Sunday, May 4, 2014

UKAWA: Tumeungana kujenga serikali imara

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umefafanua hoja ya kuanzisha ushirikiano katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ni kujenga serikali imara yenye kuheshimu matakwa ya wananchi.
UKAWA inaundwa na vyama vinavyounga mkono rasimu ya katiba ya serikali tatu iliyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba ambavyo ni CUF, CHADEMA, NCCR- Mageuzi, UDP, DP na vyama vingine ambavyo wajumbe wake walisusia Bunge la Katiba.
Mwishoni mwa wiki iliyopita wakiwa katika mikutano ya hadhara visiwani Zanzibar, baadhi ya viongozi wa UKAWA walikaririwa na vyombo vya habari kwamba wanakusudia kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi mkuu mwakani kuanzia udiwani, uwakilishi, ubunge na urais.
Akifafanua sababu za UKAWA kuingiza ajenda nyingine ya kutaka kushirikiana katika uchaguzi mkuu wa mwakani, Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema wamefanya hivyo ili mamlaka ambazo ni serikali na Bunge ziweze kuheshimu matakwa ya wananchi.
Profesa Lipumba alisema ili kuhakikisha mamlaka hizo zinatekeleza wajibu wake, zitasukumwa na UKAWA ambayo ilibaini makosa yake hapo awali na sasa imekuja kwa lengo moja la kuwatetea wananchi na kuwatimizia yale wayatakayo katika katiba na siasa.
“UKAWA haijaja kwa maswala mengine, imekuja ili ipatikane serikali imara yenye Bunge lenye kuheshimu matakwa ya wananchi… ndiyo maana tunataka kuhakikisha suala la katiba na uchaguzi vinakwenda sambamba,” alisema Profesa Lipumba.
Wakati huo huo, CUF imebariki suala la kuanzishwa kwa UKAWA na kueleza kuwa hoja zilizotolewa kwa ajili ya kuanzishwa umoja huo zina maslahi kwa wannachi na taifa kwa jumla.
Msimamo huo umetolewa na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho linaloendelea na vikao vyake jijini Dar es Salaam kwa siku tatu hadi kesho likiwa na ajenda mbili.
Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu wa CUF, Abdul Kambaya, alisema ajenda zinazojadiliwa katika mkutano huo ni kuhusu kuanzishwa kwa UKAWA na madhumuni yake pamoja na namna watakavyofanya uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Kambaya alisema wakiwa katika ajenda ya kwanza iliyohusu UKAWA ambayo ilitolewa kama taarifa na viongozi wake, ilipokelewa kwa furaha na kuwataka waendelee na msimamo huo wenye maslahi kwa wananchi na taifa.
“Pamoja na kuwataka waendelee na msimamo huo, tumewaonya wajumbe wote wa UKAWA na wajumbe wengine 201 wanaounga mkono rasimu ya Jaji Warioba kutokubali kuyumbishwa na wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wana msimamo wao.
“Nafikiri sasa viongozi wetu wa juu wamejifunza kutokana na makosa… sasa hawataki kurudia makosa na katika kufanya hivyo, naiona CCM iking’oka madarakani, wagombea udiwani, uwakilishi na ubunge katika nafasi ya UKAWA wakishinda kwa ushindi mkubwa,” alisema Kambaya.

No comments:

Post a Comment