Saturday, May 17, 2014

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, MHE.GODBLESS JONATHAN LEMA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2013/2014 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015.

UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa ‘Instrument’ ya Serikali inayoainisha majukumu kila Wizara, Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi imepewa majukumu ya kushughulikia masuala ya Usalama wa Raia, Uhamiaji na utekelezaji wa Sera za zima moto na uokoaji. Aidha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inashugulikia pia masuala ya huduma za Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji, Uraia, Vitambulisho vya Taifa, Huduma za Wakimbizi, Usajili wa Vikundi au Vyama vya Kijamii, Huduma za Zima Moto na Uokoaji na mambo mengine yanayohusu maendeleo ya rasilimali watu katika Wizara hiyo.

Mheshimiwa Spika,
Ukitazama majukumu ya Wizara hii, utaona kwamba ina majukumu mazito sana yanayohusu usalama wetu sote kama raia wa nchi hii. Ni majukumu yanayohusu maisha yetu. Hivyo wizara hii inatakiwa iwezeshwe sana kibajeti ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili wananchi na hata wageni waliopo katika nchi yetu waweze kuishi kwa usalama na amani.  Kwa kuwa Wizara hii ina taasisi chini yake  zinazohusika na ulinzi wa  maisha ya watu na mali zao, hivyo ni Wizara inayotakiwa kufuatiliwa na kusimamiwa kwa karibu sana.

  1. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2013/2014
Mheshimiwa Spika,
Katika bajeti ya Wizara hii kwa  mwaka wa fedha unaomalizika wa 2013/2014 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliitaka Serikali kufanya mambo kadhaa ili kuboresha mapungufu  tuliyoyaona katika katika kipindi hicho. Mambo hayo ni:
                           i.            Kuchukua hatua kali na madhubuti ya kukabiliana na matukio yenye sura ya ugaidi kwa mfano kulipuliwa kwa bomu  Kanisa Katoliki katika Parokia ya  Olasiti huko Arusha, kuchomwa moto kwa makanisa huko Zanzibar na Dar es Salaam,  Mapadre kuuwawa na Mashehe kumwagiwa tindikali Arusha na  Zanzibar  na matukio yanayofanana na hayo.
                         ii.            Kuongeza posho ya chakula (Ration allowance) kwa askari wa Jeshi la Polisi ili walau posho hiyo ishabihiane na posho ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)   ili waweze kukabiliana na ugumu wa maisha. Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za bunge (hansard) Waziri wa Fedha wa wakati huo Marehemu William Mgimwa alikubali posho ya chakula ya shilingi 225,000/= kwa mwezi kwa kila askari. Taarifa tulizo nazo ni kwamba posho hiyo haijalipwa mpaka leo. Je, askari waandike deni au wahesabu kwamba wamedhulimiwa?
                       iii.            Kutoa mwongozo kwa maafisa wa Jeshil la Polisi na Magereza juu ya marekebisho ya sheria kuhusu umri wao wa kustaafu ambapo marekebisho ya sheria yaliongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 50 kwenda miaka 55 kwa maafisa wa Polisi na kutoka miaka 55 kwenda miaka  60 kwa akari wa Magereza.
                       iv.            Kuondoa urasimu na utaratibu kandamizi katika Jeshi la Magereza kuhusu Mpango wa kujiendeleza kielimu kwa maafisa wa Magereza. Tuliitaka Serikali kufanya hivyo kwa kuwa, kwa mujibu wa General Service Order (GSO) na sheria nyingine za kazi, mtu akiajiriwa kwa mara ya kwanza (first appointment) na akataka kujiendeleza kimasomo nje ya kituo chake cha  kazi anatakiwa kukaa kazini kwa muda wa miaka miwili au mitatu ndipo aweze kuomba ruhusa ya kwenda masomoni. Lakinini tulipokea malalamiko kutoka kwa maafisa wa Magereza kwamba sheria hiyo haifuatwi na badala yake maafisa hao wanatakiwa wakae miaka sita kazini ndipo wapewe kibali cha kujiendeleza kimasomo.
                         v.            Kujenga nyumba za Askari wa Magereza ili kuboresha mazingira yao ya kazi na kuwafanya wasijisikie kama vile na wao ni wafungwa.
                       vi.            Kuchukua hatua ya kupunguza msongamano wa wafungwa  na mahabusu Magerezaji
                     vii.            Kuboresha lishe na huduma za afya kwa Wafungwa na Mahabusu Magerezani
                   viii.            Kuongeza fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya zima moto na uokoaji kwa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji
                       ix.            Kuwachukulia hatua askari wa Jeshi la Polisi wenye vyeo vya juu wanaowanyanyasa askari wa vyeo vya chini.
                         x.            Kuacha kulitumia Jeshi la Polisi vibaya  kwa ajili ya kulinda maslahi ya kisiasa ya CCM
                       xi.            Kuwachulia hatua kali za kisheria viongozi wa Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali waliotoa kauli za vitisho kwa waandishi wa habari walioandika habari za unyanyasaji unaofanywa na Jeshi la Polisi
                     xii.            Kutoa ukomo wa muda ambapo kila raia wa Tanzania atapatiwa Kitambulisho chake cha Taifa na kuainisha ghrama zilizotumika katika mchakato wa kutengeneza vitambulisho vya Taifa.
                   xiii.            ,Kudhibiti kuzagaa kwa silaha za moto ambazo hutumika katika matukio mengi ya kijambazi.
                   xiv.            Kuchukua hatua kali kwa watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya hapa nchini
                     xv.            Kuchukua hatua madhubuti za kupunguza matukio ya ajali barabarani ambayo yamepoteza maisha ya wananchi wengi sana wakiwemo polisi pia.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa taarifa ya utekelezaji wa masuala niliyoyataja hivi punde wakati wa majumuisho ya bajeti ya Wizara hii.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Randama ya Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi fungu 51 na randama za taasisi zilizoko chini yake yaani Fungu 93(Idara ya Uhamiaji); fungu 28(Jesh la Polisi); fungu 29 (Magereza) na fungu 14 (Idara ya Zima Moto) hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Wizara na taasisi zilipata mgawo wake wa kibajeti kwa wastani wa asilimia 70 isipokuwa idara ya zima moto na uokoaji ambayo ilipata asilimia 46.3 tu ya fedha zilizoidhinishwa. Aidha kwa Mujibu wa Randama ya Jeshi la Zimamoto, fungu 14 (uk. 2) katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14 hakuna fedha yoyote iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa Jeshi la Zima Moto.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Randama hiyo, huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kutotengewa fedha kwa ajili ya miradi ya Maendeleo. Kutokana na hali hiyo, Jeshi hilo limeshindwa kuendeleza ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makao Makuu – TAZARA, Dar es Salaam, kushindwa kukarabati na kujenga vituo vipya vya zimamoto, kushindwa kununua vitendea kazi mbalimbali ikiwemo vifaa vya maokozi na vifaa vya kuzimia moto.

Mheshimiwa Spika,
Sote ni mashahidi wa majanga ya moto, maghorofa kuporomoka, meli kuzama, mafuriko na kila aina ya majanga ambapo idara ya zima moto imekuwa ikishindwa kufanya chochote na hivyo kuwaacha wananchi wakiangamia katika majanga hayo.  Kambi Rasmi ya Upinzani inashawishika kuamini kwamba Serikali haina nia njema na usalama wa raia na ndio maana haitengi fedha hata senti moja katika miradi ya maendeleo ya Jeshi la Zima Moto. Kama Serikali haioni umuhimu wa Jeshi la Zima Moto ni bora kulifuta kuliko kuliacha wakati hailiwezeshi kufanya kazi yake.

Endelea........



  1. HALI YA USALAMA NCHINI .
Mheshimiwa  Spika ,
Hali ya Usalama Nchini imeendelea kuwa tete kutokana na sababu mbalimbali. Utafiti wa kiufuatiliaji uliofanywa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kwamba; sababu zifuatazo zinazorotesha hali ya usalama na amani hapa nchini.

                                                   i.            Ukosefu wa Ajira na Kazi zenye Kipato kwa Jamii.
Mheshimiwa Spika,
 Ukosefu wa kazi na ajira kwa Jamii umekuwa ni sababu moja ya msingi kabisa ya kuendelea kuhatarisha hali ya usalama na amani Nchini. Wananchi wengi hususan Vijana wamekuwa hawana uhakika wa ajira.  Mbali na hofu na wasiwasi mkubwa walio nao, vijana hawa kutokana na kutojua hatima ya maisha yao, bado Serikali imeendelea kuwasakama katika shughuli zao ndogo ndogo. Kitendo cha Serikali kuwafukuza mijini vijana wajasiriamali wanaofanya biashara ndogondogo kumesababisha vijana hawa kushindwa kabisa kuweza kumudu hata mlo mmoja kwa siku. Jambo hili limewakatisha tamaa vijana wengi na matokeo yake ni kwamba baadhi yao wanajiingiza katika matukio ya kihalifu ili waweze kumudu maisha yao.

Mheshimiwa  Spika,
Ili kujenga mazingira ya usalama, amani na utulivu katika nchi yetu, ni lazima sasa Serikali itambue wajibu wake wa kukuza uchumi na biashara kwa kasi ili kuongeza ajira na kazi zenye tija kwa jamii   kwani kuachia  Jeshi la Polisi kudhibiti hali ya ulinzi na usalama katika Taifa ambalo asilimia 80% ya Vijana wake wanarandaranda mitaani bila kuwa na kazi zenye uwezo wa kukidhi mahitaji  yao muhimu ni hatari kubwa sio tu kwa walinzi hawa wa amani bali pia kwa taifa zima.
Mheshimiwa  Spika,
 Hivyo ni muhimu tukafahamu kwamba propaganda na tathimini  feki kuhusu ukuaji wa uchumi zinazotelewa kila mwaka na  Serikali wakati Watu wengi wanaendelea kuishi maisha yasiyo na matumaini na wengine wakishindwa kufurahia ajira na kazi  kwa sababu ya masilahi duni na mfumuko wa bei za bidhaa unaosababishwa na uchumi kushuka kila mwaka, bila shaka sasa ni kweli kabisa kuwa hali ya usalama Tanzania ni tete na Jeshi Polisi  haliwezi kujipanga kushindana na kundi kubwa la jamii iliyojaa hasira na kupoteza matumaini  na maisha .

                                                 ii.            Maslahi ya Askari wetu katika Muktadha wa Hali ya Usalama Nchini.
Mheshimiwa Spika,
 Maisha ya Askari wa Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto ni miongoni mwa kundi katika jamii ambalo linaishi maisha ya umasikini wa kupindukia sana. Nyumba zao, mishahara yao na masilahi yao mengine mbali mbali  bado ni duni kiasi kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa ni  kebehi na dharau  kubwa sana  kwa vikosi vya ulinzi na usalama .

Mheshimiwa Spika,
 Kazi ya Jeshi ni wito. Ni hatari kubwa sana kuwa na Askari ambao wanafanya kazi bila wito kwa sababu walikosa matumaini kwingineko, hivyo wakachagua kujiunga na Jeshi kama sehemu ya biashara.

Mheshimiwa Spika,
Ni ukweli usiopingika kuwa Askari wengi wanafanya kazi kwa moyo uliovunjika na kupondeka. Aidha, wana msongo mkubwa wa mawazo sababu ya ugumu wa maisha. Hali hii  inaondoa uimara wa majeshi yetu haya kwani Jeshi imara sio tu  kuwa na silaha za kisasa peke yake  bali ni muhimu pia kuwa na askari wanaoona fahari kulinda raia na mali zao kama wajibu uliotukuka. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutambua na kuthamini kazi inayofanywa na askari wetu ambao ni sehemu ndogo ya jamii iliyojitoa mhanga kufanya kazi za hatari hata kwa maisha yao ili kuwalinda raia na mali zao

                                               iii.            Rushwa na Uadilifu kwa Jeshi la Polisi
Mheshimiwa Spika,
Jeshi la Polisi limekuwa likitajwa kuwa kinara wa rushwa na chanzo cha biashara nyingi haramu. Jambo hili zio zuri hata kidogo kwa chombo kilichokabidhiwa jukumu la kuwalinda raia na mali zao. Hata hivyo, tafiti nyingi zinaonesha kwamba mazingira mabaya ya maisha yao yaliyojengwa katika maslahi duni  ni miongoni mwa sababu zinazowasababisha kuingia katika tabia hii mbaya ambayo ni hatari kwa usalama wa Nchi .

Mheshimiwa Spika
Rushwa ndani ya Majeshi yetu ya ulinzi na usalama  ni majaribu  yanayo sababishwa na Serikali yetu. Hii ni kwa sababu mishahara  na makazi ya askari wetu ni duni, vitendea kazi vichache na duni jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa kuwa na askari wasio na
ari na shauku ya kazi ya ulinzi na usalama. Matokeo yake wanakosa nidhamu ya kazi na hivyo kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwemo rushwa na unyanyasaji wa raia. Ili kuwa na askari wenye nidhamu ya kazi, ni lazima kuwa na Serikali inayojua na kuthamini wajibu mkubwa wa vikosi vya ulinzi na usalama katika taifa. Kama vile Serikali inavyotoa mishahara mikubwa kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)na Benki kuu ili kuwapa motisha wasiibe, vivyo hivyo Serikali ingeona umuhimu wa kuwalipa na kuwatunza vyema  askari wa vikosi vya ulinzi na usalama kwa kuwa na askari wanaofanya kazi kwa moyo uliopondeka ni hatari kwa ukuaji wa uchumi na usitawi wa wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika,
Kitendo cha Serikali kupuuza maslahi mbalimbali ya askari wetu ni kuwaingiza katika majaribu mbalimbali ikiwemo rushwa, ukandamizaji na unyasaji dhidi ya raia wanaopaswa kuwalinda. Ifahamike kwamba kuwaingiza watu majaribuni ni dhambi. Aidha majaribu ya kumfanya mtu atende jambo baya yanahesabika kuwa ni dhambi. Ni katika muktadha huu, hata Bwana Yesu alipokuwa akiwafundisha wanafunzi wake kusali, aliwaambia wamwombe Mungu wakisema “….Usitutie Majaribuni bali utuokoe na Yule mwovu” Kwa hiyo Mheshimiwa Spika, Dhamira isiyokuwa na utu ya Serikali hii CCM juu ya usitawi wa nchi hii na watu wake ndio chanzo kikubwa cha askari wetu na wananchi wengine kuingia katika majaribu ya rushwa na aina mbalimbali za uhalifu.

Mheshimiwa Spika,
Ni kweli inawezekana kabisa binadamu akawa muadilifu bila kuwa na masilahi bora katika jamii, lakini vile ni ukweli usiopingika kwamba umasikini na hali duni ya maisha ndio unachangia kwa kiasi kikubwa kuondoa uadilifu na uimara wa nidhamu katika kukabiliana vishawishi vya rushwa na mambo mengine machafu yenye sura hizi.

Mheshimiwa Spika,
Kutokana na Serikali kuwa ndio mlezi wa rushwa, imekosa mamlaka ya kiuadilifu (moral authority) wa kukemea vitendo vya rushwa vinavyofanywa na taasisi mbalimbali zilizo chini yake. Kwa mfano kwa mujibu wa vyombo vya habari na kwa mujibu wa mjadala wa bajeti ya Serikali unaoendelea bungeni imeibuliwa kashfa ya wizi wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 200 ambapo Viongozi Wakuu wa Serikali wamehusishwa. Katika jambo kama hili, Serikali inatoa wapi nguvu na sauti ya kukemea rushwa  katika taasisi inazoziongoza kama vile  jeshi la Polisi .

Mheshimiwa Spika,
Kama wanaopaswa kukemea na kuzuia rushwa ni wala rushwa, ni wazi moja kwa moja  kuwa, utamaduni wa kupokea rushwa na kula rushwa katika taasisi zote za Serikali ni jambo la Kawaida, na linaoipendeza Serikali ya CCM. Kwa hiyo, hakuna hata Kiongozi mmoja mwenye mamalaka ya kiuadilifu kukemea jambo hili, kwa kuwa familia zao zinaishi, zinasoma na kufurahia  maisha  kwa ajili ya ufisadi, wizi wa mali za Umma na rushwa .

Mheshimiwa Spika,
Kwa dhati kabisa, Kambi Rasmi ya Upinzani inaikemea Serikali kujenga mazingira ya rushwa kwa askari wetu. Kwa mfano kitendo cha Serikali hii ya CCM kukigeuza kitengo cha Askari wa Usalama Barabarani kuwa kitengo cha ukusanyaji mapato kwa makosa ya kutafutiwa na kulazimishiwa barabarani ni rushwa iliyowekewa mfumo rasmi. Jambo hili ni hatari sana kwa sababu rushwa ya aina hii haiwezi kumalizika kwa kuwa ina baraka za Serikali. Hali ni mbaya zaidi kwa kuwa   katika kutekeleza jukumu hilo la askari kukusanya mapato, utaratibu umewekwa ambapo kila askari anatakiwa kutafuta kwa bidi, kulazimisha na kukamata makosa yasiyopungua sita mpaka tisa na kuyatoza faini. Mfumo huu mpya wa Serikali wa ukusanyaji wa mapato umeifanya rushwa barabarani kuwa rasmi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inafahamu kwamba Serikali imeishiwa fedha, lakini tunaisihi sana isitumie njia za ukandamizaji na uonevu kujikusanyia mapato.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya kuacha jukumu lao la msingi la kusimamia sheria za barabarani na kuanza kukusanya mapato, ajali za barabarani zimeongezeka sana.  Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2013, jumla ya ajali za barabarani zilizohusisha magari katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Pwani, Kilimanjaro, Arusha na Morogoro zilikuwa ni 459,931, na ajali hizi zilisababisha vifo vya watu 2,408 na majeruhi 16,040. Kwa upande wa bodaboda watu waliofariki kutokana na ajali ni 1,106 na majeruhi 6,581.

Mheshimiwa Spika,
Ripoti ya Haki za Binadamu ya 2013, inasema kwamba nchi inapata hasara ya kati ya asilimia 1 hadi 2 ya Pato la Taifa (GDP) kutokana na ajali za barabarani. Kwa hiyo, uamuzi wa Serikali wa kukifanya  kikosi cha usalama barabarani kuwa kitengo cha ukusanyaji mapato umekuwa ni hatari kubwa kwa maisha ya raia na uchumi wa nchi.
                                               iv.            Ukandamizaji, Ukatili na Uonevu Unaofanywa na Jeshi la Polisi.
 Mheshimiwa Spika
 Hivi karibuni kumekuwa na matukio  ya mahubusu kugoma kula , kuvua nguo hadharani  na mambo mengine yakusikitisha ili kuonyesha hisia zao juu  ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa dhidi yao. Madai makubwa ya mahabusu hao ni kwamba wanapata mateso makubwa gerezani kwa makosa ambayo wengi wao hawajayatenda. Hii maana yake ni kwamba Mahabusu wengi katika magereza yetu wamebambikizwa kesi jambo ambalo ni kinyume kabisa na utawala wa sheria na haki za binadamu.

Mheshimiwa Spika,
Ili kuondoa mwanya uliopo hivi sasa wa Polisi kuwabambikiza raia kesi na kuwaweka mahabusu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kufanyia marekebisho sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ili kuondoa fursa kwa baadhi ya askari wenye nia mbaya kutumia madaraka yao kuwabambikizia watu kesi kutokana na chuki au sababu nyingine.  Kwa mfano, kijana mmoja wa Arusha, aliingia katika ugomvi wa mapenzi na askari polisi kwa sababu ya kumgombania binti. Askari yule alitengeneza mazingira kwa kijana yule kumbakiziwa kesi ya wizi wa kutumia silaha na mauaji na kuswekwa rumande. Kijana huyo wakati alipokuwa anaendelea kuteseka mahabusu, yule askari alimwoa mwoa yule binti. Baadaye askari huyo na binti huyo ambaye sasa ni mke wa yule askari wakaenda Magereza kumtembelea yule kijana aliyekuwa mahabusu kwa uonevu kama ishara ya kuonyesha umwamba!!!!!


Mheshimiwa Spika,
Mambo kama haya hayana idadi katika magereza zetu. Ni mengi. Uonevu na unyanyasaji unaofanywa na askari wetu katika kila kona ya nchi yetu ulijidhihirisha pia bomu lilipolipuliwa  katika mkutano  wa CHADEMA wakati wakuhitimisha kampeni za marudio ya Udiwani mwaka jana ambapo  watu wanne walifariki Dunia na wengine wengi zaidi ya 100 kujeruhiwa  vibaya wakiwemo watoto wadogo na Wanawake.

Mheshimiwa Spika,
 Tuna ushaidi wa kutosha juu ya  ni nani alihusika na mlipuko huo wa bomu. Licha ya kuwa baadhi ya polisi walihusika na mlipuko huo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilimtaka Rais mara nyingi aunde tume ya Kijaji kwa ajili ya uchunguzi wa suala hili kubwa lakini hakufanya hivyo mpaka sasa.  Badala yake kumekuwa na kejeli nyingi na mizaha juu ya suala hili hatari kwani waliokufa kwenye mkutano wa CHADEMA wanaonekana hawana tofauti na mbuzi au Kondoo.

Mheshimiwa Spika,
 Sisi walengwa tuliotaka kuuwawa tunafahamu uchungu na mashaka tuliyo nayo dhidi ya maisha yetu. Hata hivyo mnaweza kuendelea kudharau jambo hili kwa sababu bado Utawala na Mamlaka yenu yanaendela kuelekeza, kupanga na kuendesha Nchi.  Lakini jambo dhahiri ni kwamba; mateso haya, damu hizi, uonevu huu utafika mwisho na kama nyie hamtakuwepo basi watoto wenu watakuwepo na ndugu zenu wengine watakuwepo kushuhudia ukomo wa ukandamizaji, utesaji, uuaji na udhalimu huu dhidi ya raia wasio na hatia.

Mheshimiwa  Spika,
Ni jambo la kusikitisha sana kwamba waliotaka kutuua pia waliendelea kupanga mipango ya kutubambikia kesi hiyo ya mauaji na ugaidi.  Lakini Mungu akawa mwema, walikamatwa vijana wengi, wamepigwa, wameteswa na wengine sina uhakika kama wataweza kuwa na uwezo wa Nguvu za kuzaa tena tena kwa jinsi ya simulizi zao walivyofanyiwa ukatili wa ajabu na wote walilazimishwa kumtaja Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema viongozi waandamizi wa CHADEMA kuwa ndio waliohusika na mlipuko wa mabomu Kanisani Olasiti na kwenye Mkutano wa kufunga Kampeni za Udiwani za CHADEMA mwaka jana.

Mheshimiwa Spika ,
 Katika vijana hawa waliopatiwa mateso makali baadhi yao walitolewa gerezani wakiwa na kesi nyingine na wakaelekezwa , wakapigwa , wakateswa na wengine kutishiwa kuuwawa wakubali kuwa mipango ya milipuko ya mabomu kanisani  Olasiti na kwenye Mkutano wa CHADEMA yaliratibiwa na Mbunge wa Arusha Mjini na viongozi wakuu wa CHADEMA. Kwa tafsiri hii, inaonekana kwamba; waliolipua bomu katika Kanisa la Olasiti, ndio hao hao waliolipua bomu katika mkutano wa CHADEMA. Hii ni kwa sababu badala ya polisi kutawatafuta wahalifu hao na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria, wanahangaika kutafuta watu wa kuwabambikizia kesi kulipua bomu kanisani ili wawaunganishe na tukio la mlipuko wa bomu katika mkutano wa CHADEMA. Kwa sababu wanawatafuta watu wa kuwabambikiza kesi ni dhahiri kwamba Serikali inajua undani wa tukio hilo.

Mheshimiwa Spika,
Uadilifu wa Jeshi la Polisi umeendelea kuwa mashakani kwani baada ya Uchaguzi  mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki , Kijana mmoja Kiongozi wa CHADEMA wa Kata ya Usa river Msafiri Mbwambo aliuwawa kwa kuchinjwa shingo.  Wauwaji  wale walikamatwa na Jeshi la Polisi lakini cha kusikitisha ni kwamba  baada ya muda  mfupi  wahalifu hawa  waliweza kutoroka mbele ya Polisi kwenye chumba cha mahakama  wakiwa wamefungwa pingu eti nakufanikiwa kumpora Askari Bunduki aina ya SMG na kukimbia nayo mpaka leo hawajaonekana wakiwa na pingu zao . Mheshimiwa Spika, huu ni upumbavu usiofikirika.

Mheshimiwa Spika
Hata wewe unaweza pia  kuziba masikio yako kana kwamba hiki kinachosemwa ni “blues” na ngojera lakini Mungu yule unayemfuata Kanisani kila asubuhi kumuomba amesikia na yuko kazini . ‘Only Time will tell’.

Mheshimiwa Spika,
 Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2013 (uk.22) watu 23 waliuwawa na vyombo vya dola kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, 2013. Kuna mateso makubwa wanayopitia wananchi kutokana na uonevu wa askari wetu.  Wanalia machozi mazito lakini hakuna msaada kwani Serikali inayopaswa kuwatazama na kuwalinda raia wake dhidi ya ukandamizaji huu , Serikali hiyo imepoteza ladha ya utu kwa hiyo kelele na mateso wanayopata Watu kwa kubambikiziwa kesi na kuwekwa mahabusu na kufungwa miaka mingi na kuuwawa, mateso hayo sasa yamegeuka kuwa laana kwa Nchi yetu.

                                                 v.            Polisi Jamii
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani ina mtazamo kwamba ni vema kuwajengea wananchi utamaduni wa kuripoti matukio ya kihalifu kwa Jeshi la Polisi kuliko kuanzisha taasisi nyingine isiyo rasmi ndani ya Jeshi la Polisi. Tunatambua kwamba Jeshi la Polisi limeanzisha mfumo huu wa Ulinzi shirikishi kwa sababu ya uchache wa askari iliyo nao. Katika Randama ya Jeshi la Polisi, fungu 28, mojawapo ya changamoto zilizotajwa ni uchache wa askari Polisi. Kwa mujibu wa randama hiyo, idadi ya askari inayohitajika nchini kwa kiwango cha kimataifa ni 90,000 wakati waliopo sasa hawafiki nusu ya idadi hiyo.  Aidha, Jeshi la Polisi linapata ugumu wa kupata taarifa za kihalifu kutoka kwa wananchi kwa sababu ya uadui uliojengeka kati ya wananchi na Jeshi la Polisi .

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Bungeni inaitaka Serikali kuongeza ufanisi katika matumizi yake ya fedha, kuzuia ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma, kuwajengea wananchi uwezo wa kiuchumi ili fedha zitakazopatikana zitumike kuajiri askari ambao ni wataalamu wenye uwezo wa kuwalinda raia na mali zao badala ya kurasimisha mfumo usio rasmi wa polisi jamii ambao wengi wao ni green guards wa CCM.  

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inalaani Jeshi la Polisi kupuuzwa huko Zanzibar kwa kuvipa mamlaka zaidi dhidi ya Jeshi la Polisi vikosi vya KMKM, JKU na KVZ katika kusimamia shughuli za Ulinzi na Usalama wa Zanzibar. Jambo hili limeondoa mamlaka ya Jeshi la Polisi ambalo lina wajibu wa kulinda raia na mali zao katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

                                               vi.            Uchochezi wa Kidini na Kikabila
Mheshimiwa Spika,
Tatizo la udini na ukabila katika taifa hili linaonekana kuendelea kukomaa. Lakini ni tatizo ambalo halitamwacha hata mmoja wetu salama. Ni tatizo ambalo hakuna mshindi atakayepatikana. Ni tatizo ambalo hata kama litaisambaratisha nchi, hata wale watakaofanikiwa kuikimbia nchi hawatakuwa salama huko wanakokwenda kwa sababu watakuwa bado na imani zao na chuki hiyo dhidi imani nyingine itaendelea popote watakapokuwa.

Mheshimiwa Spika,
Kwa vile jambo hili linatishia usalama mpana wa taifa hili, ni vema sasa Serikali ikatafakari upya na kuleta sheria mpya itakayokataza na kuwawajibisha kwa nguvu zote wale wote watakaojaribu hata kwa maneno kueneza chuki au ubaguzi dhidi ya dini, kabila au rangi. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iombe radhi na kuwaondoa madarakani viongozi wote wa Serikali walitotoa kauli za uchochezi wa kidini, kikabila na rangi.

  1. MAHUSIANO YA SERIKALI KATIKA BIASHARA HARAMU YA MADAWA YA KULEVYA NCHINI.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, haina sababu ya kupoteza muda eneo hili kwani ni ukweli usiopingika kuwa biashara hii inafanywa na viongozi wakuu wa Serikali,  hivyo basi  waamue wao wenyewe  kama wangependa kuendelea kuwa sehemu ya mateso na mauaji ya vijana wetu  katika jamii ya watu inaowaongoza.

 Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani imelazimika kufikia uamuzi huu kwa kuwa viongozi wakuu wa nchi hii walishakiri hadharani kuwa wanawafahamu kwa majina watu wanaojishughulisha na biashara hii. Ni ajabu na ni kituko kama Rais wa Nchi ambaye ndiye amiri jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama anaogopa kuwataja wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya ambao alisema kuwa anawafahamu kwa majina. Tunashawishika kuamini kwamba bila shaka watu hao ambao mpaka Rais anagwaya kuwataja watakuwa ni  malaika kutoka mbinguni au Mungu.

Mheshimiwa Spika,
Ni vema kama taifa tukatambua madhara ya madawa ya kulevya kwa vijana wetu ambao ndio nguvu kazi ya taifa. Kupuuzia na kutochukua hatua kwa wahusika wa dawa za kulevya ni kuangamiza nguvu kazi ya taifa. Nguvu kazi ya taifa ikishaharibiwa na dawa za kulevya hatuna taifa tena. Hivyo Serikali ifahamu kwamba kuendelea kulifumbia macho jambo hili ni kulihujumu taifa na huo ni usaliti mkubwa.

 MAUAJI YA RAIA NA POLISI
Mheshimiwa Spika,
Toka mwaka 2011 katika hotuba zetu kuhusu Wizara hii tumeendelea kuonesha mauaji ya raia yanayofanywa na vyombo vya dola likiwemo Jeshi la Polisi. Wakati akihitimisha hoja yake hapa Bungeni Mhe. Waziri Mku Mizengo Pinda aliahidi mbele ya Bunge lako tukufu kuwa serikali ingeunda Mahakama ya Korona kwa ajili ya kuchunguza vifo hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa vifo vyenye utata (Inquest Act).

Mheshimiwa Spika,
Serikali ilirudia kutoa ahadi ya kuanzisha Mahakama hiyo ya Korona kwa ajili ya kuchunguza vifo vilivyosababishwa na Operesheni ya kuondoa Majangili “Tokomeza” miezi michache iliyopita.

Mheshimiwa Spika,
Hadi leo ahadi hiyo ya Waziri Mkuu haijatekelezwa na badala yake Rais ameamua kuunda tume nyingine huku Bunge lako tukufu likiwa limewasilisha taarifa kuhusu Tokomeza jambo ambalo linaonesha serikali kutoamini taarifa ya Kamati ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mwaka wa 2013 taarifa zinaonesha kuwa watu 23 waliuwawa na vyombo vya dola. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii kueleza Bunge lako tukufu juu ya kukithiri kwa tabia hii isiyokoma mwaka hadi mwaka na ni hatua gani zilizochukuliwa dhidi ya askari wanaohusika na mauaji haya.

Mheshimiwa Spika,
Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi mpya kuchukulia hali kama janga ndani ya Jeshi la Polisi na hivyo awe na mkakati wa kuzuia hali hii.

Mheshimiwa Spika,
Katika hali ya kushangaza hata wananchi wameanza kuchukua sheria mkononi kwa kuwadhuru na hata kuwaua askari polisi. Kwa mwaka 2013 vituo vya polisi takribani vitano vilivamiwa na wananchi na mali kadhaa za Jeshi hilo kuharibiwa, aidha vifo kadhaa vya askari viliripotiwa kutokea katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika,
Kama matukio hayo hayatoshi wananchi kwa makundi yao katika maeneo mbalimbali ya nchi walizidi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwaua watu mbalimbali ambao wametuhumiwa kufanya makosa ya jinai kama vile wizi. Kwa mwaka jana pekee watu 1669 waliuwawa[1].

Mheshimiwa Spika,
 Upo uhalifu mwingine ambao umejitokeza katika nchi yetu ambapo watu wamekuwa wakizikwa wakiwa hai. Matukio kama ya hayo yametokea katika Wilaya Chunya na maeneo mengine katika Mkoa Mbeya.

Mheshimiwa Spika,
Hali hii ya mauaji ya raia yanayofanywa na vyombo vya dola na pia mauaji yanayofanywa na wananchi kwa wahalifu na pia kuvamia na hata kuua Polisi sio jambo la kulifanyia mzaha kabisa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuchukua hatua za dharura na kutoa taarifa Bungeni na bila kufanya hivyo italazimika kuamini kuwa serikali iliyopo madarakani imetoa Baraka kuhusu vitendo hivi vya kinyama kuendelea kutokea katika nchi yetu.



  1. UHAMIAJI HARAMU NA USALAMA KATIKA MIPAKA YA NCHI YETU
Mheshimiwa Spika,
Mipaka ya Tanzania haipo salama kabisa kwa sababu imeendelea kuwa kichaka kwa wahamiaji haramu. Hali hiyo pia inathibitika na kile kilichosemwa na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi Bungeni katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa  kuhusu kung’olewa kwa alama (beacons) za mipaka yetu katika maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo, mahusiano mabaya ya Tanzania na baadhi ya jirani zake yanafanya hali ya usalama mipakani kuwa ya hatari zaidi. Kwa mfano, kumekuwa na mvutano kati ya Rais Kikwete na Rais Kagame kwa mujibu wa vyombo vya habari. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji, kutofautiana kwa maneno kati ya Rais Kikwete na Kagame kunatosha kuwa ugomvi kati ya nchi hizi mbili kwani hili lisipotazamwa vizuri linaweza kufifisha matumani ya wananchi wa nchi hizi mbili kuishi kama ndugu ndani na nje ya mipaka yetu.

Mheshimiwa Spika,
Tanzania imejaa wageni wengi kutoka nchi mbalimbali kama vile Bangladesh, India, China, Pakistan, na nchi nyingene za Afrika na Afrika Mashariki wanaofanya kazi hapa nchini katika fani na taaluma ambazo watu wetu wanazo.  Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji kama ni sera ya Serikali hii ya CCM kutoa kipaumbele cha ajira kwa wageni katika fani, ujuzi na taaluma ambazo watanzania wanazo. Aidha, tunaitaka serikali kupitia idara ya uhamiaji na idara nyingine za serikali kupitia takwimu za wageni waliopo nchini na shughuli wanazozifanya ili kuona kama wageni hao wana uhalali wa kuendelea kuwepo na kufanya kazi nchini ikiwa hakuna kazi inayohitaji taaluma maalumu (special skills) ambazo watu wetu hawana.

  1. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Kila aliyepata fursa ya kusikiliza kwa makini maoni haya  ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  angetaka kuona tunatoa suluhisho gani juu ya nini  kifanyike kuhusu mambo haya. Hata sisi  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  tunafikiri ni vyema kushauri na kusaidia kuonyesha njia muafaka ili kuliokoa taifa letu na mateso haya, lakini tunapata wakati mgumu kuishauri Serikali ambayo imepoteza thamani ya utu dhidi ya watu wake.  Hivyo basi, kama kuna mambo ya kushauri, basi tungeshauri yafuatayo:

 Moja: Mungu asaidie Serikali hii ya CCM iondoke madarakani mapema kabla haijaharibu mfumo wa kumpata kiongozi kwa njia ya demokrasia kwani hali ikiendelea hivi; iko siku watu wataingia barabarani. Hali hii tayari imeshaanza kujitokeza kwani mwaka Kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2013 pekee watu 1669 waliuwawa kwa sababu ya watu kujichukulia sheria mkononi.  Tunajua watu watakapojitokeza kudai haki zao na kupinga uonevu  watapigwa  mabomu ya machozi, risasi, na vitisho na mateso mbali mbali lakini tunajua hawatarudi nyuma; kwani watakuwa wamedhamiria kujitetea na kuwatetea ndugu zao na nchi yao dhidi ya mateso, ukandamizaji, uonevu na dhiki inayotokana na mambo hayo.  Kinyume chake, yatakapotokea hayo,  Serikali itakuwa imetangaza ukomo wa utawala wa kidemokrasia na hilo linaweza kuwa chimbuko la machafuko na umwagaji damu, hivyo ni vyema waumini wa imani mbalimbali wafanye dua na sala ili Serikali hii ya CCM iondoshwe madarakani katika uchaguzi mkuu ujao kwa amani.

Pili: Siku Serikali hii ya CCM ikijua kuwa  nguvu ya Mfalme ni watu na sio bunduki na mabomu ya machozi,  siku hiyo ndipo mtakapoanza kupata hekima ya kuheshimu utu wa binadamu na kile kinachoonekana sasa kama mateso, udhalimu na ukandamizaji vinaweza kurekebishwa.

Tatu: Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutambua kuwa heshima ya kiongozi haijengwi kwa uwezo wa mali wala utawala bali katika kazi njema, heshima, utu, na upendo. Ikiwa Serikali itaelewa hivyo; basi wajibu wake katika kutafuta na kupigania maisha ya mtu mmoja mnyonge anayeteswa na kudhalilishwa itakuwa ndio hazina na heshima kubwa  kwa viongozi wa serikali  na taifa kwa jumla.

Mwisho:  Tunafahamu kwamba ndani ya Serikali kuna watu wengi waadilifu na wenye dhamira njema na nchi yetu. Hata hivyo, wanashindwa kuchukua uamuzi wa kukemea uovu kutokana na utamaduni wa Serikili kuwatisha na kuwawekea vikwazo mbalimbali watu wa namna hiyo. Kutokana na hali hiyo, jamii yetu imejengwa katika fikra za hofu na woga kwa mambo ambayo yanahitaji uamuzi thabiti na kauli za kijasiri ili kulinusuru taifa na maangamizi.

Mheshimiwa Spika,
 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali ijue na wananchi wote wajue kwamba; “Dhambi mbaya na kubwa kuliko zote Duniani ni woga”.  Hivyo Basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawaasa viongozi wachache wenye dhamira njema  kwamba waache woga wasimamie misingi ya haki na ukweli  hata kama gharama zake ni Maisha yao kwani msingi wa Taifa letu la kesho unajengwa na viongozi na  utawala ulioko madarakani leo.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba kuwasilisha.



Godbless Jonathan Lema (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI NA
WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Imesomwa leo, tarehe 15 Mei, 2014




[1] LHRC Report, 2013, pg 29

No comments:

Post a Comment