Sunday, March 30, 2014

Ukawa sasa yapania kufanya ziara nchi nzima

Dar es Salaam. Muungano wa Vyama vya Upinzani (Ukawa) nje ya Bunge la Mabadiliko ya Katiba (BMK), unajiandaa kuzunguka nchi nzima kufanya kampeni ya kuelimisha umma juu ya ukiukwaji wa haki na kanuni za Bunge hilo unaofanywa na chama tawala.
Wakitoa tamko la pamoja kwa waandishi wa habari jana, Makatibu Wakuu wa Vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, Dar es Salaam walisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekuwa kikijihusisha na vitendo vingi vinavyokiuka kanuni za upatikanaji wa Katiba Mpya ikiwamo utoaji wa rushwa kwa baadhi ya wajumbe.
“Ukawa-nje tumepata taarifa ya kutolewa kwa ahadi za vyeo baada ya Bunge kwa baadhi ya wajumbe ili kuunga hoja sera za CCM,” sehemu ya tamko ilieleza kupitia kwa Dk. Willbrod Slaa.
Ukawa-nje, wanasema kuwa hata hotuba ya Rais licha ya kuonekana kuipinga rasimu iliyosomwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba iliweka wazi dhamira ya CCM kupitisha mapendekezo yao.
Katibu Mkuu wa Chadema alimpongeza Profesa Ibrahim Lipumba kwa ujasiri wake wa kukataa uongozi ndani ya BMK, ingawa kuna posho za ziada kwa kuwepo katika nafasi hiyo.
“Wingi wa wana-CCM ndani ya Bunge isiwe hoja ya kuvuruga utaratibu mzima na wanatakiwa wajue kuwa Watanzania walio nje ni wengi zaidi yao,” alisema Dk. Slaa.
Naye Mkurugenzi wa Habari wa CUF (Taifa), Abdul Kambaya alisema kuwa wajumbe wa Ukawa waliunga mkono uchaguzi wa Samuel Sitta kuliongoza Bunge hilo kutokana na uwezo wake aliounyesha wakati akiwa Spika wa Bunge lililopita, lakini isiwe sababu ya CCM kutumia fursa hiyo kama faida kwao.
“Uongozi wote wa juu wa bunge umeshikwa na watawala ambao hawawezi kuzalisha katiba nzuri ya wananchi,” alisema Kambaya.
Wajumbe hao pia walieleza kuwa utungaji wa Katiba ni suala la hoja, ushawishi, mijadala huru, maafikiano na maridhiano. Kwa kuwa mpaka sasa taifa limeshatumia zaidi ya Sh81 bilioni katika mchakato huo ni vyema kanuni zikazingatiwa.
Ukawa-nje wanaanza ziara yao leo katika Jiji la Mwanza kuhamasisha wananchi kuwa makini na mwenendo wa BMK. Ziara hizo zinaweza zikawakosa wenyeviti wa vyama hivyo, ambao nao ni Wajumbe wa BMK wanaoendelea na vikao mjini Dodoma.

No comments:

Post a Comment