Thursday, February 6, 2014

CHADEMA yapeleka kiwewe CCM


  • M4C Pamoja Daima yafanikisha mikutano 206 kwa siku 12
  • Wabunge, mawaziri waagizwa kujibu mapigo kabla ya Bunge
KWA siku 12 za Operesheni M4C Pamoja Daima, Chama cha Dekomrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekitia kiwewe Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho sasa kimelazimika kurejesha wabunge wake mikoani ili kujinusuru kutokana na kimbunga cha operesheni hiyo.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zinasema kwamba CCM imeamua kuwa wabunge wote wasambae majimboni mwao kusafisha upepo wa M4C Pamoja Daima mara baada ya vikao vya kamati za Bunge.
Kwa kawaida, wabunge huwa wanaelekea bungeni Dodoma mara baada ya vikao vya kamati za Bunge, lakini zamu hii chama kimewaelekeza wabunge, wakiwamo mawaziri wote, kurudi mikoani kwa ajili ya kujibu mapigo ya CHADEMA kabla ya kwenda bungeni.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema uamuzi huu wa CCM ni uthibitisho wa athari kubwa za Operesheni M4C Pamoja Daima, ambayo viongozi wa CHADEMA wameimarisha chama na kukiweka pamoja zaidi katika kupigania maslahi ya umma.
Katika wiki mbili hizo, CHADEMA kimefanikiwa kufanya mikutano 206 na kuhamasisha wananchi katika majimbo 166 ya uchaguzi, huku kikifanikiwa kushinikiza serikali iboreshe daftari la kudumu la wapiga kura.
Hata kabla ya CHADEMA kuhitimisha operesheni hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kuboresha daftari hilo kabla ya kura ya maoni ya katiba mpya.
Kwa mujibu wa CHADEMA, wananchi wapatao milioni tano waliofikia umri wa kupiga kura hawajaandikishwa, kwani serikali imekuwa inadai haina hela za kufanyia kazi hiyo.
Viongozi wa CHADEMA walisema wakati wa operesheni hiyo, kwamba serikali imekuwa inagoma kuandikisha wananchi, huku ikijua ni kinyume cha sheria kutofanya hivyo; kwani inapaswa kuboresha daftari hilo mara mbili katika miaka mitano.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, wamekuwa wakisisitiza kuwa serikali isipofanya hivyo, chama hicho kitachukua hatua mbadala ili kuhakikisha wananchi wanajiandikisha na wanashiriki katika kura ya kupitisha katiba mpya.
Uchambuzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha pia kwamba kupitia mikutano ya hadhara na ya ndani, CHADEMA kimefanikiwa kuponya majeraha ya kisiasa miongoni mwa viongozi na wanachama katika baadhi ya maeneo.
Katika Mkoa wa Kagera kwa mfano, Mbowe alifanikiwa kupatanisha Mwenyekiti wa Mkoa, Wilfred Lwakatare na Katibu wa Mkoa, Conchesta Rwamlaza, ambao wamekuwa na ‘bifu’ ya muda mrefu na kutishia kugawa chama makundi kutokana na mgogoro wa Manispaa ya Bukoba uliomng’oa aliyekuwa meya, Anatory Amani.
Amani alikuwa amefanikiwa kugawa CHADEMA katika makundi mawili, moja likitaka ang’oke na jingine likiepuka kumwajibisha kwa mantiki kwamba kitendo hicho kingemnufaisha kisiasa Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki, ambaye aliunga mkono hoja ya CHADEMA ya kumng’oa Amani kwa tuhuma za ufisadi.
Rwamlaza ndiye alikuwa kinara wa upande wa CHADEMA uliokuwa unataka Amani ang’oke, jambo lililosababisha upande mwingine kumtuhumu kwamba anafanya kazi na Kagasheki.
Hata hivyo, Mbowe alipofika Bukoba, alimshukuru Rwamlaza na madiwani wote wa CHADEMA na CCM waliosimama kidete kumwondoa Amani, kwani msimamo wa chama katika suala hilo unafahamika.
Baadaye katika kikao cha ndani, aliwasuluhisha Lwakatare na Rwamlaza, mbele ya Baraza la Mashauriano la Mkoa, umoja na amani vikarejea.
Operesheni hiyo ilifanyika katika mikoa 22 ya Tanzania Bara na kuongeza hamasa ya kisiasa miongoni mwa wanaCHADEMA na wananchi, huku ikisaidia kupokea wanachama wapya kutoka vyama vingine, hasa CCM.
CHADEMA imetumia fursa hiyo pia kunadi wagombea wake wa udiwani katika kata zinazofanya uchaguzi katika maeneo mbalimbali.
Chama hicho kilibeba ajenda tisa zikiwamo mchakato wa katiba mpya katika hatua ya Bunge la Katiba, kura ya maoni; daftari la kudumu la wapigakura.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Benson Kigaila, aliliambia gazeti hili kuwa walikuwa wanafanya mikutano mitano hadi saba katika mkoa mmoja kwa siku kwa sababu ya mfumo waliotumia.
“Kama tungekuwa tunatumia magari kwa muda wa wiki hii moja tungekuwa tumeweza kufika katika mkoa mmoja, na hivyo mkakati wetu wa kutembea nchi nzima ndani ya wiki mbili usingefanikiwa.
“Na operesheni hizi zinagharamiwa kwa asilimia kubwa na michango ya wanachama na wafadhili wetu, na matumizi mazuri ya pesa za ruzuku ambazo huwa tunatenga kila tukipata mwisho wa mwezi,” alisema.
Kigaila alisema kuwa wanaCHADEMA, na viongozi wa chama wapo tayari kuchangia operesheni hizo kwa kuwa wanatambua umuhimu wake.

No comments:

Post a Comment