Friday, March 21, 2014

Sitta atakiwa kuwa mkali, kutumia kanuni

Wadau wamemtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, kuwa mkali na kutembea juu ya kanuni na kutokubali kuyumbishwa na matakwa ya chama au kundi fulani.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Paul Loisulie, alisema Sitta, bado anaweza kuliongoza bunge hilo na tukio la Jumatatu ni fundisho kwake na awe makini na asijaribu kupindisha kanuni wala kupendelea upande wowote.

Mkazi wa Manispaa ya Dodoma, Ally Saidi, alisema Sitta bado ana uwezo isipokuwa anataka kutofuata kanuni zilizotungwa kwa ajili ya kuongoza na ni vyema vyema akafuata kanuni ili kuacha kufanya mambo yanayowakwaza wajumbe wa Bunge hilo.

Maganga Maganga mkazi wa Arusha, alisema Sitta anafaa kuwa mwenyekiti, lakini sasa anaonekana ameanza tatizo la kukubali kuburuzwa na chama chake (CCM) na hizo ni dalili mbaya.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema upo umuhimu wa Rais, Jakaya Kikwete, kutengua uteuzi wa baadhi ya wajumbe ndani ya Bunge hilo kutokana na kushindwa kutenda mambo yaliyokusudiwa na kujikita katika zomea zomea na vurugu nyinginezo.

“Tukemee, kuna mambo yanajitokeza si mazuri, hayaonyeshi umuhimu wa chombo husika (Bunge),” anasema.

Aidha, alimuomba Sitta kuwa mkali na kuturuhusu badahi ya wajumbe kufanya mambo yasiyostahili ili kuwa na majadiliano ya kina na mazuri.

Mfanyabiashara, Patrick Boisafi, mkazi wa manispaa ya Moshi, alisema tabia kuzomea na kupiga kelele wakati Bunge linaendelea ni mambo yanayofanywa na watu ambao hawajastaarabika.

Askofu wa Kanisa la Kinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Stephen Munga, alisema hakuna matazamio makubwa ya kupata Katiba kwa kuwa muda mwingi umekwisha kwa watu kujizana na kupiga kelele kwa mabo yasiyo ya msingi.

Mkazi wa Morogoro, Rehema Eliseria, alisema kufuatia wabunge waliopo bungeni chini ya mwenyekiti Sitta wanaweza kufanya vyema sana licha kilichotokea Jumatatu bungeni .

No comments:

Post a Comment