Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, John Mnyika amesema zipo kila dalili kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinayo rasimu yake mbadala ambayo ndiyo inayopiganiwa na wajumbe wanaotokana na chama hicho ili ipitishwe na Bunge Maalum la Katiba.
Mnyika aliyasema hayo jana wakati yeye na baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani kuamua kutoka kwenye kikao cha Bunge Maalum la Katiba kwa madai kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hili, Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa akiongoza kikao hicho kuwaburuza.
Alisema CCM inafanya kila mbinu ikiwa ni pamoja na kuchakachua kanuni za bunge hilo ili iweze kufanikisha lengo lake la kupitisha rasimu yake mbadala.
“Kuna mambo ambayo hayavumiliki na tutayapinga kwa gharama yoyote, hatuwezi kukubali kuchezewa mchezo mchafu wa aina hii na CCM, kwani inavyoonekana wanayo rasimu yao ambayo wanaitaka tupitishe kama Bunge Maalum la Katiba, sasa sisi hapa hatutengenezi katiba ya CCM, bali tunaandaa Rasimu ya Katiba inayoendana na matakwa ya wananchi wote wa Tanzania,” alisema Mnyika.
Akifafanua zaidi, Mnyika alisema kuwa dalili za CCM kuwa na rasimu yake mbadala zinaonekana waziwazi kwenye vikao vya kamati, ambako kila mjumbe anayesimama kuchangia huwa anasoma karatasi, na katika uchunguzi wake amebaini kuwa maandishi wanayosoma wajumbe hao yanafanana.
Alisema jambo la kushangaza zaidi ni kwamba kila kinachosomwa na Mjumbe kutoka CCM kwenye vikao vya kamati hushangiliwa na kuungwa mkono na wajumbe wenzake na unapofika wakati kupiga kura wajumbe hao wa CCM husimamiana kuhakikisha kuwa mawazo yao ndiyo yanayopitishwa.
Mnyika alisema kuwa pamoja na mbinu hizo chafu, kuna mambo yanayowabana wana-CCM kufanikisha azma yao hiyo na ndiyo sababu wanalazimika hata kurekebisha kanuni ili mambo yaende kama yalivyopangwa.
Alisema hata kwenye kikao cha Bunge Maalum kilichofanyika jana asubuhi kwa ajili ya kupitisha azimio la marekebisho ya kanuni, Makamu Mwenyekiti alikuwa amepewa maelekezo ya watu wanaopaswa kuchangia na watu hao walipokamilika alitaka amalize mjadala bila ya kusikiliza hoja za wabunge wengine, jambo ambalo liliwachefua wabunge wa upinzani na kuamua kutoka nje ya ukumbi.
“Kinachofanyika ndani ya ukumbi wa Bunge hakikutokea kwa bahati mbaya, Mwenyekiti amepewa maelekezo ya watu wanaopaswa kuzungumza na walipokamilika kama walivyopanga asimame mjumbe atoe hoja ya kumaliza majadiliano, hatujapewa muda na sisi tulete jedwali la marekebisho kama ambavyo kanuni zinaagiza, lakini wanataka tufanye uamuzi, sisi tunaona huku ni kuburuzwa na hatutakubali,” alisema Mnyika.
No comments:
Post a Comment