1. UTANGULIZI:
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru mwenyezi
mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya bunge hili
kutoa maoni ya kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa
mwaka 2014/15.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii pia kutoa shukrani kwa Kiongozi wa
Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kuniamini na kuniteua kuwa
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Ofisi ya Rais- Mahusiano na
Uratibu. Kipekee naishukuru familia yangu (Mume wangu na watoto wangu wapendwa)
kwa kinitia moyo katika kazi zangu za kibunge na kichama. Aidha wananchi wote
wa Mkoa wa Mara hususani wa Wilaya ya Tarime kwa ushirikiano wanaonipa katika
kutekeleza majukumu yangu.
Mheshimiwa Spika,Mpango
huu wa maendeleo wa mwaka 2014/15 ni sehemu ya nne ya Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano (2011/12-2015/16) kama ulivyopitishwa na Bunge hili, na pia ni
sehemu ya kwanza ya utekelezaji wa Dira ya maendeleo ya Taifa ya 2025. Dira 2025 imeundwa na nguzo kuu tano
ambazo ni: (i)Kuboresha hali ya maisha ya Watanzania (ii) Kuwepo kwa mazingira
ya amani,usalama na umoja (iii) Kujenga utawala bora (iv) Kuwepo jamii
iliyoelimika vyema na inayojifunza, na (v) Kujenga uchumi imara unaoweza
kukabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine.
Mheshimiwa
Spika, Hoja ya
msingi ni kwa kiasi gani Serikali ya CCM imefanikisha utekelezaji wa nguzo ya
kwanza ya Dira 2025, ambayo ni kuboresha hali ya maisha ya Watanzania?
Mheshimiwa
Spika, Mpango wa maendeleo wa miaka
mitano unasema wazi kuwa sera ya matumizi haioneshi msisitizo maalum wa
kupunguza matumizi ili yaendane na makusanyo ya ndani. Aidha lile lengo la
kutumia asilimia 22 ya makusanyo ya ndani kwa matumizi ya kawaida limeshindikana
kabisa[1]. Kwa
sasa mwaka wa fedha 2014/15 makusanyo ya ndani ni shilingi trilioni 12.178 na
matumizi ya kawaida ni shilingi trilioni 13.408. Aidha, hili linajidhihirisha
wazi katika taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Mheshimiwa Spika, njia
ya kubana matumizi kwa kuondoa udhaifu wa kukarabati barabara mara kwa mara,
kuwa na kipindi maalum cha kukarabati barabara mara baada ya kukabidhiwa kwa Serikali nalo nitatizo kubwa
linalotumia mabilioni ya fedha za walipa kodi. Taarifa ya Mpango wa miaka
mitano inaonesha kwamba kwa mujibu wa makadirio ya benki ya dunia kiasi cha
dola za kimarekani bilioni 2.4 kwa mwaka zinatumika kukarabati barabara katika
bara la Afrika. Na hili kwa ushauri wao lingeweza kuepukwa kama kungekuwa na
kipindi maalum cha ukaratabati “timely preventive maintenance” na pia
kuna mapungufu kadhaa yanayoendana na udhaifu wa Serikali kushindwa kuwa
makini. Kama vile kushindwa kukusanya kodi, kuwa na watumishi wengi wasiokuwa
na tija[2] n.k
Mheshimiwa
Spika, Kama kweli Serikali inataka
kufikia malengo ya millenia, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kuzingatia matakwa ya mpango katika matumizi kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda wananchi wafahamu kwamba Mapendekezo
ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa ya 2014/15 yaliyoletwa na Serikali ili
yajadiliwe na Bunge hili ni ya nne
katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16). Kwa maneno mengine ni kwamba imebaki miaka
miwili tu kukamilisha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
(2011/12 – 2015/16)
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda pia
kuwajulisha wananchi kwamba wakati imebaki miaka miwili tu kwa Serikali
kukamilisha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano,
umebaki mwaka mmoja tu kwa upande wa Chama cha Mapinduzi kukamilisha
utekelezaji wa Mpango huo.
Mheshimiwa Spika, Ilani ya CCM ya
mwaka 2005 inasema nanukuu “Kukuza uchumi kwa kiwango cha zaidi ya
asilimia kumi (10%) kwa mwaka ifikapo 2010 kutoka ukuaji wa sasa wa asilimia
sita nukta saba (6.7%)” Pia “Kuanza
kupunguza umaskini wa watu wetu kwa namna iliyo dhahiri”, haya yalikuwa ni malengo ya kufikia
mwaka 2010, ambapo hadi sasa uchumi haujafikia asilimia 10, pia Asilimia 28.1
ya Watazania wote wanaishi chini ya mstari wa umaskini (below poverty line kwa
takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2012), hii ni sawa na Watanzania milioni 12.
Endelea....
Mheshimiwa
Spika,Kwa kipindi chote cha utekelezaji wa bajeti serikali haijafanikiwa
kuwa na bajeti yenye uhalisia wa kupunguza umaskini wa watanzania, kwani Bajeti
inayolenga kupunguza umaskini ni ile ambayo inalenga kupunguza mzigo wa kodi kwa wananchi, ni ile ambayo inatengeneza ajira nyingi, ni ile ambayo
inakuza uwekezaji hasa wa ndani, ni
ile inayomfanya Mtanzania aweze kuweka
akiba (savings), ni ile ambayo inalenga kuinua maisha ya walio wengi ambao
wako vijijini, ile inayolenga uchumi
umilikiwe na Watanzania, ile inayolenga kukuza
ujasiriamali na ile inayokuza ulaji
(increased consumption).
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bajeti
zote tangu tuanze utekelezaji wa mpango wa taifa, pia utekelezaji wa ilani ya
CCM, na kwa kuwa sisi sote tunayo nia ya
kuwaondoa watanzania katika umaskini, ni kwa vipi sasa serikali imejipanga kuhakiki
mipango yetu inaendana na sera zetu za bajeti ili tuweze kuoanisha mipango na
utekelzaji wake? Kama wataalamu tunao, rasilimali tunazo, nia tunayo, ni kwa
vipi tunashindwa?
Mheshimiwa Spika, Ni vema sasa
serikali iliambie bunge lako nini kikwazo cha kutekeleza mpango wa maendeleo?
Au ni hila za CCM kuwafanya watanzania waendelee kuwa maskini kwa maslahi ya
kisiasa? Vema bila kujali itikadi zetu tuungane pamoja kwa nia ya kuwatoa
watanzania katika umasikini mkubwa kwani ni ukweli kwamba hawatakiwi kuwa huko
kutokana na utajiri wa nchi hii ulivyokuwa mkubwa. Hali hii haikubaliki kabisa. Inabidi tutanzue kitendawili
hiki cha kuwa nchi tajiri sana kwa wingi wa rasilimali ila watu wake ni
masikini.
Aidha, Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa Sura ya Tisa (9) Ibara ya 212 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2010 inasema kwamba:
“Chama Cha Mapinduzi katika miaka
mitano ijayo,(yaani 2010 - 2015) kinaelekeza nguvu kubwa katikakutimiza lengo
la msingi la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 kwa kuendeleza jitihada za
ujenzi wa uchumi wa kisasa na taifa linalojitegemea. Katika kuzingatia jukumu hilo Ilani hii ya CCM ya 2010 hadi 2015 inatangaza nia ya
modenaizesheni ya uchumi. Modenaizesheni ya uchumi ndiyo njia ya uhakika
itakayobadili na kuleta mapinduzi katika uchumi wa nchi, kujenga msingi
wauchumi wa kati unaoongozwa na viwanda, kuondoa umasikini wa wananchi wetu kwa
kiwango kikubwa na hivyo kuwezesha nchi yetu kujitegemea…………...”
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka wananchi wapime na kufanya tathmini
wenyewe juu ya mambo yafuatayo:
i.
Miaka mitatu ya utekelezaji wa Mpango wa
Maendeleo wa Miaka Mitano kwa Upande wa Serikali na Miaka Minne ya Utekelezaji
wa Mpango huo huo kwa upande wa CCM imeleta mabadiliko katika maisha yao kama
ilivyokusudiwa na mpango huu?
ii.
Je, ni kweli kwamba Mkakati wa CCM
wa kufanya mapinduzi ya Uchumi (Modenizationi ya uchumi) uliotangazwa na ilani
ya uchaguzi ya CCM ya 2010 umefanikiwa?
iii.
Je, ni kweli kwamba msingi wa uchumi
wa Tanzania unaongozwa na viwanda kama CCM ilivyoahidi kwenye ilani yake ya
uchaguzi ya 2010?
iv.
Je, ni kweli kwamba umasikini wa
wananchi umepungua zaidi kuliko miaka mitatu au minne iliyopita kama CCM
ilivyoahidi kupunguza umasikini kwa wananchi na kuleta maisha bora kwa kila
Mtanzania?
v.
Je, ni kweli kwamba sasa hivi
Tanzania ina uwezo zaidi wa kujitegemea kuliko miaka mitatu au minne iliyopita
kama ambavyo CCM iliahidi kwamba kabla ya 2015 Tanzania itakuwa na uchumi imara
na hivyo kujitegemea?
vi.
Je ni kweli kwamba hali ya ajira
hasa kwa vijana ni bora zaidi kuliko miaka mitatu au minne iliyopita kama
ambavyo Serikali ya CCM ilivyoahidi kutoa ajira ili kupunguza umasikini wa
kipato?
vii.
Je, ni kweli kwamba ugumu wa maisha
umepungua zaidi kuliko miaka mitatu au minne iliyopita kama ambavyo Serikali ya
CCM ilivyoahidi kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania?
viii.
Je,
bajeti za Serikali kwa miaka minne iliyopita zimeweza kuondoa tatizo la umasikini kwa watanzania?
Mheshimiwa Spika, Mpango wa maendeleo wa mwaka 2014/15 ni
sehemu ya Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano ambao nao ni sehemu ya Kwanza
kati ya sehemu tatu za mipango ya nchi ili kufikia dira ya maendeleo ya mwaka
2025. Lengo la ujumla la sehemu ya kwanza ya dira ya 2025 ni “kutoa fursa
ili hazina ya raslimali za nchi zitumike ipasavyo kwa kuweka mazingira wezeshi
na kutanua wigo wa ukuaji wa uchumi ili watu maskini waweze kukua kiuchumi”.
Mheshimiwa Spika,Kambi
Rasmi ya Upinzani inapenda kurudia kauli ambayo tumekuwa tukiieleza Serikali kuwa
Mpango mzuri haupimwi kwa vigezo vya jinsi Kitabu cha Hotuba ya Bajeti kilivyopangwa
vizuri, maneno mazuri yaliyomo katika hotuba hiyo, au nadharia ya malengo ya
kisiasa yanavyonyumbuliwa katika hotuba hiyo.
Mheshimiwa Spika,
utengaji wa asilimia kati ya 25 na 30 ya bajeti kuanzia mwaka 2012 hadi sasa
kwa matumizi ya maendeleo ni kwenda kinyume cha Mpango wa maendeleo[3]
ambao umeeleza vyema kwamba kwa utekelezaji wa sehemu ya kwanza ya mpango wa
miaka mitano Serikali itenge si chini ya asilimia 35 kila mwaka kwa ajili ya
miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Mpango
mzuri wa Maendeleo kimsingi ni takwimu ya jinsi tarakimu za mapato na matumizi
zilivyopangwa na utekelezaji wake. Kinyume na hapo mpango uliowekwa vizuri
kwenye hotuba bila ya kuwepo kwa mkakati wa utekelezaji wa mpango huo ni kazi
bure. Kwa sababu hiyo hotuba ya Kambi Rasmi kwa mwaka huu, inajikita katika uchambuzi wa takwimu mbalimbali zilizomo katika mpango
uliopita na mpango wa mwaka huu wa fedha ili kuonyesha kwa jinsi gani Mpango
unaoletwa na Serikali usivyokuwa na mashiko katika utekelezaji wake. Kwani
fedha za utekelezaji ndio kigezo kikuu cha kutuonesha tutokako, tulipo na wapi tunakokwenda
kama nchi.
Aidha
Kigezo hiki ndicho pia kinaonyesha kama vipaumbele vyetu viko sahihi, kama
tunasimamia fedha na rasilimali zetu vizuri, kama tunachukua hatua wakati mwafaka
ili kudhibiti ubadhirifu, wizi na ufisadi au ni business as usual?
2. HALI YA UCHUMI WA TAIFA
Mheshimiwa Spika, taarifa
ya hali ya uchumi inaonesha kuwa Pato la Taifa katika mwaka 2013 lilikua kwa
asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.9 kwa mwaka 2012. Shughuli
ndogo ambazo zilikua kwa kasi kubwa katika mwaka 2013 ni pamoja na mawasiliano
asilimia 22.8; ujenzi asilimia 8.6; biashara ya jumla na rejareja asilimia 8.3;
na hoteli na migahawa asilimia 6.3. Kwa upande mwingine ukuaji wa sekta ya
kilimo ulibaki kama ilivyokuwa mwaka 2012 wa asilimia 4.3. Hii ilitokana na
kupungua kwa kasi ya ukuaji wa shughuli ndogo za mazao kutoka asilimia 4.7
mwaka 2012 hadi asilimia 4.5 mwaka 2013.
Aidha,
Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa
kasi ndogo ya ukuaji wa sekta ndogo ya mifugo na uwindaji ya asilimia 3.1 hadi
3.8 na misitu kutoka asilimia 2.4 hadi 3.3. Pia shughuli zingine ambazo ukuaji
wake ulipungua katika mwaka 2013 ni bidhaa za viwandani asilimia 8.2 hadi 7.7;
umeme na gesi asilimia 6.0 hadi 4.4; uchukuzi asilimia 7.1 hadi 6.2; na uvuvi
asilimia 2.9 hadi 2.2.
Mheshimiwa Spika,
Matokeo ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa Tanzania Bara kwa
Mwaka 2011/12 unaonesha kuwa “Kiwango
cha Umaskini wa Mahitaji ya Msingi kwa mtu mmoja kwa mwezi ni Shilingi za
Tanzania 36,482/= na Kiwango cha
Umaskini wa Chakula kwa mwezi kwa mtu mzima ni Shilingi za Tanzania 26,085/=.
Kwa kutumia takwimu hizi, matokeo yanaonesha kuwa zaidi ya robo (asilimia 28.2)
ya watu wote waishio Tanzania Bara wako chini ya mstari wa kiwango cha umaskini
wa mahitaji ya msingi na asilimia 9.7 ya watu wote wapo chini ya mstari wa
umaskini wa chakula[4]”.
2.1.
MWENENDO
WA VIWANGO VYA RIBA
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha kupitia
Benki Kuu, inayo wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sera za fedha na sheria
zinazohusu mashirika ya fedha na benki. Jukumu hili huambatana na wajibu wa
kudhibiti mfumuko wa bei (inflation), ambalo wizara imejitahidi kulitekeleza.
Hata hivyo, Wizara
imeshindwa kusimamia viwango vya riba vinavyotozwa na mabenki pamoja na taasisi
za fedha. Wakati mfumuko wa bei umeshuka
toka asilimia 19.8 Disemba 2011 na kufikia asilimia 6 mwezi
Machi 2014, viwango vya riba katika mabenki na asasi za fedha vimeendelea kuwa
vya juu.
Mheshimiwa Spika, riba halisi ‘(real
interest rate)’ ambayo inakadiriwa kama tofauti ya ‘nominal
interest rate’ na ‘inflation rate’ hivi sasa ni kati
ya asilimia 12 – 18. Hakuna shughuli ya kiuchumi ya kawaida unayoweza kuifanya
na kuweza kulipa riba za juu kiasi hiki.
Mwananchi wa
kawaida akiweka akiba yake analipwa riba ‘(saving deposit rate)’ ya asilimia 3
wakati mfumko wa bei wa sasa ni asilimia 6. Hata wakati mfumko wa bei ulipokuwa
asilimia 19.8 riba aliyolipwa mwananchi wa kawaida anayeweka akiba ilikuwa
asilimia 2.9. Mabenki yetu hayampi mwananchi wa kawaida motisha wa kuweka akiba
bali yanambana mjasiriamali kwa kumtoza riba kubwa.
Mheshimiwa Spika,
Riba katika benki na asasi za fedha imeendelea kuwa juu, mojawapo ya sababu ya
kiwango hiki kuwa juu ni Serikali kuwa
mmoja wa wakopaji wakubwa kutoka katika mabenki na asasi za fedha za hapa
nchini. Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania iliyotolewa mwezi Machi 2014 imeainisha
kuwa Serikali imekopa kutoka kwenye vyanzo vya ndani zaidi ya shilingi Trilioni
moja katika kipindi cha Mwezi Machi 2013 hadi Machi 2014. Hali hii imesababisha
ushindani usio wa haki baina ya serikali
na wananchi wanaokopa katika mabenki
hayo (crowding effect). Anayeumia kwa hali hii ya ushindani na serikali
ni mkopaji mdogo.
Mheshimiwa Spika, ukopaji wa
serikali kama ulivyoelezwa hapo juu unachangia kufanya riba ziwe za juu. Riba
inayolipwa na serikali kwa ’Treasury Bills’ ya mwaka mmoja mpaka mwezi Disemba 2013 ilikuwa asilimia
15.63. Kwa mabenki mengi kuwekeza kwenye hatifungani za serikali ‘(treasury
bills and bonds)’ kuna faida kubwa ya uhakika ambapo kumkopesha mjasiriamali wa
kawaida kuna ‘risk’ kubwa ya kutolipwa.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na kuwepo
na mabenki mengi mfumo wetu wa fedha haufanyi
kazi ya kukusanya akiba kwa wingi na kuiwekeza kwa wajasiriamali wandani
ili kukuza uchumi na kuongeza ajira. (Mfumo wa riba upo kwenye Quarterly
Economic Report of March 2014 ya Benki Kuu Table 3.13).
Mheshimiwa Spika, kupungua
kwa riba za benki kutaongeza fursa za kukopa na kusaidia wananchi kukuza
mitaji. Hali hii itasaidia ongezeko la ajira ambalo ni tatizo kubwa sana nchini,
kukua kwa uchumi wa taifa, idadi ya walipa kodi itaongezeka na ustawi wa
wananchi utaimarika.
3. UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA
2013/14
Mheshimiwa Spika, kitendo cha kutenga asilimia 30 ya bajeti toka mwaka 2012
hadi mwaka huu kama fedha za maendeleo, na hili ni kwenda kinyume na matakwa ya
mpango wa maendeleo wa miaka mitano,
kifungu cha 4.5.1 ambacho kinasisitiza kutenga si chini ya asilimia 35 ya
bajeti kuu. Mapungufu haya maana yake ni kwamba tuko nyuma sana katika kufikia
malengo ya millenia.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kwa mara nyingine kukusanya mitaji ya ndani kutoka kwa
watanzania wenyewe kwani miradi mingi ni kwa ajili ya maendeleo yetu na hili
linaondoa dhana nzima ya uchumi inayoitwa “tragedy of the common”
Mheshimiwa Spika, Mpango
wa Serikali wa Maendeleo kwa mwaka 2013/14 ulikuwa ni kuzingatia vipaumbele
vile vile vya mpango wa miaka mitano ambavyo ni:
a. Miundombinu, b. Kilimo, c.
Viwanda vinavyotumia malighafi za ndani, d. Maendeleo ya rasilimali watu na
ujuzi, na mwisho ni e. Uendelezaji wa huduma za utalii, biashara na fedha.
Mheshimiwa Spika, Taarifa
za Serikali zinaonesha kuwa kumekuwepo na mafanikio makubwa katika utekelezaji
wa mpango kwa mwaka wa fedha unaoishia mwezi juni, lakini jambo la ajabu ni
kwamba takwimu za wizara ya fedha zinaonesha kwamba utekeleza wa bajeti kwa
fedha za maendeleo kwa fedha za ndani hadi mwezi Mei fedha zilizotolewa ni
asilimia 52.2 na fedha za nje ni asilimia 39.6 tu. Na hivyo kufanya jumla ya
fedha za maendeleo zilizopatikana kuwa asilimia 46.2 tu.
Mheshimiwa Spika, Hoja ya msingi hapa
kama sekta za kipaumbele kwa mujibu wa mpango zimepewa fedha ambayo haikidhi
kuleta matokeo ambayo yalitarajiwa katika mpango wa miaka mitano pamoja na dira
ya maendeleo ya mwaka 2025. Ufuatao ni mgawo wa fedha za maendeleo kama
zilivyotolewa na Hazina.
Na.
|
Jina la Sekta
|
Asilimia ya fedha za maendeleo
zilizotolewa hadi Mei 2014
|
1.
|
Sekta ya Kilimo
|
73
|
2.
|
Sekta ya Maji
|
26.4
|
3.
|
Sekta Nishati
|
49.1
|
4.
|
Sekta ya Ujenzi
|
56.7
|
5.
|
Sekta ya Uchukuzi
|
42.8
|
6.
|
Sekta ya Viwanda
|
52.1
|
7.
|
Sekta ya
Maliasili na Utalii
|
15.6
|
8.
|
Sekta Elimu
|
39.8
|
9.
|
Sekta ya Afya
|
28.3
|
10.
|
Sekta ya Ardhi
|
21.8
|
Chanzo:
Taarifa ya Waziri wa Fedha-
Mheshimiwa Spika,
Inasikitisha kuona taarifa za serikali zinajaa hadaa kwa wananchi kwa
kuwasilisha takwimu na tathmini zisizo halisi na zenye kudanganya umma. Kwa
ujumla taarifa hizi ama zinalenga kuonyesha mafanikio makubwa yamefikiwa na
serikali katika kutoa huduma kwa jamii au kuonesha kukamilisha miradi ya
maendeleo kwa kiasi kikubwa huku uhalisia ukiwa ni tofauti kabisa na
yanayoandikwa.
Mheshimiwa Spika,
Katika taarifa ya utekelezaji miradi ya maendeleo ya mwaka 2013/14 (uk.8)
inaonekana kuwa katika sekta ya kilimo mafanikio mengi yamepatikana kwa kutaja
mambo yasiyopimika na haswa yasiyo na uhusiano na vipimo vya mafanikio.
a.
KILIMO
Mheshimiwa Spika,
Mafanikio ya sekta ya kilimo hupimwa kwa kuangalia mambo yafuatayo:
·
Uzalishaji katika mazao ya kilimo na
mchango wa uzalishaji huo wa kilimo kwenye pato la Taifa
·
Upatikanaji wa masoko kwa mazao ya
kilimo, bei ya mazao kulingana na faida kwa wakulima na kufikika kwa masoko;
·
Lishe na uhakika wa chakula kwa
familia na Taifa unaotokana na mafanikio ya uzalishaji; na
·
Maboresho ya mbinu na pembejeo za
uzalishaji katika sekta.
Mheshimiwa Spika,
Lakini ukiangalia taarifa za serikali zinaongelea mambo tofauti na ambayo
yanawahadaa wananchi kufikiria kuna mafanikio ambayo kwenye uhalisia hayapo.
Hivi sasa tunashuhudia kuendelea kudorola mchango wa kilimo kwenye pato la
Taifa ambapo sasa ni 4.3 ikilinganishwa na 4.6 mwaka 2008. Ieleweke kwamba
licha ya kilimo kuwa nguzo muhimu katika uchumi wetu na kwamba watanzania
takribani asilimia 80 wanategemea kilimo katika kuendesha shughuli zao za
maendeleo, sekta hii ndio inachangia mchango mdogo zaidi kwa sekta zote
zilizobakia ukiachia Uvuvi unaohujumiwa, ambapo viwanda na Ujenzi vinachangia 7.5% huku sekta ya Huduma
ikichangia 8.2%.
Mheshimiwa Spika, sehemu
kubwa ya bajeti ya maendeleo kwenye sekta ya kilimo kwa miaka kati ya 2010/11
hadi 2013/14 imekuwa inakwenda kwenye idara ya maendeleo ya mazao na kufuatiwa
iliyokuwa idara ya Umwagiliaji na huduma za ufundi. Ni kweli kwamba idara zote
hizi ni muhimu, lakini Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kama fedha hizo
zingelikuwa zinaingizwa moja kwa moja kwenye benki ya kilimo na wakulima kukopa
ni dhahiri kilimo kingekuwa na tija zaidi kuliko ilivyosasa kwani thamani ya
fedha hizo kwenye kilimo haionekani.
Mheshimiwa
Spika, Kilimo ndiyo sekta kiongozi katika kuliingizia
taifa fedha za kigeni na kubwa zaidi ndiyo sekta inayoongoza kwa kutoa ajira.
Hivyo basi ili kukifanya kilimo kuwa na tija zaidi badala ya kuweka motisha za
kikodi kuwaleta wawekezaji kutoka nje ili kuwekeza kwenye kilimo. Kambi Rasmi
ya Upinzani inaona lingekuwa ni jambo bora kwa kuweka mpango wa kutoa mikopo
kwa kuiwezesha benki ya kilimo kufanya kazi na kuwafikia wakulima wengi zaidi
na hivyo uwekezaji katika kilimo ukafanywa na wananchi wenyewe na faida itakayopatikana
itarudi humu nchini tofauti na kama uwekezaji utafanywa na wageni. Hili ni
muhimu sana kwani kutakuwa na “multiplier
effect”kama uwekezaji katika kilimo utajikita hapa hapa.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kama ambavyo imesema
hapo awali kuwa fedha nyingi zinazowekwa kwenye sekta ya mazao kama zitawekwa
kwenye benki ya kilimo ni dhahiri fedha hizo zitatumika kwa tija zaidi na nzuri
zaidi zitarudi na kuingia tena kwenye mzunguko wa kukopesha. Aidha, kwa njia
hii ni dhahiri ajira zitaongezeka mara dufu na itapunguza wimbi la vijana
kuhamia mijini.
Mheshimiwa
Spika, Aidha, mkakati wowote ambao unahusu uwekezaji
katika kilimo ambao hauhusu wakulima wadogo na wa kati maana yake ni kwamba
bado wakulima wadogo wataendelea kuwa ni manamba katika mashamba makubwa ya
wawekezaji ambao ndio mpango wa Serikali ya CCM. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona
kwamba mpango huu utaendeleza mtindo wa kuwapora ardhi wananchi na
kuwamilikisha wageni. Jambo hili siyo haki na linapingwa kwa nguvu zote.
b. ELIMU
Mheshimiwa Spika,
Vivyo hivyo kwenye sekta ya elimu ambako vigezo vya ukuaji na mafanikio ya
elimu vimeachwa huku serikali ikizungumzia mambo ya utekelezaji tu. Vigezo vya
mafanikio ya elimu ni pamoja na Ubora wa Elimu, Ufaulu wa Wanafunzi ikiwa ni
pamoja na kuwa na ujuzi wa kumudu matakwa ya kiwango walichofikia, idadi ya
wahitimu ikilinganishwa na mahitaji ya soko, watoto waliopo, walioandikishwa na
waliomaliza mafunzo. Hata hivyo tungeliweza kuongelea mafanikio kwa kuondoa
kero, lakini taarifa hii hata kero za walimu na ukosefu wa madawati
hazizungumzwi. Hii ni kuwahadaa wananchi na kulidanganya bunge.
Mheshimiwa Spika, Elimu
yetu hasa inayotolewa kwenye shule za Serikali itaendelea kuwa duni sababu ya
uwekezaji mdogo unaofanyika kutokana na ukweli kwamba, sera, sheria na kanuni
zilizowekwa ili kuiendeleza elimu serikali haizifuati, badala yake vigezo hivyo
vinawekwa kwenye shule binafsi. Mfano mzuri ni pale sera inaposema kuwa shule
haitasajliwa hadi iwe na vyoo, viwanja vya michezo, maabara n.k
Mheshimiwa Spika, Ni
shule ngapi za kata zinaanzishwa bila ya kuwepo kwa matakwa hayo ya kisheria?
Huu ni udhaifu unaotokana na ukweli kwamba, Serikali inamiliki shule,
inasimamia shule inatunga mitaala, inatunga mitihani ni kwa vipi serikali iwe
kama mchezaji, mchezeshaji na msimamizi wa mchezo. Ni lazima serikali ikubali
kubakia na jukumu la kusimamia ubora wa elimu na kuruhusu uendeshaji wa elimu
kuchukuliwa na chombo kingine, vinginevyo tutabaki kulalamika miaka yote kuwa “out
put ya elimu ailingani na in put inayowekwa katika elimu”
Mheshimiwa Spika, Ni
muda mwafaka sasa Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kubadili usimamizi
wa Sekta ya elimu kwa serikali kuwa msimamiaji wa ubora wa elimu na sio mtoaji
wa elimu, kwani kufanya hivyo inaua dhana ya ushindani baina ya watoaji wa
elimu. Huu ni upofu wa wataalam wetu au washauri wetu katika sekta ya elimu.
Mheshimiwa Spika,
kumekuwepo na mjadala mkubwa kwamba mashule na vyuo binafsi zinatoza karo kubwa
kiasi kwamba wananchi wenye kipato cha chini hawawezi kusomesha watoto wao
kwenye shule hizo. Hoja ya msingi ni kwanini inakuwa hivyo?
Mheshimiwa Spika,
shule hizo binafsi zinakumbwa na ubaguzi ule ule wa Serikali ambapo shule hizo
zinatakiwa kulipa kodi kadhaa na ili shule hizo ziendelee kuwepo ni lazima
wapandishe karo kwa wanafunzi, na hapo ndipo ughali unapoonekana wazi. Kodi
hizo ni zifuatao:
1.
Corporation tax
2.
Value Added TAX
3.
Skills & Development Levy
4.
Land Rent
5.
Local Government taxes:
a.
Property tax
b.
City Service levies
c.
Tax for sign board
6.
Fire brigade Inspection fees
7.
Work permit fee for teachers
(Wanaotoka nje kwa ajili ya masomo ya sayansi).
c. SEKTA YA NISHATI
Mheshimiwa Spika,
Katika sekta ya nishati serikali ilikuwa na lengo la kuwafikishia umeme asilimia
30 ya wananchi kwa kuwaunganishia umeme watumiaji 150,000 ifikapo Julai 2014.
Huku wizara ikiripoti kuwaunganishia umeme wananchi 70,002 tu, taarifa ya
serikali zinazopigiwa chapuo na Katibu Mkuu wa CCM zinadai kuwafikia asilimia 36
ya wananchi kabla hata ya Julai 2014. Na ili kuona kwamba serikali imepanga kwa
makusudi kabisa kuwahadaa wananchi kupitia takwimu ni pale mhe Steven Wassira
katika taarifa yake ya mpango mwezi Aprili aliainisha wananchi 70,002 tu ndio
waliounganishiwa umeme kati ya July 2013 na Aprili 2014( nah ii ni kwa kipindi
cha miezi 9),lakini kwenye hotuba yake ya 12 Juni 2014 ameainisha kuwa ni
wananchi 138,931 wameunganishiwa umeme, hii inaonyesha ongezeko la wananchi
68,931 ndani ya miezi miwili tu? Huu ni uongo wa wazi kwa wananchi na Bunge
hili huku wakijua kuwa taarifa hizi hazina ukweli wowote. Zaidi ya hapo ni kuwa
hali halisi iliyopo kwa wananchi ni vilio kwa vijiji kutofikiwa na nishati hiyo
huku baadhi ya vijiji vikiwa wameunganishiwa wakaazi wachache tu.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa ya utafiti wa bajeti ya Kaya iliyotolewa mwaka huu
inasema, “Matokeo yameonesha kuwa mwaka 2011/12 asilimia 18 ya kaya za Tanzania
Bara zinaishi katika nyumba zilizounganishwa na umeme wa gridi ya Taifa. Hili ni ongezeko la asilimia 6 ukilinganisha na matokeo
ya mwaka 2007. Nyumba nyingi Maeneo Mengine ya Mjini zimeunganishwa katika
umeme wa gridi ya Taifa kuliko Maeneo ya Vijijini. Utafiti huu pia umebaini
asilimia 68 ya kaya zilizopo Dar es Salaam na asilimia 36 katika Maeneo Mengine
ya Mjini zimeunganishwa katika gridi ya Taifa. Aidha, takribani asilimia 4 ya
kaya za Maeneo ya Vijijini ndizo zilizounganishwa katika umeme wa gridi ya
Taifa[5]”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi inaitaka Serikali ilieleze Bunge na wananchi, kama ni ukweli
kwamba asilimia zaidi ya 75 ya watanzania wanaishi vijijini na kwa mujibu wa
tafiti hizo za idara ya taifa ya takwimu kuwa ni asilimia 4 tu ya wananchi waishio
vijijini ndio waliounganishwa kwa gridi ya Taifa. Je hizo asilimia 36 za maeneo
ya mijini ndio zinazoongelewa na waheshimiwa wanaowakilisha wananchi waishio
vijijini?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani itakuwa haijatenda haki kama haitaomba kupatiwa
majibu katika sakata zima la IPTL, PAP na ESCROW akaunti. Hivyo basi kwa niaba
ya wananchi inahoji yafuatayo:
1. Kosa
la kwanza IPTL haikuweza kukamilisha mradi wake 1995 kwenye kipindi cha dharula
na badala yake ikakamilisha mwaka 1998.
Baada ya kumaliza mwaka1998 IPTL ililalamikiwa na tanesco ICSID kwamba imekuza
gharama za uwekezaji na hivyo kukuza gharama za umeme. Mwaka 2001 uamuzi wa
ICSID ukatoka ikabainika ni kweli IPTL ilikuza gharama kwa kiasi cha dola
27milioni. Serikali ilikuwa na haki ya kupewa fedha zilizokuwa zimelipwa kama
capacity charge.
2. Mwaka 2002 IPTL ikaanza kuiuzia umeme Tanesco
lakini mwaka 2004 Tanesco ikabaini kuwa IPTL ilidanganya kuhusu mtaji. IPTL
ilisema 30% ya mtaji ilikuwa nao kama equity sawa na dola 36milion ambayo ni
shilingi bilioni 36 na kwamba 70% ilikopa. Lakini baada ya ukaguzi ikabainika
kuwa IPTL haikuweka dola 36milion kama equity bali dola 50 ambapo kwa exchange
rate ya wakati huo ya 1:1000, dola50 ilikuwa sawa na Tsh elfu 50 ambazo hata
fundi baiskeli angeweza kuwekeza.
3. Kutokana na kasoro hiyo Tanesco ikataka
gharama ya umeme (tarrif) ishuke kwa sababu bei ilizingatia equity ya tshs bilioni
36 kumbe ni tsh 50000. Mabishano yakaendelea mpaka 2006. Mwaka 2006 Serikali na
Tanesco ikashinikiza ifunguliwe akaunt maalumu (escrow) ili malipo yawekwe huko
mpaka mgogoro utapokwisha kuhusu bei sahihi ndipo pesa hiyo igawanywe kwa
kuzingatia bei sahihi baina ya pande mbili ndio maana ilikuwa kosa kwa Waziri
Mkuu, Mheshimiwa Pinda kusema pesa yote ya escrow eti ni ya IPTL kabla ya
uamuzi kuhusu bei haujafikiwa.
4.
Mwaka 2008 IPTL iliposhindwa
kujiendesha ikawekwa chini ya receivership chini ya RITA ambapo ni RITA ikawa
inasimamia gharama za uendeshaji. Mwaka 2013 September ikatoka hukumu ya
mahakama kuu chini ya Jaji Utamwa ilojichanganya baada ya VIP mwenye 30%
kushtaki na kutaka IPTL iondolewe chini ya receivership na mali zote za IPTL
ipewe kampuni ya PAP ya singasinga anaitwa Sethi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze watanzania ni kwanini ilifungua
ESCROW ACCOUNT kama ilikuwa ni haki kwa IPTL kulipwa capacity charge hiyo?Na kama
kulikuwa na uhalali wa kufunguliwa kwa hiyo akaunti ni kwanini sasa fedha zote
zimelipwa na Serikali kukosa hata shilingi?
Mheshimiwa Spika, Sekta
ya nishati hasa gesi imekuwa ndio
tegemeo la kuitoa nchi yetu katika hali ya umasikini tuliyonayo kwa sasa na
kutusukuma hatua kadhaa mbele. Jambo hili linawezekana ikiwa kutakuwepo na
ubunifu wa mkakati makini na sio mkakati wa kutegemea wawekezaji toka nje kwani
mind set za watawala zimelalia huko, na hawaamini kabisa kama watanzania wazawa
wanaweza kuwekeza katika sekta hii ya gesi.
Mheshimiwa Spika, Kwa
sasa gesi ya kupikia majumbani imekuwa inapanda kila kukicha na fedha za kigeni
zinazotumika kuagiza gesi hiyo nje ya nchi ni nyingi sana. Kambi Rasmi ya
Upinzani inaona lingekuwa ni jambo la busara kama gesi asili inachakatwa na
kujazwa kwenye mitungi kwa ajili ya matumizi ya majumbani badala ya kutegemea
mpango wa TPDC wa kusambaza gesi kwa njia ya mabomba kama mfumo wa maji ulivyo.
Uwekezaji huu unaweza kutuchukua miaka 20 ijayo hadi wananchi kuona manufaa ya
nchi kuwa na gesi.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa jambo hili linawezekana kabisa na watanzania
wanaweza kuwekeza katika viwanda vya ku-“compress gas” na kuiweka kwenye liquid
form na kuijaza kwenye mitungi na kuisambaza kama ambavyo soda au bia
zinasambazwa kwa watumiaji. Mfumo huu utaokoa mabilioni ya fedha za kigeni
zinazotumika kuagiza gesi ya kutumia majumbani na pia utasaidia kuokoa
mazingira yanayoharibika kutokana na ukataji wa mkaa unaotishia maeneo mengi ya
nchi yetu kugeuka jangwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa uwekezaji wa aina hii hauhitaji mtaji kutoka
nje, bali wananchi kwa wingi wao wanaweza kutoa mtaji huu na wao wakawa ni
wanahisa katika uwekezaji huu, kianachotakiwa ni ubunifu wa jinsi ya
kuwashirikisha wananchi katika uwekezaji huu. Faida itabaki hapa hapa nchini
kinyume na ilivyo sasa.
Mheshimiwa Spika,
Katika sekta ya maji, taarifa ya utekelezaji miradi ya maendeleo inaonesha kuwa
serikali imefanikiwa kuongeza kasi ya kuwafikishia huduma za maji safi
wananchi kutoka 300,000 hadi 500,000
hadi watu 2,390,000 kwa miezi sita tu ya utekelezaji bajeti ya 2013/14. Hii
haijalishi kuwa wizara hii hadi kufikia Juni 2014 ilipowasilisha taarifa yake
ya utekelezaji bajeti na kuomba bajeti ya 2014/15 ilikuwa imepatiwa jumla ya
27% tu ya bajeti. Hii maana yake ni kwamba kwa kipindi cha miaka zaidi ya
hamsini ya uhuru watu waliopatiwa maji
safi na salama vijijini ni 500,000 lakini kwa miezi sita tu idadi hiyo
imeongezeka kwa takriban asilimia 260 na kufikia watu 2,390,000. Kwa hali ya
kawaida ni nani anaweza amini miujiza hii?
Mheshimiwa Spika,
Kuhusu utekelezaji wa jumla wa miradi ya maendeleo kulingana na Mpango wa
Maendeleo wa Miaka 5, taarifa ya serikali inaonesha kati ya miradi 80
iliyopangwa kutekelezwa, hadi Aprili 2014 (huu ukiwa ni mwaka wanne wa
utekelezaji mpango) HAKUNA hata mradi mmoja uliokamilika. Kati yake miradi 13
inaendelea vizuri huku minne mingine ikiwa ya kuridhisha, na iliyobaki 63 ikiwa
katika hali isiyoridhisha na au imekwama. Iwapo utekelezaji huu ungewekwa
kwenye GREDI za ufaulu wa kielimu ungekuwa kama ifuatavyo:
Division
I = 0;
Division
II = 13;
Division
III = 4;
Division
IV = 51; na
Division
0 = 12
Je
malengo ya mpango ya 2025 yatafikiwa kwa utekelezaji wenye tathimini
(evaluation) ya kufeli kama nilivyoinisha kwenye gredi za ufaulu.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka huu wa fedha wa 2014/15, mwaka wa mwisho wa utekelezaji Mpango huu,
serikali imeomba jumla ya TShs 5.445 Trilioni kutekeleza ukamilishaji miradi
hiyo huku kukiwa na uhakika kabisa kuwa haiwezi kukamilisha ahadi hizi hewa.
Eneo
jengine la hadaa ni pale serikali inaposhindwa kuwaeleza wananchi na Bunge
sababu za kushindwa kwake. Kwa mfano miradi wa Ujenzi ya barabara za Dumila –
Kilosa na ule wa Dumila – Turiani imekwama kwa zaidi ya mwaka sasa huku matuta
yake yakiota majani na wakandarasi kulalamikia malipo. Hakuna mahala popote
kwenye taarifa hizi serikali inaelezea utekelezaji miradi hii. Miradi kama hii
ipo mingi nchini ambayo hutekelezwa kimyakimya na au kutelekezwa kwa miaka
kadhaa bila ukamilishaji na kuwaacha wananchi kwenye dhiki zaidi kuliko awali.
Mheshimiwa Spika,
ardhi ni kichocheo kimojawapo cha kukuza uchumi na pia chanzo kikuu cha mapato
kama kitatumika vyema. Serikali kwa makusudi imeshindwa kukusanya kodi ya ardhi
kwa nyumba nyingi zilizopo maeneo ya mijini na badala yake imekuwa ikitumia
fedha nyingi kwenda kupima maeneo ambayo wamiliki wake hata hawalipi kodi. Ina
kadiriwa kwamba karibu asilimia kati ya 30 na 60 ya nyumba za mijini hazina
hati jambo linalopelekea kupoteza mapato ya kodi ya ardhi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi inaitaka Serikali kuondoa ukiritimba usiokuwa na maana na kupunguza
gharama za utoaji wa hati za nyumba na viwanja na ikibidi hati zitolewe na
wananchi walipie taratibu huku wakilipa kodi ya ardhi. Tunaamini jambo hili
liko ndani ya uwezo wa mamlaka husika.
Mheshimiwa Spika, kwa kuangalia hali halisi iliyopo kwa wananchi na yale yaliyoandikwa
kwenye nyaraka za Serikali, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba, sababu
zifuatazo ndizo zimepelekea hali hiyo:
- Tunapanga maendeleo yetu kwa kutegemea misaada
au uwezeshaji toka kwa wahisani (Misaada na mikopo 30% +)
- Tunapanga mipango ambayo hatuwezi kuitekeleza.
Miradi mingi inachukua muda zaidi ya muda pangwa na hivyo kuongeza
gharama.
- Miradi mingi ya maendeleo haina uhalisia wa
malengo/mahitaji ya jamii lengwa (Miradi inakuwa si shirikishi na hivyo
utekelezaji wake hauhusishi wananchi).
- Serikali haijatekeleza vipaumbele ilivyoviweka
(Yaani kupanga bajeti yake kulingana na maazimio iliyoridhia).
- Serikali kushindwa kutoa fedha za maendeleo
hata zile zilizopangwa kwenye bajeti yake, kupeleka kiasi ambacho sicho
kilichopangwa kwenye bajeti kwa ajili ya utekelezaji.
- Miradi mingi inayokamilika kutokidhi viwango,
jambo linalosababisha ukarabati wa mara kwa mara kwa muda mfupi.
4. UWEKEZAJI WA PAMOJA KATI YA
SERIKALI NA SEKTA BINAFSI
Mheshimiwa Spika,
Serikali inakosa fedha za kuendesha miradi mikubwa ya maendeleo, aidha kwa
kuwadharau wananchi inadhani wenye mitaji ni lazima watoke nje ya nchi. Hili ni
kosa kubwa sana.
Mheshimiwa Spika,
Kampuni ya Uwekezaji ya Taifa-NICOL iliundwa na wazawa kwa ubunifu wao
wakazunguka nchi nzima kukusanya mtaji kwa watanzania na walifanikiwa mabilioni
ya shilingi kwa ajili ya kufanya uwekezaji. Hoja ni kwanini Serikali inashindwa
kuwaamini watanzania kuwa wawekezaji katika miradi mbalimbali ambayo ni dhahiri
fedha za wananchi zinaweza kurudi haraka? Miradi kama ya reli ambayo mzigo wa
kutoka na kurudi DRC ni wa uhakika, hivyo mtaji kurudi kwa wanahisa ni haraka.
Miradi ya Umeme kwa kutumia maji ya mto Rufiji (Stiglers Gorge). Mtaji wa
Kufufua shirika la Ndege la Tanzania, wakati tuna makampuni mengi ya wazawa
yanayojihusisha na utalii (Tour Operators) na Taasisi zinazojihusisha na Utalii
zilizo chini ya Serikali kama TANAPA, na NGORONGORO CONSERVATION AUTHORITY.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inasema Serikali imechoka kwa kukosa ubunifu wa jinsi
ya kupata mtaji toka ndani ya nchi wakati kuna sheria ya PPP inayoruhusu
uwekezaji wa pamoja na Sekta binafsi ambayo ni wananchi. Tunarudia tena WAZAWA
WANA FEDHA ZA KUTOSHA KUENDESHA NCHI YAO BADALA YA KILA KUKICHA KUKIMBILIA NJE
5. TAKWIMU
Mheshimiwa Spika, Takwimu
ndio hitajio la kwanza katika kupanga mipango na katika kufanya tathmini ya
mipango yako. Hivyo basi katika mkakati wa kukuza uchumi na kuondoa umasikini
tumekuwa tukipatiwa takwimu zinazoonesha kuwa katika yale malengo mbalimbali ya
kupunguza umasikini tuko katika hatua bora na ya kujivunia. Mfano taarifa ya
Mkukuta ilikuwa inaonesha kuwa lile lengo la kuwapatia wananchi maji safi na
salama kwa mwaka 2009 ilikwishafikia asilimia 57.8, lakini baada ya kupitia
upya ikagundulika kwamba ni asilimia 40 tu. Hii maana yake nini? Hii ni hadaa
kwa wananchi na wadau wa maendeleo kwa kutaka kuficha madhaifu au ni kutumia
takwimu zisizo sahihi jambo ambalo linapelekea kupanga mipango ambayo haina
uhalisia na kutunga sera ambazo haziwezi kututoa katika umasikini tulionao
japokuwa fedha zipo lakini matumizi hayaendani na hali halisi.
6. MICHEZO NA SANAA
Mheshimiwa Spika,
kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikipendekeza uendelezaji
wa sekta ya michezo kama mojawapo ya vyanzo vya mapato nchini. Umuhimu wa
Serikali katika kuwekeza kwenye michezo, ni pamoja na kuongeza mapato, kutoa
nafasi za ajira na pia katika kudumisha amani na utamaduni wa Mtanzania.
Shabaha
kubwa ya uendelezaji wa viwanja vya michezo nchini ni katika kuijengea Serikali
uwezo wa kukusanya mapato zaidi. Hii inawezekana kwa Serikali kuwekeza katika
viwanja vya michezo vilivyopo ambavyo vimehodhiwa na chama tawala. Baadhi ya
Viwanja vyenye uwezo wa kuliongezea taifa mapato makubwa ikiwa vitaendelezwa ni
pamoja na uwanja wa Samora-Iringa, Sheikh Amri Abeid- Arusha, CCM Kirumba
–Mwanza, Sokoine-Mbeya na Jamhuri-Dodoma. Kwa uchambuzi wa kina, viwanja hivyo
vya michezo vimejengwa katika maeneo muhimu kishabaha, ambayo yana uwezo wa
kuingizia taifa mapato kutokana na
mwamko wa wananchi hasa katika michezo.
Mheshimiwa Spika,
uwanja wa kisasa wa Benjamin Mkapa maarufu kama uwanja wa Taifa ambao ulijengwa
kwa kushirikiana na Serikali ya China kwa thamani ya Shilingi Bilioni 56.4,
umeweza kuiongezea Serikali mapato kwa kiasi kikubwa kutokana na makusanyo
yanayotokana na mechi za mpira wa miguu pekee. Kwa mujibu wa aliyekuwa Naibu
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Amos Makalla wakati
akijibu swali Bungeni Aprili 2013, alieleza kuwa tangu Uwanja wa Taifa uanze
kutumika mwezi Agosti, 2007 hadi kufikia mwezi Februari mwaka 2013, ulikuwa
umeingiza shilingi 1,533,697,666 kwa makusanyo yanayopitia Wizara ya Habari,
Vijana, Tamaduni na Michezo ambazo hizo ni nje ya mapato yanayokusanywa kupitia
kodi ya ongezeko la thamani (VAT) yanayowasilishwa na Shirikisho la Mpira wa
Miguu nchini (TFF).
Mheshimiwa Spika,
pamoja na kuwa uwanja huu wa kisasa
umeendelea kutumika kwa ajili ya michezo na matamasha mbalimbali, ukusanyaji
wake wa mapato haujaridhisha kutokana na kutokuwepo kwa mfumo wa kielektroniki
wa ukusanyaji wa mapato hali inayochangia ukusanyaji hafifu wa mapato na mianya
ya ubadhirifu unaotokana na kutokuwepo
kwa ufuatiliaji wa kiteknolojia.
Kambi
rasmi ya Upinzani, inapendekeza yafuatayo yafanyike ili kuweza kutumia sekta ya
michezo kwa kupitia ujenzi wa viwanja vya kisasa vya michezo nchini na kuongeza
ukusanyaji wa mapato;
Mosi,
kuvirejesha viwanja vyote vya michezo vilivyohodhiwa na Chama cha Mapinduzi kwa
Serikali ili viwe mali ya umma kama ambavyo viliwahi kuwa chini ya Baba wa
Taifa,
Pili,
kuviendeleza viwanja hivi kwa kuingia ubia na makampuni makubwa ya uwekezaji
ama na nchi wahisani ili kurejesha hadhi ya viwanja vitakavyoendana na mahitaji
ya kisasa ya viwango na ubora wa viwanja vya michezo
Tatu,
kuhakikisha kuwa uwanja wa Taifa hautumiki katika michezo ya aina yoyote bila
ya mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato ili kuzuia ubadhirifu
wa mapato katika mechi mbalimbali unaofanywa na watendaji wasiowaaminifu.
Nne,
kupunguza misamaha ya kodi katika makampuni makubwa na kwa walipa kodi wakubwa
na fedha hizo zitumike kuboresha baadhi ya viwanja ili kuinua uchumi na kutoa
fursa za ajira zitakazotokana na uwekezaji wa viwanja nchini.
Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kufuta misamaha ya kodi
ambayo kwa mwaka 2013/2014 ilifikia trilioni 1.5, ambapo kwa gharama ya
shilingi bilioni 56.4 zilizotumika kujenga uwanja wa taifa , misamaha hiyo ya
kodi ya trilioni 11.5 zingeweza kujenga viwanja 27 vya kisasa nchini, 25 kwa
mikoa yote ya Tanzania Bara na viwanja viwili vya kisasa Zanzibar.
6.1. UENDELEZAJI WA SEKTA YA SANAA
NCHINI
Mheshimiwa Spika,
lengo la kuendeleza sanaa nchini ni kuongeza nafasi za ajira pamoja na kuongeza
vipato ili kukuza uchumi nchini. Sanaa
ikipewa kipaumble pamoja na kurasimishwa ina uwezo wa kuliongezea taifa mapato
yatokanayo na kazi za wasanii kama ilivyo kwa soko la filamu nchini Nigeria.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Nigeria imetangazwa kuwa ndilo Taifa lenye uchumi
mkubwa barani Africa na kuipita Afrika Kusini. Pato Ghafi la Ndani (Gross Domestic Product ‘GDP’) la
Nigeria limefikia Dola Billion 509 huku lile la Afrika ya Kusini likifikia Dola
Bilioni 322. Kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya Nigeria, Nigeria imekuwa Taifa
lenye uchumi mkubwa Afrika baada ya wanauchumi wa nchi hiyo kuziongeza sekta za
Mawasiliano na Filamu (Nollywood) kwenye takwimu. Ni dhahiri kuwa soko la Filamu
la Nigeria linatoa mchango mkubwa mno katika ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.
Kabla ya hapo Nigeria ilionekana kama taifa linalotegemea zaidi uuzaji wa
mafuta na ilikadiriwa kuwa pato la mafuta lilichangia asilimia 32 kwenye GDP
lakini ripoti ya wanauchumi hivi karibuni imeonesha sasa pato la mafuta
huchangia Asilimia 15 tu ya pato ghafi la ndani. Nollywood ndiyo
sekta ya pili kwa kutoa ajira katika nchi ya Nigeria baada ya sekta ya
kilimo, na mchango wake kwa Taifa ni mkubwa sana kwani ina thamani ya Naira
bilioni 853.9 (Dola za Marekani bilioni 5.1). Hii ni ishara ya jinsi gani sekta
ya filamu inavyoweza kukuza na kubadili uchumi wa nchi yoyote, kwa njia ya
utoaji wa ajira kama itachukuliwa kwa umakini mkubwa. Matokeo ya
kukubalika kwa sinema pia huwafanya watayarishaji wa sinema, waigizaji na
watendaji wengine kuwa na heshima kwenye jamii na hata kisiasa.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa sekta ya filamu ikiwa ni mojawapo ya kazi za sanaa ina
umuhimu mkubwa katika kubadilisha sera za kiuchumi kuliko sasa ambapo Serikali
inawatumia wasanii wa filamu kama daraja lao la kutimiza malengo ya kisiasa na
si katika kuiboresha tasnia nzima ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi. Mojawapo ya
mafanikio ambayo Serikali ya CCM imekua ikiyafanya wimbo ni pamoja na kulinda haki
za wasanii na kazi zao, wakati huo huo Serikali hii imeshindwa kuandaa Sera ya
Sanaa itakayorasimisha sekta hii katika mfumo wa kiuchumi. Aidha, Serikali
haina takwimu za uhalisia wala utafiti
wowote uliofanywa kuijua nguvu ya soko la sanaa nchini, hakuna miundombinu ya
soko la sanaa, wala thamani ya mchango wa sekta hii katika uchumi wa taifa
hautambuliwi ipasavyo. Kukosekana kwa hayo yote ni dhahiri kuwa kazi za sanaa
hazilindwi, hazikuzwi, hazitangazwi, hazitambuliki na wala hazipewi umuhimu
unaostahili kama ambavyo sekta iliyo rasmi inavyopaswa kuwa. Serikali
imeshindwa kuitilia maanani, kuchukua hatua stahiki, kutoa takwimu halisi za
mchango wa sekta hii kwenye uchumi wa taifa pamoja na ukuaji wa kasi wa sekta
hii hali inayosababisha ishindwe kupata pato halisi linalotokana na sekta hii.
Mheshimiwa Spika, Shughuli nyingi zinafanyika kiholela bila wahusika kuwa na hakimiliki na
sehemu kubwa ya mchango wake kwa pato la taifa haijarekodiwa katika vitabu vya
mapato vya taifa. Hii inaonesha kuwa mchango wa sekta hii katika pato la taifa
ni mkubwa zaidi kuliko takwimu zinavyoonyesha. Ili kama Taifa, tuweze kupiga
hatua na kuimarisha sekta ya hakimiliki ni lazima sasa serikali iache porojo za
kuwaongopea wasanii kuwa wanautambua mchango wao, bali ielekeze nguvu kuhakikisha kuwa sera
madhubuti za kusimamia sekta ya sanaa nchini zinatungwa pamoja na sheria na kanuni zinazostahiki ili kuboresha
uendeshaji wa sekta hii nchini. Uwepo wa sera bora zitachochea maendeleo ya kisekta,
mazingira ya ubunifu yenye ushindani na salama ambayo serikali itayatumia
kuendeleza sekta hii na kutambua thamani ya kazi za ubunifu.
Mheshimiwa Spika, sekta ya hakimiliki nchini mwaka 2009 ilichangia kiasi cha Sh676 bilioni
sawa na asilimia 4.6 ya Pato la Taifa (GDP), likiwa ni zaidi katika uchumi wa
taifa kuliko sekta ya hoteli, migahawa na madini. Taarifa hiyo ambayo imetolewa
hivi karibuni kwa lugha ya Kiingereza ikiwa na jina: ‘The Economic Contribution
of Copyright-Based Industries’ kwa mwaka 2012, imebainisha kwamba sekta ya madini
imechangia asilimia 2.6 ya GDP wakati hoteli na migahawa imechangia asilimia
4.5, sekta ya hakimiliki imefanya vyema. Pia sekta hii imeajiri watu wengi
zaidi ya wale walioajiriwa na sekta ya afya na ustawi wa jamii, fedha, majumba
ya kukodisha, huduma za biashara, ujenzi, usafirishaji, mawasiliano, madini,
umeme, gesi na sekta ya maji. Mchango wa sekta ya hakimiliki kwa malipo ya
wafanyakazi, ulikuwa Sh 80.474 bilioni sawa na asilimia 5.
Aidha, nchi kadhaa ambazo sasa zimeendelea zilikuwa na
uchumi sawa na Tanganyika (sasa
Tanzania) wakati tukipata uhuru mwaka 1961, nchi hizo ni pamoja na Singapore,
Korea Kusini, Thailand, Malaysia na kadhalika, ila kilichowafanya kutuacha
kimaendeleo na kupata maendeleo ya haraka ni ulinzi na uendelezaji wa Miliki
Bunifu katika kazi za sanaa. Leo hii Korea Kusini imekuwa ni Taifa kubwa na
lenye mchango katika kazi za sanaa Barani Asia kwa sababu tu ya kulitambua
kundi la wasanii na kuweka mazingira mazuri ya ulinzi wa Miliki Bunifu kiasi
cha kubatizwa jina la Marekani ya Asia. Korea imefanikiwa sana kueneza
utamaduni wake katika nchi zingine za Asia, na walitumia fursa ya mtikisiko wa
kiuchumi uliozikumba nchi za Asia mwaka 1997, ambapo wao waliamua kuwekeza
katika sanaa na utamaduni kwa lengo la kuzalisha na kuuza nje kama bidhaa. Hata
Rais wa wakati huo, Kim Dae-jung, alipenda kujiita Rais wa Utamaduni na
alianzisha mradi huo na kutenga dola za Kimarekani milioni 148.5. Leo hii,
Tanzania inashindwa nini katika kuirasimisha sanaa ambayo CCM inaitumia
kujipatia kura?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, inaelekeza nguvu zake za kuhakikisha kuwa muswada
wa Sera ya sanaa unaletwa Bungeni ili kufanikisha utungaji wa Sheria na Kanuni
utakaongoza kazi mbalimbali za sanaa nchini ili kuweza kuongeza fursa za ajira
na ukusanyaji wa mapato kwa taifa zima kwa ujumla.
7. MAENEO
YA KIPAUMBELE KATIKA MWAKA WA 2014/15
Mheshimiwa Spika, taarifa
ya mpango huu umeainisha maeneo ya kitaifa ya kimkakati kwa mwaka wa 2014/15
ambayo ni miundombinu, kilimo, viwanda, maendeleo ya rasilimali watu, huduma za
fedha na utalii huku maeneo mengine
muhimu kwa ukuaji wa uchumi yakiwa ni elimu/mafunzo ya ufundi, afya na
ustawi wa jamii, mifugo na uvuvi, misitu na wanyamapori ,madini, ardhi, nyumba
na makazi, usafiri wa anga, hali ya hewa, biashara na masoko, ushirikiano wa
kikanda na kimataifa, utawala bora, vitambulisho vya taifa, sensa ya watu na
makazi, kazi na ajira pamoja na mazingira.
8.
REAL ESTATE REGULATORY AUTHORITY
Mheshimiwa Spika, katika ushauri wetu kwa bajeti ya mpango iliyopita
tuliitaka Serikali kuanzisha mamlaka ya kudhibiti sekta hii kwani fedha nyingi
za kodi ya majengo na kodi ya ardhi (Property tax and Land Rent) hazikusanywi
na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
Mheshimiwa
Spika, kuanzishwa kwa
mamlaka hii ni dhahiri kodi itakusanywa kulingana na ardhi ilipo katika miji na
majiji (land value depend on location). Ni ukweli kwamba tumekuwa tukikosa
mapato mengi sana kutokana na kukosekana kwa mdhibiti katika sekta hii ya ardhi
yenye majengo.
9.
KUKUZA UCHUMI VIJIJINI (Rural growth)
Mheshimiwa Spika, kukuza
uchumi vijiji ni kipaumbele cha kwanza kwa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa miaka
kadhaa iliyopita na kitaendelea kuwa kipaumbele chetu. Kambi Rasmi ya Upinzani
inaamini kuwa kama mkatakati utawekwa kwa kila Halmashauri za vijijiji za
kutengeneza mazingira ya kutoa ajira rasmi zipatazo mia tano kila mwaka basi
zitakuwa zimepiga hatua kukabiliana na wimbi kubwa la vijana kukimbilia mijini
kwa ajili ya kutafuta ajira.
Mheshimiwa Spika,
kwa kuwa mazingira ya vijijini yanatofautiana na kwa kuwa rasilimali zilizo katika maeneo ya
wilaya za vijijini zinatafoutiana pia kati ya wilaya na wilaya, hivyo basi
Serikali kuu inatakiwa kuweka kiwango
mkakati (threshold) cha maendeleo kinachotakiwa kufikiwa na kila Wilaya kulingana
na fedha zilizotengwa kwa ajili kukuza uchumi vijijini.
Mheshimiwa Spika,
kwa njia hii, mabadiliko ya kimaendeleo yataonekana zaidi kuanzisha mifuko ya
uwezeshaji ambayo wanafaikaji ni wale
waishio mijini zaidi na kwa upande wa wilayani ni wale wenye uwezo tayari.
Mheshimiwa Spika,
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imeainisha maeneo yafuatayo kama vipaumbele vya
Mpango wa Taifa wa Maendeleo:
- Kukuza Uchumi Vijijini
- Miundombinu
na Usafiri wa anga
3.
Ardhi, Nyumba na Makaazi
4.
Elimu na Afya
5.
Michezo na Sanaa
10. UGHARAMIAJI WA MPANGO
Mheshimiwa Spika,
mpango wa maendeleo wa serikali
kwa mwaka 2014/2015 ni dira ya kuakisi mpango wa kibajeti kwa mwaka 2014/2015, na ili kuweza kutekeleza mpango
kwa ufanisi ni dhahiri kuwepo kwa
umuhimu wa kubainisha vyanzo vya mapato vya uhakika ambavyo vitawezesha
kugharimia miradi ya maendeleo inayokusudiwa, kuna haja ya serikali sasa
kutafakari kwa kina na kuona kazi
kubwa inayofanywa na kambi rasmi
ya upinzani bungeni kuishauri serikali juu ya uongezaji wa mapato ya ndani ili
kupunguza utegemezi wa kibajeti kila mwaka
inaweza kuijengea heshma nchi yetu na pia kuboresha huduma kwa wananchi
wake na si kwa kutegemea mapato ya nje ambayo yameendelea kuidhoofisha nchi
yetu mbele ya uso wa dunia kwa kuwa taifa tegemezi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, inapendekeza
kukusanya
mapato ya ndani 25% ya GDP ili kuweza
kuendesha miradi yetu wenyewe. Uwezo wa makusanyo hadi kufikia hapo tunao, kwanza
ni kupambana na makampuni makubwa ya kimataifa ili yalipe kodi stahiki na
kuacha ujanja wa kukwepa kodi, kuondoa misamaha ya kodi na kuzuia upoteaji
mapato ya ndani, Kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi wa kada zote kulipa kodi kwa kuwawekea mazingira wezeshi
na aminisho ya matumizi ya kodi zao. Ni dhahiri kuwa mapato ya
ndani yaweza kutekeleza vipaumbele vyetu ili kukabiliana na matatizo tuliyoainisha.
Mheshimiwa Spika, katika miaka kadhaa
kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa nia njema ya kuijenga nchi yetu
ilipendekeza mambo kadhaa ili kuweza
kuongeza mapato ya serikali na moja ya mambo yaliyopendekezwa ni kuhakikisha kwamba serikali inakusanya kodi kwa
kiwango cha asilimia 30 kama ‘ongezeko la mtaji’ (‘capital gains’) kutokana na
mauziano ya Kampuni yoyote ambayo mali zake zipo Tanzania. Je, utekelezaji wa ushauri huo umefika wapi?
Mheshimiwa Spika,
lakini pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kupunguza misamaha ya
kodi hadi kufikia asilimia moja ya pato la Taifa kama wenzetu wa Uganda na
Kenya. Serikali ilikubaliana na pendekezo hili kwa maneno lakini imeshindwa
kulitekeleza licha ya kutoa ahadi za kufanya hivyo kila mwaka. Hivi sasa misamaha ya kodi imefikia asilimia 4.1 ya Pato
la Taifa.
Mheshimiwa Spika, bajeti mbadala itatoa mgawanyo wa fedha kwa vipaumbele
hivyo katika utekelezaji wake.
11.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi yenye wachumi wazuri na waliobobea na
ukweli ni kwamba nchi jirani zimekuwa zikipanga mipango yake kwa kutumia
wataalam wetu. Ni ukweli kwamba mipango ya hao wanaotumia mipango na wataalam
wetu wameendelea kuliko sisi. Hoja kubwa ya kujiuliza ni kwanini kama mipango
mizuri tunayo na wataalam tunao mambo hayaonekani kuwa yanasonga mbele?
Mheshimiwa Spika, tatizo la msingi hapa ni kuwa nchi zilizoendelea uchumi
ndio unatakiwa kuongoza mfumo wa siasa, lakini kwetu sisi siasa ndio inaongoza mfumo
wa uchumi kwa maana mipango yetu inapangwa kwa kuangalia zaidi matakwa ya
kisiasa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kujikita zaidi kwenye
kutekeleza mpango na sio kwenda kwa matakwa ya viongozi wa kisiasa kama
inavyofanya hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, Mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa, ni aibu kubwa kwa nchi
makini na tajiri kama Tanzania kuendelea kupangisha ofisi kwa ajili ya mabalozi
wake nje ya nchi wakati nchi inamiliki viwanja katika mataifa hayo, Serikali
pia imeendelea kupanga nyumba za watumishi na maofisi kwa gharama za juu. Aidha,
katika hilo ni kwa vipi nchi makini inauza nyumba za watumishi wake hasa madaktari na kuwapatia viwanja vya
kujenga nyumba zao maeneo ya mbali na sehemu wanazotolea huduma. Hii ndiyo
mipango ya Serikali ya CCM au ni wizi wa viongozi Serikali? Hujuma hizi kwa
taifa zinazofanywa na Mawaziri waliopewa dhamana ya kusimamia raslimali za
watanzania lakini wanashindwa, Kambi Rasmi ya Upinzani inawataka Mawaziri
wahusika wajipime kama kweli bado wanafaa kuendelea kuwa watumishi wa wananchi.
Mheshimiwa Spika, katika mazingira tatanishi kama haya ni lini tunaweza
kujitapa kuwa tunafikia malengo ya milenia?
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya kambi Rasmi ya
Upinzani, naomba kuwasilisha.
……………….
Esther Nicholas Matiko(Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani- Ofisi ya Rais
Mahusiano na Uratibu
16.06.2014
No comments:
Post a Comment