Saturday, March 15, 2014

Ubunge Chalinze: Majibu ya mgombea wa CHADEMA kwa mgombea wa CUF

MAJIBU/MAELEZO YA PINGAMIZI LILILOWEKWA NA BWANA FABIAN L.SKAUKI DHIDI YANGU MIMI MATAYO M.TORONGEY MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA CHALINZE KUPITIA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA).

UTANGULIZI
Kwa mujibu wa ibara ya 67 (1) ya Katiba ya Jamhuri Muungano wa Tanzania (1977) inaeleza wazi kuwa ili mtu ateuliwe kuwa mgombea ubunge ni lazima awe na sifa zifuatazo;
(i)-Awe raia wa Tanzania
(ii)-Awe ametimiza umri wa miaka ishirini na moja
(iii)-Awe anajua kusoma na kuandika kwa Kiswahili au Kiingereza
(iv)-Awe ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa
(v)-Awe hajatiwa hatiani na mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kodi yoyote ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi.
Aidha, Kwa mujibu wa Ibara ya 67 (2) na -(3) -ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania 1977; hata kama mtu ana sifa zote za kugombea -hataruhusiwa kugombea Ubunge kama :
(i)-Ni raia wa nchi nyingine; au
(ii)-Kwa mujibu wa Sheria iliyotumika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imethibitishwa rasmi kwamba mtu huyo ana ugonjwa wa akili; au
(iii)--Amehukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa muda usiozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu; au
(iv)-Katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu amepata kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja sheria ya maadili ya viongozi wa Umma; au
(v)-Siyo mwanachama na siyo Mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa; au
(vi)-Ikiwa mtu huyo ana maslahi yoyote katika mikataba na serikali ya Jamhuri ya Muungano au serikali ya mapinduzi Zanzibar wa aina yoyote aliyowekewa miiko maalumu kwa mujibu washeria iliyotungwa na Bunge, na iwapo amekiuka miiko hiyo; au
(vii)-Ameshika madaraka ya Afisa Mwandamizi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, isipokuwa madaraka ambayo Rais anaweza au anatakiwa kukabidhi kwa Mbunge kwa Mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, au sheria iliyotungwa na Bunge; au
(viii)-Kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge inayoshughulikia makosa yanayohusika na uchaguzi wa aina yoyote, mtu huyo amezuiliwa kuandikishwa kama Mpiga kura au kupiga kura katika uchaguzi wa Wabunge.
(ix)-Ni mgombea Urais /Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, kwa mujibu wa masharti kwa vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kifungu cha 5.3 kimeweka masharti ya Uteuzi wa Mgombea Ubunge na kuweka kama ifuatavyo;
(i)-Awe amedhaminiwa na wapiga kura wasiopungua ishirini na tano waliojiandikisha kupiga kura katika Jimbo hilo.
(ii)-Mgombea haruhusiwi kujidhamini yeye mwenyewe
(iii)-Awe na dhamana ya shilingi 50,000/=
(iv)-Awe ametoa tamko la kisheria mbele ya hakimu kwamba anazo sifa zinazotakiwa ili kugombea Ubunge
Vilevile, kwa mujibu wa masharti kwa vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kifungu cha 6.0 kimeweka utaratibu wa Pingamizi dhidi ya uteuzi wa Mgombea Ubunge:
Na Kifungu cha 6.3, kimeweka sababu za kuweka Pingamizi kuwa ni:
(i)-Maelezo yaliyopo katika fomu ya uteuzi hayatoshi kumtambulisha Mgombea;
(ii)-Fomu ya Uteuzi haitimizi au haikuwasilishwa kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sharia;
(iii)--Kutokana na maelezo yaliyoandikwa katika fomu ya uteuzi ni dhahiri kwamba Mgombea uchaguzi hana sifa zinazotakiwa;
(iv)-Uthibitisho wa Msimamizi wa Uchaguzi unaopaswa kutolewa haukutolewa; (v)-Mgombea hana sifa zote zinazotakiwa;
(vi)-Hakuna uthibitisho kuwa Mgombea amelipa dhamana ya shilingi elfu hamsini (50,000/=); na
(vii)-Hakuna picha ya Mgombea.
(viii)-Mgombea hakujaza fomu Na.10 kuthibisha kuwa ataheshimu na kutekeleza maadili ya Uchaguzi.
Baada ya utangulizi huo hapo juu ambao unaonyesha dhahiri kuwa hapakuwa na sababu yoyote ya mimi kuwekewa pingamizi na Mgombea ubunge wa Chama cha CUF, kwani hakufuata masharti ya Katiba, Sheria na maelekezo yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kwetu kama wagombea, kwani aliamua kutunga mambo ambayo yapo nje ya utaratibu na hayakidhi haja, hayakufuata Katiba, matakwa ya kisheria na hata maelekezo yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.


Nayasema yote haya kutokana na ukweli kuwa mimi nimekidhi sifa zote za kuwa Mgombea Ubunge na nimetimiza masharti yote yaliyowekwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutokana nabarua yako ya tarehe -13 Machi, 2014 yenye kumbukumbu namba HWB/E.50/21/76-nalazimika kujibu pingamizi hilo kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya Uchaguzi sura Na.343 kifungu Na.40 (5)-kuhusu pingamizi,-hata kama halina nguvu kwa mujibu wa katiba, sheria na maelekezo ya Tume ya taifa ya uchaguzi hoja kwa hoja kama ifuatayvo. -

ENDELEA.......




MAJIBU YA HOJA ZA PINGAMIZI LA FABIAN LEONARD SKAUKI:


1.-HOJA YA KWANZA;-Kwamba mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimejaza taarifa za uongo kwenye fomu zangu kuwa kazi ninayoifanya ni BIASHARA na kusema kuwa ni taarifa za uongo kwa kuwa sikuweka vielelezo vya kuonyesha kuwa mimi ninafanya kazi hiyo, na kuwa sijulikani ninafanya kazi gani .

MAJIBU YA HOJA YA KWANZA : Pingamizi na sababu zilizotolewa na Mgombea wa chama cha wananchi CUF Bwana Fabian L.Skauki hazina mashiko na kuwa yeye ameamua kukupotosha kuwa mimi sio mfanyabiashara kwa kuwa sikuweka vielelezo, japo ni wazi kuwa sikupaswa kuweka vielelezo vyovyote kwani fomu haikuwa inanitaka kuweka vielelezo vya aina yoyote kama ambavyo hata yeye hakuweka vielelezo kuwa anafanya shughuli gani. Ninasikitika kuwa hata wewe Msimamizi umekubaliana na hoja hii dhaifu ya pingamizi na kunitaka mimi kuijibu wakati unajua wazi kuwa haina mshiko wala mantiki kwa mujibu wa sheria za uchaguzi. Naambatanisha leseni yangu ya Biashara yenye jina langu namba B.No. 01299270-iliyotolewa tarehe 19/09/2011 na huo ni uthibitisho kuwa mimi ni mfanya biashara (kielelezo A) -


2.-HOJA YA PILI: Kwamba, mimi Mathayo Torongey sijui kusoma wala kuandika Kiswahili au Kiingereza, na kwamba nimedanganya na hivyo sina sifa za kuwa Mgombea Ubunge.


MAJIBU YA HOJA YA PILI; Kwanza,-nieleze wazi kuwa nimesikitishwa sana na tuhuma hizi ambazo zina lengo la kunichafua mbele ya jamii na Taifa kwa ujumla, zina lengo la kuichafua jamii ya watanzania kutoka familia za wakulima na wafugaji, watu ambao wana kipato kidogo na ambao wanaishi vijijini kuwa ni watu wa hovyo na hawajui kusoma wala kuandika, ni tuhuma za kuwadhalilisha watanzania ambao ni kutoka jamii za wananchi wa vijijini wanaotafuta fursa ya kuchaguliwa kwamba ni watu wa wanaoomba nafasi wakiwa hawajui kusoma wala kuandika, kwa kweli nasikitika sana kwa hili na lilikuwa tusi ambalo msimamizi wa uchaguzi hukupaswa kulipokea. Aidha, nashindwa kutoa ushahidi hapa kwani hata wewe umeziamini tuhuma hizi kuwa mimi sijui kusoma wala kuandika na ndio maana ukanitaka nizijibu, japo ni ukweli ulio wazi kuwa sahihi yangu kwenye fomu haikuwa ya "kuweka dole gumba" niliweka sahihi kwa kuandika na mbele yako na sikuandikiwa.


Pili;-Yafaa mgombea huyu pamoja na wale wote waliomtuma wakatoa ushahidi wake kwako kuwa mimi Mathayo Mang'unda Torongey-sijui kusoma wala kuandika, na hii itamsaidia kuaminika mbele ya jamii ya wananchi wa Chalinze ambao anataka kuwaongoza. Hata hivyo naomba nitoe majibu mbele yako kwa maandishi na kwa kusoma kitu ambacho wewe utataka nisome na kuandika ili uwe uthibitisho kwako kuwa najua kusoma na kuandika .


3.-HOJA YA TATU: Kwamba, mimi Mathayo Torongey nimedanganya kwa kughushi/kufoji sahihi za wadhamini walionidhamini kuwa Mgombea -na kuwa sahihi zote zimefojiwa na hazifanani na zile zilizokuwepo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura na kuwa sahihi zote hizi zimesainiwa na mtu mmoja ambaye sio mhusika .


MAJIBU YA HOJA YA TATU: Kwanza, nieleze wazi kuwa nilipokamilisha kujaza fomu zangu na kudhaminiwa na wadhamini 25 kwa mujibu wa sheria , nilikuja ofisini kwako na tukakagua kwa pamoja majina ya wadhamini wote waliokuwepo kwenye fomu zangu na nilikuja na shahada zote za wapiga kura ambao walinidhamini na wewe ulizikagua na kuridhika kuwa walikuwa ni wapiga kura sahihi na saini zao zilikuwa sahihi na uliandika hilo kama uthibitisho wako kwenye fomu zangu za uteuzi na ndio maana uliniteua kuwa mgombea .


Pili,-Namshangaa mweka Pingamizi kwa kuja na tuhuma kuwa saini za wapiga kura zinatofautiana na saini zilizoko kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura ,hii ni kutokana na ukweli kuwa kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura hakuna saini za wapiga kura isipokuwa saini zipo kwenye vitambulisho vya wapiga kura, na vitambulisho hivyo niliviwasilisha kwako na wewe kama msimamizi wa uchaguzi baada ya kukagua vitambulisho hivyo uliridhika kuwa saini za wadhamini wangu zilikuwa sahihi na ndio maana uliniteua kuwa Mgombea na kuweka "uthibitisho wako" katika kifungu-F.-kwa maandishi kwenye fomu zangu za uteuzi. Naomba kunukuu maelezo yako uliyoyaandika kwenye fomu yangu ya uteuzi tarehe 12.03.2014 saa 9.05 Alasiri kama ifuatavyo ‘(i) Nimekagua majina yote ya waliomdhamini mgombea aliyetajwa hapa naninathibitisha kwamba wote wameandikishwa kuwa wapiga kura katika Daftari la kudumu la wapiga kura katika Jimbo la Chalinze'


Tatu,-Mweka pingamizi anatakiwa kuthibitisha kwako kuwa saini hizo zimeghushiwa kwani ni ukweli ulio wazi kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu kughushi ni kosa la Jinai na hivyo ushahidi wake huo unaweza kuwasilishwa mbele ya vyombo vya dola kwa hatua zaidi.


Nne,-mweka pingamizi ana wajibu wa kuthibitisha kuwa saini hizo zinafanana zote kwani ni ukweli uliowazi kuwa saini za wadhamini wangu hazifanani kutokana na kuwa wapo wadhamini ambao waliweka "dole gumba" kuthibitisha saini zao na wengine walisaini kwa maandishi, sasa kufanana anakosema ni kwa aina gani? Kwamba alama ya dole gumba ina fanana na saini ya kuandika?!


Tano,-yafaa mweka pingamizi na wale wote ambao walishirikiana naye kuweka hoja hii katika pingamizi hili kujitokeza na kueleza kwa uwazi lengo la kuweka pingamizi hili ambalo ni la kutungwa na lenye nia ovu dhidi yangu, Chama changu na Wananchi wote wa Jimbo la Chalinze.


4.-HOJA YA NNE Hoja ya mweka pingamizi iliyonihusu mimi Mgombea wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) ilidai kuwa nimeshindwa kutimiza mahitaji ya kisheria ya kuwa na wadhamini wasiopungua 25, badala yake nimedhaminiwa na wadhamini 28 ambao kati yao wadhamini 7 sio wapiga kura halali wa jimbo la CHALINZE, na kwamba Taarifa zao na namba zilizojazwa hazifanani. Hivyo nabakiwa na wadhamini halali 21 ambao kisheria hawatoshi kutimiza matakwa ya kisheria. Majina ya wadhamini hao ambao hawakidhi matakwa ya kisheria na namba zao kutajwa kuwa ni:- 1. HABIBU ALLY SAIDI - 16886275 2. MOHAMMED RAMADHANI - 30376567 3. ABDULKADIR ALLY - 49264905 4. SHABANI SULEYMAN - 16984045 5. JUMA MRISHO - 48759563 6. RAJABU ALLY - 16872368 7. MANENO MIRAJI - 16872059 MAJIBU YA HOJA YA NNE (4).


Mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimekidhi vigezo na masharti ya wadhamini wote 25 wanaotakiwa kwa mujibu wa sheria kama nilivyo orodhesha kwenye fomu ya wadhamini na hivyo basi pingamizi namba nne lililowekwa na mgombea ubunge wa chama -cha The Civic United Front (CUF) Kuwa Bwana HABIBU ALLY SAIDI mwenye namba 16886275 kuwa sio mdhamini halali, nikiri kuwa ni kweli sio mdhamini wangu halali; Mdhamini wangu halali ni Bwana HABIBU ALLY DAUDI-mwenye namba --16886275.


Na vilevile ni kweli kwamba Bwana MOHAMMED RAMADHANI mwenye ‘30376567' si mdhamini wangu halali, Mdhamini wangu halali ni Bwana MOHAMMED RAMADHANI mwenye namba 30576567. Pia napenda kukuthibitishia bila chembe ya shaka kuwa Bwana ABDULKADIR ALLY-mwenye namba 49264905-aliyezaliwa wilaya ya Bagamoyo tarehe 17/04/1974 ni mdhamini wangu halali aliye andikishwa tarehe 02. 03. 2010 kwenye kituo cha shule ya msingi Mkoko kata ya Msata halmashauri ya Bagamoyo mkoa wa Pwani.


Hata hivyo amesema Bwana SHABANI SULEYMAN mwenye namba -16984045 si mdhamini wangu halali, Napenda kuthibitishia kuwa mdhamini wangu halali ni Bwana SHABANI SELEMANI-mwenye namba 16984045 -na si Bwana SHABANI SULEYMAN.


Hata hivyo, nadhibitisha kuwa Bwana -JUMA MRISHO-mwenye namba 48759563, aliyesema sio mdhamini wangu halali ni halali kwani amezaliwa tarehe 04.04.1981 wilaya ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa kijiji cha Msinune halmashauri ya Bagamoyo mkoa wa Pwani na shahada yake ya kupigia kura imeandikishwa kwenye kituo cha shule ya msingi Msinune, hivyo ni mdhamini wangu halali na amekidhi vigezo vya kunidhamini sawa na Bwana RAJABU ALLY-mwenye namba 16872368-aliyezaliwa tarehe 28.09.1979 wilaya ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa kijiji cha Kiwangwa mkoa wa Pwani naye ni mdhamini halali aliyejiandikisha kwenye kituo cha Kibaoni ofisini; Kama ilivyo kwa mdhamini halali Bwana MANENO MIRAJI-mwenye namba 16872059 aliyezaliwa wilaya ya Bagamoyo kata ya Kiwangwa mkoa Pwani na kaandikishwa kituo cha Kibaoni Ofisini.


Muweka pingamizi angekuwa sahihi Kama ningekuwa sijatoa uthibitisho kwa msimamizi wa uchaguzi. Hoja yake ingekuwa na uzito unao bebwa na kifungu 6.3 (iv) kwenye kitabu cha tume ya taifa ya uchaguzi cha maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea uchaguzi wa urais, ubunge na madiwani kinasema, "Uthibitisho wa msimamizi wa uchaguzi unaopaswa kutolewa haukutolewa".-Lakini kwenye fomu namba 88 F ukurasa 8, -"UTHIBITISHO WA MSIMAMIZI WA UCHAGUZI" -msimamizi wa uchaguzi kwenye F( i) amekiri kukagua na kuthibitisha ya kuwa wadhamini wote walioandikishwa kuwa wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura katika jimbo la CHALINZE ni halali. - Kwa maana hiyo, udhibitisho wa msimamizi wa uchaguzi ni kwamba wadhamini wangu ni halali hivyo hoja ya muweka pingamizi kwenye swala la wadhamini haina mashiko na msimamizi wa uchaguzi hakupaswa kupokea pingamizi hilo bali alipaswa kulitupa kabla ya kufikiria kulileta kwangu. Hata hivyo, nichukue fursa hii adhimu kumuelimisha muweka pingamizi wa chama cha wananchi CUF (Civic United Front) ya kuwa majina yanaweza kufanana kwenye kituo kimoja au kituo kingine -ama kata nyingine au wilaya na mkoa mwingine lakini namba ya kadi halali ya mpiga kura haiwezi kufafana na kadi ya mpiga kura mwingine halali, kwa mfano kwenye kituo 00006347 kata ya Bwilungu jimbo la CHALINZE wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani mpiga kura HAMZA ATHUMANI-mwenye shahada namba 17023223--anafanana jina na HAMZA ATHUMANI-mwenye shahada namba 1702107-sawa na Bwana BONELA SHABANI MADEGA-mwenye shahada namba 19534653-na BONELA SHABANI MADEGA-mwenye shahada namba 19525475. Hawa wote wakitazamwa kwa majina kwa jicho la muweka pingamizi wa CUF wataonekana ni mtu mmoja au ni mapacha wakati uhalisia ni watu tofauti wanao tofautishwa na namba za shahada zao halali za kupigia kura.


5.-HOJA YA TANO. Kuwa Mimi Mathayo Mang'unda Torongey nimedanganya Uraia wangu na kuwa mimi sio Mtanzania wa kuzaliwa -kwa kuwa sikuweka vielelezo vyovyote halali.


MAJIBU YA HOJA YA TANO . Napenda kurudia kuwa huenda mweka pingamizi ameamua kukupotosha na kuandika taarifa za uongo kwa lengo ambalo yeye na wale wote waliomtuma wanalijua wao. Napenda kurudia kuthibitisha kama nilivyoandika kwenye fomu zangu za kuomba uteuzi kuwa mimi ni mzaliwa wa Kijiji cha Kaloleni katika Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro nchini Tanzania . Naomba kuweka kielelezo -"B" kuthibitisha uraia wangu wa Kuzaliwa kama ifuatavyo;


1.-Naweka nakala ya kitambulisho changu cha kuandikishwa kuwa mpiga kura katika Jimbo la Ubungo chenye namba *46670962*.-Na kwa mujibu wa sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 ,kifungu cha 10 (1) ‘sifa na kukosa sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura na kupiga kura' kinasomeka ‘Hakutakuwa na mtu zaidi ya raia wa Tanzania ambaye ametimiza umri wa miaka kumi na nane na ambaye hajapoteza sifa kwa masharti ya Sheria hii au sheria nyingine yoyote ya Bunge atakayestahili kuandikishwa kuwa mpiga kura kwa mujibu wa masharti ya sheria hii' Hivyo kwa kuwa nimekidhi vigezo vya kuwa mpiga kura ,mimi ni raia halali, naambatanisha nakala ya shahada yangu ya Mpiga kura kama kielelezo ‘C'.


- Aidha, ukisoma majibu ya tume ya taifa ya uchaguzi kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na wagombea wa CHADEMA dhidi ya uraia wa wagombea wa CCM Sioi Sumari-2012-na Godfrey Mgimwa 2014 -katika majimbo ya Arumeru Mashariki na Kalenga ,Tume iliamua kuwa jukumu la kuthibisha /kutoa vielelezo kuhusu tuhuma za uraia wa mgombea ni kwa mtoa tuhuma (who allegies-must prove), hivyo mweka pingamizi atakiwe -kuwasilisha vielelezo vya tuhuma zake kwako ili kuthibitisha madai yake kuhusu uraia wangu.


HITIMISHO. Baada ya maelezo tajwa hapo juu na uthibitisho ambao nimeuwasilisha kwako naomba kukujulisha kuwa mimi nina sifa zote kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mgombea halali wa ubunge jimbo la Chalinze na yafaa ukatupilia mbali pingamizi lililowekwa dhidi yangu kama jinsi ambavyo ulipaswa kulitupilia mbali kabla hujalileta kwangu kwani lilikosa sifa na vigezo vya kuwa pingamizi. -
…………………………………

Mathayo Mang'unda Torongey
Mgombea Ubunge wa CHADEMA jimbo la CHALINZE.
14 Machi, 2014.

3 comments:

  1. SAFYY, IVI KISHERIA UYU MBWIGA HAWEZI KUKAMATWA KWA KOSA LA DEFAMATION? KAMA INAWEZEKANA HALAKA AWEKWE NDANI

    ReplyDelete
  2. Mambo vip CHADEMA mnawafuata buriani NCCR, ama mtaacha tamaa za madaraka na kumrudisha zitto kundini kiroo safi, maana naona hata kwenye blog yenu hayupo lakini tunawaona watu ambao hata siuo wawakilishi wa wananchi bungeni wanatabasamu blogini.

    ReplyDelete
  3. Ni aibu sana kuona wajumbe wa bunge la katiba wakiongozwa kimawazo na mtu wakati wao pia ni watu wenye akili timamu na walioaminiwa katika kufanya maamuzi yao binafsi. rai yangu kwao wajitambue kifikra na wawajibike kwa nchi yao na si kufuata mawazo ya mtu yoyote.

    ReplyDelete