Saturday, April 12, 2014

Sitta aizika rasmi hoja ya Mnyika

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, amezima jaribio la Mjumbe, John Mnyika, kutaka kutumia hoja ya Hati za Muungano kuahirisha Bunge hilo.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), alitaka uwasilishaji wa ripoti za kamati zilizochambua sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba,usimamishwe kwanza hadi wajumbe watakapopata nakala halisi zilizothibitishwa za hati ya makubaliano ya Muungano.

Jana asubuhi, Mnyika alikuwa wa kwanza kusimama Bunge lilipoanza shughuli zake na kumkumbusha Mwenyekiti kuwa aliwasilisha hoja ya kuomba nakala hizo zilizothibitishwa.

Akitoa maamuzi, Sitta alimtaka Mnyika kuwasilisha hoja mahsusi bungeni ijadiliwe na maamuzi yafanywe na wajumbe wote na akamuru shughuli za Bunge ziendelee.
Mazungumzo baina ya Mnyika na Sitta yalikuwa kama ifuatavyo:

Mnyika: Naomba niwasilishe kwa kunukuu kanuni na fasili, ambazo zinaeleza kuwa jambo lolote linalohusu haki za Bunge hili Maalumu litawasilishwa kwa kufuata kanuni ya 27(1) inayoagiza kuwa hatua hiyo itachukuliwa baada ya mwenyekiti kuarifiwa mapema kuhusu jambo hilo.

Sitta: Tukianzia hapo wewe ulimuarifu lini Mwenyekiti?

Mnyika: Mheshimiwa Mwenyekiti nilikuarifu mapema mara mbili.

Sitta: Wapi?

Mnyika: Mapema asubuhi ya leo (jana) na pia nakala ya barua, ambayo niliwasilisha mapema leo (jana) asubuhi.

Sitta: Hoja yako nini sasa?

Mnyika:
 Kwa mujibu wa kanuni fasili ya pili kuwa endapo Mwenyekiti atapata taarifa mapema ataamua kwamba, hoja inayowasilishwa kwenye Bunge Maalumu ina umuhimu,  mjumbe atapewa nafasi kuiwasilisha na kutoa maelezo ya hoja na kuthibitisha kuwa zinahusu haki za Bunge.

Kadhalika, jambo hilo linapewa kipaumbele kabla ya lingine linalofuata. Kwa hiyo, naomba kuwasilisha hoja ya Haki za Bunge ya kupewa nakala halisi iliyothibitishwa ya Hati za Muungano kabla kuendelea na majadaliano ya taarifa za kamati.

Naomba nipewa nafasi ya kuwasilisha hoja kwa mujibu wa kanuni ya nne inayohusu haki za Bunge inayozingatia kanuni ya nne ya wabunge kupewa nyaraka wanazohitaji.

Sitta:
 Kwa mujibu wa kanuni, ni dhahiri kabisa kuwa Mnyika ametoa hoja, lakini kuzuia mjadala wa Bunge Maalumu usiendelee hadi hapo atakapopewa nakala halisi za hati ya Muungano.

Sitta: Sasa kama ni hivyo, mimi nakuruhusu Mnyika utoe hoja mahsusi bungeni ili Bunge liijadili na liamue iletwe tuijadili. Lakini vinginevyo kila mmoja akiwa analeta ombi ooh sijaona karatasi Fulani, tusiendelee, naomba tusiendelee. Naona hapo tutazidi kuchelewa.

Sitta: Katibu tuendelee.
Baada ya maelezo hayo, Bunge liliendelea na kusikiliza taarifa za kamati kwa kusikiliza mjadala kutoka kamati namba mbili uliowasilishwa bungeni na Mwenyekiti, Shamshi Vuai Nahodha.

No comments:

Post a Comment