Wednesday, January 8, 2014

Mnyika apendekeza Ubungo iwe Manispaa

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, ametaka jimbo lake lipewe hadhi ya kuwa Manispaa kutokana na kasi ya ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam, na kwamba itasaidia kuhimili ukubwa wa eneo kijiografia ambalo kwa sasa unailemea Wilaya ya Kinondoni.

Aitoa pendekezo hilo katika kikao maalum cha kamati ya fedha cha kujadili mapendekezo ya kuongeza maeneo mapya ya utawala katika mkoa wa Dar es Salaam.

Alishauri kuwa, Manispaa itumike badala ya wilaya kutokana na uhalisia na ukuaji wa kasi sambamba na kuwapo na Manispaa ya Kigamboni na Ubungo ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kusimamia vyema mipango miji, kuujenga vyema mji na kujisimamia kihuduma kwani Manispaa ya Kinondoni na Temeke zinaongoza kwa kasi ya ukuaji.

“Katika ukuaji wa kasi unaoendelea jiji la Dar es Salaam maeneo yaliyopo katika wilaya hasa ya Kinondoni na Temeke ndiyo ambayo yanaongoza pia katika ukuaji huo wa kasi wa kimakazi na shughuli za kiuchumi kama viwanda na uwekezaji hivyo ni vyema zikaongezwa Manispaa za Ubungo na Kigamboni ili kuongeza ufanisi wa ukuaji wa jiji,” alisema Mnyika.

Aidha alipendekeza hitaji la kuwapo kwa jiji la Dar es Salaam kama chombo kikuu juu ya Manispaa zote tano zinazopendekezwa zitakazokuwapo na kwamba Meya wa jiji hili achaguliwe na wananchi kwani itatoa fursa katika utendaji na uwajibikaji imara ambao unaweza kupimwa na wananchi.

No comments:

Post a Comment