Thursday, March 27, 2014

Kanuni zaibua tena mdahalo Bunge la Katiba, Ukawa wahoji kwa nini zibadilishwe



Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umepinga mabadiliko yanayotarajiwa toka kwa Kamati ya Kanuni, wakidai yanaenda kinyume na azimio lililopitishwa na Bunge hilo kwa nia ya kuleta maridhiano.
Uamuzi huo umetangazwa mjini Dodoma na viongozi wa UKAWA mara baada ya kikao cha Bunge kuahirishwa leo asubuhi kufuatia Kamati hiyo ya Kanuni kushindwa kukamilisha kazi yake.
“Mchakato wa Katiba sio idadi ya wingi wa watu ndani ya Bunge,” ameeleza Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, akisisitiza kuwa CCM wasifikiri wanaweza kulazimisha maamuzi kwa kuwa tu wana wajumbe wengi katika Bunge Maalum la Katiba.
“Huu mchakato ni mchakato wa umma, sio mchakato wa Bunge peke yetu,” aliongeza Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema).
Wana-UKAWA hao wamesisitiza kamwe hawatakubali mabadiliko yoyote ya kanuni, isipokuwa yale tu ya vipengele vya 37 and 38 vinavyoelekeza namna ya kupiga kura.
Kwa mtazamo wa Mbowe, harakati zinazoendelea za “kufumua kanuni” dakika za mwisho mwisho ni “hila” zinazoonyesha kile alichokiita “dhamira mbaya.”
Kiongozi mwingine wa Ukawa, James Mbatia amehoji uhalali wa mabadiliko hayo ya kanuni, akisema:
“Kama tuliridhiana kwa pamoja sote kwamba kanuni ni hizi hapa, huyo mwenye [mandate] nyingine ametoka wapi, kwa madaraka gani, kwa ujanja gani?”
“Hatutakubali,” amesisitiza Mbatia, akisema Ukawa “itafanya maamuzi mapana, kwa maslahi mapana ya Watanzania na si kikundi cha Chama Cha Mapinduzi.”

No comments:

Post a Comment