HATIMAE Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Dodoma, kimempitisha rasmi Mwimbaji
wa Nyimbo za Injili wa Kanisa Kuu la Kianglikana Dodoma, Josiah Mtonyi, kugombea
udiwani wa Kata ya Mpwayungu, wilaya ya Chamwino.
Katibu Mkuu wa Chadema
mkoani Dodoma, Stephen Masawe, amethibitisha Chama chake kumpitisha
Mtonyi kugombea nafasi hiyo na kwamba ameshachukua fomu na wana uhakika atatoa
ushindani wenye ushindi kwa sababu mgombea wao anakubalika na wananchi wa Kata
kwa ubora na uaminifu.
Mtonyi alichukua fomu
hiyo katika Ofisi ya Kata hiyo mwishoni mwa wiki saa 10.18 jioni kwa Kaimu
Mtendaji wa Kata ya Mpwayungu ambaye pia ni Mratibu wa Elimu Kata, Mwalimu Ester
Musa, akisindikizwa na Umati wa watu kwa vifijo, ngoma na nderemo, wakiwemo
viongozi wa Chadema Mkoa.
Uchaguzi huo unafanyika kutokana na baadhi ya Madiwani kufariki,
kupoteza Sifa na kujiuzulu ambapo Kata hiyo iko wazi kutokana na kifo cha
aliyekuwa Diwani wa Kata na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chamwino Dodoma,
Laurent Hoya, aliyefariki Agosti 16, mwaka jana.
Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) hivi karibuni ilitangaza uchaguzi mdogo wa madiwani
katika kata 27 za Halmashauri 23Februari 9, 2014.
Mtonyi ambaye ni Mhitimu wa Shahada ya Maendeleo Vijijini ya
Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro, ameahidi kuwapatia Maendeleo ya Kielimu,
Kiuchumi, Kiafya, Kijamii, Kisiasa na Kimawasiliano wananchi hao, kwa kile
alichosema, wamemsomesha kwa tabu hadi alipofikia hapo, hivyo anataka
kuwatumikia.
Mgombea Mtonyi (Chadema), atapambana vikali na Mgombea mwenzake
wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Edward Mgaya, ambaye alipitishwa na Chama chake
hivi karibuni, ambapo aliwashinda wenzake wanne katika kura za maoni katika
Kata hiyo.
Aidha Wananchi waliohojiwa katika vitongoji na vijiji
vinavyozunguka Kata ya Mpwayungu, wamesema hawana sababu ya kutomchagua Msomi
Mtonyi wakidai ana sifa na ueledi wote, hana Kashifa wala tone la ufisadi,
ameitendea Haki Jamii hiyo Kielimu na kadharika, hivyo wanaamini atawasaidia
kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment