali ambazo hazijafanyiwa kazi. Hali hii imepelekea kushindwa kukusanya mapato yanayokusudiwa na hivyo kufanya tushindwe kutekeleza bajeti kwa mapato yetu.

 Kushindwa utekelezaji wa kukusanya mapato ya Serikali unafafanuliwa kwa mifano ifuatayo:

(i)           Uwekezaji na Kodi (FDI and Tax Liability)

69.               Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania imekuwa ikiweka vivutio kadhaa katika uwekezaji ili kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi. Vivutio hivyo vinajumuisha misamaha ya kulipa kodi mbalimbali kwa baadhi ya huduma na uwekezaji kama vile kodi ya mapato, ushuru wa forodha na kodi ya ongezeko la thamani (VAT).  Hata hivyo, kodi inayosamehewa kwa wawekezaji kwa kiasi huikosesha serikali mapato ambayo ingepata kwa wawekezaji  kwa kulipa kodi stahiki.

(ii)          Vivutio vya Kodi katika Sekta ya Madini (Tax incentives for Extractive Sector)

70.               Mheshimiwa Spika, makampuni ya uwekezaji kwenye utafutaji na uchimbaji madini nchini wanapatiwa vivutio kadhaa kuendeleza shughuli zao nchini. Kulingana na Cheti cha Vivutio cha TIC, vivutio hivi ni pamoja na:-
·        Kufutwa kabisa kodi kwenye mafuta ya mitambo na magari  kwa muda wote wa utafutaji madini na mwaka mmoja wa kwanza wa uzalishaji ambapo watalipa 5% tu,
·        Msamaha wa mapato juu ya mtaji,
·        Msamaha wa kulipa VAT kwa kuagiza bidhaa nje ya nchi na hata ndani; hii ni pamoja na makampuni na wakandarasi wao,
·        Kulimbikiza madeni juu ya gharama za uzalishaji na kutolipia kodi (The ability to offset against taxable income the cost of all capital equipment including machinery or property incurred in a mining operation),
·        Hulipia kodi ya stempu kwa 0.3% tu kinyume cha sheria inayoitaka kuwa 4%,
·        Baada ya kulipa kodi ya 0.3% makampuni hulipa  Dola za Marekani 200,000 tu kwa mwaka bila kujali ukubwa wa shughuli za uzalishaji, faida na uchafuzi mazingira na madhara mengine kwa jamii,



(iii)        Msamaha wa Kodi kwa Wawekezaji wa Kimkakati

71.               Mheshimiwa Spika, mwekezaji yeyote (toka nje) awekezaye zaidi ya Dola za Marekani milioni 20  hupewa hadhi ya mwekezaji wa Kimkakati (‘Strategic Investor Status’). Hawa hupewa misamaha ya kodi na huingia mikataba na serikali kwa ajili hiyo. Kwa mfano, makampuni yanayojiorodhesha kwenye soko la mitaji la Dar es Salaam (DSE) kwa umiliki wa angalau asilimia 30 (with at least 30 per cent of their shares issued to the public) hulipia asilimia 25 tu ya kodi ya makampuni. Makampuni haya husamehewa pia kodi ya VAT kwenye Bima, Elimu, Huduma za Fedha na Utalii.

72.               Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG) misamaha ya kodi iliyotolewa kwa makampuni ya uchimbaji madini pekee kwa mwaka 2011 ilikuwa shilingi billioni 109.885 huku misamaha iliyotolewa na TIC ikifikia shilingi. bilioni 239.667


(iv)          Upotevu wa Mapato katika Sekta ya Madini

73.               Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni moja ya nchi zinazozalisha Dhahabu kwa wingi Afrika, ilitegemewa kuwa sekta hiyo ingechangia sana kwenye ukuaji wa kiuchumi wa nchi, hili halijafikiwa. Taarifa za shirika la fedha Duniana (International Monetary Fund - IMF) zinabainisha kuwa kati ya mwaka (2008 – 2011) mapato ghafi ya dhahabu yaliongezeka toka Dola za Marekani millioni 500 hadi bilioni 1.5  kwa sababu ya kuongezeka kwa uzalishaji na bei ya dhahabu kuongezeka dhamani,  lakini mapato kwa serikali yalibaki kuwa  Dola za Marekani  milioni 100 kwa mwaka kwa wastani.

74.               Mheshimiwa Spika, hali hii imesababishwa kwa kiasi kikubwa kwa msamaha wa kodi kwa makampuni (Corporate income tax holidays). Hakuna kampuni hata moja liliyolipa kodi hii hadi 2012. Taarifa ya IMF inaonesha pia kwa kuzingatia hali hii, hakuna mategemeo kuwa kipato kutokana na madini kitaongezeka hivi karibuni.

75.               Mheshimiwa Spika, pamoja na kupitishwa sheria mpya ya madini ya mwaka 2010, migodi iliyopo bado inaendelea kulindwa na mikataba iliyoingiwa kwa kutumia sheria iliyofutwa. Makubaliano ya kati ya Serikali na makapuni hayo inaonesha kuwa Tanzania inapoteza fedha nyingi sana, kwa mifano:

(i)           Taarifa ya Tume ya Bomani ilikadiria serikali ilipoteza  sh. bilioni 39.8  mwaka 2006/7 na sh. bilioni 59 mwaka  2007/8 kutokana na msamaha wa kodi ya mafuta tu (fuel levy exemptions)  kwa makampuni sita tu. Kufikia mwishoni mwa  mwaka 2011, makampuni ya uchimbaji madini yalikuwa yanadai takribani Dola za Marekani miioni  274 kurejeshewa kutokana na msamaha wa kodi hiyo toka 2002. 
(ii)          Makampuni yamepewa haki ya kumiliki  madini yake, ikiwemo haki ya kuuza hisa na mitaji yake bila kulipa kodi ya mapato (capital gains tax).
(iii)        Mikataba na sheria inawapa makampuni ruksa ya kutumia hasara wanazopata kufidia kulipa kodi.
(iv)        Mwaka 2010, Tanzania Minerals Audit Agency (TMAA) ilikagua makampuni 12 na kugundua mapungufu/udanganyifu wa matumizi ya makampuni wa  Dola za Marekani milioni 705.8, ambapo serikali ilikosa  mapato ya Dola za Marekani 176 milioni. Hii ilikuwa mara ya kwanza TMAA kufanya ukaguzi, je, kwa miaka 10 kabla ya hapo serikali ilipoteza kiasi gani cha mapato?

76.               Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Viongozi wa Kidini juu ya Haki za kiuchumi na Umoja (A report commissioned by the Interfaith Standing Committee on Economic Justice and the Integrity of Creation) iliyoitwa The One Billion Dollar Question iliyotokana na utafiti wa kutafuta mianya na kiasi cha upotevu wa mapato kwa nchi katika sekta ya madini, upotevu wa mapato ulikadiriwa kufikia  Dola za Marekani bilioni 1.07  kwa mwaka 2009/10 kwa njia ya misamaha ya kodi, ukwepaji kodi, uhamilishaji mitaji na vivutio vya kodi kwa uwekezaji.

77.               Mheshimiwa Spika, upotevu huo wa  Dola za Marekani bilioni 1.07  (takribani sh trilioni 1.7) ilikuwa ni takribani  asilimia 17  ya bajeti yote ya serikali kwa mwaka 2009/10.

78.               Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa TRA misamaha ya kodi kwa mwaka 2011/12 ilikuwa sh. trlioni 1.80 kwa taasisi na watu mbali mbali:

Taasisi
 Kodi za Nje& Mapato
 Mapato Ndani
 Jumla 2011/12
 Jumla 2010/11
MDAs
        9,603,414,035.00
                                     -  
           9,603,414,035.00
        35,867,200,000.00
Mashirika Umma
      15,699,616,106.00
                                     -  
         15,699,616,106.00
          8,131,200,000.00
Taasisi Dini
            436,967,358.00
                                     -  
               436,967,358.00
          1,569,300,000.00
AZAKI
        7,542,700,000.00
                                     -  
           7,542,700,000.00
        25,462,600,000.00
Balozi/UN
      10,194,000,000.00
                                     -  
         10,194,000,000.00
                                        -  
Maduka Jeshi
        2,454,600,000.00
                                     -  
           2,454,600,000.00
                                        -  
Miradi Ufadhili
   225,039,689,862.00
                                     -  
      225,039,689,862.00
      115,758,100,000.00
Binafsi/Kampuni
   304,045,656,449.00
                                     -  
      304,045,656,449.00
      182,706,100,000.00
Uchimaji Madini
   140,637,400,000.00
                                     -  
      140,637,400,000.00
      109,885,900,000.00
TIC
   280,961,890,898.00
                                     -  
      280,961,890,898.00
      239,667,300,000.00
Misamaha VAT
                                      -  
   801,859,513,440.00
      801,859,513,440.00
      279,845,200,000.00
Maduka Huru
                                      -  
        7,726,106,679.00
           7,726,106,679.00
        17,427,400,000.00
Jumla
   996,615,934,708.00
   809,585,620,119.00
   1,806,201,554,827.00
  1,016,320,300,000.00
Chanzo: CAG, 2012. Office of the Controller and Auditor General AGR/CG/2011/2012 p.31

79.               Mheshimiwa Spika, ingawa mapato ya serikali yameongezeka kwa miaka mitano ilopita kutoka sh. trilioni 3.379 kwa 2007/08 hadi sh. trilioni 6.703 kwa 2011/2012, hata hivyo inaonesha misamaha ya kodi imekuwa ni wastani wa  asilimia 3.52  ya GDP kati ya 2007/2008 na 2008/09.  Mwaka 2009/10  ilipungua hadi  asilimia 2.1 ya GDP. Aidha, iliongezeka tena hadi  asilimia 2.9 mwaka 2010/2011 na kwa mwaka   2011/2012 ilifikia asilimia  4.3


80.               Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuimarisha na kulinganisha mipango na mifumo yake ya kukusanya kodi na kutoa misamaha, na haswa kuweka ukomo wa misamaha ya kodi kuwa si zaidi ya 1% ya Pato la Taifa. Hatua hii inatakiwa iwekewe kipindi maalum cha kufikia lengo.




MAENEO MAPYA YA KUONGEZA MAPATO

A.  Kodi kwa Sekta Isiyo Rasmi

81.               Mheshimiwa Spika, mazingira wanayojengewa wafanya biashara wadogo wa sekta isiyo rasmi inawafanya kufanya biashara kwa taabu, bila mitaji ya uhakika na faida kidogo kiasi kinachowahamashisha kukwepa kodi. Kutokuwepo mifumo wezeshi  ya ufanyaji biashara na utitiri wa kodi unapunguza uwezekano wa  wafanya biashara wadogo kulipa kodi kwa hiyari. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wajasirimali wadogo ili waweze kupata faida na kulipa kodi kwa Serikali.

B.  Wachimbaji Madini Wadogo

82.               Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wanahitajika kulipia mrabaha (royalties) kwa serikali kwa mujibu wa sheria ya madini ya 2010. Ni wajibu wa serikali kuweka  mazingira  mazuri na rafiki ya kuwawezesha  wachimbaji wadogo  waweze kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi kwa serikali.


C.  Mapato ya kodi ya Ardhi na Mali Asili

83.               Mheshimiwa Spika, mauzo na matumizi ya ardhi na maliasili nyingine hayajatiliwa mkazo kwenye vyanzo vya mapato ya serikali. Hii inajumuisha ardhi inayotumika kibiashara na kukodishwa kwa uzalishaji na biashara. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka mkazo katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na ardhi na maliasili.

D.  Mauzo ya Mazao ya Misitu

84.               Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa mapato kutokana na mauzo ya mazao ya misitu yamekuwa yakiingizia serikali fedha nyingi, tafiti zinaonesha kuwa usimamizi na ukusanyaji mapato haya unaweza  kuongeza kipato cha serikali iwapo itawekwa nguvu kuimarisha ukusanyaji mapato haya. Ernst&Young, 2012 wamekadiria zaidi ya 40% ya mapato ya serikalii hupotea katika sekta hii. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuongeza uwezo wa kukusanya zaidi ya  30% ya mapato yanayokusanywa sasa.

E.  Mapato ya Uwindaji wa Kitalii

85.               Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2010 mapato yatokanayo na uwindaji wa kitalii yalikuwa juu kidogo ya Shs. 33 billioni, wakati maboresho ya ukusanyaji mapato kwa mwaka 2011 yaliongeza mapato hadi Shs.79 billioni. Uwezekano ni mkubwa kuongeza mapato haya iwapo rushwa, usimamizi dhaifu na udhibiti wa mfumo wa kukusanya mapato utafanyiwa marekebisho chanya.



F.   Mrabaha wa Madini (Royalties)

86.               Mheshimiwa Spika, kulingana na taarifa za kamati ya Taifa ya Tanzania Extractive Industry Transparency Initiative (TEITI), mbinu chafu na usiri ni Miongoni mwa mambo yanayoghubika sekta ya uchimbaji madini. TEITI imeweka wazi pia kuwa kuna tofauti kubwa kati ya viwango vinavyoripotiwa kulipwa na Makampuni ya madini na zile za serikali kama mrabaha, huku makampuni yakionesha yanalipa fedha nyingi kuliko serikali inavyosema.

87.               Mheshimiwa Spika, wakati ushahidi wa nyaraka za makampuni umeidhihirishia TEITI kuwa makampuni yamelipa, hakukuwa na nyaraka zinazoonesha malipo yalipokelewa  serikalini.

G.  Taasisi za Kibiashara za Serikali

88.               Mheshimiwa Spika, Makampuni ya Serikali na wakala zake zinazoendesha shughuli kibiashara na au kutoa huduma pia zinakusanya mapato. Hata hivyo taasisi hizi zinapaswa  kwa mujibu wa Finance Act No. 13 of 2008 and the Treasury Circular No. 8 of 2008/09 kuchangia fedha hizi kwenye Mfuko Mkuu wa fedha wa serikali (Consolidated Fund). Hakuna taarifa zinazoonesha kuwa taasisi hizi zimewahi kuchangia kama matakwa ya sheria (Finance Act No.13 of 2008, Treasury Circular No. 8 of 2008/09 na Katiba ya JMT Ibara ya 135 (2).
Taasisi zilizochunguzwa ni:
·        Tanzania National Parks (TANAPA),
·        Ngorongoro Conservation Area Authority (NCAA)
·        Energy and Water utilities Regulatory Authority (EWURA); na 
·        Tanzania Communication Regulatory Authority (TCRA).

H.  Mamlaka ya Bandari

89.               Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa za Benki ya Dunia, Tanzania inapoteza takribani Dola za Marekani  bilioni 1.8   sawa na  Shs.  trilioni 2.88 ambazo ni karibu asilimia 16 ya bajeti yote ya nchi kwa mwaka 2013/14.  Endapo  bandari ya Dar es salaam ingetumika ipasavyo kwa viwango vya kimataifa (ufanisi na kuaminika) ingeongeza mapato kwa kiasi kikubwa kwenye bajeti ya serikali. Kazi hii inawezekana kabisa kufanyika kwa njia ya ushirikishwaji wa sekta binafsi kwa njia ya   “Public Private Partenership”- PPP. Pia, Bandari za Tanga, Mtwara nazo zijumuishwe kwenye utaratibu huu wa PPP.









  V.        MAPATO MBADALA
MAPATO MBADALA
NA.
AINA YA CHANZO
JUMLA YA SHILINGI
1.
Kudhibiti ukwepaji Kodi na udanganyifu
  1,931,300,000,000.
2.
Kuongeza Ufanisi TRA
   708,112,000,000.
3.
Dhibiti Misamaha hadi kufikia 1% ya pato la Taifa.
 1,386,000,000,000.
4.
Kuongeza ufanisi Bandari DSM kwa 50% tu.
1,440,000,000,000.

5.
Pesa – Fasta, tozo la 15% kwenye faida ya wakala wa makampuni ya simu.
    268,800,000,000.
6.
Tozo ya 1% ya manunuzi yote ya nje na tozo ya 0.5% ya mauzo yote ya nje-itatengwa Kwa ajili ya ukarabati wa  miundombinu ya Reli (Special Railways development levy)
226,110,000,000.
7.
**Mrabaha wa 5% kwenye uvuvi wa samaki-bahari kuu kwa meli 68.
14,025,000,000.
8.
Marekebisho ya kodi sekta ya misitu
220,416,000,000.

JUMLA YA MAPATO YA VYANZO MBADALA
6,194,763,000,000.

Note: **    Meli zilizopatiwa leseni kuvua bahari kuu ni meli 68 na kwa makisio kila meli kwa mwaka inavua wastani wa tani 500 sawa na kilo 500,000.
-         Kwa meli zote zitavua kilo  kwa mwaka kilo  34,000,000
-         Kilo moja ya samaki inauzwa USD 5  sawa na Tshs 8250/-
(Kwa exchange rate ya sh. 1650 kwa USD 1)
-         Hivyo kilo    34,000,000  X  Sh. 8250  sawa na  shilingi  280,500,000,000/-
Mrabaha ni 5%  sawa na shilingi 14,025,000,000/-


 VI.        Sura ya Bajeti
SURA YA BAJETI MBADALA MWAKA 2014/15


MAPATO
%
SHILINGI MILIONI
A
Mapato ya ndani
84.38

18,372,797.00

i)Mapato ya Kodi (TRA)

17,272,850.00


ii)Mapato yasiyo ya Kodi

1,099,947.00

B
Mapato ya Halmashauri
  2.12

458,471.00
C
Mikopo na misaada ya Kibajeti

922,168
   
D
Mikopo na Misaada ya miradi ya maendeleo ikijumuisha MCA (T)

2,019,431


JUMLA YA MIKOPO NA MISAADA YA NJE
13.50

2,941,599.00

 JUMLA YA MAPATO YOTE
100.00

21,772,867.00






MATUMIZI



E
Matumizi ya Kawaida
57.33

12,482,384.66

(i)           Deni la Taifa
19.07
4,152,085.74


(ii)          Mishahara
27.73
6,037,616.02
 

(iii)        Matumizi Mengineyo
10.53
2,292,682.89


Wizara                1,879,999.97                   




Mikoa                      45,853.66         




Halmashauri          366,829.26    



H
Matumizi ya Maendeleo
42.67

9,290,482.34

(i)Fedha za ndani

6,348,883.34


(ii)Fedha za Nje 

2,941,599.00


JUMLA YA MATUMIZI YOTE
100

21,772,867.00


VII.        ULINGANISHO KATI YA BAJETI YA SERIKALI NA BAJETI           MBADALA YA UPINZANI

TOFAUTI KATI YA BAJETI YA SERIKALI NA BAJETI MBADALA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KWA MWAKA 2014/2015.


BAJETI MBADALA YA KAMBI YA UPINZANI 2014/2015
BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2014/2015
1
Bajeti isiyo na Mikopo ya kibiashara hivyo bajeti inalenga kulipunguzia taifa mzigo wa madeni.
Bajeti ya Serikali ina mikopo yenye masharti ya kibiashara ya shilingi trilioni 4.3 na hivyo bajeti hii inawaongezea wananchi mzigo wa madeni.
2
Bajeti inayoendelea kusisitiza umuhimu wa kuwalipa pensheni wazee wote nchini wenye umri wa   miaka 60 na kuendelea.
Bajeti ya Serikali iko kimya kabisa kuhusu malipo ya pensheni kwa wazee wote nchini.
3
Bajeti inayoendelea kusisitiza kushusha kiwango cha  tozo ya kodi ya mapato ya ajira kwa wafanyakazi (PAYE) hadi kufikia asilimia 9.
Bajeti ya Serikali imeendelea kuwakandamiza wafanyakazi kwa kutoza asilimia 12 ya  kodi ya mapato ya ajira (PAYE)  kwa wafanyakazi.
4
Bajeti ya Upinzani imeainisha vyanzo vipya  vya mapato ya ndani na hivyo  inayojitegemea kwa asilimia 84.38
Bajeti ya Serikali ni  tegemezi kwa asilimia 36.4 kutokana na kukopa kwa kiwango kikubwa na hivyo  kuongeza deni la taifa.
5
Bajeti Mbadala, mapato ya ndani ni asilimia 34.55 ya pato la Taifa
Bajeti ya Serikali, mapato ya ndani ni asilimia 23 ya pato la taifa.
6
Bajeti inayolenga kupunguza misamaha ya Kodi hadi kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa ili kuongeza mapato ya ndani.
Bajeti ya Serikali imetaja tu azma ya kupunguza misamaha ya kodi lakini haijataja ni kwa asilimia ngapi ya pato la taifa wala haijaainisha watakaofutiwa misamaha hiyo.
7
Bajeti inayolenga kutekeleza kikamilifu  miradi ya maendeleo kwa kutenga asilimia 42.67 ya bajeti yote kugharamia miradi ya maendeleo.
Asilimia 22 ya Bajeti yote ya  Serikali inakwenda kulipa deni la Taifa na asilimia 67.5 ni  matumizi ya kawaida. Hivyo miradi ya maendeleo haijapewa kipaumbele.
8
Bajeti inayolenga kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo ambavyo havimuumizi mwananchi wa kawaida
Bajeti ya Serikali imelenga kukusanya mapato kutoka katika bidhaa zinazotumiwa kila siku na wananchi kama vile vinywaji na hivyo kuwaongezea wananchi ugumu wa maisha.
9
Matumizi ya Kawaida ni asilimia 57.33 tu ya bajeti yote
Matumizi ya Kawaida ni  67.5%
10
Bajeti ya kumsaidia mwananchi wa kawaida kutoka katika wimbi la umaskini.
Bajeti isiyo mtambua mwananchi maskini na kuongeza matumizi makubwa kwa watawala.





VIII.        MGAWANYO WA MAPATO

MGAWO WA FEDHA  ZA MAENDELEO KWA VIPAUMBELE VYA BAJETI MBADALA


NA.
JINA LA SEKTA
SHILINGI MILIONI
1.
Kukuza uchumi Vijijini-(Rural Growth)- 35.3%
3,279,540.266
2.
Miundombinu na Usafiri wa Anga    17.8%
1,653,705.856
3.
Ardhi, Nyumba na Makaazi             12.6%
1,170,600.775
4.
Huduma za Jamii Elimu na Afya 27.6%
2,564,173.126
5.
Michezo na Sanaa          6.7%
622462.317

JUMLA YA FEDHA ZA MAENDELEO
9,290,482.340



 IX.        HITIMISHO

90.               Mheshimiwa Spika, ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,  kwamba hatua zote zinazochukuliwa za kufanya mabadiliko katika kukuza Utu wa Binadamu,  ni lazima Viongozi wawe na nyenzo kuu ya Maarifa (elimu na uzoefu). Bila ya maarifa uongozi utakuwa Unababaisha. Uaminifu na uadilifu kwetu sisi Wabunge ni muhimu sana, ili tuweze kuisimamia na kuishauri Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63(2).

91.               Mheshimiwa Spika, Ni msingi mkuu wa kanuni ya Demokrasia ulimwenguni kuwa sheria zote na mamlaka za kusimamia na  kutoza kodi zizingatie uwakilishi wa wananchi ambao ndio walipa kodi. Serikali yetu inaendeshwa kwa ridhaa ya Watanzania ambao tumekubali kuchangia matumizi ya serikali kwa kulipa kodi.   Walipa kodi watashiriki mchakato mzima kama wanaridhika kwamba hakuna hila katika mabadiliko. Mabadiliko yo yote yatafanikiwa tu, ikiwa nia na lengo ni kupanua  Uhuru wa raia na kulinda Utu wao.

92.               Mheshimiwa Spika, Adui wa mabadiliko endelevu ni Unafiki na Ufisadi.

93.               Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, namwomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwajalia Hekima na Busara  wewe binafsi, Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge na Katibu wa Bunge kwa dhamana mliyopewa ya kulitumikia, kulisimamia na kuliongoza Bunge hili tukufu. Aidha, nawashukuru wote walioshiriki katika kuandaa maoni ya hotuba hii.

94.                Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
  
James Francis Mbatia (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya Fedha

16 Juni, 2014

3 comments:

  1. Let's educate the Tanzania citizen on the importance of having a National ID cad that will enable them to participate fully on the coming General Election.This is an IDEAL CHADEMA WE HAVE TO LIVE ON EVEN IF IT COST OUR LIFE.This is a key to step into power to refrain this country from the hands of fierce and unfaithful leaders full of bribe and conspiracy against the National development.

    ReplyDelete
  2. Hello, Je, wewe kuangalia kwa mkopo wa biashara, mkopo binafsi, nyumbani mkopo,
    nk.? Sisi kwa sasa ni sadaka binafsi na biashara mkopo kwa mtu yeyote
    nia ya mtu binafsi katika 2% riba kutoka 1 kwa miaka 30.
    Jina:
    Tarehe ya kuzaliwa:
    jinsia:
    Hali ya ndoa:
    anwani:
    mji:
    nchi:
    simu:
    Kiasi cha mkopo:
    Mkopo Duration:
    Net mapato kwa mwezi.
    Kuwasiliana nasi: creditsolutionhome@outlook.com

    ReplyDelete
  3. Vizuri kuanzisha mwenyewe, mimi ni Mr Richard Raymond Taasisi binafsi i kutoa mkopo saa 2% kiwango cha riba. Hii ni fursa ya fedha katika hatua yako mlango, kuomba leo na kupata mkopo wako haraka. Kuna wengi huko nje kutafuta nafasi ya kifedha au misaada yote juu ya maeneo na bado bado hawawezi kupata one.But hii ni fursa ya fedha katika hatua yako mlango na kama vile huwezi kumudu miss nafasi hii. Huduma hii ni kutoa kwa wote watu binafsi, makampuni, watu biashara na wanawake. Kiasi cha mkopo kati inapatikana kutoka kiasi yoyote ya uchaguzi wako Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kupitia email: citiloanfinancelimited@gmail.com

    LOAN FOMU kujaza na RETURN.

    Full Jina ....................................

    Binafsi simu ............................

    Nchi ...........................................

    Mitaani ......................................

    Hali ..............................

    Umri .............................................

    Je, kutumika kabla? .......................

    Hali ya ndoa .................................

    Kiasi cha mkopo zinahitajika kama mkopo .....................................

    Mkopo Duration .................................

    Kazi ....................................

    Mapato kwa mwezi .............................

    Katika kukiri ya maelezo haya, Tutakuwa kutuma wewe masharti yetu pamoja na ulipaji wa ratiba na Kama wewe kukubaliana na sheria na masharti, unaweza kusimama kupata mkopo wako ndani ya 24hours. Hii inategemea uzito wako na uharaka katika kupata mkopo.
    Mimi kwa furaha wakisubiri majibu yako mwepesi,

    Wako mwaminifu,

    Richard Raymond

    ReplyDelete