Sunday, February 2, 2014

Chadema yataka Mwekezaji Mtibwa anyang’anywe Kiwanda.

 La sivyo kitaongoza maandano ya kumng’oa.

Na Bryceson Mathias, Mtibwa, Mvomero
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka serikali kumnyang’anya Mwekezaji wa kiwanda cha sukari Mtibwa rasimali hiyo, kwa kuwa ameshindwa kuwalipa wakulima na Wafanyakazi, hivyo kutishia maisha, ustawi, maendeleo, uchumi na afya wananchi zao.
Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata ya Mtibwa, Luka Mwakambaya (CHADEMA), ikiwa ni siku chache baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Antony Mtaka, kusimamisha uzalishaji wa kiwanda hicho hadi wakulima na Wafanyakazi hao watakapolipwa Malipo yao sh.Bil. 1.9/-.
Hatua zote hizo zimekuja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kumnanga Mkuu wa Wilaya hiyo Mtaka, kuwa hatua yake ya kukifunga Kiwanda hicho alikurupuka, na kwamba alichostaahili kufanya ni kuhakikisha anapata njia mbadala ya wananchi hao kupata Malipo yao na si siasa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Diwani Mwakambaya, ameiijua juu Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na watendaji wake, kwamba hawana uchungu na maisha ya wananchi wanaonyanyasika ndani ya nchi yao, kutokana na kushindwa kumuadabisha mwekezaji wa Kiwanda hicho.
“Wananchi wanashindwa kulipa matibabu ya ndugu zao Hospitali ya Bwagala, Wanafunzi wameshindwa kupelekwa shule, wanashindwa kuvaa na kujikimu wenyewe kwa mahitaji, kutokana na mwekezaji kuhodhi Malipo ya wakulima wadogo wa miwa na mishahara ya Wafanyakazi.
“Ninafanya upembuzi yakinifu wa majina ya wastaafu zaidi ya 110 waliokufa bila kupata mafao na haki zao stahili, huku wengine wakiwa wamelipwa kati ya Laki 5/- au Mil.1/- ijapokuwa wamefanya kazi zaidi ya miaka 32 na wengine kufukuzwa bila sababu”. Alisema Mwakambaya.
Mwakambaya alisema, katika ahadi aliyoitoa Meneja wa Kiwanda, Hamad Yahaya, siku ya Mkutano wa hadahara baina ya Mkuu wa Wilaya Mtaka na Wakulima na Wafanyakazi, aliahidi kuingiza fedha sh. 1.9/- bilioni kuanzia leo (jana), lakini fedha iliyoingizwa kwenye chama kimoja cha wakulima ni Mil.70/- tu.
Alisema hali hiyo ni dharau na matusi kwa wakulima na Wafanyakazi wanaoteseka na familia zao nchini kwao, kana kwamba wako Somalia, hivyo akadai anasikilizia kikao cha kesho na Mtaka kitakuwaje laa sivyo, wataiomba Polisi iwalinde mlangoni kwa mwekezaji watakakoweka mikeka.
Katika Kikao na Mkuu wa Wilaya (Mtaka) Mwenyekiti wa Halamashauri ya Wilaya ya Mvomero na Diwani wa Kata ya Diongoya, John Van Zealand (CCM), pia alimjia Juu mwekezaji kwa kushindwa kuwalipa wakulima na Wafanyakazi hao, na kudai hata Malipo tu ya Halmashauri halipi, je ya wananchi!
Wanaharakati mbalimbali wa ndani na nje ya Mtibwa, wameuunga mkono kusudi la wakulima na Wafanyakazi ambao hadi tunaenda mitamboni hawako kazini, kufanya maandano ya amani ya kuitaka serikali imnyang’anye mwekezaji huyo kiwanda, maana anakiuka haki za binadamu, na kwamba wako tayari kuongoza maandamano hayo kudai haki hiyo.

No comments:

Post a Comment