Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Temeke, Joseph Yona (32), ametekwa nyara na kujeruhiwa vibaya kwa kipigo kisha kutupwa katika vichaka eneo la Tegeta Ununio, wilayani Kinondoni a watu wasiojulikana.
Yona ambaye alitekwa juzi akiwa katika eneo la Mtoni kwa Aziz Ali, amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Yona ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema alisema jana kwamba alitekwa yapata saa 5.00 usiku wa kuamkia jana na watu ambao awali, walijitambulisha kuwa ni polisi.
“Tulikuwa tumekaa na vijana wanne wa Tawi la Ukombozi, Chadema la Temeke, ndipo ghafla wakajitokeza watu kama sita hivi wakaja moja kwa moja na kuninyanyua huku wakiniambia twende kituo cha polisi,” alisema.
Alisema baada ya kuingia ndani ya gari ambalo lilikuwa linafanana na yale ya polisi alivuliwa fulana na kufungwa macho na mikono.
Alisema baada ya mwendo uliochukua kitambo kidogo, gari hilo lilisimamishwa na watu hao wakamshusha chini na kumpeleka sehemu iliyokuwa na bonde huku wakiendelea kumpiga kabla ya kumtelekeza na kutoweka.
“Njiani nilijaribu kuwasihi wasiniue kwa kuwa nina watoto wadogo wawili ambao wananihitaji, niliwasisitiza watambue na kwamba nao wana watoto wafikirie, wakaniuliza kwa nini naivuruga Chadema kwa tamko nililolitoa hivi karibuni kutokana na mgogoro unaoendelea,” alisema.
Alisema kuwa alijitetea kwa kuwataka wakasome vizuri tamko lake, lakini waliendelea kumpiga na kumtaka aombe msamaha kwa kuishambulia Kamati Kuu ya chama hicho, jambo ambalo hakuwa tayari kulifanya kwa kuwa hakuona kama kuna kosa alilolifanya.
“Walinitupa na kutimua mbio wakiniacha nikiwa na maumivu makali. Nilitulia kwa muda na kujitahidi kuinuka na kupiga hatua kwenda nyumba zilizokuwa jirani kuomba msaada, hapo sikuwa na simu wala nauli,” alisema.
Alisema kuwa alipata msaada wa fulana na kuwasiliana na ndugu zake na polisi ambao baada ya muda walifika na kumpeleka Muhimbili kwa matibabu.
Hivi karibuni, Yona alitoa tamko la kupinga hatua ya Zitto kuvuliwa nyadhifa zake na Kamati Kuu ya chama hicho.
Kova aunda jopo la uchunguzi
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa ameunda jopo la wapelelezi wanane watakaoongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Jaffari Mohamed kuchunguza tukio hilo.
Chadema yalaani
Kwa upande wake, Chadema kimeeleza kupokea kwa mshtuko taarifa za tukio la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Yona.
Katika taarifa yake iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano, chama hicho kimeliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo kililoliita kuwa ni la kihuni na mengine ya namna hiyo yenye lengo ya ukatili dhidi ya binadamu, ili ukweli ujulikane na haki itendeke kwa sheria kuchukua mkondo wake.
Pia kimewataka wanachama na Watanzania kwa ujumla kutulia, hasa pale watu wenye hila na malengo yao wanapoanza kukihusisha na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment