Saturday, March 29, 2014

Mbowe-Tumalize mjadala kwa maridhiano badala ya vijembe

Baada ya mvutano mkali ndani ya Bunge Maalum la Katiba, Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe, ameshauri wajumbe kumaliza mjadala kwa maridhiano badala ya kulumbana na kurushiana vijembe.
 
 Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, alitoa ushauri huo juzi wakati akichangia mjadala wa mabadiliko ya kanuni ya 37 na 38 ya bunge hilo, yalipendekezwa na Kamati ya Kanuni ya Bunge hilo kuwa kila mbunge awe huru  kupiga kura ya wazi au ya siri.
 
Alisema mjadala unaoendelea  hautafika mwisho kutokana na pande mbili zinazokinzana kila moja kushikilia msimamo wake, hali ambayo inasababisha baadhi ya wabunge kutoka kwenye mada ya msingi na kuanza kudhalilishana.
 
“Mimi sitaki kujikita kwenye kura ya siri wala kura ya wazi, isipokuwa napenda kushauri kuwa suala hili ili lipate ufumbuzi tulipeleke kwenye kamati ya maridhiano badala ya kuendelea kulumbana kwani naamini kuwa tunaweza kuzungumza kwa muda mrefu na hatutafikia uamuzi,” alisema Mbowe.
 
Aliwaambia wajumbe kuwa yapo mambo mengi na mazito ambayo tayari yamekwishaamuliwa na bunge hilo kwa maridhiano, haoni sababu ya kuendelea na mjadala usiokuwa na mwisho badala ya kutumia njia hiyo ya maridhiano ambayo tayari imekwishaonyesha njia kwa baadhi ya mambo.
 
Wazo hilo liliungwa mkono na baadhi ya wajumbe hilo akiwemo Teddy Ladislaus, ambaye anawakilisha wanafunzi wa elimu ya juu.
 
Katika kuonyesha kuwa mawazo ya Mbowe yalizingatiwa na Mwenyekiti, kabla ya kuahirisha kikao hicho, Mwenyekiti Samwel Sitta aliteua baadhi ya wajumbe kuingia kwenye kamati ya muda ya maridhiano na kuwataka wakutane usiku huo.
 
Baadhi ya wajumbe kamati ya Muda ya Maridhiano ni Profesa James Mwandosya, Anne Kilango Malechela, Profesa Ibrahim Lipumba, Mbowe, Peter Mzirai, James Mbatia, Anna Abdallah, Dk. Asha Rose Migiro , Askofu Dornald Mtetemela, Amon Mpanju, Fredrick Werema na Hamad Rashid.
 
Kamati hiyo ilitakiwa kujadili suala hilo na kuwasilisha mapendekezo yake kwa Mwenyekiti kabla ya kupelekwa bungeni ili kutoa uamuzi wa mwisho.
 
Kanuni ya 37 na 38 ziliwekwa kiporo mwezi uliopita wakati wa kupitisha kanuni nyingine kutokana na wajumbe kushindwa kufikia mwafaka baada ya baadhi yao kutaka itumike kura ya siri wakati wa kufanya maamuzi huku wengine wakitaka iwe ni kura ya wazi.
 
Licha ya kanuni hizo juzi kuletwa bungeni kwa mara ya pili, bado wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba waliendelea kuvutana na kutofikia makubaliano, hali iliyomlazimu Freeman Mbowe kupendekeza suala hilo liamuliwe kwa maridhiano.

No comments:

Post a Comment