MAONI YA WAJUMBE WALIO WA
WACHACHE KATIKA KAMATI NAMBA NNE KUHUSU SURA YA KWANZA NA SURA YA SITA YA
RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
[Kanuni ya 32(4) ya Kanuni za Bunge Maalum, 2014]
UTANGULIZI
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sura ya Kwanza na Sura ya
Sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (‘Rasimu’) ndizo
msingi ambao Rasimu yote imejengwa juu yao. Wakati Sura ya Kwanza inagusa suala
la muundo wa Muungano katika ibara moja tu kati ya ibara tisa, Sura yote ya
Sita inahusu ‘Muundo wa Jamhuri ya Muungano.’ Suala la Muungano na hasa Muundo
wake limetawala mjadala wa kisiasa na kikatiba wa Tanzania kwa zaidi ya miaka
thelathini. Ndio maana katika waraka wake wa siri kwa Halmashauri Kuu ya Chama
cha Mapinduzi (‘CCM’), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya chama hicho
imetamka kwamba “muundo wa Muungano ndiyo
moyo wa Rasimu na ndiyo unaoamua ibara nyingine zikae vipi.”
Suala hili pia limetawala mchakato
wa Katiba Mpya tangu ulipoanza miaka mitatu iliyopita. Kama alivyosema
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Joseph Sinde Warioba wakati wa
kuwasilisha Ripoti ya Tume yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa
Zanzibar tarehe 30 Disemba, 2013: “Moja
ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa hisia kali tangu Rasimu ya awali
ilipotolewa ... ni Muungano wa Tanzania. Jambo kubwa limekuwa juu ya muundo wa
Muungano.”[1]
Umuhimu wa suala hili
unathibitishwa pia na uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum kuelekeza
kwamba Kamati zake Namba Moja hadi Kumi na Mbili zianze kujadili Sura ya Kwanza
na ya Sita ya Rasimu. Haya ni maoni ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba
Nne juu ya Sura hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mjadala wa Kamati Namba Nne
kuhusu Sura za Kwanza na Sita za Rasimu unathibitisha pia umuhimu wa suala la
muundo wa Muungano katika mjadala mzima wa Rasimu. Kama Taarifa ya Kamati yetu inavyoonyesha,
Kamati Namba Nne imeshindwa kufanya uamuzi kuhusu suala hili katika ibara za 1
na 60 za Rasimu. Katika ibara ya 1 ya Sura ya Kwanza, wajumbe walio wengi
walipata kura 22, ambayo ndiyo theluthi mbili ya kura za wajumbe wote 33 wa
Tanzania Bara wa Kamati Namba Nne. Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe walio wengi
walipata kura 9 ambayo ni pungufu ya kura 13 zinazohitajika ili kufikisha idadi
ya theluthi mbili ya wajumbe wote 19 wa Zanzibar.
Kwa upande wa ibara ya 60,
wajumbe walio wengi walipata kura 22 za wajumbe kutoka Tanzania Bara, ambazo ni
theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote 33 kutoka Tanzania Bara. Aidha, kwa
Zanzibar, wajumbe walio wengi walipata kura 8, ambazo pia ni pungufu ya kura 13
zinazotakiwa kufikisha idadi ya theluthi mbili ya wajumbe wote 19 kutoka Zanzibar.
Kwa sababu hiyo, ibara za 1 na 60 za Rasimu hazikupitishwa au kuamuliwa na
Kamati Namba Nne kama inavyotakiwa na kifungu cha 26(2) cha Sheria na kanuni ya
64(1) ya Kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sasa tunaomba kwa ridhaa
yako, tuwasilishe hoja na sababu za maoni ya wajumbe walio wachache katika
Kamati Namba Nne kuhusu Sura hizi mbili ambazo ndio ‘moyo wa Rasimu.’
SURA YA KWANZA
Sura ya Kwanza ya Rasimu
inahusu ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Sehemu ya Kwanza ya Sura hiyo
inazungumzia ‘jina, mipaka, alama, lugha na tunu za Taifa.’ Ibara ya 1
inaitambulisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ibara ya 2 inatangaza ‘eneo la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’; na ibara ya 3 inaweka utaratibu wa ‘alama na
sikukuu za Taifa.’ Vile vile ibara ya 4 inaweka utaratibu wa lugha ya Taifa na
lugha za alama, wakati ibara ya 5 inahusu ‘tunu za Taifa.’
Kwa upande wake, Sehemu ya
Pili ya Sura ya Kwanza inaweka masharti ya ‘mamlaka ya wananchi, utii na
hifadhi ya Katiba. Ibara ya 6 ya Sehemu hiyo inatoa ufafanuzi wa ‘mamlaka ya
wananchi’; ibara ya 7 inafafanua uhusiano kati ya ‘watu na Serikali’; ibara ya
8 inashurutisha ‘ukuu na utii wa Katiba’; na ibara ya 9 na ya mwisho inaweka
‘hifadhi ya utawala wa Katiba.’
Endelea..........
IBARA YA 1
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kama maelezo yake ya pembeni
(marginal note) yanavyoonyesha, ibara
ya 1 inaitambulisha ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Ibara ya 1(1) inatamka
kwamba “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ni Shirikisho lenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili
za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati za
Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.”
Kwa upande wake, ibara ya
1(2) inafafanua kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania “ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya
siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za
binadamu na lisilofungamana na dini.” Mwisho, ibara ya 1(3) inatukumbusha
kwamba “Hati ya Makubaliano ya Muungano
... ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba hii, kwa
kadri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa Makubaliano hayo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Wajumbe walio wachache wa
Kamati Namba Nne wanapendekeza mabadiliko ya jina la nchi yetu kutoka jina la
sasa la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ kuwa jina jipya la ‘Shirikisho la
Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.’ Aidha, wajumbe hao wanapendekeza kuacha
kutajwa kwa Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 katika ibara ya 1(1)
na (3) ya Rasimu. Badala yake, inapendekezwa kwamba Katiba hii ndiyo iwe msingi
wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.
Kwa mapendekezo haya, ibara
ya 1(1) itasomeka kama ifuatavyo: “Shirikisho
la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho ambalo limetokana na
Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar.” Kwa mantiki hiyo, ibara ya 1(2) itasomeka: “Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho la
kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu,
kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na lisilofungamana
na dini.” Aidha, ibara ya 1(3) itasomeka: “Katiba hii ndio msingi mkuu wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na
Zanzibar.” Zifuatazo ni hoja na sababu za mapendekezo haya.
SHIRIKISHO
AU MUUNGANO?
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Katika nusu karne ya uhai
wake, nchi yetu imeitwa ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Hata hivyo, katika
kipindi chote hicho, Katiba na Sheria za nchi yetu hazijawahi kufafanua kwa
uwazi aina au haiba ya ‘Muungano’ huu. Matokeo ya kukosekana kwa ufafanuzi huu
ni kwamba katika nusu karne hiyo, kumekuwa na mjadala mkubwa wa kikatiba,
kisiasa na kitaaluma kuhusu suala la kama Jamhuri ya Muungano ni dola ya
muungano (a unitary state), au ni
dola ya shirikisho (a federal state).
Majibu ya swali hili yamekuwa na athari za moja kwa utambulisho, haki, maslahi
na wajibu wa Washirika wa Muungano huo, yaani Tanganyika na Zanzibar, na hasa
kwa wananchi wa nchi hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kukosekana kwa ufafanuzi wa
aina ya muungano wetu haujawa suala la mijadala ya kisiasa na kikatiba peke
yake, bali kumekuwa ni chanzo cha migogoro mikubwa ya kisiasa baina ya Serikali
ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Migogoro hii ilianza
tangu mwanzo kabisa wa Muungano wakati wa sakata la kuwa na ubalozi wa
iliyokuwa Ujerumani Magharibi kwa upande wa Tanganyika na ubalozi wa iliyokuwa
Ujerumani Mashariki kwa upande wa Zanzibar.
Aidha, kati ya mwaka
1964-1967 ulizuka mgogoro mkubwa kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar katika
iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu ya
Tanzania; kuunganishwa kwa vyama vya ASP na TANU na kuundwa kwa CCM mwaka 1977,
na katika mjadala wa marekebisho ya Katiba wa mwaka na baadae ‘kuchafuka kwa
hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ mwaka 1983/1984.
Baadae mwaka 1988 ulitokea
mgogoro mkubwa uliopelekea kung’olewa madarakani kwa Waziri Kiongozi wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad na baadae kufukuzwa
katika CCM; wakati wa harakati za kudai kura ya maoni kuhusiana na Muungano
mwaka 1989/1990; wakati wa mjadala wa kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya
siasa mwaka 1991; wakati wa sakata la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za
Kiislamu (Organization of Islamic Countries - OIC) mwaka 1993; wakati wa mjadala
wa G-55 na madai ya kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano
mwaka 1994, na Uchaguzi Mkuu wa 1995 huko Zanzibar.
Milenia Mpya ilipoanza
ilianza na mgogoro kuhusu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 uliopelekea
mauaji ya Januari 2001 huko Zanzibar. Mgogoro huo ulifuatiwa na mgogoro juu ya suala
la ugunduzi wa mafuta visiwani Zanzibar; harakati za kuanzishwa kwa Shirikisho
la Afrika Mashariki na hivi karibuni kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya
Katiba ya Zanzibar ya 1984 mwaka 2010.
Zaidi ya migogoro hii,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Mapinduzi zanzibar zimeunda tume na
kamati nyingi ili kupata dawa ya ‘Kero za Muungano.’ Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar peke yake imeunda tume na kamati 13 katika kipindi kifupi cha miaka 12
kuanzia mwaka 1992 hadi 2004; wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeunda
tume na kamati nane kushughulikia matatizo hayo. Licha ya jitihada zote hizo,
‘Kero za Muungano’ hazijapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Tangu miaka ya mwanzo ya Jamhuri
ya Muungano kulikuwa na mitazamo miwili tofauti miongoni mwa waasisi na
viongozi wakuu wa Jamhuri ya Muungano. Mitazamo hii tofauti inathibitishwa na
kauli ya Mwalimu Julius K. Nyerere, mwasisi na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya
Muungano katika Mkutano Maalum wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanyika Dodoma
kati ya tarehe 24-30 Januari, 1984: “...
Muungano wa Tanzania ukiangalia kwa jicho la Zanzibar ni wa shirikisho lakini
ukiangalia kutoka upande wa Tanzania Bara ni Serikali moja.”[2]
Mwalimu alikuwa akimjibu
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar wakati huo, Alhaj
Aboud Jumbe Mwinyi aliyesema kwamba Muungano wa Tanzania umeunda Shirikisho (Federation) na sio Serikali moja (Unitary State). Mjadala huo ulipelekea
‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ na kung’olewa madarakani kwa
Jumbe, Waziri Kiongozi wake Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu Bashir Kwaw
Swanzy. Aidha, Wolfgang Dourado, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati
Hati ya Muungano inasainiwa, na mkosoaji mkubwa wa Muungano huo, aliwekwa
kizuizini kwa kuunga mkono hoja za Rais Aboud Jumbe.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Miaka kumi baada ya
‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ Jamhuri ya Muungano
ilikabiliwa na mgogoro mwingine tena wa kikatiba na kisiasa, mara hii ukitokana
na Zanzibar kujiunga na OIC. Kitendo hicho kilizua tafrani kubwa ya kisiasa
pale Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipopitisha Azimio la kutaka kuanzishwa kwa
Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwezi Agosti, 1993. Azimio hilo liliungwa
mkono na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kitendo kilichomfanya Mwalimu Nyerere
kuingilia kati na kuzima jaribio hilo.
Baadae Mwalimu aliandika kitabu
alichokiita Uongozi Wetu na Hatima ya
Tanzania kilichochapishwa mwaka 1994. Katika kitabu chake, Mwalimu anarejea
mkanganyiko ambao umekuwepo kuhusu aina ya Muungano huu kwa maneno yafuatayo:
“Nchi
zinapoungana na kuwa nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili:
Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake, na nchi mpya inayozaliwa
itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja. Katika mfumo wa pili kila nchi
itajivua madaraka fulani ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho, na
itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki. Mambo
yatakayoshikwa na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka
ya nchi zilizoungana, basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi
moja, bali zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo
fulani fulani.... Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi moja yenye
serikali tatu, Serikali ya shirikisho na serikali mbili za zile nchi mbili za
awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.”[3]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mwaka ambao Mwalimu Nyerere
alichapisha Uongozi Wetu na Hatima ya
Tanzania, Makamu Mwenyekiti wake wa CCM na Makamu Rais wake hadi Januari
1984, Alhaj Aboud Jumbe, aliyekuwa pia Waziri wa Afya wa Zanzibar wakati
Muungano unazaliwa na baadae Rais wa Pili wa Zanzibar, naye alichapisha The Partnership: Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar: Miaka 30 ya Dhoruba.[4]
Katika kitabu hicho, Alhaj Jumbe anathibitisha kwamba “Ibara za Mkataba wa Muungano ziliweka bayana mfumo ambao serikali kuu
na serikali shiriki katika Muungano kuwa na nguvu zinazoendeana, yaani, mfumo
wa shirikisho ambao kuna mgawiko wa mahakama, baraza la kutunga sheria na urais
baina ya serikali kuu na serikali mbili au zaidi, na kila serikali ikiwa na
nguvu kamili ndani ya mamlaka yake.”[5]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Aina ya dola iliyotokana na
Hati ya Makubaliano ya Muungano haikuwahangaisha waasisi wa Muungano ama
viongozi wake wakuu peke yao. Hata ndani ya makorido ya mamlaka, mjadala juu ya
suala hili umekuwa mkubwa na umeundiwa Tume na Kamati mbali mbali za
kulichunguza. Kwa mfano, hata kabla ya kuchapishwa kwa Uongozi Wetu na Hatima
ya Tanzania na The Partner-ship, tarehe 6 Aprili, 1992, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Salmin Amour aliunda Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Kujenga
Hoja Juu ya Masuala ya Muungano wa Tanzania, maarufu kama Kamati ya Amina
Salum Ali kutokana na jina la Mwenyekiti wake. Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna,
ambaye ni mjumbe wa Bunge hili Maalum, alikuwa Katibu wa Kamati hiyo.
Pamoja na mambo mengine,
Kamati ya Amina Salum Ali ililichunguza suala la aina ya Muungano uliozaliwa na
Hati ya Makubaliano ya Muungano. Jibu la Kamati hiyo lilikubaliana na nusu ya
hoja ya Mwalimu Nyerere na nusu ya hoja ya Alhaj Aboud Jumbe: “... Muungano wa Tanzania, haidhuru unaitwa
‘Union’, lakini uko kati na kati baina ya ‘Union’ na Shirikisho. Kuwepo kwa Serikali
ya Muungano yenye madaraka makubwa ni kielelezo cha sura ya ‘Union’. Sura hii
inazidi kutiliwa nguvu na kile kitendo cha Tanganyika kuvua madaraka yake yote
na kuyaingiza katika Serikali ya Muungano. Kwa upande mwengine kuwepo kwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye madaraka kamili Zanzibar juu ya mambo
yote yasiyokuwa ya Muungano, ni kielelezo dhahiri cha sura ya Shirikisho. Kwa
hivyo, Muungano huu ni wa aina yake.”[6]
MTAZAMO WA KITAALUMA
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Hati ya Makubaliano ya
Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar imejadiliwa
sana na kwa miaka mingi katika ulingo wa kitaaluma. Mjadala huu umehusu, kwa
kiasi kikubwa, aina na muundo wa Muungano huu. Katika kitabu chake Tanzania: The Legal Foundations of the Union,
kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwezi Januari, 1990, Profesa Issa
Shivji alisema, baada ya uchambuzi wa kina wa Hati ya Muungano, kwamba
Makubaliano ya Muungano yalitengeneza katiba ya shirikisho. Kwa mujibu wa
Profesa Shivji, katiba za shirikisho zina sifa kuu zifuatazo ambazo alisema
zipo katika Hati ya Muungano:[7]
- Kuna mgawanyo
wa wazi wa madaraka kati ya serikali kuu na serikali za sehemu za muungano
ambayo yapo katika ngazi moja;
- Mamlaka ya
serikali kuu yaliyowekewa mipaka ya wazi wakati mamlaka yaliyobaki yako
mikononi mwa serikali za sehemu za muungano;
- Serikali
zote, yaani serikali kuu na serikali za sehemu za muungano zinagusa maisha
ya wananchi wao moja kwa moja tofauti na serikali ya mkataba (confederation) ambako serikali za
sehemu ndizo zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.[8]
Kwa maneno ya
Profesa Shivji, kwa kuyaangalia Makubaliano ya Muungano kutoka upande wa
Zanzibar na Tanganyika na kwa ujumla wao, “...
msingi wa shirikisho ndio wenye nguvu na Makubaliano ya Muungano yanaweza kutafsiriwa
kwa usahihi kama katiba ya shirikisho.”[9]
Kwingineko katika kitabu hicho, Profesa Shivji alidai kwamba: “Kwa vyovyote vile, ni wazi kwamba
Makubaliano ya Muungano sio katiba ya muungano (unitary constitution).”[10]
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Msimamo wa Profesa
Shivji kuhusu Makubaliano ya Muungano kuwa ni katiba ya shirikisho umeshikiliwa
kwa miaka mingi na wasomi wengine wa Muungano huu. Hivyo, kwa mfano, katika
kitabu chao cha Tanzania Treaty Practice kilichochapishwa
mwaka 1973, Earl E. Seaton na S.T. Maliti walikubali kwamba Makubaliano ya
Muungano yaliunda katiba ya shirikisho na sio katiba ya muungano.
Miaka kumi baadae,
Wolfgang Dourado, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati Hati ya
Muungano inasainiwa, naye alidai kwamba Makubaliano ya Muungano hayakutengeneza
dola la muungano bali yalitengeneza ‘shirikisho la kweli.’[11]
Wasomi wengine ambao wameitaja Katiba ya Tanzania kama katiba ya shirikisho na
wala sio ya muungano ni Profesa B.P. Srivastava katika makala yake ya mwaka
1984 ‘The Constitution of the United
Republic of Tanzania 1977: Some Salient Features, Some Riddles’[12],
na Profesa Palamagamba J.A.M. Kabudi, katika International Law Examination of the Union of Tanganyika and Zanzibar:
A Federal or Unitary State?, ambayo ni matokeo ya utafiti aliouwasilisha
mwaka 1986 kwa ajili ya Shahada yake ya Uzamili ya Kitivo cha Sheria cha Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 2009 The Legal Foundations of the Union
kilichapishwa kwa mara ya pili, mara hii kikiwa na Utangulizi wa Profesa Yash Ghai,
Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa kwanza kutoka
Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Kenya
iliyozaa Katiba Mpya ya Kenya ya mwaka 2010.
Kwenye Utangulizi
wake Profesa Ghai anasema kwamba licha ya Tanzania kutokuwepo katika orodha za
mashirikisho zilizoandaliwa na wasomi au na Jukwaa la Kimataifa la Mashirikisho
(International Forum of Federations);
na licha ya Katiba ya Tanzania kutokutumia neno ‘shirikisho’, bado Tanzania ni
shirikisho.
“Tanzania
inakidhi vigezo vingi vya rasmi vya shirikisho: mahusiano kati ya sehemu zake
tofauti yamewekwa katika katiba, ambayo ni sheria kuu, na hayawezi kubadilishwa
katika ushirikisho wao bila kuungwa mkono na idadi mahsusi ya wabunge wa kutoka
Zanzibar na Bara ... wakipiga kura tofauti tofauti. Katiba inaweza kufanyiwa
marejeo na mahakama. Kuna aina mbili za serikali (serikali kuu na serikali za
sehemu za shirikisho), kila moja ikiwa na mamlaka yaliyoainishwa wazi. Kuna
mabunge ya shirikisho na ya sehemu yake ... na sheria za shirikisho na za
sehemu yake zikitumika katika nchi.”[13]
MTAZAMO WA TUME
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba
(‘Tume’) imetoa maelezo marefu kuhusu madhumuni, lengo na sababu za mapendekezo
ya ibara ya 1 ya Rasimu. Pamoja na mengine, kwa mujibu wa Tume, “... lengo la ibara hii ni kuainisha aina na
hadhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Muungano wa Shirikisho lenye
Mamlaka Kamili (Sovereign Federal State). Hatua hii ina lengo la kuimarisha
Muungano kwa kuipa Mamlaka ya Kidola Jamhuri ya Muungano na kubainisha
utambulisho, uwezo na mamlaka ya Nchi Washirika katika Muungano.”[14]
Malengo mengine ambayo Tume
imeyataja malengo mengine kuwa ni “...
kuainisha mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Muungano na kupanua misingi muhimu ya
nchi ...”; na kuonyesha kuwa “Hati ya
Muungano ya 1964 ndio chimbuko la Muungano wa Tanzania ... na ... kuipa hadhi
ya kikatiba Hati hiyo ... kwa ... (kuiingiza) ndani ya Katiba kama ibara
inayosimama yenyewe.”[15]
Tume imetaja sababu za
mapendekezo haya kuwa ni kutekeleza matakwa ya kifungu cha 9(2)(a) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83,
yaliyoitaka Tume “... kuongozwa na
misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya jamii ya kuhifadhi na kudumisha kuwepo
kwa Jamhuri ya Muungano.”[16]
Aidha, kwa mujibu wa Tume, mapendekezo haya yatahifadhi asili, taswira na hadhi
ya Jamhuri ya Muungano katika jumuiya ya kimataifa kama inavyotakiwa na Mkataba wa Montevideo Kuhusu Haki na Wajibu
wa Nchi wa mwaka 1933, ambao unatambua nchi yenye muundo wa shirikisho kuwa
ni dola katika sheria za kimataifa.[17]
Tume imetambua ukweli wa
kihistoria kwamba kumekuwepo mjadala wa miaka mingi miongoni mwa Watanzania “kuhusu aina ya Muungano uliopo Tanzania
iwapo ni shirikisho au la.”[18]
Kwa sababu hiyo, pendekezo hili litaondoa
“utata wa aina na muundo wa Muungano ambao umesababisha kuvunjwa kwa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano na Serikali zote mbili mara kadhaa.”[19]
Tume iliridhika kwamba
Jamhuri ya Muungano ni Shirikisho. Kwa maneno yake: “Shirikisho hili linatokana na muungano wa hiari wa Tanganyika na
Zanzibar ambazo zilikuwa Jamhuri zenye mamlaka kamili kabla ya kuungana tarehe
26 Aprili 1964.”[20]
Tume inafafanua kwamba, kwa kawaida nchi ambazo zimeingia katika muungano
zinaweza kuchukua moja kati ya sura tatu:
i.
Muungano
wa Serikali Moja (Unitary State);
ii.
Muungano
wa Shirikisho (Federation); na
iii.
Muungano
wa Mkataba (Confederation).
Kwa mujibu wa Tume, “... mfumo wa shirikisho unakuwepo pale
ambapo nchi mbili au zaidi zimeungana na hazikuunda serikali moja. Kwa maana
hiyo shirikisho ... linamaanisha mfumo wa utawala wa nchi wenye sifa zifuatazo:
- Kunakuwa na ngazi mbili za serikali
zonazotawala eneo moja la nchi na raia wale wale; moja ikisimamia mambo ya
muungano (shirikisho) na nyingine mambo yasiyo ya muungano (yasiyo ya
shirikisho);
- Kila ngazi ya serikali, yaani ile ya
shirikisho na ile ya nchi washirika inakuwa na mamlaka kamili na maeneo ya
utendaji na uhakikisho wa kikatiba wa uhuru wa kutoingiliana baina ya
serikali hizo katika maeneo waliyo na madaraka nayo bila ya
kushauriana....;
- Katika muundo huu, serikali ya muungano
ndiyo yenye mamlaka juu ya masuala yote yaliyokubaliwa kuwa ya muungano
(shirikisho). Serikali za nchi washirika zinakuwa na mamlaka ya kikatiba
ya kushughulikia mambo yasiyo ya muungano katika maeneo yao ya utawala; na
- Katika muungano wa shirikisho mamlaka kuu
ya kidola (sovereign
powers and functions) yapo chini
ya serikali ya shirikisho (muungano).”[21]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Pamoja na kushindwa kufikisha
idadi ya kura inayotakiwa na kifungu cha 26(2) cha Sheria na kanuni ya 64(1),
Wajumbe walio wengi – karibu wote wanachama wa CCM – wamependekeza kufutwa kwa
ibara ya 1(1) na (2) ya Rasimu. Badala yake, wajumbe hao wanapendekeza ibara
mpya ya 1(1) isomeke kama ifuatavyo: “Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ni nchi yenye mamlaka kamili ambayo imetokana na
Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar,
ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.”[22]
Tofauti pekee ya mapendekezo
haya na mapendekezo ya ibara ya 1(1) ya Rasimu ni neno ‘Shirikisho.’ Hii ina
maana kwamba, licha ya ushahidi mkubwa wa kitaalamu tuliouonyesha hapa, wajumbe
walio wengi wa Kamati Namba Nne wanaamini kwamba Jamhuri ya Muungano sio
Shirikisho. Kwa mapendekezo haya, wajumbe na wanachama hawa wa CCM
wanapendekeza kuendeleza status quo,
yaani sintofahamu ya kama Muungano huu ulitengeneza dola ya ki-Shirikisho au
dola ya ki-Muungano, ambayo imeugubika Muungano kwa nusu karne ya uhai wake.
Mapendekezo haya yataendeleza pia migogoro ya kikatiba na ya kisiasa ambayo
imekuwa ni sehemu ya uhai wa Muungano huu katika kipindi hicho hadi kubatizwa
jina la ‘Kero za Muungano.’
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kwa kuzingatia uchambuzi huu,
ni wazi kwamba kuendelea kutumia jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ kunaendeleza
hisia potofu kwamba Makubaliano ya Muungano yalianzisha dola ya muungano (unitary state) na sio dola ya shirikisho
(federal state). Aidha, kufanya hivyo
ni kuendeleza migogoro ya kisiasa na ya kikatiba ambayo, kama tulivyoonesha,
imetokana na kukosekana kwa ufafanuzi juu ya aina ya muungano uliotokana na
Hati ya Makubaliano ya Muungano. Hii, kwa maoni yetu, haiwezi kuwa dawa ya
matatizo ya Muungano huu.
Kwa sababu hiyo, ili kuweka
wazi aina ya muungano uliozaliwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano; ili
kuondoa hisia potofu kwamba Makubaliano hayo yalizaa dola ya muungano, ili
kupata ufumbuzi wa kudumu wa ‘Kero za Muungano’, tunapendekeza kwamba maneno
‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ yaliyoko katika ibara ya 1 na ya 2 na katika
ibara nyingine zote za Rasimu yafutwe, na badala yake maneno ‘Shirikisho la Jamhuri
za Tanganyika na Zanzibar’ yaingizwe katika ibara husika.
Mapendekezo yetu yana manufaa
makubwa yafuatayo. Kwanza, yanaweka wazi kwamba muungano huu ni wa dola ya ki-Shirikisho
na wala sio dola ya ki-Muungano. Pili, mapendekezo haya yanaweka bayana ukweli
kwamba ni nchi mbili huru, yaani Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar ndizo zilizoungana. Uzoefu wa nchi nyingine zilizoungana unaonyesha
kwamba jina la muungano huweka bayana kwamba zilizoungana ni nchi zaidi ya
moja. Mifano ya wazi ya jambo hili ni majina ya Marekani (United States of
America); Uingereza (United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland), na
Umoja wa Falme za Kiarabu (United Arab Emirates). Aidha, Urusi ya zamani
ilijulikana kama (Union of Soviet Socialist Republics) na Yugoslavia ya zamani
ilikuwa inaitwa Federal Socialist Republics of Yugoslavia.
EXIT ‘TANGANYIKA’ ENTER ‘TANZANIA’!
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kuna sababu nyingine ya
kuacha kutumia jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Sababu hiyo ni utata
wa kisheria na kikatiba ambao umegubika jina la ‘Tanzania’ tangu lilipoanza
kutumiwa nusu karne iliyopita. Ili kufahamu vyema jambo hili ni vizuri kuanzia
‘Hati ya Kuzaliwa ya Muungano’, yaani Hati ya Makubaliano ya Muungano. Kwa
maudhui yake, Hati hiyo inaonyesha wazi kwamba jina la Jamhuri mpya
itakayoundwa kwa mujibu wake ni ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.’
Jina hili linathibitishwa na Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar,[23]
iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Tanganyika, siku tatu tu baada ya Hati ya
Muungano kusainiwa: “Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitakuwa, kuanzia Siku ya Muungano na
milele baada ya hapo, zimeungana kuwa Jamhuri moja yenye mamlaka kamili
itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.”[24]
Sheria hiyo ilitungwa na
Bunge Maalum, sio na Bunge la kawaida, na kwa sababu hiyo ina haiba ya katiba.
Ndio maana tangu mwaka 1965 kwenye Katiba ya Muda, na hadi sasa kwenye Katiba
ya Jamhuri ya Muungano, Sheria hiyo ni Nyongeza kwenye Katiba ya Jamhuri ya
Muungano na haiwezi kubadilishwa bila kuungwa mkono na theluthi mbili ya
wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakikaa kama wajumbe wa Bunge
Maalum.[25]
Hata hivyo, mnamo tarehe 3
Disemba, 1964, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar – likiwa
limekaa kama Bunge la kawaida - lilitunga Sheria
ya Kutangaza Jina la Jamhuri ya Muungano, ya mwaka 1964, yaani, The United Republic (Declaration of Name)
Act, 1964.[26]
Sheria hiyo ilibadilisha masharti ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano ambacho kilitangaza
jina la Jamhuri ya Muungano kuwa ni ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.’
Kifungu cha 2(1) cha Sheria
hiyo mpya kilitamka kwamba: “Bila kujali
masharti ya kifungu cha 4 cha Sheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,
inatangazwa kwamba kuanzia sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
itajulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria zilizopo za
Tanganyika na Zanzibar zitatafsiriwa hivyo hivyo.” Mabadiliko haya ya jina
la Jamhuri ya Muungano ni mfano mwingine wa utamaduni wa ukiukaji sheria (culture of illegality) ambao umegubika
Muungano huu tangu siku ya kwanza ya kuzaliwa kwake:
(a)
Kwa
mujibu wa aya ya (iv) ya Hati ya Makubaliano ya Muungano, Bunge la Jamhuri ya
Muungano halikuwa na mamlaka ya kubadilisha jina la Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar;
(b)
Kwa
kuwa Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano ilitungwa na Bunge Maalum, na
kwa hiyo ina haiba ya Katiba, Sheria ya Kutangaza Jina la Jamhuri ya Muungano –
ambayo ni sheria ya kawaida – ni batili kwa vile na kwa kiasi inavyokinzana na
Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano;
(c)
Jina
la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ lilianza kutumiwa hata kabla ya Sheria ya Kutangaza Jina la Jamhuri ya
Muungano kutungwa:
(i)
Kifungu
cha 2(2) cha Sheria hiyo kinasema kwamba “kutajwa
kwa Jamhuri ya Muungano kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi
chochote kati ya tarehe ishirini na nane ya Oktoba, 1964 na kuanza kutumika kwa
Sheria hii kutachukuliwa kuwa ni kutajwa kihalali na muafaka na uhalali wa
tendo lolote hautahojiwa kwa sababu tu ya matumizi ya (jina hilo) badala ya
lile la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.” Hii inadhihirisha
kwamba jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ lilianza kutumika tarehe 28
Oktoba, 1964, bila ya uhalali wowote wa kisheria[27];
(ii)
Tarehe
2 Novemba, 1964, yaani mwezi mmoja kabla ya Sheria
ya Kutangaza Jina la Jamhuri ya Muungano kutungwa, Ubalozi wa Kudumu wa
Jamhuri ya Tanganyika katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani,
ulimtumia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa waraka wa kidiplomasia (note verbale) ukimjulisha kwamba “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar, kuanzia sasa, itajulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Waraka huo haukuwa
na jina, cheo wala sahihi ya Ofisa wa Ubalozi wa Kudumu aliyeutuma lakini
uligongwa muhuri wenye nembo ya taifa iliyoandikwa ‘Jamhuri ya Tanganyika.’
Kifungu cha 12 cha Sheria ya Nembo za
Taifa, yaani National Emblems Act,
Sura ya 10 ya Sheria za Tanzania, kinaelekeza kwamba “popote nembo ya taifa inapotumiwa katika waraka au kitu chochote,
matumizi hayo yatahalalishwa au kuthibitishwa na sahihi ya mtunzaji wa nembo
hiyo.”
Kwa vile note verbale iliyomjulisha Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya jina la Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwekewa nembo
ya taifa ya Tanganyika bila kusainiwa na mtunzaji wa nembo hiyo, ni wazi kwamba note verbale hiyo haikuwa na uhalali
wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kwa sababu ya mazingira ya
kisiasa ya utawala wa kiimla wa chama kimoja, kwa miaka mingi ilikuwa vigumu
kuhoji uhalali wa matumizi ya jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Hata
hivyo, wapo watu wachache ambao wamehoji uhalali wa jina hili. Hivyo, kwa
mfano, marehemu George Liundi, aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kwanza
mara baada ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vya siasa nchini aliwahi kusema
yafuatayo katika Kongamano la Vyama vya Siasa lililofanyika katika Hotel ya
Golden Tulip, Dar es Salaam, kati ya tarehe 12-14 Disemba, 2002:
“Prior
to the enactment of the Interim Constitution of 1965, another constitutional
problem appears to have been created by the change of name of the United
Republic of Tanganyika and Zanzibar to the United Republic of Tanzania, with
effect from 11th December 1964.... This change of name calls for
scrutiny, because on the face of it the measure appears to have put into
question the constitutional status (in terms of national sovereignty) of both
the territories formerly constituting the Republic of Tanganyika and Zanzibar
respectively.”
Kwa maneno mengine:
“Kabla
ya kutungwa kwa Katiba ya Mpito ya 1965, tatizo lingine la kikatiba linaelekea
lilitengenezwa na mabadiliko ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar kwenda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzia tarehe 11 Disemba,
1964.... Mabadiliko haya ya jina yanahitaji kuchunguzwa kwa sababu, kwa juu juu
tu hatua hii inaonekana ilihoji hadhi ya kikatiba (kwa maana ya uhuru wa
kitaifa) wa maeneo ambayo yalijumuisha Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.”[28]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Ni wazi, kwa misingi hii ya
kisheria, jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ ni batili kisheria, licha
ya ukweli kwamba limetumika kwa nusu karne. Kwa maoni yetu, kama kweli
tunaamini – kama inavyopendekeza Tume - kwamba ‘msingi mkuu’ wa Jamhuri ya
Muungano ni Hati ya Makubaliano ya Muungano, wakati umefika wa kuyaheshimu
Makubaliano ya Muungano kwa kurudisha matumizi ya jina lililotumiwa katika
Makubaliano hayo, yaani Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
‘HATI YA MAKUBALIANO YA
MUUNGANO’
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Tarehe 22 Aprili, 1964 Rais
wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius K. Nyerere, na Rais wa Jamhuri ya Watu
wa Zanzibar, Sheikh Abedi Amani Karume walitia saini Hati ya Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hati hiyo ndiyo inayotajwa katika ibara ya
1(1) na (3) ya Rasimu. Wakati wa mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Sita, wajumbe
wa Kamati Namba Nne – kama ilivyokuwa kwa wajumbe wa Kamati nyingine za Bunge
lako tukufu – waliletewa nakala ya Sheria
ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano, Sheria Na. 22 ya 1964, yaani The Union of Tanganyika and Zanzibar Act,
Sura ya 557 ya Sheria za Tanzania. Nakala ya Sheria hiyo ilitolewa baada ya
baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum kuomba kupatiwa nakala halisi ya Hati ya
Makubaliano ya Muungano iliyosainiwa na Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume.
Ijapokuwa nakala ya Sheria ya
Kuthibitisha Mapatano ya Muungano waliyogawiwa wajumbe imeambatanisha Hati ya Makubaliano ya Muungano kati ya
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kama Nyongeza ya
Sheria hiyo, hicho sicho walichoomba wajumbe wa Bunge Maalum. Nakala ya Sheria
ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano sio, na haiwezi kuwa, mbadala wa nakala
halisi ya Hati ya Makubaliano ya Muungano. Hii ni kwa sababu, Nyongeza ya
Sheria waliyogawiwa wajumbe – ambayo inadaiwa kuwa ndio Hati ya Makubaliano ya
Muungano - haina saini za Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume. Ni vigumu, kwa
hiyo, kuthibitisha kama kweli kile kinachodaiwa kuwa ni Hati ya Makubaliano ya
Muungano ndicho hicho walichokubaliana waasisi hao wa Muungano kwa kutia saini
zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Suala la kushindwa kupatikana
kwa nakala halisi ya Hati ya Makubaliano ya Muungano sio jambo dogo. Suala hili
ndio ufunguo wa kuelewa mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisiasa ambao umeugubika
Muungano katika nusu karne ya maisha yake. Hii ni kwa sababu, katika kipindi
chote hicho, kumekuwa na mgogoro mkubwa kuhusu kitu gani hasa Mwalimu Nyerere
na Sheikh Karume walikubaliana kwa niaba ya nchi zao. Bila kupatikana kwa
nakala halisi ya Hati, uhalali mzima wa Muungano wenyewe, na wa mambo yote
yaliyofanyika kwa jina la Muungano kwa takriban nusu karne, unakuwa kwenye
mashaka makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Siku moja baada ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuzaliwa, yaani tarehe 27 Aprili 1964,
Mwanasheria Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. C.A.
Stavropoulos alimwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. U Thant, waraka
wa kiofisi uliohusu ‘Uanachama Katika Umoja wa Mataifa wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar.’ Kwa mujibu wa Bw. Stavropoulos, waraka wake
ulitokana na taarifa za vyombo vya habari zilizoonyesha kwamba Tanganyika na
Zanzibar, ‘ambazo kabla zilikuwa
wanachama tofauti wa Umoja wa Mataifa’, zilikuwa zimeungana na kuunda dola
moja yenye uwakilishi wa pamoja nchi za nje. Kwa vile Serikali za Jamhuri ya
Tanganyika na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zilikuwa hazijapeleka
taarifa rasmi Umoja wa Mataifa juu ya Muungano wa nchi zao, Bw. Stavropoulos
alipendekeza kwamba “mwakilishi wa
Tanganyika ataarifiwe juu ya haja ya kupata tamko rasmi kutoka kwa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano ... kuhusu kuanzishwa kwa Jamhuri hiyo ... na hati mpya za
utambulisho wa mwakilishi mmoja kutoka Jamhuri (ya Muungano). (Itakuwa vizuri
vile vile kwa mwakilishi husika kutupatia nakala ya makubaliano yaliyopelekea
Muungano huo.)”
Ijapokuwa tarehe 6 Mei, 1964,
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ilipeleka taarifa ya maandishi iliyodai kuambatanisha nakala ya Hati ya
Makubaliano ya Muungano, kuna mashaka ya msingi kama kweli Hati hiyo ilipelekwa
Umoja wa Mataifa. Hii ni kwa sababu, tarehe 14 Mei, 1964, yaani wiki moja
baadae na takriban wiki tatu baada ya Muungano, Bw. Stavropoulos alimwandikia Deputy Chief de Cabinet wa Umoja wa
Mataifa Bw. Jose Rolz-Bennett kumwelekeza apeleke ujumbe wa simu ya maandishi
kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuhusu masharti ya kusajili Hati ya
Makubaliano ya Muungano katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kama
inavyotakiwa na ibara ya 102 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa. “... Serikali inayosajili inatakiwa
kuwasilisha kwa Sekretarieti nakala moja ya Makubaliano iliyothibitishwa kwamba
ni nakala ya kweli na kamili ... nakala mbili za ziada na taarifa inayohusu
tarehe na namna ya kutiliwa nguvu Makubaliano hayo.”[29]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sasa kuna uthibitisho kwamba
Serikali ya Jamhuri ya Muungano haijawahi kuwasilisha Hati ya Makubaliano ya
Muungano katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa. Tarehe 25 Machi 2009, Afisa
Habari za Kisheria kwenye Kitengo cha Mikataba ya Kimataifa katika Ofisi
inayoshughulikia masuala ya kisheria ya Umoja wa Mataifa Bw. Andrei Kolomoets, alimtaarifu
mtafiti mmoja kwa maandishi kwamba: “Hakuna
ushahidi wowote kwamba Hati ya Makubaliano ya Muungano ilisajiliwa kwenye
Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa. Kama ingesajiliwa, kungelikuwa na hati ya
usajili iliyoambatanishwa. Nimeangalia, hakuna kitu hicho.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kwa miaka yote hamsini ya
Muungano, nakala ya Hati ya Makubaliano ya Muungano haijawahi kuonyeshwa
hadharani. Aidha, hata ilipodaiwa mahakamani katika Mahakama Kuu ya Zanzibar,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Iddi Pandu Hassan, alisema
katika barua yake ya tarehe 22 Juni, 2005 kwamba: “Ofisi yangu haikuweka kumbu kumbu ya nakala ya mkataba wa asili
(original) wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hapo tarehe 26 Aprili, 1964.”[30]
Kwa ushahidi huu kutoka Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa, na wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, hakuna
shaka tena kwamba Hati ya Makubaliano inayozungumzwa katika ibara 1(1) na (3)
ya Rasimu haijawahi kuwepo. Hii ndio kusema kwamba hakuna ajuaye ni kitu gani
hasa Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume walisaini siku hiyo ya tarehe 22 Aprili,
1964. Kwa maoni yetu, hiki ndio chanzo cha sintofahamu na migogoro yote kuhusu
Muungano huu.
UTEKELEZAJI WA ‘MAKUBALIANO
YA MUUNGANO’
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Hata kama tukikubali, in arguendo, kwamba kile kilichopo
kwenye Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano ndio Hati yenyewe ya
Makubaliano ya Muungano, bado kuna hoja kubwa na ya msingi kwamba Hati hiyo
haiwezi kuwa msingi wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar
tunalolipendekeza. Hii ni kwa sababu, katika miaka hamsini tangu kusainiwa kwa
Hati ya Makubaliano ya Muungano na kuzaliwa kwa Muungano, Makubaliano hayo
yamechakachuliwa na kuvunjwa karibu kila mahali na kwa kipindi chote cha kuwepo
kwa Jamhuri ya Muungano. Kabla hatujaanika uchakachuaji huu, ni muhimu
tuyarejelee masharti yaliyomo kwenye hiyo inayoitwa Hati ya Makubaliano ya
Muungano.
Aya ya (i) ya Hati ya
Makubaliano inatamka kwamba “Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitaungana na kuwa Jamhuri moja
huru.” Aya ya (ii) inaweka Kipindi cha Mpito cha kuanzia tarehe ya kuanza
kwa Muungano hadi tarehe ya Bunge Maalum kukutana na kupitisha Katiba kwa ajili
ya Jamhuri ya Muungano. Katika kipindi hicho “... Jamhuri ya Muungano itaongozwa kwa mujibu wa masharti ya aya za
(iii) hadi (vi) za Hati ya Makubaliano.”
Masharti hayo ni kuwa katika
kipindi hicho cha mpito, Jamhuri ya Muungano itaongozwa na Katiba ya Tanganyika
ambayo itarekebishwa ili kuwezesha kuwepo kwa bunge na serikali ya na kwa ajili
ya Zanzibar ambayo itaundwa kwa mujibu wa sheria za Zanzibar na yenye mamlaka
kamili ndani ya Zanzibar kwa mambo yote isipokuwa kwa mambo ambayo yametengwa
kwa ajili ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.[31]
Aidha, kutakuwa na Makamu
wawili wa Rais ambapo mmoja wao (ambaye kwa kawaida ni mkazi wa Zanzibar)
atakuwa Mkuu wa Serikali ya na kwa ajili ya Zanzibar na atakuwa msaidizi mkuu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika utekelezaji wa majukumu yake kuhusu
Zanzibar.[32]
Vile vile, kutakuwa na uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano[33];
na mambo mengine yatakayohitajika ili kuipa uwezo Jamhuri ya Muungano na Hati
za Muungano.[34]
Masharti mengine ni kuwapo
kwa orodha ya Mambo ya Muungano ambayo Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
zilipewa mamlaka kamili kwa Jamhuri ya Muungano yote nje ya mamlaka yake kamili
kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano ya na kwa ajili ya Tanganyika.[35]
Mambo ya Muungano ni pamoja na Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; mambo
ya nje; ulinzi; polisi; mamlaka ya hali ya hatari; uraia; uhamiaji; biashara ya
nje na mikopo; utumishi wa umma wa Jamhuri ya Muungano; kodi ya mapato, kodi ya
mashirika na ushuru wa forodha na wa bidhaa; na bandari, usafiri wa anga, posta
na simu.
Masharti mengine ni kwamba
sheria zilizokuwepo Tanganyika na Zanzibar kabla ya Muungano zitaendelea
kutumika ‘katika maeneo yao’ hadi hapo zitakaporekebishwa ili kutilia nguvu
Muungano na Hati za Muungano; au sheria mpya zitakapotungwa na mamlaka husika
au kutolewa kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya utekelezaji wa
Mambo ya Muungano kwa upande wa Zanzibar. Masharti ya mwisho ni kutangazwa kwa
Mwalimu Julius K. Nyerere kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano[36],
na Sheikh Abeid Karume kuwa Makamu wa Rais kutoka Zanzibar.[37]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kwa mujibu wa aya ya (vii) ya
Hati ya Muungano, Rais wa Jamhuri ya Muungano alipaswa, kwa makubaliano na
Makamu wa Kwanza wa Rais, kuteua Tume kwa ajili ya kuandaa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano[38];
na kuitisha Bunge Maalum lenye wawakilishi kutoka Tanganyika na kutoka Zanzibar
na kwa idadi watakayoamua kwa lengo la kujadili na kupitisha Katiba ya Jamhuri
ya Muungano.[39]
Bunge hilo Maalum lilitakiwa kuitishwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia
tarehe ya kuzaliwa Muungano, yaani tarehe 26 Aprili, 1964.[40]
Hiki ndicho kilikuwa kipindi cha mpito kinachotajwa katika aya ya (ii) ya Hati
ya Makubaliano.
Aya ya (viii) na ya mwisho ya
Hati ya Makubaliano ililazimu Hati ya Makubaliano ya Muungano kuthibitishwa kwa
Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri la Zanzibar
kutunga sheria za kuridhia Hati ya Makubaliano na kuanzishwa kwa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar kwa mujibu wa Hati ya Makubaliano.
HISTORIA YA UCHAKACHUAJI
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sasa tunaomba tuthibitishe
hoja yetu kwamba miaka hamsini ya Hati ya Makubaliano ya Muungano na ya
Muungano ni nusu karne ya uchakachuaji na ya nchi yetu kuishi kwa uongo na ujanja
ujanja:
- Wakati Bunge
la Tanganyika liliitishwa kwa dharura tarehe 25 Aprili, 1964 ili kupitisha
sheria ya kuthibitisha Hati ya Makubaliano ya Muungano, na lilipitisha Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, upo ushahidi wa kutosha kwamba
Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri la Zanzibar halijawahi kutunga
sheria yoyote ya kuthibitisha Hati ya Makubaliano ya Muungano kwa kipindi
chote cha maisha ya Muungano huu:
(a)
Profesa
Issa G. Shivji katika kitabu chake Pan
Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika – Zanzibar Union amethibitisha
kwamba kile kinachoitwa Sheria ya Kuthibitisha Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ya mwaka 1964 “... iliandaliwa
na kuandikwa na maafisa wa sheria wa Tanganyika wakiwa Tanganyika.... Hii ni
kwa sababu ya ukweli wa kisiasa uliokuwapo wakati huo ambapo Baraza la
Mapinduzi kwa ujumla wake halikuukubali Muungano. Hakuna shaka kwamba Muungano
‘ulilazimishwa.’ Hivyo, maafisa wa kisheria wa kigeni wa Serikali ya Tanganyika
(waliokuwa pia marafiki wa Nyerere) walitumia mbinu ya kisheria ya kuchapisha
Sheria ya Kuthibitisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, 1964, (inayodaiwa
kutungwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar) waliyoitengeneza wao, katika Gazeti
rasmi la Serikali ya Jamhuri ya Muungano chini ya saini ya (Kaimu Mwanasheria
Mkuu wa Tanganyika) P.R. Nines Fifoot.”
(b)
Aliyekuwa
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu wa Baraza la Mwaziri wa Serikali ya
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kati ya tarehe 18 Januari na Juni 1964, Salim Said
Rashid ametamka yafuatayo kwa kiapo cha tarehe 22 Aprili 2006:
(i)
Kwamba
hakuwahi “... kupokea maagizo kutoka kwa
Rais wa Zanzibar kwa ajili ya kuitisha kikao cha kujadili na kupitisha mkataba
wa kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika.”
(ii)
Kwamba
“suala la kuunganisha Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika halikuwahi kujadiliwa na kikao chochote cha
Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Zanzibar au kujadiliwa
na taasisi yoyote ya Serikali ya Zanzibar.”
(iii)
Kwamba
anakumbuka “... kupokea maagizo kutoka
kwa Rais wa Zanzibar kuwa anataka kuufanya Muungano na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na baadae alinionyesha mapendekezo ya rasimu
ya Muungano kati ya Jamhuri ya (Watu wa) Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika.”
(iv)
Kwamba
“... rasimu hiyo ililetwa na Mawaziri
kutoka Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na kukabidhiwa Rais ikiwa tayari
imeshaandikwa kuunganishwa Jamhuri hizi mbili.”
(v)
Kwamba
baada ya kuonyeshwa mapendekezo hayo ya Muungano, “... niliagizwa na Rais wa Zanzibar nisimwonyeshe mtu yoyote na wala
asipewe Mwanasheria wa Serikali ya Zanzibar.”
(vi)
Kwamba
“... sikupata maagizo yoyote kutoka kwa
Rais ili kuwajulisha viongozi wa Baraza la Mapinduzi juu ya kuitisha kikao au
kuja kushuhudia makubaliano ya kuunganisha nchi ya Zanzibar yakitiwa sahihi.”
(vii)
Kwamba,
kwa sababu hiyo, “... hakuna shughuli
yoyote au kikao kilichofanyika kwa ajili ya kutia saini mkataba wa Muungano kwa
mujibu wa decree Na. 5 ya mwaka 1964 ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar.”
(viii)
Bw.
Rashid anaelezea utaratibu wa kisheria uliotakiwa kufuatwa: “... Kwa mujibu wa Presidential Decree ya
1964, kila jambo lilitakiwa kujadiliwa na kikao cha Baraza la Mapinduzi na
kuarifiwa Mwanasheria Mkuu atayarishe presidential decree kwa mujibu wa
utaratibu na baadae sisi tusaini nikiwa mimi Katibu wa Baraza la Mapinduzi na
Baraza la Mawaziri Zanzibar na asaini Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
baadae kutolewa katika official gazette (gazeti rasmi la serikali) huo ndio
ulikuwa utaratibu.”
(ix)
Kwamba
kwa sababu utaratibu huo ulikiukwa, “...
kitendo cha kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika
hakikupata Baraka za Baraza la Mapinduzi na kuthibitishwa na kikao halali cha
Baraza la Mawaziri la Zanzibar.”
(c)
Katika
kitabu chake The Partner-ship, Alhaj
Aboud Jumbe amesema yafuatayo kuhusu kusainiwa kwa Makubaliano ya Muungano:
(i)
“Ilikuwa ni
asubuhi ya Aprili 22, 1964 pale Julius Kambarage Nyerere alipowasili Zanzibar.
Rais huyo wa Jamhuri ya Tanganyika alikuja na nakala ya mapendekezo ya Mkataba uliotayarishwa
Tanganyika na ulioandikwa kwa lugha ya Kiingereza. Waraka huo uliwakilisha
jumla ya makubaliano ambayo yalifikiwa siku hiyo hiyo baina ya Rais wa Jamhuri
ya Tanganyika, Julius Nyerere na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Abedi
Amani Karume. Makubaliano hayo kwanza kabisa yalitiwa sahihi katika Ikulu ya
Zanzibar na hapo baadae kuwa ndio Mkataba wa Muungano, 1964.”
(ii)
Aidha,
“mimi nilikuwa Mjumbe wa Baraza la
Mapinduzi, kwa wakati mmoja au mwengine, kwa cheo kimoja au chengine kutokea
kuanzishwa kwa Baraza hilo hapo Januari 1964 hadi mwaka 1984 na nimeshindwa
katika kumbukumbu zangu kupata ushahidi wa kufanyika kikao cha Baraza la
Mapinduzi kama ni Zanzibar au Dar es Salaam ili kuthibitisha Mkataba wa
Muungano.”
Kwa hiyo, Makubaliano ya
Muungano yalipata ridhaa ya upande mmoja tu, yaani Watanganyika kwa kupitia
Bunge lao, wakati Wazanzibari kwa kupitia Bunge lao, yaani Baraza la Mapinduzi,
hawakuwahi kutoa ridhaa yao kwa Muungano huu. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba - kwa
sababu hiyo - Jamhuri ya Muungano ilizaliwa bila uhalali wowote wa kisheria.
Kwa maneno ya Profesa Shivji, “Hakuna
shaka kwamba Muungano ‘ulilazimishwa.’”
(d)
Katika
kitabu chake kiitwacho 50 Years of
Independence: A Concise Political History of Tanzania, kilichochapishwa
Januari ya mwaka huu 2014, Mzee Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM
na Katibu Mtendaji wake wa kwanza amesema yafuatayo kuhusu mambo yaliyofanyika
baada ya Makubaliano ya Muungano kusainiwa:
(i)
Tarehe
26 Aprili, 1964, yaani Siku ya Muungano, Rais Nyerere alitunga Presidential
Decree (Amri ya Rais) iliyoitwa The
Transitional Provisions Decree, 1964, yaani, Amri ya Masharti ya Mpito ya mwaka 1964, iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali la siku hiyo.[41]
“Amri hiyo iliwabadilisha watu waliokuwa
watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na kuwafanya watumishi wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano.[42]
Mahakama Kuu ya Tanganyika iligeuzwa kuwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano[43];
na nembo ya taifa ya Jamhuri ya Tanganyika iligeuzwa kuwa nembo ya taifa ya
Jamhuri ya Muungano.”[44]
(ii)
Tarehe
hiyo hiyo, Rais Nyerere alitunga Amri nyingine ya Rais iliyoitwa The Interim Constitution Decree, 1964,
yaani, Amri ya Katiba ya Muda ya mwaka
1964.[45]
“Amri hii iliitangaza Katiba ya
Tanganyika kuwa ndiyo Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano.[46]
Kifungu cha 4 cha Amri hii ndicho kilichoipatia Serikali ya Muungano majukumu
kuhusu mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano yote na vile vile kwa
mambo yasiyokuwa ya Muungano kwa upande wa Tanganyika.”
(iii)
Tarehe
15 Juni 1964 Mwalimu Nyerere alitunga Amri nyingine tena iliyoitwa The Transitional Provisions (No. 2) Decree,
1964, yaani, Amri ya Masharti ya
Mpito (Na. 2) ya mwaka 1964. Amri hii ilielekeza kwamba mahali popote
ambapo sheria zilizopo zimetaja jina la ‘Tanganyika’ basi jina hilo lifutwe na
badala yake jina la ‘Jamhuri ya Muungano’ liwekwe. Vile vile, Amri hiyo
ilielekeza, mahali popote ambapo ‘Serikali ya Tanganyika’ imetajwa, au kwenye
jambo au kitu chochote ambacho kwa namna yoyote kinamilikiwa au kinahusishwa na
Serikali hiyo, basi itachukuliwa kuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano ndiyo
iliyotajwa.
(iv)
Kwa
maneno ya Mzee Msekwa mwenyewe: “Tanganyika
was thus decreed out of existence. The cumulative effect of these legislative
measures was that the political entity which was Tanganyika, was decreed
totally out of existence. That is the reason why even the name of the
geographical unit formerly known as Tanganyika, had to be changed to Tanzania
Mainland.” Tafsiri ya maneno haya ni kwamba “uhai wa Tanganyika ulitolewa kwa njia hiyo ya amri. Athari za jumla za
Amri hizi ni kwamba eneo la kisiasa ambalo ndio ilikuwa Tanganyika lilitolewa
uhai wake moja kwa moja kwa amri. Hii ndiyo sababu hata jina la eneo la
kijiografia lililojulikana zamani kama Tanganyika ilibidi libadilishwe na kuwa Tanzania
Bara.”
- Vitendo vya
kuivika Jamhuri ya Tanganyika joho la Muungano na kuigeuza kuwa ndio
Jamhuri ya Muungano hakikuwa na uhalali wowote kwa mujibu wa Makubaliano
ya Muungano:
(a)
Aya
ya (v) ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ilitamka wazi kwamba “sheria zilizopo za Tanganyika na za
Zanzibar zitaendelea kutiliwa nguvu katika maeneo yao....” Kwa maana hiyo:
(i)
Rais
Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano wala
chini ya Katiba na Sheria za Tanganyika ya kugeuza sheria zote za Jamhuri ya
Tanganyika kuwa sheria za Jamhuri ya Muungano hata kwa mambo yasiyokuwa ya
Muungano;
(ii)
Rais
Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano wala kwa
mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kuwageuza watumishi wote wa Jamhuri
ya Tanganyika kuwa watumishi wa Jamhuri ya Muungano hata kwa mambo yasiyokuwa
ya Muungano;
(iii)
Rais
Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano au kwa
mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kugeuza Mahakama Kuu ya Tanganyika
kuwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano;
(iv)
Rais
Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano au kwa
mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kugeuza Nembo ya Taifa ya Jamhuri
ya Tanganyika kuwa Nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano. Nembo za Taifa, yaani
‘Bibi na Bwana’ inayotumika hadi leo hii ni Nembo ya Taifa ya Jamhuri ya
Tanganyika!
(v)
Rais
Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano au kwa
mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kufuta matumizi ya jina la
Tanganyika katika sheria zote za Jamhuri ya Tanganyika au katika mambo au vitu
vyote vilivyokuwa vinamilikiwa ama kuhusishwa na Jamhuri ya Tanganyika hata kwa
mambo yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika;
(vi)
Rais
Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano au kwa
mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya ‘kutoa uhai wa nchi ya Tanganyika
kwa njia ya Amri ya Rais’ au kwa njia nyingine yoyote ya kisheria na kuigeuza
kuwa Jamhuri ya Muungano.
MAMBO YA MUUNGANO
NA KUMEZWA KWA ZANZIBAR
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kama tulivyokwishaonesha, kwa
mujibu wa aya ya (iv) ya Makubaliano ya Muungano na kifungu cha 5(1) cha Sheria
ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano, Mambo ya Muungano yaliyokubaliwa kwenye
Makubaliano ya Muungano yalikuwa kumi na moja. Haya ni mambo yaliyoko katika
vipengele vya 1 hadi 11 vya Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya sasa ya Jamhuri ya
Muungano.
Hata hivyo, kati ya mwaka
1964 and 1973 mambo mengine sita – yanayoonekana katika vipengele 12 hadi 16
vya Nyongeza ya Kwanza – yaliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano. Hivyo
basi, mwaka 1965 masuala ya fedha, sarafu na benki yaliongezwa; mwaka 1967
leseni ya viwanda na takwimu, elimu ya juu na mambo yaliyokuwa katika Nyongeza
ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa; mwaka 1968
yaliongezwa mambo ya maliasili ya mafuta, petroli na gesi asilia; na mwaka 1973
mambo yanayohusu Baraza la Mitihani la Taifa yaliongezwa.
Aidha, Mabadiliko ya Tano ya
Katiba ya mwaka 1984 yaligawa kipengele cha Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki na kutengeneza vipengele vinne vinavyojitegemea katika
orodha ya Mambo ya Muungano, yaani usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti,
utabiri wa hali ya hewa na takwimu. Vile vile, Mabadiliko hayo yaliongeza kitu kipya
katika orodha ya Mambo ya Muungano: Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Aidha,
kipengele cha 3, yaani ulinzi, kilifanyiwa marekebisho na kuwa ‘ulinzi na
usalama.’ Na mwaka 1992 ‘uandikishwaji wa vyama vya siasa’ nao uliongezwa
katika orodha ya Mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mambo yote yaliyoongezwa
katika orodha ya Mambo ya Muungano baada ya mwaka 1964 yalikuwa nje ya
Makubaliano ya Muungano na nje ya Sheria ya Mapatano ya Muungano na kwa hiyo
yalikuwa batili. Hii ni kwa sababu Sheria ya Mapatano ya Muungano – na sio
Katiba za Muda za 1964 au 1965 au ya sasa - ndio Sheria Mama iliyozaa Muungano
na kuweka mgawanyo wa madaraka kati ya mamlaka za Jamhuri ya Muungano na
mamlaka za Zanzibar. Sheria ya Mapatano ya Muungano ilitungwa na Bunge la
Katiba tofauti na sheria za kawaida.
Aidha, Katiba ya Muda, 1965 iliyotawala Tanzania hadi 1977 iliiweka Sheria
ya Mapatano ya Muungano kama Nyongeza ya Pili katika Katiba na kuweka masharti
kwamba Sheria hiyo haiwezi kurekebishwa bila marekebisho hayo kuungwa mkono na
theluthi mbili ya Wabunge wote wa Tanganyika na wale wa Zanzibar. Vile vile,
Katiba ya sasa ya Muungano inataja
kwamba moja ya Sheria ambazo mabadiliko yake yahitaji kuungwa mkono na theluthi
mbili ya Wabunge wote ni “Sura ya 557
(Toleo la 1965), Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ya mwaka 1964.”[47]
Zaidi ya hayo, kwa mujibu wa
Katiba hiyo, Orodha ya Mambo ya Muungano haiwezi kufanyiwa ‘mabadiliko yoyote’
bila kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanganyika na
theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Zanzibar.[48]
Utafiti wetu umethibitisha kwamba hakuna nyongeza ya Mambo ya Muungano hata
moja iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kutumia utaratibu wa
kupigiwa kura ya kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge wote wa Tanganyika
na idadi hiyo hiyo ya wabunge wa kutoka Zanzibar.
Kifungu cha 5 cha Sheria ya
Muungano, ambacho ndicho chenye misingi mikuu ya Muungano hakijawahi
kurekebishwa tangu Sheria yenyewe ilipotungwa mwaka 1964. Badala yake, Bunge
limekuwa na tabia ya kukwepa kuigusa kabisa Sheria ya Muungano na badala yake
limekuwa likifanya marekebisho ya orodha ya Mambo ya Muungano iliyowekwa kwa
mara ya kwanza katika Katiba za Muda za mwaka 1964 na 1965 kwa kuongeza
vipengele katika orodha hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Lengo la marekebisho haya limekuwa
mara zote ni kuinyang’anya Zanzibar mamlaka yake chini ya Makubaliano ya
Muungano na Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano. Ndio maana katika Mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM Kuhusu
Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar yaliyotolewa tarehe 27 Januari, 1983, CCM ilitamka kwamba “... msingi wa kuwa na orodha ya mambo ya
muungano katika Katiba ni kuonyesha mamlaka ya Serikali ya Zanzibar ambayo
yalikabidhiwa kwa Serikali ya Muungano; na msingi wa kuongeza mambo zaidi
katika orodha ya mambo ya muungano, kama ambavyo imefanyika mara kwa mara, ni
kuhamisha mamlaka zaidi ya Serikali ya Zanzibar kwenda kwa Serikali ya
Muungano.”
Profesa Shivji anasema -
katika The Legal Foundations of the Union
- kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano halikupewa mamlaka ya kuongeza Mambo ya
Muungano bali lilipewa mamlaka ya kutunga sheria zinazohusu Mambo ya Muungano
kama yalivyofafanuliwa katika Sheria ya Muungano. Kwa maana hiyo, nyongeza zote
zilizofanyika katika orodha ya Mambo ya Muungano tangu mwaka 1964 zilikiuka
Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano na ni batili. Ndio maana, kwa
muda mrefu, Wazanzibari wamelalamikia masuala haya, hasa hasa masuala ya fedha,
sarafu na mafuta na gesi asilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Vitendo hivi vya kukiuka
Makubaliano ya Muungano vilipata Baraka za kikatiba mwaka 1984 wakati ibara
mpya ya 64(4) ya Katiba ya sasa ya Muungano ilipotungwa: “Katiba yoyote iliyotungwa na Bunge kuhusu jambo lolote haitatumika
Tanzania Zanzibar ila kwa mujibu wa masharti yafuatayo:
(a)
Sheria hiyo iwe
imetamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vile vile Tanzania Zanzibar au
iwe inafuta inabadilisha, kurekebisha au kufuta Sheria inayotumika Tanzania
Zanzibar; au
(b)
Sheria hiyo iwe
inabadilisha au kurekebisha au kufuta sheria iliyokuwa inatumika tangu zamani
Tanzania Bara ambayo ilikuwa inatumika pia Tanzania Zanzibar kwa mujibu wa
Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964, au kwa mujibu wa
Sheria yoyote ambayo ilitamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vile vile
Tanzania Zanzibar....”
Ibara hii ya Katiba ililipa
Bunge la Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kutunga ‘sheria yoyote’ kuhusu ‘jambo
lolote’, hata kama sio la Muungano na sheria hiyo itatumika Tanzania Zanzibar!
Ibara hii inakiuka moja kwa moja masharti ya aya ya iii(a) ya Makubaliano ya
Muungano ambayo ilisema wazi kwamba Bunge la Zanzibar “... litakuwa na mamlaka kamili ndani ya Zanzibar kwa mambo yale ambayo
hayajawekwa chini ya mamlaka ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano....”
Aidha, ibara hiyo inakinzana na ibara ndogo ya (2) ya ibara ya 64 inayotamka
kwamba “mamlaka yoyote ya kutunga sheria
katika Tanzania Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo mambo ya Muungano yatakuwa
mikononi mwa Baraza la Wawakilishi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Vitendo vya kupuuza
Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano vilifikia
kilele chake tarehe 21 Novemba, 2000 pale Mahakama ya Rufani ya Tanzania
ilipotamka – katika kesi ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar dhidi ya Machano Khamis Ali na Wenzake 17 – kwamba Zanzibar sio
nchi na wala sio dola. Bali, kwa mujibu wa Mahakama ya Rufani, “hakuna ubishi wa aina yoyote kwamba Jamhuri
ya Muungano ni nchi moja na dola moja.” Kama tulivyokwisha kuonyesha, suala
la Mahakama ya Rufani ya Tanzania yenyewe kuwa suala la Muungano liliingizwa
kwenye orodha ya Mambo ya Muungano kinyemela na kinyume na Makubaliano ya
Muungano na Sheria ya Muungano. Jibu la Wazanzibari juu ya ukiukwaji wa muda
mrefu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano
hayo lilikuwa ni kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar
mwaka 2010.
NCHI MOJA AU NCHI MBILI?
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Tarehe 13 Agosti, 2010,
wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano likiwa limevunjwa kwa ajili ya maandalizi
ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha Sheria
ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, 1984. Mabadiliko haya yaliweka
msingi wa kikatiba wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar inayoshirikisha
CCM na Chama cha Wananchi (CUF). Kwa sababu hiyo, Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba imepigiwa upatu kama Katiba ya Muafaka na, kwa kiasi fulani, hii ni
kweli.
Hata hivyo, Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba imekwenda mbali zaidi. Sheria hii sio tu imehoji uhalali
wa orodha ya Mambo ya Muungano ya tangu mwaka 1964 na nyongeza zake
zilizofuata, bali pia imehoji pia misingi muhimu ya Sheria ya Muungano
iliyoridhia Makubaliano ya Muungano. Kwa mtazamo huu, Katiba ya sasa ya
Zanzibar inaelekea kuwa ni tangazo la uhuru wa Zanzibar zaidi kuliko waraka wa
muafaka kati ya vyama viwili vilivyokuwa mahasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Aya ya (i) ya Makubaliano ya
Muungano na kifungu cha 4 cha Sheria ya Muungano vilitangaza muungano wa
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuundwa kwa “Jamhuri moja huru itakayoitwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.” Makubaliano ya Muungano hayakuua nchi
washirika wa Muungano huu. Hii inathibitishwa sio tu na masharti ya Makubaliano
ya Muungano yanayoashiria kuendelea kutumika kwa sheria za Tanganyika na
Zanzibar ‘katika maeneo yao’ tu, bali vifungu vya Katiba zilizofuatia
Makubaliano ya Muungano.
Hivyo basi, hata baada ya
mabadiliko ya jina kwenda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba na sheria
mbali mbali ziliendelea kutumia jina la Tanganyika na Zanzibar. Kwa mfano, Sheria ya Kuongeza Muda wa Kuitisha Bunge la
Katiba, 1965[49],
iliyosainiwa na Rais Nyerere tarehe 24 Machi, 1965, inataja, katika vifungu
vyote vitatu, ‘Sheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’
Aidha, Sheria ya Kutangaza Katiba ya Muda ya Tanzania ya tarehe 11 Julai,
1965[50],
ilitangaza kwamba ‘Tanzania ni Jamhuri Huru ya Muungano’[51];
kwamba eneo lake ni “... eneo lote la Tanganyika
na Zanzibar ...”[52]
na kwamba chama kimoja cha siasa “... kwa
Tanganyika kitakuwa Tanganyika African National Union (TANU)....”[53]
Kwa wakati wote wa uhai wake, Katiba ya Muda haikuwahi kutamka kuwa Tanzania ni
nchi moja. Kwa upande wake, licha ya kuanza kutumia jina la Tanzania Bara na
Tanzania Visiwani kwa mara ya kwanza[54],
Toleo la Kwanza la Katiba ya sasa ya Muungano lilitamka kwamba Tanzania ni
‘Jamhuri ya Muungano.’[55]
Hapa pia hapakuwa na tamko la ‘nchi moja.’
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Maneno ya ibara ya 1 ya
Katiba ya sasa ya Muungano kwamba “Tanzania
ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano” yaliingia katika kamusi ya kikatiba
na kisiasa ya nchi hii kufuatia ‘kuchafuka kwa hali ya kisiasa ya Zanzibar’ na
kung’olewa madarakani kwa Rais Aboud Jumbe. Kufuatia hali hiyo, Katiba ya
Jamhuri ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa[56]
ambayo, pamoja na mengine, yalitangaza kuwa “Tanzania
ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.”[57]
Kwa sababu ya upinzani mkubwa wa Wazanzibari, Marekebisho hayo ya Katiba yaliondoa
pia maneno ‘Tanzania Visiwani’ na kuweka ‘Tanzania Zanzibar’ badala yake.
Maneno ‘Tanzania Bara’ yalibaki kama yalivyowekwa mwaka 1977.
Kwa maana hiyo, dhana ya
Tanzania kama nchi moja haijatokana na Makubaliano ya Muungano bali ilitokana
na siasa za Muungano, yaani mvutano kati ya viongozi wa Tanganyika wakiwa
wamevalia joho la Jamhuri ya Muungano na viongozi wa Zanzibar waliotaka uhuru
zaidi kwa nchi yao. Pili, dhana hiyo haina umri mkubwa sana kuliko
inavyodhaniwa, kwani iliingia kwenye Katiba mwaka 1984, miaka thelathini
iliyopita, na miaka ishirini baada ya Muungano.
Tatu, Makubaliano ya Muungano
hayakuua Tanganyika, licha ya mabadiliko mengi ya kikatiba na ya kisheria ya
tangu siku za mwanzo kabisa za Muungano. Bali kilichoiondoa Tanganyika katika
lugha ya kikatiba na kisheria ni Katiba ya sasa ya Muungano pale ilipoacha
kutumia neno Tanganyika na badala yake ikaingiza neno ‘Tanzania Bara’ mwaka
1977.
Sasa mabadiliko haya ya
Katiba ya Muungano yamehojiwa na maneno ya ibara ya 2 ya Katiba mpya ya Zanzibar
yanayotamka kwamba “Zanzibar ni miongoni
mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Kwa maneno
haya, Zanzibar imeturudisha rasmi kwenye Makubaliano ya Muungano kwamba Jamhuri
ya Muungano haikuzaliwa kutokana na kifo cha nchi mbili zilizoungana, bali nchi
hizo zimeendelea kuwepo. Kwa maana hiyo, Katiba ya Zanzibar ni tangazo la uhuru
wa Tanganyika vile vile, kwani kwa miaka hamsini Tanganyika imejificha nyuma ya
pazia la Tanzania.
Ibara ya 2(2) ya Katiba ya
Muungano inampa Rais wa Jamhuri ya Muungano – kwa kushauriana kwanza na Rais wa
Zanzibar - mamlaka ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo
mengineyo. Vile vile, ibara ya 61(3) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa
Zanzibar mamlaka ya kuteua Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar ‘baada ya
kushauriana na Rais.’ Masuala ya mgawanyo wa nchi katika mikoa na mamlaka za
mikoa hiyo sio, na hayajawahi kuwa, Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya
Muungano. Vile vile hayapo katika orodha ya Mambo ya Muungano.
Ni wazi kwa hiyo, kwamba
ibara za 2(2) na 61(3) za Katiba ya Muungano zilikuwa zinakiuka matakwa ya
Sheria ya Muungano na kwa hiyo ni batili. Sasa wazanzibari ‘wamejitangazia
uhuru’ kwa kutangaza – katika ibara ya 2A ya Katiba mpya ya Zanzibar – kwamba “... Rais (wa Zanzibar) aweza kuigawa
Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu
uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.” Aidha, kwa ibara
ya 61(1), Rais wa Zanzibar hawajibiki tena kushauriana na Rais wa Muungano pale
anapofanya uteuzi wa wakuu wa mikoa ya Zanzibar.
Wakati ambapo Sheria ya
Muungano ilikuwa imetambua na kuhifadhi mamlaka ya Rais wa Zanzibar kama mkuu
wa dola ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Tanzania – katika Kesi ya Machano Khamis Ali na Wenzake –
ilitishia moja kwa moja msingi huo kwa kutamka kwamba Zanzibar sio nchi na wala
sio dola na kwa hiyo haiwezi kutishiwa na kosa la uhaini. Sasa ibara ya 26(1)
ya Katiba mpya Zanzibar ‘imerudisha’ dola ya Zanzibar kwa kutamka kwamba “kutakuwa na Rais wa Zanzibar ambaye atakuwa
Mkuu wa Nchi ya Zanzibar, Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi.”
Aidha, kwa kutambua kwamba
‘Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano’ sio moja ya Mambo ya Muungano kwa
mujibu wa Sheria ya Muungano, Katiba ya sasa ya Zanzibar imetamka kwamba katika
kesi zinazohusu ‘kinga za haki za lazima, wajibu na uhuru wa mtu binafsi’,
uamuzi wa majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar “... utakuwa ni wa mwisho na hautokatiwa rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa
ya Tanzania.”
Kifungu cha 5(1)(a)(iii) na
(iv) cha Sheria ya Muungano kinataja ‘ulinzi’ na ‘polisi’ kama sehemu ya mambo
kumi na moja ya Muungano. Na hivyo ndivyo inavyosema aya ya (iv)(c) na (d) ya
Makubaliano ya Muungano. Ijapokuwa ‘ulinzi’ ulichakachuliwa baadae kwa
kuongezwa maneno ‘na usalama’, bado ni sahihi kusema kwamba masuala ya ulinzi
na polisi ni masuala halali ambayo Sheria ya Muungano iliyakasimu kwa Serikali
ya Muungano. Na kwa sababu hiyo, ni sahihi kwa Katiba ya Muungano kutamka –
kama inavyofanya katika ibara ya 33(2) - kwamba “Rais (wa Jamhuri ya Muungano) atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa
Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.”
Hata hivyo, katika kile
kinachoonekana kama hojaji kubwa ya msingi huu wa Makubaliano ya Muungano na
Sheria ya Muungano, ibara ya 121 ya Katiba ya sasa ya Zanzibar imeunda majeshi
ya Zanzibar inayoyaita ‘Idara Maalum.’ Majeshi haya, kwa mujibu wa ibara ya
121(2) ni Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU); Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo
(KMKM); Chuo cha Mafunzo (cha wahalifu), na Idara Maalum nyingine yoyote ambayo
Rais wa Zanzibar anaweza kuianzisha ‘ikiwa ataona inafaa....’
Kuthibitisha kwamba Idara
Maalum ni majeshi, ibara ya 121(4) inakataza watumishi wa Idara Maalum ‘...
kujishughulisha na mambo ya siasa....’ Makatazo haya hayatofautiani na makatazo
ya wanajeshi kujiunga na vyama vya siasa yaliyoko katika ibara ya 147(3) ya
Katiba ya Muungano.
Sio tu kwamba Katiba mpya ya
Zanzibar inaanzisha majeshi bali pia inamfanya Rais wa Zanzibar kuwa Amiri
Jeshi Mkuu wa majeshi hayo. Kwa mujibu wa ibara ya 123(1) ya Katiba hiyo, “Rais atakuwa Kamanda Mkuu wa Idara Maalum na
atakuwa na uwezo wa kufanya chochote kile anachohisi, kwa maslahi ya Taifa (la
Zanzibar), kinafaa.” Kwa maoni yetu, hakuna tofauti yoyote ya msingi kati
ya maneno ‘Amiri Jeshi Mkuu’ na ‘Kamanda Mkuu’ bali, kwa kiasi kikubwa, ni
mpangilio wa maneno hayo tu.
Aidha, kwa mujibu wa ibara ya
123(2), mamlaka ya Rais wa Zanzibar chini ya ibara ndogo ya (1) yanaingiza “... uwezo wa kutoa amri ya kufanya shughuli
yoyote inayohusiana na Idara hiyo kwa manufaa ya Taifa.” Kwa maoni yetu,
haya ni mamlaka ya kutangaza au kuendesha vita ambayo, kwa mujibu wa ibara ya
44(1) ya Katiba ya Muungano, ni mamlaka pekee ya Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Kifungu cha 5(1)(b) cha
Sheria ya Muungano kilitamka kwamba muundo wa Serikali ya Zanzibar utakuwa kama
utakavyoamuliwa na sheria za Zanzibar pekee. Na hivyo ndivyo ilivyokubaliwa
katika aya ya (iii)(a) ya Makubaliano ya Muungano. Hata hivyo, licha ya muundo
wa Serikali ya Zanzibar kutokuwepo katika orodha ya Mambo ya Muungano, Katiba
ya Muungano imetenga Sura ya Nne nzima kuzungumzia ‘Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.’
Kwa mujibu wa Profesa Shivji
katika The Legal Foundations of the Union,
Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano “...
haina ulazima wowote na ni kuingilia, bila kualikwa, kwenye mambo ambayo yako
ndani ya mamlaka pekee ya Zanzibar.” Ndio maana Katiba mpya ya Zanzibar –
kwa usahihi kabisa - imefanya mabadiliko katika muundo wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar bila ya kuzingatia matakwa ya Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Katiba mpya ya Zanzibar sio
tu kwamba ‘imetangaza uhuru’ wa Zanzibar kwa kuhoji misingi muhimu ya
Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano, bali pia
imehakikisha kwamba uhuru huo utalindwa dhidi ya tishio lolote la Serikali ya
Muungano. Hii imefanywa kwa kuweka utaratibu wa kuwepo kura ya maoni ya wananchi
wa Zanzibar kuhusu mabadiliko ya vifungu kadhaa vya Katiba ya Zanzibar. Kwa
mujibu wa ibara ya 80A(1) ya Katiba hiyo, “...
Baraza la Wawakilishi halitaweza kufanya mabadiliko ya Katiba kuhusiana na
sharti lolote lililomo katika kifungu chochote kilichoainishwa katika kijifungu
cha (2) cha kifungu hiki, mpaka kwanza mabadiliko hayo yakubaliwe na wananchi
kwa kura ya maoni.”
Vifungu vinavyohitaji kura ya
maoni ni vifungu vyote vya Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Kwanza inayohusu
Zanzibar kama nchi na/au dola; kifungu cha 9 kinachohusu Serikali na watu wa
Zanzibar; vifungu vyote vya Sura ya Tatu inayohusu kinga ya haki za lazima,
wajibu na uhuru wa mtu binafsi; na kifungu cha 26 kinachohusu Rais wa Zanzibar
na mamlaka yake. Vifungu vingine ni pamoja na kifungu cha 28 kinachohusu muda
wa urais; Sehemu ya Pili na ya Tatu ya Sura ya Nne zinazohusu Makamu wawili wa
Rais, Baraza la Mawaziri na Baraza la Mapinduzi; kifungu cha 80A kinachohifadhi
haki ya kura ya maoni; na vifungu vya 121 na 123 vinavyohusu Idara Maalum na
mambo yanayohusiana nayo.
Kuweka masharti ya kura ya
maoni kuhusu mabadiliko ya vifungu tajwa vya Katiba mpya ya Zanzibar kuna
athari ya moja kwa moja kwa uhai wa Muungano wetu. Hii ni kwa sababu hata
vifungu ambavyo tumeonyesha kwamba vinakiuka misingi mikuu ya Makubaliano ya
Muungano na Sheria ya Muungano haviwezi kubadilishwa bila kura ya maoni ya
Wazanzibari. Kwa maneno mengine, kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar,
masuala ya kama Tanzania ni nchi moja au la, majeshi ya ulinzi, polisi, n.k.
ambayo yamekuwa Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na
Sheria ya Muungano sio Mambo ya Muungano tena hadi hapo wananchi wa Zanzibar
watakapoamua – kwa kura ya maoni – kuyarudisha kwa mamlaka ya Muungano. Huku ni
kutangaza uhuru wa Zanzibar bila kutaja neno uhuru!
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kwa mtazamo wa Katiba ya sasa
ya Zanzibar, hakuna tena ‘nchi moja’ inayozungumzwa katika Katiba ya sasa ya Muungano
bali tuna ‘nchi mbili’ zinazozungumzwa katika Makubaliano ya Muungano. Kwa
mtazamo huo huo, masuala ya ulinzi na usalama, polisi, n.k. sio tena Mambo ya
Muungano kwa sababu sasa kila nchi ina majeshi yake na kila moja ina Amiri
Jeshi Mkuu wake. Aidha, tuna marais wawili, wakuu wa nchi wawili na viongozi wa
serikali wawili.
Mabadiliko haya ya kikatiba
yanadhihirishwa wazi na taratibu za kiitifaki wakati wa Sherehe za Mapinduzi
Zanzibar ambako siku hizi Rais wa Zanzibar ndiye anayekagua gwaride rasmi la
vikosi vya ulinzi na usalama, kupigiwa mizinga ishirini na moja na anakuwa wa
mwisho kuingia, na wa mwisho kutoka, uwanjani huku Rais wa Jamhuri ya Muungano
akiwa wa pili kiitifaki.
Kwa upande mwingine, kwa
mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, Rais wa Muungano hana tena mamlaka ya
kugawa mikoa na wilaya kwa upande wa Zanzibar, na wala hawezi kumshauri tena
Rais wa Zanzibar anapoteua Wakuu wa Mikoa wa Tanzania Zanzibar. Aidha, Mahakama
ya Rufani ya Tanzania – licha ya kuwa moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa
Katiba ya Muungano - haina tena mamlaka ya kusikiliza na kuamua rufaa zinazohusu
haki za msingi na uhuru wa mtu binafsi zinazotoka Zanzibar. Yote haya hayapo na
hayajawahi kuwapo katika Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano.
MUUNGANO USIO WA USAWA
Tangu mwanzo Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar haukuwa Muungano wa usawa. Huu ni Muungano ulioipa
Tanganyika – ikiwa imevalia koti la Jamhuri ya Muungano - mamlaka ya kuingilia
uhuru na mamlaka ya Zanzibar. Hii inathibitishwa na Hati ya Makubaliano ya
Muungano yenyewe. Kwanza, kwa kutamka kwamba katika kipindi cha mpito “Katiba ya Jamhuri ya Muungano itakuwa ni
Katiba ya Tanganyika...”, ni wazi kwamba Mshirika wa Muungano aliyekuwa na
nguvu katika Muungano huu ni Tanganyika.
Pili, kwa kuweka orodha ya
mambo 11 ya Muungano, ni wazi kwamba Zanzibar ilinyang’anywa mamlaka juu ya
masuala hayo na mamlaka hayo yalihamishiwa kwa Tanganyika ikiwa imevaa koti la
Jamhuri ya Muungano. Kwa maana hiyo, Zanzibar ilinyang’anywa mamlaka yake juu
ya masuala ya nchi za nje, ulinzi, polisi, mamlaka ya hali ya hatari, uraia,
uhamiaji, biashara ya nje na mikopo na masuala mbali mbali ya kodi. Hati ya
Makubaliano ya Muungano yenyewe inasema wazi kwamba “Bunge na Serikali (ya Jamhuri ya Muungano) litakuwa na mamlaka kamili
kwenye mambo hayo kwa Jamhuri ya Muungano na, kwa nyongeza, mamlaka kamili kwa
ajili ya mambo mengine yote ya na kwa ajili ya Tanganyika.”
Tatu, kwa kutangaza kwamba
rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Mwalimu Nyerere na Makamu wa
kwanza wa Rais atakuwa Sheikh Abeid Karume; na kwa kutangaza kwamba Makamu wa
Kwanza wa Rais atakuwa ndiye msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
katika utekelezaji wa majukumu yake ya kiutendaji kuhusu Zanzibar, ni wazi
kwamba Hati ya Makubaliano ya Muungano nafasi ya chini (subordinate position) ya Zanzibar katika Muungano.
Nne, kwa kuzifanya alama za
utaifa (national emblems) za
Tanganyika kuwa ndio alama za taifa za Jamhuri ya Muungano, kuna-emphasize superior position ya
Tanganyika ndani ya Muungano na subaltern
position ya Zanzibar katika Muungano huu. Ukweli huo huo unahusu masuala ya
kuzifanya taasisi na watumishi wa Serikali ya Tanganyika kuwa ndio taasisi na
watumishi wa Jamhuri ya Muungano. Kama Maalim Seif Shariff Hamad anavyomalizia
Maoni yake kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 13 Januari, 2013: “Mfumo (wa Muungano) uliopo sasa hauinufaishi
Zanzibar na hivyo haukubaliki kwa Wazanzibari. Koti la Muungano kama lilivyo
sasa linabana sana. Wakati umefika tushone koti jipya kwa mujibu wa mahitaji ya
zama hizi.”[58]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Baada ya nusu karne ya
ukiukaji wa Hati ya Makubaliano ya Muungano, na kwa hali ya sasa ya kisiasa na
kikatiba ya Zanzibar, ni wazi Hati ya Makubaliano ya Muungano haiwezi kuwa
msingi wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar tunayoipendekeza.
Aidha, Katiba Mpya haiwezi kuwa ni mwendelezo wa Hati ya Makubaliano ya
Muungano ambayo, kama ambavyo tumeonyesha, haijawahi kuheshimiwa katika miaka
hamsini tangu kusainiwa kwake.
Kwa maoni ya wajumbe walio
wachache wa Kamati Namba Nne, wakati umefika wa kujenga mahusiano kati ya nchi
hizi mbili katika msingi ulio imara zaidi na wa usawa zaidi. Ndio maana
tunapendekeza kwamba Katiba Mpya ndiyo iwe msingi wa Shirikisho la Jamhuri za
Tanganyika na Zanzibar.
Ibara ya 2
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Ibara ya 2 ya Rasimu
inafafanua eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Eneo la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya
bahari na eneo lote la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari.” Wajumbe
walio wachache wa Kamati Namba Nne wanapendekeza ibara hiyo ifutwe yote na kuandikwa
upya kama ifuatavyo: “Eneo la Shirikisho
la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha
sehemu yake ya bahari, maziwa na mito, pamoja na eneo lake la anga; na eneo
lote la Zanzibar ikiwa ni pamoja na visiwa vidogo vinvyozunguka Visiwa vya
Unguja na Pemba na eneo lake la bahari pamoja na eneo lake la anga.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mapendekezo haya ya wajumbe
walio wachache katika Kamati Namba Nne yanashawishi kutambuliwa na kufafanuliwa
kwa mipaka ya nchi hizi mbili Washirika wa Muungano. Hii itasaidia kuepusha
migogoro inayoweza kujitokeza hasa hasa kuhusu rasilmali zinazopatikana
baharini kama vile mafuta, gesi asilia na rasilmali uvuvi. Aidha, kwa sababu ya
kuwepo kwa migogoro ya mipaka katika maeneo ya maji kama ule kati ya Jamhuri ya
Muungano na Malawi, wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanafikiri
kwamba ni muhimu kwa Sheria kuu ya nchi kutamka na kufafanua mipaka yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, 1977, imefafanua eneo la Jamhuri ya Muungano kama ifuatavyo: “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la
Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya
bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.”[59]
Aidha, ibara ya 1 ya Katiba ya Zanzibar, 1984, inafafanua ‘Zanzibar na mipaka
yake’ kama ifuatavyo: “Zanzibar ni nchi
ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na
Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”
Wajumbe walio wachache wa
Kamati Namba Nne wanatambua ukweli kwamba ufafanuzi wa mipaka ya Jamhuri ya
Muungano uliopo katika Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano ni mfinyu sana na
hautoshelezi mahitaji ya sasa ya kiuchumi na kisiasa. Kwanza, licha ya Jamhuri
ya Muungano kupakana na maziwa kama vile Victoria, Tanganyika na Nyasa ambayo
tunayachangia na nchi jirani za Kenya, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo, Zambia, Malawi na Msumbiji; na Mto Ruvuma tunaouchangia na Msumbiji,
maelezo haya ya Katiba ya sasa hayatambui uwepo wa maeneo hayo.
Pili, Katiba ya sasa ya
Jamhuri ya Muungano haitofautishi kati ya eneo la bahari la Tanganyika na eneo
la bahari la Zanzibar. Hii ni hatari kwani inaweza kuwa chanzo cha migogoro ya
mipaka kati ya nchi hizi mbili hasa kwa vile masuala ya rasilmali asilia
zilizoko baharini zimeondolewa kinyemela katika orodha ya mambo ya Muungano ama
yanapendekezwa na Rasimu kuondolewa katika orodha hiyo.
Tatu, Katiba ya sasa ya
Jamhuri ya Muungano na hata ya Zanzibar hazitambui milki ya Jamhuri ya Muungano
au ya Zanzibar juu ya anga la Jamhuri ya Muungano au la Zanzibar. Anga ni
rasilmali muhimu hasa katika masuala ya usafiri wa anga, na mawasiliano ya simu
na redio. Mapendekezo haya ya wajumbe walio wachache kuhusu eneo la nchi yetu
yatatua matatizo yaliyotajwa hapa.
IBARA YA 3
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Ibara ya 3 ya Rasimu inahusu
‘Alama na Sikukuu za Taifa.’ Ibara ya 3(1) inapendekeza Alama za Taifa kuwa ni
Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa na Nembo ya Taifa kama zitakavyoainishwa
katika sheria husika za nchi. Kwa upande wake, ibara ya 3(2) inapendekeza Sikukuu
za Kitaifa kuwa ni “Siku ya Uhuru wa
Tanganyika itakayoadhimishwa tarehe 9 Disemba; Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar
itakayoadhimishwa tarehe 12 Januari; Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
itakayoadhimishwa tarehe 26 Aprili; na Sikukuu nyingine zitakazoainishwa na
sheria za nchi.” Kwa mujibu wa ibara 3(3), kila Sikukuu ya Kitaifa itakuwa
ni siku ya mapumziko.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Alama za Taifa ni suala
muhimu sana kwa utambulisho wa historia na utamaduni wa nchi yoyote. Kwa sababu
mbali mbali za kihistoria tulizozielezea kwa kirefu katika maoni yetu kuhusu
ibara 1 ya Rasimu, suala la alama za taifa za Jamhuri ya Muungano limejaa utata
mtupu. Kwa upande mmoja, alama za taifa ambazo zimeendelea kutumika katika
kipindi chote cha miaka hamsini ya Muungano ni Alama za Taifa la Tanganyika
ambazo zilifanywa kuwa za Jamhuri ya Muungano pale Tanganyika ilipovikwa joho
la Jamhuri ya Muungano kati ya tarehe 26 Aprili na 15 Juni, 1964.
Mfano mzuri ni wa Nembo ya
Taifa, maarufu kama ‘Bibi na Bwana.’ Alama hiyo ya Taifa iliwekwa na Sheria ya Nembo ya Taifa, Sura ya 504 ya
Sheria za Tanganyika, yaani The
Public Seal Act, Chapter 504 of the Laws, ya mwaka 1962 na ilianza kutumika
Siku ya Jamhuri, yaani tarehe 9 Disemba 1962. Hata hivyo, kufuatia kuzaliwa kwa
Muungano, Alama hiyo ya Taifa la Tanganyika iligeuzwa na kuwa Nembo ya Taifa ya
Jamhuri ya Muungano kwa kutumia Amri ya Masharti ya Mpito ya Mwalimu Nyerere ya
tarehe 26 Aprili, 1964.
Kwa upande mwingine, matumizi
ya Alama nyingine za Taifa ni kielelezo kingine cha utamaduni wa ukiukaji
sheria ambao umejengeka katika nusu karne ya Muungano. Suala hili linahusu
Bendera ya Taifa na Wimbo wa Taifa. Kwanza, wakati Bendera ya sasa ya Taifa
ilianza kutumika kufuatia kushushwa kwa Bendera za Taifa za Tanganyika na
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar katika Umoja wa Mataifa, baada ya maelekezo ya
Mwanasheria Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stavropoulos ya tarehe 13 Mei, 1964, Bunge
la Jamhuri ya Muungano halikutunga sheria yoyote ya kuwezesha uwepo wa Alama
hii muhimu ya Taifa hadi tarehe 7 Mei, 1971, zaidi ya miaka saba baada ya
kuzaliwa Muungano!
Pili, baada ya kutungwa kwake
na ikiwa na lengo la kuficha ukweli kwamba Bendera ya Taifa ilikuwa imetumika kwa
zaidi ya miaka saba bila uhalali wowote wa kisheria, Sheria ya Bendera ya Taifa na Nembo ya Taifa,[60]
yaani The National Flag and Coat of Arms
Act, ilitamka kwamba Bendera ya Taifa imeanza kutumika tangu tarehe 26
Aprili 1964,[61]
yapata miaka saba kabla sheria yenyewe haijatungwa!
Tatu, licha ya ukweli kwamba
‘Bibi na Bwana’ ilianza kutumika tangu tarehe 9 Disemba, 1962, na licha ya
Mwalimu Nyerere kuigeuza Nembo hiyo ya Tanganyika kuwa ya Jamhuri ya Muungano
kwa Amri yake ya tarehe 26 Aprili, 1964, kifungu cha 4 cha Sheria ya Bendera ya Taifa na Nembo ya Taifa kilishurutisha kwamba
‘Bibi na Bwana’ nayo itakuwa Nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano kuanzia
tarehe 26 Aprili, 1964.
Nne, Wimbo wa Taifa
unaotumiwa sasa, yaani ‘Mungu Ibariki Afrika’, ni Wimbo wa Taifa wa Tanganyika ambao
ulifanywa kuwa Wimbo wa Taifa wa Jamhuri ya Muungano bila ya msingi wowote wa
kisheria. Hii ni kwa sababu, Sheria ya
Alama za Taifa haitambui Wimbo wa Taifa kama mojawapo ya Alama za Taifa.
Aidha, Amri ya Masharti ya Mpito ya
Mwalimu Nyerere iliyohalalisha Nembo ya Taifa ya Tanganyika kutumika kama Nembo
ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano haikuhusu Wimbo wa Taifa.
Kwa nchi na serikali ambayo
imejidai kwa ‘upekee’ wake katika mambo mengi, kushindwa kutambua hata Wimbo
wake Taifa ni kitendo cha fedheha kubwa sana kwa nchi yetu na wale ambao
wameitawala tangu uhuru. Nchi nyingine za ki-Afrika zimetupita mbali katika
kuenzi Alama zao za Taifa kwa kuzitambua kikatiba. Hivyo, kwa mfano, ibara ya
9(1) na (2) na Nyongeza ya Pili ya
Katiba ya Kenya, 2010, imefafanua Alama za Taifa za Kenya pamoja na kuweka
maneno ya Wimbo wa Taifa wa nchi hiyo. Vivyo hivyo, ibara ya 4 na Nyongeza ya Nne ya Katiba ya Zimbabwe, 2013,
nayo imeweka Alama za Taifa za Zimbabwe pamoja na maneno na muziki wa Wimbo wa
Taifa wa nchi hiyo. Sisi, tunaojidai kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine
duniani, hatujaitaja Bendera yetu ya Taifa mahali popote katika Katiba na
Sheria zetu!
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Zaidi ya kupendekeza nyongeza
ndogo kwenye ibara ya 3(2), wajumbe walio wengi wa Kamati Namba Nne hawakuona
tatizo lolote la mapendekezo ya ibara ya 3 ya Rasimu. Hata hivyo, mkanganyiko
ambao tumeuonyesha kuhusu jambo hili muhimu unaonyesha haja kubwa ya kuwa na
mwanzo mpya kikatiba katika masuala ya Alama za Taifa. Kwa sababu hiyo, wajumbe
walio wachache wanapendekeza kwamba ibara ya 3(1) ya Rasimu ifanyiwe
marekebisho ili iweze kusomeka ifuatavyo:
“3(1) Alama za Taifa zitakuwa ni:
(a)
Bendera
ya Taifa ya Shirikisho na Bendera za Taifa za Nchi Washirika wa Shirikisho;
(b)
Wimbo
wa Taifa wa Shirikisho na Nyimbo za Taifa za Nchi Washirika wa Shirikisho;
(c)
Nembo
ya Taifa ya Shirikisho na Nembo za Taifa za Nchi Washirika wa Shirikisho,
kama
zitakavyoainishwa katika sheria husika za nchi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Wajumbe walio wachache wa
Kamati Namba Nne wanapendekeza pia marekebisho katika ibara ya 3(2) ya Rasimu.
Kama ilivyo hivi sasa, ibara hiyo inaendeleza upotoshaji wa historia ya Jamhuri
ya Muungano na ya nchi washirika wa Muungano. Kwanza, kupendekeza kuendelea
kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Tanganyika wakati Tanganyika yenyewe haitambuliwi
kikatiba ni kuendeleza unafiki wa kikatiba na wa kisiasa ambao umeendelea kwa
nusu karne. Kama taifa, hatuwezi kuendelea kuishi katika uongo kwa namna hii.
Pili, Zanzibar haikupata
uhuru wake Siku ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964. Zanzibar ilipata uhuru
wake siku ya tarehe 10 Disemba, 1963, ikiwa na Serikali halali iliyochaguliwa
na wananchi kwenye uchaguzi huru na wa haki kwa mujibu wa sheria zilizokuwepo
wakati huo. Uhuru huo ulitambuliwa na jumuiya ya kimataifa pale Zanzibar
ilipokubaliwa kujiunga kama mwanachama wa 99 wa Umoja wa Mataifa tarehe 16
Disemba, 1963.[62]
Hata Sheikh Abedi Karume, aliyekuja kushikilia uongozi wa Zanzibar ya baada ya
Mapinduzi na mwasisi wa Muungano, alitambua uhuru huo wa Zanzibar. Katika
hotuba yake ya kuukaribisha Uhuru wa Dola ya Zanzibar wa tarehe 10 Disemba,
1963, Sheikh Karume alitamka maneno yafuatayo:
“Leo
tarehe 10 Disemba, 1963, ZANZIBAR imekuwa Huru. Hii leo sisi watu wa visiwa
hivi tumepata haki ya kuchukuwa mahala petu kuwa ni Dola sawa na nyengine
katika umoja wa Nchi za Dola za Commonwealth. Kwa uchache, kuwa mwanachama
katika umoja huo, kuna maana kwamba nchi hii ni huru chini ya mpango wa
Sirikali ambayo msingi wake umejengwa juu ya kuendelea kwa ridhaa ya wananchi.
“Ili
kufikilia matarajio yetu hayo tunayo moja katika Katiba zenye msingi madhubuti
iliyohusika na shuruti za haki za binadamu, haki za mambo ya siasa na uhuru wa
dola yoyote nyengine. Ni wajibu wa watu wote wa dola yetu mpya, kila mmoja
katika sisi bila ya kujali fikra zetu za siasa au madaraka yetu kusaidia kweli
kweli Katiba yetu iweze kufanya kazi. Pamoja na manufaa, haki na uhuru ambayo
yote hayo yamepatikana baada ya nchi kuwa huru.”
Mwezi mmoja baada ya kutamka
maneno hayo, ‘Sirikali ambayo msingi wake umejengwa juu ya ... ridhaa ya
wananchi’ ilipinduliwa kwa nguvu za kijeshi, na Sheikh Karume akafanywa kuwa
Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyotokana na Mapinduzi hayo!
Ukweli huu wa kihistoria,
hata kama utakuwa ni mchungu kwa baadhi ya watu, unahitaji kutambuliwa ili
kuiwezesha nchi yetu kuwa na mapatano na mwafaka wa kitaifa. Na mahali pa
kuanzia mchakato wa mapatano ya kitaifa ni kufichua historia hii iliyofichwa
kwa nusu karne kwa kuifanya Siku ya Uhuru wa Zanzibar kuwa Sikukuu ya Kitaifa
sawa na Siku ya Uhuru wa Tanganyika na Siku ya Mapinduzi. Kwa sababu hiyo,
wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanapendekeza marekebisho yafuatayo
katika ibara ya 3(2) ya Rasimu:
(a)
Kwa
kufuta aya yote ya (c) na kuibadilisha na aya mpya ya (c) itakayosomeka ‘Siku
ya Uhuru wa Zanzibar itakayoadhimishwa tarehe 10 Disemba.’
(b)
Kwa
kuingiza aya mpya ya (d) itakayosomeka ‘Siku ya Shirikisho la Jamhuri za
Tanganyika na Zanzibar itakayoadhimishwa katika tarehe ya kupitishwa Katiba
Mpya ya Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.’
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mapendekezo haya yanaiondoa
Siku ya Muungano kama Sikukuu ya Kitaifa. Kwa sababu ambazo tumezielezea kwa
kirefu kuhusiana na ibara ya 1 ya Rasimu, ni wazi kwamba Muungano wa aina hii
haustahili kuendelea kupewa enzi ya kuwa na Sikukuu yake ya Kitaifa.
IBARA YA 4
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Wajumbe wa Kamati Namba Nne
walikuwa na mjadala mkali sana kuhusu mapendekezo ya ibara ya 4 ya Rasimu.
Ibara hiyo inahusu ‘Lugha ya Taifa na lugha za alama.’ Ibara ya 4(1) inakifanya
Kiswahili kuwa Lugha ya Taifa ambayo “... itatumika katika mawasiliano rasmi ya
kitaifa na kiserikali.” Ibara ya 4(2) inaruhusu matumizi ya lugha ya Kiingereza
au ‘lugha nyingine yoyote’ kama “... lugha rasmi ya mawasiliano ya kiserikali
pale itakapohitajika.” Mwisho, ibara ya 4(3) inaitaka Serikali kuweka “...
mazingira yatakayowezesha kuwepo kwa mawasiliano mbadala zikiwemo lugha za
alama, maandishi yaliyokuzwa na nukta nundu kwenye sehemu muhimu za umma na
katika vyombo vya habari vinavyotangaza habari zake kitaifa kwa ajili ya watu
wenye mahitaji maalum.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Wajumbe walio wachache wa
Kamati Namba Nne wanapendekeza marekebisho yafuatayo katika ibara ya 4 ya Rasimu.
“4(1)
Lugha ya Taifa ya Shirikisho itakuwa ni Kiswahili na itatumika katika shughuli
zote za umma na mawasiliano yote rasmi ya kitaifa na kiserikali.
“4(2)
Kiswahili kitakuwa ndio Lugha ya Mahakama za Shirikisho na pia Lugha ya Mabunge
ya Shirikisho na Sheria, Muswada, Maazimio na nyaraka nyingine za kibunge
zitakuwa katika Lugha ya Kiswahili.
“4(3)
Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1) na (2), lugha ya Kiingereza au
lugha nyingine yoyote inaweza kutumika kuwa lugha rasmi ya mawasiliano ya kiserikali
pale itakapohitajika.
“4(4)
Mamlaka ya nchi-
(a)
zitakuza na
kulinda utajiri wa lugha za watu wa Shirikisho la Jamhuri; na
(b)
zitakuza
uendelezaji na matumizi ya lugha za
makabila na jumuiya za Shirikisho la Jamhuri pamoja na kuweka mazingira
yatakayowezesha kuwepo kwa mawasiliano mbadala zikiwemo lugha za alama,
maandishi yaliyokuzwa na nukta nundu kwenye sehemu muhimu za umma na katika
vyombo vya habari vinavyotangaza habari zake kitaifa kwa ajili ya watu wenye
mahitaji maalum.”
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Sababu za
mapendekezo haya ya wajumbe walio wachache zinajionyesha wazi. Tanzania ni nchi
ya asili ya Kiswahili. Hata hivyo, na licha ya matamko ya wanasiasa na watawala
katika kipindi chote cha uhuru wa Tanganyika na Zanzibar na tangu Muungano wa
mwaka 1964, Kiswahili hakijawahi kutambuliwa rasmi kikatiba kama Lugha ya Taifa
au hata lugha rasmi ya shughuli za kiserikali. Tofauti pekee ni Zanzibar ambayo
Katiba yake imetambua Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Baraza la Wawakilishi
Zanzibar na lugha ya sheria za Zanzibar.[63]
Hata Kenya, ambayo Kiswahili chake ni cha kuungaunga, imetambua Kiswahili kuwa
Lugha ya Taifa ya Jamhuri ya Kenya na moja ya lugha mbili rasmi za nchi hiyo.[64]
Sababu ya pili ni
haja ya kuondokana na utamaduni tuliourithi kutoka kwa wakoloni ambao ulifanya
Kiswahili iwe na hadhi ya chini kulinganisha na Kiingereza katika shughuli za
kiserikali, kimahakama na kibunge. Hadi sasa lugha rasmi ya Muswada na Sheria
zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ni Kiingereza.
Hata pale ambapo
Sheria imetafsiriwa kwenda kwenye Kiswahili, kama ambavyo imetokea mara kwa
mara, sheria za tafsiri za sheria zimeelekeza kwamba panapotokea mgongano wa
kisheria kati ya lugha hizo mbili, basi lugha iliyotungiwa sheria hiyo, yaani
Kiingereza, ndiyo inayotiliwa nguvu na tafsiri ya Kiswahili inatanguka.
Aidha, licha ya
sheria za nchi kuweka bayana kwamba lugha ya Mahakama ni Kiswahili au Kiingereza,
sheria hizo zimesisitiza kwamba lugha ya kumbukumbu za Mahakama itakuwa ni
Kiingereza. Katiba Mpya ni fursa muhimu ya kupandisha hadhi lugha yetu ya taifa
kwa kuifanya kuwa lugha ya shughuli zote za kiserikali, kimahakama na kibunge.
Tatu, Katiba Mpya
inatupa fursa muhimu ya kutambua, kulinda na kukuza lugha zetu za asili na
lugha za alama. Lugha ni sehemu muhimu ya utambulisho na utajiri wetu wa
kiutamaduni. Hata hivyo, tangu uhuru, lugha za makabila yetu zimepigwa vita
kuwa kuzitambua, kuzikuza na kuziendeleza kutajenga ukabila na utengano wa
kitaifa. Aidha, dhana potofu imejengwa kwamba kukuza na kuendeleza Kiswahili
ndio njia pekee ya kujenga umoja na utengamano wa kitaifa.
Mwelekeo wa sasa
wa kikatiba katika nchi za Afrika ni kutambua na kuendeleza lugha za watu wa
Afrika kama sehemu ya utu wetu, utambulisho wetu na utajiri wetu wa
kiutamaduni. Kwa mfano, Katiba za nchi za Ghana,[65]
Kenya[66]
na Zimbabwe[67]
zimetambua lugha za asili za nchi zao kama sehemu ya utambulisho na utajiri wao
wa kiutamaduni.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Ibara za 5, 6 na 9
za Rasimu zilipitishwa na Kamati Namba Nne kwa kuungwa mkono na theluthi mbili
za wajumbe wote wa Kamati kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe
wote wa kutoka Zanzibar kama inavyotakiwa na kifungu cha 26(2) cha Sheria na
kanuni ya 64(1) ya Kanuni. Hivyo, kwa mujibu wa kanuni ya 32(3) ya Kanuni,
maoni haya hayahusu ibara hizo za Rasimu.
IBARA YA 8
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Ibara ya 8 ya
Rasimu inahusu ‘Ukuu na utii wa Katiba’ na ilizua mjadala mkali sana katika
Kamati Namba Nne. Wajumbe walio wengi kwenye Kamati hawakupendekeza marekebisho
yoyote katika ibara hiyo. Hata hivyo, wajumbe hao walipiga kura kupinga
marekebisho yaliyopendekezwa na wajumbe walio wachache.
Mapendekezo hayo
ni kwamba ibara ya 8(1) iongezewe maneno ‘kwa kadri yatakavyohusika na utekelezaji
wa mambo ya Muungano.’ Lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha kwamba Katiba
ya Shirikisho la Jamhuri inakuwa na ukuu katika mambo yote yanayohusu
Shirikisho, na Katiba za Nchi Washirika zinakuwa na ukuu katika masuala yote
yanayohusu Nchi Washirika ambayo sio mambo ya Shirikisho. Mapendekezo haya
yatalinda u-shirikisho wa nchi yetu na mamlaka ya Nchi Washirika katika masuala
yasiyo ya Shirikisho.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Mapendekezo haya hayaongezi
kitu chochote kipya katika kamusi ya kikatiba ya nchi yetu. Hii ni kwa sababu,
hata ibara ya 64(5) ya Katiba ya sasa ya Muungano inayohusu ukuu wa Katiba ya
Muungano imeweka wazi kwamba ukuu huo unahusu mambo ya Muungano tu: “Bila ya kuathiri kutumika kwa Katiba ya
Zanzibar ... kuhusu mambo yote ya Tanzania Zanzibar yasiyo mambo ya Muungano,
Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na
endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii,
Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka
Katiba, itakuwa batili.”
Ukuu huu wa Katiba
ya Jamhuri ya Muungano katika mambo ya Muungano pekee unathibitishwa pia na
ibara ya 4 ya Katiba ya Zanzibar inayohusu ukuu wa Katiba ya Zanzibar: “Katiba hii ni Katiba ya Zanzibar na itakuwa
na nguvu za kisheria nchini kote na isipokuwa kutokana na kifungu cha 80 ikiwa
sheria yoyote inatofautiana na Katiba hii, basi Katiba hii ndiyo itayokuwa na
nguvu na sheria hiyo itakuwa batili kwa kiwango kile ambacho kinahitilafiana.”
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Kama ambavyo
tumeeleza kwa kirefu kuhusu ibara ya 1 ya Rasimu, kwa miaka hamsini ya Muungano
wetu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano imenyakua mamlaka ya Zanzibar kwa mambo
ambayo hayakuwa mambo ya Muungano kwa mujibu wa Hati ya Makubaliano ya
Muungano. Hilo limefanyika kwa njia mbali mbali lakini kwa kiasi kikubwa kwa
kuongeza orodha ya mambo ya Muungano kwenye Katiba au kwa kutunga sheria za
kawaida na kuzifanya kuwa sheria za Muungano.
Endapo mapendekezo
ya ibara ya 8 ya Rasimu yataachwa yalivyo bila kurekebishwa, athari yake kubwa
itakuwa ni kufuta kabisa haiba ya u-shirikisho (federalism) ambayo imekuwa
sehemu ya mfumo wetu wa kikatiba kwa nusu karne. Hakutakuwa tena na tofauti
kati ya mambo ya shirikisho na mambo yasiyo ya shirikisho yaliyoko chini ya mamlaka
ya Nchi Washirika.
Aidha, itakuwa ni
halali kwa mamlaka za shirikisho kuingilia mambo yasiyo ya shirikisho ya Nchi
Washirika kwa kisingizio cha ukuu wa Katiba ya Shirikisho. Pendekezo hili
litakuwa na madhara makubwa sana kikatiba na kisiasa na litapelekea migogoro
isiyoisha baina ya Nchi Washirika na Shirikisho la Jamhuri. Wajumbe walio
wachache wa Kamati Namba Nne wanaliomba Bunge lako tukufu kukubali mapendekezo
ya marekebisho ya ibara ya 8 ili kulinda federal
character ya nchi yetu.
SURA YA SITA
IBARA YA 60
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Rasimu ya Katiba Mpya
inapendekeza mabadiliko makubwa katika muundo wa Jamhuri ya Muungano katika
maeneo mawili. Kwanza, ibara ya 60(1) ya Rasimu inapendekeza “... muundo wa shirikisho lenye serikali tatu
ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar; na Serikali ya Tanzania Bara.”
Pili, Rasimu inapendekeza
mabadiliko makubwa katika orodha ya Mambo ya Muungano. Kwa mujibu wa aya za 62(1)
na 63 za Rasimu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya
utekelezaji kwa mambo yote yaliyoorodheshwa katika Nyongeza ya Katiba kuwa
Mambo ya Muungano. Mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa katika Nyongeza hiyo ni
Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama, uraia na
uhamiaji na sarafu na Benki Kuu. Mambo mengine ya Muungano ni mambo ya nje,
usajili wa vyama vya siasa na ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi
yatokanayo na mambo ya Muungano. Kwa ujumla, Rasimu inapendekeza kuwa na Mambo
ya Muungano saba.
Kama ambavyo tumeonyesha
katika Sura ya Kwanza, suala la Mambo ya Muungano limekuwa na utata mkubwa
katika miaka hamsini ya Muungano. Sasa Rasimu inapendekeza Mambo ya Muungano
kuwa saba, na kati ya hayo ni Mambo matano tu – Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya
Muungano, ulinzi na usalama, uraia, uhamiaji na mambo ya nje - ambayo
yalikuwepo kwenye orodha ya mwanzo ya Mambo ya Muungano. Na katika Mambo 11
yaliyoongezwa baada ya Muungano, ni mambo mawili tu – sarafu na Benki Kuu na
usajili wa vyama vya siasa – ambayo yamebaki katika Rasimu. Kwa ujumla, Rasimu
inapendekeza kuondoa Mambo 16 yaliyopo katika orodha ya sasa ya Mambo ya
Muungano na kuongeza jambo moja jipya – ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya
kodi yatokanayo na mambo ya Muungano – katika orodha hiyo.
Mapendekezo ya Rasimu kuhusu
Mambo ya Muungano yanaashiria mabadiliko makubwa katika muundo wa sasa wa
Muungano, na katika Hati za Makubaliano ya Muungano zilizosainiwa mwaka 1964. Kama
tulivyoonesha kuhusu ibara ya 1 ya Rasimu, mapendekezo haya ya ibara ya 60 Rasimu
hayawezi kuitwa ‘Mwendelezo wa Hati ya Makubaliano ya Muungano.’
SHIRIKISHO LA SERIKALI TATU
Mapendekezo ya muundo wa
shirikisho lenye serikali tatu na Mambo ya Muungano yamezua mjadala mkubwa wa
kisiasa na kitaaluma. Katika mhadhara wake juu ya Rasimu ya Kwanza, Profesa
Shivji alihoji madai ya aya ya 1(3) ya Rasimu. Kwa mujibu wa Profesa Shivji, “... Hati (ya Makubaliano ya Muungano)
iliweka serikali mbili; sasa iweje rasimu inayozungumzia serikali tatu iwe na
msingi ambao ulijengeka kwenye serikali mbili?... Katiba iliyojikita kwenye
serikali tatu haiwezi, kwa vyovyote vile, ikawa mwendelezo wa Hati (za
Makubaliano ya Muungano).”[68]
Kama lilivyo jina la mhadhara
wake, hoja hii ya Profesa Shivji ina ‘utatanishi’ mkubwa, kwani kumekuwa na
mabishano makubwa na ya kihistoria kuhusu tafsiri halisi ya Makubaliano ya
Muungano juu ya muundo wa Muungano. Katika kitabu chake Pan Africanism or Pragmatism?, Profesa Shivji mwenyewe amedai
kwamba Rais wa pili wa Zanzibar Aboud Jumbe Mwinyi na wasaidizi wake wa karibu
waling’olewa madarakani mwaka 1984 kwa sababu ya kuhoji, pamoja na mambo
mengine, muundo wa Muungano wa Serikali Mbili kwa madai kwamba Hati za
Makubaliano ya Muungano zilikuwa zimeweka utaratibu wa muundo wa shirikisho
lenye Serikali Tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Miaka kumi na saba kabla ya
kuchapishwa kitabu hicho, Tume ya Nyalali iliyoteuliwa na Rais Ali Hassan
Mwinyi kuchunguza kama Tanzania iendelee kuwa na chama kimoja cha siasa au
vyama vingi ilipendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu.[69]
Mwaka mmoja baadaye, mwasisi wa Muungano na Rais wake wa kwanza, Mwalimu
Nyerere aliandika yafuatayo kuhusu madai ya Rais Jumbe yaliyopelekea ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya
kisiasa’ Zanzibar: “Huko nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar
wapinzani wa Muungano wamewahi kudai tufanye referendum kwa Zanzibar kuhusu
Muungano. Tukakataa kwa sababu safi kabisa.”[70]
Katika kitabu hicho hicho,
Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo juu ya kilichotokea kwenye Bunge la Jamhuri
ya Muungano mwaka 1993:
“Tarehe
30 Julai, 1993 wakati mkutano wa bunge la bajeti ukiendelea, zaidi ya wabunge
50 kwa pamoja walitoa taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni ambayo
inadai (kwamba) kuendelea na mfumo huu wa Muungano usiowaridhisha wananchi
wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea kudumu kwa Muungano.... Hivyo
basi wabunge hawa wanaliomba Bunge ... liazimie kwamba Serikali ... ilete
Muswada Bungeni kabla ya Februari 1994, kurekebisha katiba ya Jamhuri ya
Muungano ili kuwezesha uundaji wa ‘Serikali ya Tanganyika’ ndani ya Muungano....
Tarehe 20 Agosti, 1993
wabunge wahusika waliwasilisha taarifa nyingine ... iliyokuwa inalitaka Bunge
... liazimie kwamba Serikali ... iandae kura ya maoni ambayo itafanyika kabla
ya 31 Desemba, 1994 ili kupata maoni ya wananchi wa Tanzania juu ya kuundwa kwa
“Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muundo wa Muungano....”
Aidha, miaka kumi na moja
kabla ya kuchapishwa kwa kitabu cha Profesa Shivji, Tume ya Kissanga
iliyoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuchunguza masuala mbali mbali ya kikatiba,
nayo ilipendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu.
MUUNDO WA SERIKALI MBILI
UMESHINDWA!!!
Mapendekezo ya kubadili
muundo wa Muungano yaliyotolewa na Tume mbali mbali za kikatiba pamoja na
Rasimu yanathibitisha mambo mawili. Kwanza, Muungano umekuwa na migogoro
isiyoisha na ambayo haijapatiwa ufumbuzi hadi sasa. Jambo la pili ni kwamba,
baada ya karibu nusu karne ya maisha yake, muundo wa Muungano wenye Serikali
mbili umeshindwa na hauwezi tena kutatua migogoro ya Muungano.
Sehemu kubwa ya migogoro hiyo
inatokana na historia ya kuanzishwa kwake. Kama ambavyo wasomi wa historia ya
Muungano wameonyesha, Muungano huu ulianzishwa kwa sababu ya shinikizo la
mataifa makubwa ya Magharibi yaliyokuwa na hofu kwamba Mapinduzi ya Zanzibar
yangeleta siasa za kijamaa katika pwani ya Afrika Mashariki kwa sababu, mara tu
baada ya Mapinduzi hayo, Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ilitambuliwa na nchi za
kijamaa za wakati huo. Aidha, watawala wa nchi za Afrika Mashariki, na hasa
waasisi wa Muungano Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, walikuwa na
hofu ya tawala zao kupinduliwa kutokana na mfano wa Mapinduzi ya Zanzibar.
Sababu zote hizi zilipelekea
Muungano kufanywa kwa siri kubwa, na kwa vyovyote vile, bila kupata ridhaa ya
wananchi wa Tanganyika au Zanzibar au ya vyombo vyao vya uwakilishi. Kama
ambavyo tumekwishaonesha katika maoni haya, sio tu kwamba Baraza la Mapinduzi
lililokuwa linatawala Zanzibar wakati huo lilikataa pendekezo la Muungano, bali
pia halikutunga sheria ya kuridhia Hati za Makubaliano ya Muungano baada ya
Sheikh Karume kuamua kuunganisha Zanzibar na Tanganyika bila ridhaa ya Baraza
la Mapinduzi!
Kwa upande wake, Bunge la
Tanganyika liliitishwa kwa dharura siku tatu baada ya kusainiwa kwa Hati za
Makubaliano ya Muungano na kutakiwa kupitisha Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar siku hiyo hiyo kwa
kutumia hati ya dharura! Sheria hiyo ilipitishwa bila mjadala wowote wa maana
na kesho yake, tarehe 26 Aprili, 1964, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ukazaliwa rasmi! Kwa hiyo, kama ambavyo Profesa Shivji na wasomi wengine wa
Muungano wameonyesha, Muungano ulizaliwa bila uhalali wa kisheria wala baraka
za kisiasa za wananchi wa nchi hizi mbili.
Sehemu nyingine kubwa ya
migogoro ya Muungano imetokana sio kwa sababu ya namna ulivyozaliwa, bali na
utekelezaji wa masharti ya Hati za Makubaliano ya Muungano. Hii ni kwa sababu,
wakati Muungano umetukuzwa katika majukwaa ya kisiasa, umekuwa ukikiukwa kwa
vitendo - hasa hasa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano - wakati wote wa
historia yake ya karibu miaka hamsini. Kama tulivyoonesha, mbinu kubwa
iliyotumiwa kukiuka masharti ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ilikuwa
kuongeza Mambo ya Muungano kwenye orodha ya Mambo ya Muungano yaliyokuwa kwenye
Hati za Makubaliano ya Muungano zilizosainiwa mwaka 1964.
‘KERO ZA MUUNGANO’ AU
‘MUUNGANO WA KERO’?
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mfano mwingine unaoonyesha
kwamba muundo wa Muungano wa Serikali Mbili umeshindwa kutatua matatizo ya
Muungano ni kile kinachojulikana katika kamusi ya kisiasa ya nchi yetu kama
‘Kero za Muungano.’ Tangu kung’olewa madarakani kwa Rais Jumbe mwaka 1984,
mjadala wowote juu ya ‘Hati ya Kuzaliwa’ ya Muungano – kama Jumbe alivyoziita
Hati za Makubaliano ya Muungano wakati akijitetea mbele ya Kikao Maalum cha
Halmashauri Kuu ya CCM – imekuwa, kwa maneno ya Jumbe, ‘dhambi.’ Na tangu
wakati huo, migogoro inayohusu Mambo ya Muungano imeacha kutaja ‘Hati za
Makubaliano ya Muungano’, badala yake migogoro hiyo imefichwa ndani ya lugha ya
‘Kero za Muungano.’
Kinachoitwa ‘kero za
Muungano’ kiuhalisia ni migogoro juu ya Mambo mbali mbali ya Muungano kati ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Hii
inadhihirishwa na ‘Hoja za Muungano’ zilizojadiliwa katika vikao mbali mbali
vilivyofanywa kati ya Serikali zote mbili kati ya Oktoba 2012 na Machi 2013:
hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya
Afrika Mashariki; usajili wa vyombo vya moto; malalamiko ya wafanya biashara wa
Zanzibar kutozwa kodi mara mbili; mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha;
mgawanyo wa mapato; ushiriki wa Zanzibar katika taasisi za nje; utafutaji na
uchimbaji mafuta na gesi asili; ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi
za Muungano; uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa bahari kuu; ongezeko la gharama
za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO; na ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Katika ‘hoja’ hizi ni
ongezeko la gharama za umeme kati ya TANESCO na ZECO pekee ambayo haina
uhusiano wowote na masuala ya Muungano. Kwa upande mwingine, hisa za Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, wafanya
biashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili; mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya
Fedha na mgawanyo wa mapato yana uhusiano wa moja kwa moja na ‘mikopo na
biashara za nchi za nje’, ‘kodi ya mapato na ushuru wa forodha’, mambo
yanayohusiana na ‘sarafu na fedha’ yaliyoko katika orodha ya Mambo ya Muungano
ambayo ni Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Muungano.
Aidha, ushiriki wa Zanzibar
katika taasisi za nje na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni masuala yenye
uhusiano wa moja kwa moja na ‘mambo ya nchi za nje’ kwenye orodha ya Mambo ya
Muungano. Vile vile, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili yanahusiana
na ‘maliasili ya mafuta ... na gesi asilia’ katika orodha ya Mambo ya Muungano;
wakati uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu yanahusiana moja kwa moja na
‘Katiba ya Tanzania’ inayotangaza sehemu ya bahari inayopakana na Tanzania kuwa
ni sehemu ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwisho, ‘hoja’ ya ajira
kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano iko katika ‘utumishi
katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano’ kwenye orodha ya Mambo ya Muungano.
UTARATIBU WA KUTATUA MIGOGORO
YA MUUNGANO UMESHINDWA!!!
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Tumeonyesha jinsi ambavyo
‘Kero za Muungano’ zimekuwa sehemu ya historia yote ya Muungano. Kwa mujibu wa
Katiba ya Muungano, kero hizi zinazohusu tafsiri ya masuala ya Muungano
zilitakiwa kuamuliwa na Mahakama Maalum ya Katiba iliyoundwa chini ya ibara ya
125 ya Katiba. Idadi ya wajumbe wa Mahakama hiyo haijatajwa lakini ibara ya
127(1) inatamka kwamba wajumbe wake ni “...
nusu ya jumla ya wajumbe wote watakaoteuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
na nusu nyingine ... watateuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.” Kwa
mujibu wa ibara ya 128(2) ya Katiba, akidi ya kikao cha Mahakama hiyo ni
wajumbe wote; na “kila suala linalohitaji
uamuzi ... litaamuliwa kwa kufuata kauli ya theluthi mbili ya wajumbe kutoka
Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Zanzibar.” (ibara ya 128(3) Na kwa mujibu wa ibara ya
126(3), uamuzi wa Mahakama Maalum ya Katiba “... utakuwa ndio wa mwisho (na) hakutakuwa na haki ya kukata rufaa
popote.”
Licha ya Katiba ya Muungano
kuweka utaratibu huu wa kutatua migogoro ya tafsiri ya Katiba kuhusu masuala ya
Muungano, Mahakama Maalum ya Katiba haijawahi kuitishwa kusikiliza migogoro
mingi kuhusu tafsiri ya Katiba kuhusu masuala ya Muungano. Jaribio pekee la
kukiitisha chombo hiki cha kikatiba kutatua migogoro hiyo lilizimwa mwaka 1984
wakati aliyekuwa Rais wa Zanzibar Aboud Jumbe, Waziri Kiongozi Ramadhani Haji
Faki na Mwanasheria Mkuu Bashir Kwaw Swanzy walipong’olewa madarakani kwa kile
kilichoitwa ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa’ Zanzibar. Profesa Shivji
yupo sahihi anaposema - katika Pan
Africanism or Pragmatism? – kwamba ‘pengine Mahakama hiyo haikupaswa
kufanya kazi’!
Badala ya kutatua matatizo ya
Muungano kwa njia zilizowekwa kikatiba, Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar zimeanzisha taratibu za kirasimu zilizoko nje kabisa ya
mfumo wa kikatiba wa Muungano. Ndio maana Taarifa
ya Utekelezaji Bajeti Mwaka wa Fedha 2012/13: Kipindi cha 01 Julai hadi 31
Desemba, 2012, iliyowasilishwa Bungeni tarehe 23 Januari mwaka huu
inaelezea uratibu wa vikao vitatu vya Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
iliyoundwa mwaka 2006 ili “...
kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Mambo ya
Muungano....”
Vile vile, kwa mujibu wa Taarifa hiyo, vikao vya Kamati ya
Makatibu Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar na mawaziri wa Serikali hizo vilivyokaa kati ya tareje 20 Desemba 2012
na 13 Januari 2013 vilikutana kujadili ‘Hoja za Muungano.’ Haihitaji msisitizo
kusema kwamba vikao hivyo vyote havitambuliwi kikatiba. Katika mazingira haya,
ni halali kuuliza swali kama pande zote mbili za Muungano zinataka kuendelea na
Muungano kabla hata ya kujadili muundo wake.
MUUNGANO AU UHURU???
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Katika mhadhara wake wa kuaga
Kigoda cha Mwalimu, Profesa Shivji amehitimisha uchambuzi wake wa Rasimu kwa
kusema kwamba muundo wa Muungano unaopendekezwa “... ni tegemezi na ... ni dhaifu kwa sababu umejengwa juu ya mchanga wa
dhamira na nia nzuri badala ya msingi wa mawe ya nguvu za kikatiba zilizowekwa
na wananchi wenyewe. Ni kama kwamba suala la Muungano ni (la) ujirani mwema
badala ya umoja wa nchi.”[71]
Kwingineko katika mhadhara huo, mwanazuoni huyu maarufu ‘amediriki kusema’
kwamba “muundo wenyewe wa serikali tatu
uliopendekezwa (na Rasimu) ni compromise
kati ya wale waliosimamia serikali mbili na wale waliopigania muungano wa
mkataba, kwa maneno sahihi, kuuvunja muungano.”[72]
Ijapokuwa hajasema wazi wazi,
Profesa Shivji anaonyesha kupendelea kwamba muundo wa sasa wa Muungano wa
serikali mbili ni bora zaidi na hauna budi kuendelea. Kwa maneno yake, “... compromise inazaa uamuzi legelege. Compromise juu ya muundo ... imezaa muundo wa
muungano legelege. Kuna maeneo mengi ... yatazaa migogoro ambayo hatimaye
inaweza kuuvunja Muungano. Kero za Muungano zitaendelea, safari hii kutoka
pande zote mbili.”[73]
Si sahihi kupuuza hoja na
kauli za mwanazuoni huyu maarufu. Hata hivyo, ni muhimu kuhoji uhalali wake kwa
kuangalia historia halisi ya Muungano wetu. Kwanza kabisa, kama ambavyo Profesa
Shivji mwenyewe amedhihirisha katika maandishi yake ya zaidi ya miaka ishirini,
Muungano huu haujawahi kuwa Muungano wa watu wa Tanganyika na Zanzibar, bali
ulikuwa na umeendelea kuwa Muungano wa watawala kwa maslahi ya watawala wa
ndani ya nchi yetu na wa nchi za kibeberu!
Pili, Muungano huu wa
watawala haujawahi kuheshimiwa na watawala wenyewe kwa miaka yote ya uwepo
wake, kama ambavyo historia ya Mambo ya Muungano na utaratibu wa kutatua
migogoro yake inavyothibitisha.
Tatu, kwa kuangalia mwelekeo
wa siasa za sasa za kikatiba za Zanzibar, ni wazi kwamba wananchi wa Zanzibar
wanapendelea uhuru kuliko kuendelea na Muungano huu. Profesa Shivji anathibitisha
hili kwa kauli yake kwamba “Wazanzibari
kwa muda mrefu tu wamedai haki yao ya kujiamulia mambo yao wenyewe.”[74]
Nne, kwa sababu ya kuwa Muungano wa watawala badala ya kuwa Muungano wa
wananchi; kwa sababu ya kutoheshimiwa na watawala hao; na kwa sababu ya
mwelekeo wa siasa za Zanzibar za sasa, ‘Kero za Muungano’ haziwezi kutatuliwa
kwa kutumia muundo wa sasa wa Serikali mbili. Compromise ya serikali tatu, katika mazingira haya, ni njia pekee
iliyobaki ya kuwa na Muungano, hata kama ni muundo dhaifu na legelege kama
anavyolalamika Profesa Shivji! Nje ya serikali tatu ni uhuru kamili wa
‘Washirika wa Muungano’ na kuzaliwa upya kwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar.
BILA MUUNGANO KUWEPO NI
VITA???
Katika hitimisho la mhadhara
wake, Profesa Shivji ametoa ‘picha ya kiama’ (doomsday scenario) endapo Muungano utavunjika kwa sababu ya
kukubaliwa muundo wa shirikisho lenye serikali tatu: “Muungano ukivunjika hakuna mwananchi atakayenusurika, awe wa Tanganyika
au wa Zanzibar.”[75]
Kwingineko katika hitimisho
la mhadhara huo, msomi huyu maarufu anaendeleza dhana yake ya ‘serikali tatu ni
kiama’: “Suala la Muungano sio letu tu.
Kuna nchi za kibeberu zina maslahi makubwa ya rasilmali pamoja na ya kijeshi
katika eneo letu, hasa Bahari ya Hindi. Tukibeza mambo haya nyeti kwa sababu tu
ya uchu wa madaraka ya viongozi wachache, tutawapeleka watu wetu kwenye hali
mbaya.”[76]
Ili kutilia nguvu hoja yake kwamba kuvunjika kwa Muungano kutaleta vita,
Profesa Shivji ametumia mifano ya vita na migogoro ya mipaka iliyotokea baada
Urusi ya Kisovieti, Shirikisho la Yugoslavia na, katika Afrika, Sudan
kuvunjika.
Hoja hii ya Profesa Shivji na
mifano yake inastahili majibu. Kwanza, mifano aliyoitumia ni ya upande mmoja na
ya kiitikadi zaidi. Hii ni kwa sababu kuna mifano ya nchi zilizovunja muungano
wao bila kuwepo vita au migogoro ya mipaka. Jamhuri za Czech na Slovakia
zilizotokana na kuvunjika kwa Jamhuri ya zamani ya Czechoslovakia ni mfano
mzuri. Haiyumkini kwamba Profesa Shivji anaufahamu mfano huu vizuri.
Pili, kuna nchi nyingi ambazo
zimepigana vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu kwa sababu ya kulazimisha
muungano usiokubaliwa na upande mmoja au mwingine katika umoja huo. Ethiopia na
Eritrea ni mfano mmojawapo. Mwaka 1952 Ethiopia ilisaini makubaliano kati yake
na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yaliyoifanya Eritrea sehemu ya Shirikisho la
Ethiopia na hivyo kumaliza utawala wa Uingereza katika koloni hilo la zamani la
Italia.
Hata hivyo, tarehe 14
Novemba, 1962, Mfalme Haile Selassie I wa Ethiopia alivunja makubaliano hayo
kwa nguvu na kuifanya Eritrea kuwa sehemu ya Himaya yake. Vita vya ukombozi
vilivyosababishwa na kitendo hicho vilichukua karibu miaka thelathini hadi
Ethiopia iliposhindwa mwaka 1991 na Eritrea kujipatia uhuru kamili.[77]
Vile vile Profesa Shivji anaufahamu mfano huu vizuri sana, kwa sababu alikuwa
mmoja wa wanazuoni wengi waliounga mkono wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa
Eritrea (Eritrean People’s Liberation
Front - EPLF), kilichoongoza mapambano ya uhuru wa nchi hiyo.
Sudan ya zamani ni mfano
mwingine wa vita vilivyosababishwa na kulazimisha muungano usiotakiwa na upande
mmoja.[78] Mnamo
Februari, 1953, Uingereza na Misri zilizokuwa zinatawala Sudan ya Kusini na ya
Kaskazini kama maeneo tofauti kwa utaratibu wa Condominium zilikubaliana kukabidhi uhuru kwa shirikisho la Sudan
ifikapo tarehe 1 Januari, 1956. Hata hivyo, kabla ya tarehe hiyo kufika,
viongozi wa Sudan Kaskazini walikiuka makubaliano ya kuunda serikali ya
shirikisho. Matokeo yake ni kwamba wananchi wa Sudan Kusini waliasi na kuanzisha
kile kinachojulikana katika historia kama Vita ya Kwanza ya Wenyewe kwa Wenyewe
ya Sudan (First Sudanese Civil War au
Anyanya I Rebellion). Vita hiyo
ilianza Agosti, 1955 na ilimalizika kwa kusainiwa kwa Makubaliano ya Amani ya
Addis Ababa ya mwaka 1972. Makubaliano hayo yalirudisha mfumo wa Shirikisho
ulioipa Sudan Kusini mamlaka makubwa ya utawala wa ndani. Makubaliano ya Addis
Ababa hayakudumu muda mrefu kwa sababu Serikali Kuu ya Sudan iliyahujumu.
Matokeo yake, mwaka 1978 Maasi ya Anyanya II yalianza tena. Makubaliano ya
Addis Ababa yalivunjika kabisa mwaka 1983 na Vita ya Pili ya Wenyewe kwa
Wenyewe ya Sudan (Second Sudanese Civil
War) ilianza mwaka 1983 hadi ilipoisha baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa
Amani wa Nairobi wa tarehe 9 Januari, 2005.
Chini ya Mkataba wa Amani wa
Nairobi, Sudan Kusini ilijitawala kwa masuala ya ndani kwa miaka sita hadi 2011
wananchi wa Sudan Kusini walipopiga kura ya maoni na kuamua kujitenga na Sudan
ya Kaskazini. Tarehe 9 Julai, 2011, Jamhuri ya Sudan Kusini ilizaliwa kama nchi
huru. Ni kweli kwamba bado kuna mgogoro wa mpaka kati ya Jamhuri hiyo mpya na
Sudan Kaskazini. Hata hivyo, mgogoro huo hauwezi kulinganishwa na vita vya
wenyewe kwa wenyewe iliyochukua miaka hamsini kuanzia 1955 hadi 2005! Hapana
shaka kwamba Profesa Shivji anaifahamu historia hii vema, kwani zama za ujana
wake alisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Dk. John Garang,
mwasisi wa Chama/Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Sudan (Sudanese People’s Liberation Movement/Army – SPLM/A).
Tatu, zipo nchi ambazo
zinaendelea kuwa na vita kwa sababu ya kulazimisha umoja ambao upande mmoja
unaukataa. India (mgogoro wa Jimbo la Kashmir), Hispania (Jimbo la Basque) na
Angola (Jimbo la Cabinda) ni mifano mizuri. Ni vigumu kuamini kwamba Profesa
Shivji hafahamu mifano ya nchi hizi pia. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba hoja
serikali tatu = kuvunja Muungano = vita na maangamizi ni hoja yenye lengo la
kutisha wananchi ili wasiweze kujadili masuala yote yanayohusu Muungano ikiwamo
kuachana nao.
Na nne, hoja ya Profesa
Shivji kwamba wanaodai kuwe na Muungano wa shirikisho lenye serikali tatu ni
‘viongozi wachache’ wenye ‘uchu wa madaraka’ ni ya kusikitisha sana. Hii ni
sawa sawa na kuwaita Rais Aboud Jumbe na wasaidizi wake, au wajumbe wa Tume ya
Nyalali, au ya Kissanga au hata ya sasa ya Warioba, au Wabunge wa G55, waroho
wa madaraka kwa sababu tu hawakukubaliana na mfumo wa serikali mbili ambao
Shivji mwenyewe amekiri mara nyingi umeshindwa kutatua matatizo na ‘Kero za
Muungano’!
SERIKALI TATU NI GHARAMA
KUBWA!!!
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Tangu kuchapishwa kwa Rasimu,
kumejitokeza kauli kwamba kuwa na muundo wa Muungano wenye serikali tatu
itakuwa ni gharama kubwa kwa nchi maskini kama ya kwetu. Viongozi na makada wa
CCM wameidaka hoja hii ya gharama za Muungano kama ndio turufu yao ya kuendelea
na muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili. Katika Ufafanuzi wake, CCM imedai kwamba “gharama za uendeshaji wa Serikali zilizopo hivi sasa ni kubwa. Kuwepo
kwa Serikali ya tatu kutakuwa ni gharama ya ziada na hivyo kuwa mzigo mkubwa
kwa wananchi.”
Kwa upande wake, Profesa
Shivji amezungumzia suala hili kama ifuatavyo: “Kwa upande wa gharama, ni wazi kwamba kuendesha serikali ya muungano
kutakuwa na gharama kubwa. Kazi inayofanywa na taasisi moja au idara moja
katika muundo uliopo sasa itahitaji taasisi mbili. Kwa mfano, badala ya kuwa na
Tume moja ya uchaguzi, sasa kutakuwa na tume mbili, moja ya Muungano na
nyingine ya Bara. (Ukiongeza ya Zanzibar kutakuwa na Tume tatu za uchaguzi. Na
hivyo hivyo kuhusu tume nyingine. Ukiangalia juu juu tu, licha ya taasisi na
idara za kawaida katika serikali, kuna tume karibu nane na mabaraza mawili
yenye wajumbe wazito ambao bila shaka watakuwa na mishahara minono na
marupurupu poa. Wananchi wamekwishaanza kuonyesha wasiwasi wao kwa kuwaongezea
mzigo wa kubeba serikali kamili nyingine, zaidi ya hizi mbili tulizonazo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Hoja hii ya gharama za
kuendesha serikali tatu ni red herring,
yaani ina lengo la kuwatoa wananchi kwenye mjadala wa msingi juu ya kushindwa
kwa muundo wa sasa wa Muungano kutatua ‘Kero za Muungano’, kwa kuwaaminisha
kwamba muundo wa sasa una gharama nafuu zaidi kuliko muundo wa serikali tatu.
Kwanza, kwa kadri ya ufahamu wetu, hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyefanya
uchambuzi wa ulinganifu wa gharama za kuendesha serikali – iwe moja, mbili au
tatu – katika nchi yetu. Hata Ufafanuzi wa
CCM uko kimya juu ya jambo hili. Kwa sababu hiyo, hakuna ushahidi wowote wa
kuthibitisha kwamba kuendesha serikali tatu ni ghali zaidi kuliko kuendesha
serikali mbili. Kwa vyovyote vile, kama suala la gharama za kuendeshea serikali
ndio jambo muhimu zaidi katika kuamua muundo wa Muungano, kwa nini tusiwe na
serikali moja tu, kuliko mbili za sasa au tatu zinazopendekezwa na Rasimu?
Pili, na muhimu zaidi, kama
tukichukua mapendekezo ya Mambo ya Muungano kama kigezo cha kupima ukubwa wa
serikali – na kwa hiyo gharama za kuiendeshea – basi gharama za serikali ya
Muungano zinaweza kuwa ndogo sana. Hii ni kwa sababu, haiwezekani – kwa mambo
saba ya Muungano yanayopendekezwa na Rasimu – kuwa na serikali kubwa ya
Muungano. Kwa Mambo hayo ya Muungano, hakutakuwa na zaidi ya wizara nne za
Serikali ya Muungano. Hivyo, kwa mfano, kutakuwa na wizara ya katiba na sheria
itakayoshughulikia masuala ya Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano; wizara
ya ulinzi itakayokuwa na majukumu ya ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano;
wizara ya fedha itakayoshughulikia masuala ya sarafu na benki kuu, na ushuru wa
bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano; na wizara ya
mambo ya nje. Masuala yaliyobaki, yaani uraia na uhamiaji na usajili wa vyama
vya siasa hayastahili kuwa na wizara zinazojitegemea kwa hiyo yanaweza kuwekwa
chini ya mojawapo ya wizara zilizotajwa hapo juu.
Ibara ya 98(2) ya Rasimu
inapendekeza ukomo wa ukubwa wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano kuwa
mawaziri wasiozidi kumi na tano. Kwa upande mwingine, ibara ya 98(3) inaelekeza
kwamba “Serikali ya Jamhuri ya Muungano
itakuwa na Wizara kwa kuzingatia mamlaka ya Serikali kwa mujibu wa Katiba hii.”
Sasa kama mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano yako kwenye mambo saba ya
Muungano kwa mujibu wa Rasimu hii, je, hao mawaziri wasiozidi kumi na tano
watatoka wapi na watatimiza majukumu gani? Ni wazi kabisa kwamba mapendekezo ya
ibara ya 98(2) yanakinzana na matakwa ya ibara za 62(1) na 63 zinazohusu
mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya Mambo ya Muungano.
Kwa mtazamo huo huo wa ibara ya
98(3) na orodha ya Mambo ya Muungano kama kipimo cha ukubwa wa Serikali ya
Muungano, taasisi nyingine zinazopendekezwa na Rasimu haziwezi kuwa kubwa sana
na nyingine hazitakuwepo kabisa. Kwa mfano, Katibu Mkuu Kiongozi na Makatibu
Wakuu wanaopendekezwa katika ibara za 105 na 106 za Rasimu hawawezi kuzidi
idadi ya Wizara nne zilizotajwa hapo juu zitakazoshughulikia Mambo ya Muungano.
Kwa maana hiyo, kwa kuzingatia idadi ya Makatibu Wakuu wenyewe, Kamati Maalumu
ya Makatibu Wakuu inayoelezwa katika ibara ya 107; na Sekretarieti ya Baraza la
Mawaziri inayotajwa katika ibara ya 108, hazina maana wala umuhimu wowote
kikatiba.
Au tuchukue mapendekezo
yanayohusu Bunge la Jamhuri ya Muungano. Kwa mujibu wa ibara ya 105(4) ya
Rasimu, kila Jimbo la Uchaguzi litawakilishwa na wabunge wawili kwa kuzingatia
jinsia zao. Ibara ya 113(2)(a) inabainisha ‘Jimbo la Uchaguzi’ kuwa ni kila
mkoa kwa upande wa Tanzania Bara na wilaya kwa upande wa Zanzibar. Aidha, kwa
mujibu wa ibara ya 113(2)(b), kutakuwa na wabunge watano wa kuteuliwa na Rais
kuwakilisha watu wenye ulemavu. Tukichukua idadi ya mikoa ishirini na tano ya
Tanzania Bara na wilaya 10 za Zanzibar kwa sasa, Bunge la Jamhuri ya Muungano
litakuwa na wabunge 75.
Kwa mapendekezo ya muundo wa
serikali tatu, Bunge la Zanzibar litakuwa na Wabunge hamsini wa majimbo ya sasa
ya uchaguzi; wakati bunge la Tanganyika litakuwa na wabunge 189 wa majimbo ya
uchaguzi ya sasa. Kwa maana hiyo, muundo wa Muungano wa serikali tatu utakuwa
na mabunge matatu yenye jumla ya wabunge 314.
Kwa kulinganisha, Bunge la
Jamhuri ya Muungano la sasa lina idadi ya wabunge 239 wa majimbo ya uchaguzi –
189 wa majimbo ya uchaguzi ya Tanzania Bara na hamsini ya Zanzibar. Vile vile,
kuna wabunge 102 wa Viti Maalumu, 10 wa kuteuliwa na Rais na watano
wanaowakilisha Baraza la wawakilishi Zanzibar na Mwanasheria Mkuu, kwa idadi ya
jumla ya wabunge 357.
Kwa upande wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar, kuna wawakilishi hamsini wanaowakilisha majimbo ya
uchaguzi, kumi wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar, ishirini wa Viti Maalum na
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, kufanya jumla ya wawakilishi themanini na moja.
Kwa maana hiyo, kwa muundo wa sasa wa Muungano, mabunge mawili tuliyonayo yana
idadi ya wabunge 438. Idadi hiyo ni kubwa kuliko idadi ya wabunge wa mabunge
matatu yatakayokuwepo chini ya muundo wa serikali tatu kwa wabunge 124!
Na sio Bunge ambalo linaweza
kuwa na gharama ndogo kuliko gharama za sasa. Taasisi za Muungano
zinazopendekezwa kama vile Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali (ibara ya
109); Tume ya Utumishi wa Mahakama (ibara ya 180); na Tume ya Utumishi wa Umma
(ibara ya 186) haziwezi kuwa kubwa sana kwa kuzingatia ukubwa wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Rasimu.
Aidha, uwepo wa taasisi
nyingine kama vile Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji (ibara ya 200) na
Tume ya Haki za Binadamu (ibara ya 208) unakinzana na matakwa ya aya za 62(1)
na 63 za Rasimu na kwa hiyo haziwezi kugharimiwa na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano!
Vile vile, majukumu ya
utekelezaji wa Mambo mengine ya Muungano kama uchaguzi na usajili wa vyama vya
siasa yanaweza kutekelezwa na taasisi husika za Washirika wa Muungano kwa
makubaliano na masharti maalumu chini ya aya ya 59(3) ya Rasimu. Hii nayo
itapunguza gharama za kuendesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Ni wazi – kwa mtazamo huu –
kwamba gharama za kuendeshea muundo wa shirikisho lenye serikali tatu zinaweza
kuwa hata ndogo kuliko gharama za kuendeshea muundo wa Muungano wa serikali
mbili za sasa.
FAIDA ZA MUUNGANO NI KWA
WAZANZIBARI PEKE YAO?
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Pendekezo la Rasimu kuhusu
muundo wa Serikali tatu limeleta hoja juu ya faida za Muungano kwa kila upande
wa Washirika wa Muungano. Hivyo, kwa mfano, katika Ufafanuzi wake CCM imedai kwamba pendekezo hili litaleta “... urasimu na utata wa kisheria katika
umiliki na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.” CCM inafafanua
zaidi juu ya jambo hili: “Urasimu wa
kibiashara na umilikaji ardhi utaongezeka kwa sababu biashara, ardhi na
umilikaji wa mali wa aina nyingine si mambo ya Muungano.”
Kwingineko katika Ufafanuzi wake, CCM inadhihirisha
kwamba msimamo wake juu ya muundo wa Serikali tatu unatokana na hofu ya athari
za muundo huo kwa maslahi ya kiuchumi ya Wazanzibari walioko, au wenye vitega
uchumi, Tanzania Bara. Hivyo basi, “muundo
wa Serikali mbili una urasimu mdogo wa kisheria na hivyo kutoa fursa nyingi za
kiuchumi na kijamii hususan kwa Wazanzibari ambao eneo lao la ardhi ni dogo
wakati idadi ya wakaazi inaongezeka mwaka hadi mwaka.” Aidha, kwa mujibu wa
CCM, “muundo uliopo unawawezesha
Wazanzibari kumiliki ardhi na rasilmali nyingine zilizoko Tanzania Bara kama
raia wa Tanzania, ingawaje ardhi na rasilmali nyingine za kiuchumi si masuala
ya Muungano.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Inajulikana kwamba, kwa
mujibu wa sheria za Zanzibar, Watanzania Bara hawana haki ya kumiliki ardhi
Zanzibar, licha ya kuwa raia wa Tanzania. Aidha, licha ya kuwa raia wa
Tanzania, Watanzania Bara wanaoajiriwa katika sekta binafsi Zanzibar wanatakiwa
kutimiza masharti ya vibali vya ajira
sawa na raia yeyote wa nchi za kigeni. Yote haya ni nje ya ukweli kwamba
Watanzania Bara hawawezi kuajiriwa katika taasisi yoyote ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, tofauti na Wazanzibari ambao wanaajiriwa na taasisi za
Serikali ya Jamhuri ya Muungano hata kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano.
Vile vile, yote haya ni nje
ya ukweli kwamba wakati Wazanzibari wanaweza kikatiba kushiriki shughuli za
kisiasa na kiutawala Tanzania Bara hata kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano,
Watanzania Bara hawana uwezo huo. Hivyo basi, kwa utaratibu huu, Wabunge wa
Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wanashiriki katika mijadala ya
mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara, Wazanzibari wanashikilia nafasi za
juu za kisiasa kama vile uwaziri katika wizara zisizokuwa za Muungano na Baraza
la Wawakilishi Zanzibar lina uwakilishi maalum katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano. Wananchi wa Tanzania Bara hawana haki ya kushiriki katika mambo haya
kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Upinzani wa CCM dhidi ya
pendekezo la Rasimu juu ya muundo wa Serikali tatu unadhihirisha ushawishi
mkubwa wa Zanzibar katika siasa za ndani ya CCM, hasa hasa katika zama hizi za
vyama vingi na vita za makundi mbali mbali ndani ya chama hicho. Katika
mazingira haya, mtu yeyote anayetaka kupitishwa kuwa mgombea urais kwa kupitia
CCM anakuwa anahitaji kura za CCM Zanzibar ili kushinda katika kinyang’anyiro
hicho.
Kwa kauli ya Mwalimu Nyerere
katika kitabu chake Uongozi Wetu na
Hatima ya Tanzania: “Sababu moja
kubwa iliyofanya viongozi wetu wasitake kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ... ni umuhimu
wa kura za Zanzibar katika kumteua mwanachama wa CCM kuwa Mgombea wa Urais wa
Jamhuri ya Muungano. Kwa kiongozi yeyote anayeliona jambo hilo kuwa ni muhimu
kupita mengine yote, kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ni dhambi ambayo haina budi iepukwe
kwa kila njia.” Hofu hii ya ‘kuwaudhi’ Wazanzibari ndio imepelekea CCM
kutaka kulinda maslahi ya kiuchumi ya Wazanzibari kwa kukataa muundo wa
Serikali tatu.
[1] Hotuba ya Mwenyekiti wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Mhe. Joseph S. Warioba, Wakati wa Kukabidhi Ripoti ya
Tume kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete na Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, 30 Desemba, 2013,
Dar es Salaam. Imenukuliwa kutoka Baraza la Katiba Zanzibar, Katiba Tuitakayo: Muhtasari wa Rasimu ya
Pili na Mapendekezo, Januari, 2014.
[2] Imenukuliwa kutoka Bango
Kitita la Randama ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Februari, 2014, uk. 4
[3] Imenukuliwa kutoka kwenye Bango
Kitita la Randama..., uk. 135.
[4] Tafsiri ya Kiswahili ya kitabu hiki ilichapishwa na Amana
Publishers, Dar es Salaam, mwaka 1995.
[5] Ibid., uk. 24.
[6] Kamati Maalum ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Muhtasari Mkuu wa Taarifa ya Kamati ya BLM ya Kujenga Hoja Juu ya
Masuala ya Muungano wa Tanzania, aya ya 36, uk. 12.
[7] Tume pia imezitaja sifa hizi kuwa ndio sifa za msingi za nchi
inayofuata mfumo wa shirikisho. Angalia Bango
Kitita la Randama..., uk. 6-7.
[8] Tanzania: The Legal
Foundations of the Union, Second Expanded Edition, uk. 35.
[9] Ibid., uk. 37
[10] Ibid., uk. 34
[11] ‘The Consolidation of the Union: A Basic Re-Appraisal.’ Makala hii
iliwasilishwa katika Semina iliyoandaliwa na Chama cha Mawakili Tanganyika
tarehe 27-29 Julai, 1983, na baadae kuchapishwa katika kitabu kilichohaririwa
na Maprofesa Chris M. Peter na Haroub Othman, Zanzibar and the Union Question, kilichochapishwa na Kituo cha
Huduma za Kisheria cha Zanzibar mwaka 2006.
[12] Eastern African Law Review
(1981-1983), 73-137
[13] The Legal Foundations ...
ibid., uk. xi-xii.
[14] uk. 1
[15] Ibid., uk. 2-3
[16] Ibid., uk. 1
[17] Ibid., uk. 2
[18] Ibid., uk. 2
[19] Ibid., uk. 1
[20] Bango Kitita la Randama ... uk. 5
[21] Ibid., uk. 5-7
[22] Mapendekezo ya Wajumbe wa
Kamati Na. 4 ya Bunge Maalum Kuhusu Marekebisho ya Sura ya Kwanza ya Rasimu ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
[23] Sheria Na. 22 ya mwaka 1964,
Sura ya 557.
[24] Ibid., kifungu cha 4.
[25] Ibara ya 98(1)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
1977.
[26] Sheria Na. 61 ya 1964.
Sheria hii ilipata ridhaa ya Rais Nyerere tarehe 10 Disemba, 1964.
[27] Angalia pia kifungu cha 3(2) cha Sheria hiyo.
[28] Imenukuliwa kutoka Juma Duni Haji, Nyerere na Siasa za Muungano Zanzibar: Mapinduzi Kayapindua 1964,
uk. 36.
[29] Mawasiliano haya yanapatikana katika kitabu cha Harith Ghassany, Kwaheri
Ukoloni, Kwaheri Uhuru: Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia,
kilichochapishwa nchini Marekani mwaka 2010, kurasa 414-420.
[30] Ref. L.D/760/Vol. XXXIV/66 ya tarehe 22 Juni, 2005, Kuh. ‘KUPATIWA
NAKALA YA HATI YA MKATABA WA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR.’
[31] Aya ya (iii)(a)
[32] Aya ya (iii)(b)
[33] Aya ya (iii)(c)
[34] Aya ya (iii)(d)
[35] Aya ya (iv)
[36] Aya ya (vi)(a)
[37] Aya ya (vi)(b)
[38] Aya ya (vii)(a)
[39] Aya ya (vii)(b)
[40] Aya ya (vii)(b)
[41] Tangazo la Serikali Na. 245 la
tarehe 1 Mei, 1964.
[42] Kifungu cha 3(1)
[43] Kifungu cha 6(1)
[44] Kifungu cha 10
[45] Tangazo la Serikali Na. 246
la tarehe 1 Mei, 1964.
[46] Kifungu cha 2
[47] Ibara ya 98(1)(a) ikisomwa pamoja na Nyongeza ya Pili, Orodha ya
Kwanza.
[48] Ibara ya 98(1)(b) ikisomwa pamoja na Nyongeza ya Pili, Orodha ya
Pili.
[49] Sheria Na. 18 ya mwaka 1965.
[50] Sheria Na. 43 ya mwaka 1965
[51] Ibara ya 1
[52] Ibara ya 2(1)
[53] Ibara ya 3(2)
[54] Ibara ya 2(1) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Toleo la 1977.
[55] Ibara ya 1
[56] Sheria ya Marekebisho ya Tano
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Na. 15 ya 1984.
[57] Ibara ya 1. Mabadiliko hayo pia yalilazimisha mabadiliko katika
Katiba Mpya ya Zanzibar iliyotungwa mwaka huo ambapo ibara yake ya 1 ilitamka kwamba
‘Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.’
[59] Ibara ya 2(1)
[60] Sheria Na. 15 ya 1971.
Sheria hiyo ilianza kutumika tarehe 7 Mei, 1971.
[61] Ibid., kifungu cha 3
[62] Angalia picha za ujumbe wa Zanzibar siku ya Zanzibar kukubaliwa
rasmi kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa ulioongozwa na Waziri Mkuu Mohamed
Shamte Hamadi na Waziri wa Mambo ya Nje Sheikh Ali Muhsin Barwani na Balozi wa
kwanza wa Zanzibar Umoja wa Mataifa Maalim Hilal Mohamed, Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru..., ibid., uk. 463-465
[63] Ibara ya 87 ya Katiba ya
Zanzibar, 1984.
[64] Ibara ya 7(1) na (2) ya Katiba
Mpya ya Kenya, 2010.
[65] Ibara ya 39(3) ya Katiba ya
Jamhuri ya Ghana, 1992.
[66] Ibid., ibara ya 7(3)
[67] Ibara ya 6 ya Katiba ya
Zimbabwe, 2013. Ibara ya 6(1) inatambua lugha 16 za Zimbabwe kuwa ni ‘lugha
zinazotambuliwa rasmi’; na ibara ya 6(3)(a) inaelekeza dola na taasisi na
mashirika ya serikali kuhakikisha kwamba lugha zote zinazotambuliwa rasmi
zinatumiwa kwa usawa. Aidha, ibara ya 7(a) inaielekeza mamlaka ya nchi hiyo
kuhakikisha kwamba Katiba ya Zimbabwe inatafsiriwa kwenye lugha zote
zilizotambuliwa rasmi.
[68] Issa G. Shivji, Utatanishi na
Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga Kigoda cha Mwalimu,
Dar es Salaam, Juni, 2013.
[69] Tanzania, Tume ya Rais ya
Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa Tanzania, Vitabu Vitatu,
1991.
[70] Mwalimu Julius K. Nyerere,
Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, Harare, 1993.
[71] Ibid., uk.
[72] Ibid., uk. 35
[73] Op. cit.
[74] Ibid., uk.
[75] Ibid., uk. 36
[76] Ibid., uk. 37
[77] Historia ya vita ya ukombozi wa Eritrea imeelezwa na Michela Wrong
katika kitabu chake I Didn’t it For You:
How the World Used and Abused a Small African Nation, Harper Perennial,
London, 2005.
[78] Scopas S. Poggo, War and
Conflict in Southern Sudan, 1955-1972, University of California, Santa
Barbara, 1999; Hizkias Assefa, Mediation
of Civil Wars, Approaches and Strategies – The Sudan Conflict, Westview
Press, Colorado, 1987; Edgar O’Ballance, The
Secret War in the Sudan: 1955-1972, Faber & Faber, Hamden, 1977; and
Cecil Eprile, War and Peace in the Sudan,
1955-1972, David & Charles, London, 1974.
No comments:
Post a Comment