Monday, March 31, 2014

Bawacha: Mawazo ya wananchi rasimu ya katiba yaheshimiwe

Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), limesisitiza kuwa mawazo ya wananchi ambayo yamo kwenye rasimu ya katiba ndiyo yanayopaswa kujadiliwa kwenye bunge maalum la katiba na si vinginevyo.

Mwenyekiti wa Bawacha, Suzan Lyimo, alitoa tamko hilo jana wakati akizungumza na wandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari mjini Dodoma.

Alisema kuwa Bawacha inatoa tamko hilo baada ya kuona hotuba nzuri iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko wakati akiwasilisha rasimu ya katiba kwenye bunge inabezwa na baadhi ya wanasiasa pamoja na viongozi wa serikali.

“Tumesikitishwa na baadhi ya wanasiasa na baadhi ya viongozi serikalini ambao wanabeza hotuba hii nzuri ya Jaji Warioba ambayo ilijaa weledi na utafiti wa kina, sisi wanawake wa Chadema tunaipongeza na tunasema hatuko tayari kuona mawazo ya wananchi yanachezewa ndani ya bunge hili,” alisema Lyimo.

Aliwaambia wanahabari kuwa badala yake wanawake wa Chadema walisikitishwa na kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kutoa hotuba ambayo iliegemea upande mmoja wa kukibeba Chama cha Mapinduzi badala ya kutumia fursa hiyo kuwaunganisha wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla.

Alisema kitendo cha Rais kuikosoa Tume ya Mabadiliko ya Katiba hadharani hakikuwa cha kiungwana kwa kuwa ni yeye mwenyewe aliyeiteua na pia alikuwa akiwasiliana na tume hiyo wakati ikiendelea na majumu yake hivyo alikuwa na nafasi kubwa ya kurekebisha kasoro alizoziona mapema badala ya kuwadhalilisha wajumbe wa tume hiyo hadharani.

Lyimo alisema kuwa upungufu mdogo mdogo uliomo kwenye Rasimu ya Katiba kama vile suala la usawa kutokuwa tunu za taifa, haifanyi kazi nzuri na shirikishi iliyofanywa na tume hiyo kubezwa.

Kwa nyakati tofauti kumekuwapo na makundi ya wanasiasa wakipongeza ama kubeza hotuba zilizotolewa bungeni na Jaji Warioba wakati akiwasilisha rasimu ya katiba pamoja na ile ya Rais Kikwete wakati akizindua bunge katiba.

Hata hivyo kwa kiwango kikubwa hotuba hiyo  inapingwa na wanasiasa wa kambi ya upinzani wakati wanasiasa ambao wana itikadi moja na CCM wamekuwa wakipongeza hotuba ya Rais huku wakibeza ya Jaji Warioba.

No comments:

Post a Comment