Monday, January 27, 2014

CHADEMA yaionya CCM


  • Yadai imepanga njama kuchakachua mapendekezo ya serikali tatu
  • Mbowe asema yupo tayari kufungwa kwa kosa la kudai katiba mpya
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amekionya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kuacha hila zozote zile ambazo zitasababisha kuvunjika kwa mchakato wa katiba mpya unaoelekea hatua ya Bunge Maalumu la Katiba.
Alisema waache kufikiria kufanya hivyo kwani  kwa hatua iliyofikia, Watanzania hawako tayari kurudi nyuma kuendelea na katiba ya sasa.
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA taifa aliyasema hayo juzi jioni wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, ikiwa ni sehemu ya Operesheni ya Movement For Change (M4C) iliyopewa jina la Pamoja Daima, ambayo inaendeshwa na viongozi wa chama hicho nchi nzima, wakigawanyika katika timu sita – tatu zikitumia usafiri wa helkopta na nyingine zikiwa ardhini.
Mbowe alisema kuwa yupo tayari kuwa wa kwanza kufungwa kwa kosa la kudai katiba mpya iwapo serikali itaweka mazingira ya hila ambayo yatalazimisha kukwamisha mchakato wa kupata katiba mpya, hivyo Watanzania kulazimika kuendelea na katiba ya zamani ya mwaka 1977.
Alisema kuwa watawala wasitumie hila na mwanya wowote kuitia nchi majaribuni kwa kulazimisha watu ‘kuishi’ na katiba ya sasa aliyosema imekosa uhalali wa kisiasa na kisheria, bali wanatakiwa kuhakikisha mazingira mazuri yanapatiana kwa Watanzania kujiamulia wanavyotaka kuongozwa, huku akisisitiza kuwa katiba ni uhai wa taifa, si matakwa ya chama chochote cha siasa wala mtu binafsi.
Mbowe alisema kuwa Watanzania wengi wamependekeza kuwapo kwa shirikisho la serikali tatu katika rasimu ya katiba mpya, lakini akadai kuwa zipo njama zinazofanywa za kuchakachua maamuzi hayo ya wananchi kwa ajili ya kuilinda CCM.
Alisema iwapo hila hizo za kupindua maoni ya wananchi zitafanikiwa kupenyezwa kupitia bungeni, yuko tayari kuungana na Mtanzania yeyote kuzunguka nchi nzima kuwahamasisha wananchi waikatae rasimu hiyo.
Alisisitiza kwa kusema kuwa endapo wananchi wataikataa katiba hiyo, pia  hawatakuwa tayari kurudi kuendelea kutumia katiba ya zamani inayotumika hivi sasa kama ambavyo serikali imekwishasema.
“Watawala lazima wajue. Watanzania hawa ambao wameipigania na kuililia katiba mpya kwa muda mrefu sasa, hawako tayari tena kurudi nyuma. Maana kuna kipengele cha sheria kimewekwa kwamba mchakato huu wa sasa ukishindikana kwa maana kwamba wananchi wakipiga kura ya maoni kuikataa rasimu itakayokuwa imepitishwa bungeni, eti tunaendelea na katiba ya zamani.
“Kwa hiyo kwa kutumia mwanya huo, kuna watu, tena wanaongozwa na chama kilichoko madarakani, wamejipanga kuhakikisha kwamba wanachakachua maoni ya wananchi yaliyotolewa ili ikifika wakati wa kura ya maoni wananchi waikatae, na hivyo mchakato wote unafeli, tunarudi kwenye katiba ya zamani na hivyo kuanza mwanzo tena mchakato wote.
“Kwa kweli Ngara ninawaambia kwa hilo hatuko tayari. Wananchi wametoa maoni yao mengi mengi kuhusu siasa, uchumi na jamii yazingatiwe kwenye katiba mpya, lakini watawala wako tayari kuingiza nchi majaribuni kwa sababu tu wanataka kuendelea kulinda ulaji wao. Wanataka uhai wa chama chao. Hatutakubali.
“Tena wanaojipanga kuchakachua ni wale wanaokataa serikali tatu, eti sio sera ya chama chao, alaah! Wanapata wapi jeuri hii ya kutaka katiba ya nchi iongozwe na sera za vyama vya siasa na kwa nini chama chao ndiyo kielekeze katiba iweje badala ya wenye katiba ambao ni wananchi wenyewe?
“Niko tayari. Nitakuwa wa kwanza kufungwa endapo katiba inayoandaliwa sasa itachakachuliwa na baadhi ya watu kwa sababu tu hawataki serikali tatu, kwani nitazunguka nchi nzima kuhamasisha wananchi kuikataa na baada ya kuikataa pia hatutakuwa tayari kurudia ile ya zamani.
“Haiwezekani Watanzania walio wengi wakatoa maoni kuhusu siasa za nchi, kuhusu uchumi wa nchi na mambo ya kijamii ili watengeneze mazingira ya fursa za maendeleo kwa katiba wanayoitaka wao, halafu wengine, kikundi kidogo kwa maslahi ya chama chao waichakachue eti tu kwa sababu ya maslahi yao binafsi ya kutaka kujitengenezea mazingira ya ulaji.
“Katiba ni uhai wa taifa hili. Ni uhai wa Watanzania wote siyo ya chama chochote cha siasa au ya mtu fulani, mbona Zanzibar wenyewe wametengeneza katiba yao kwanini na sisi tusingeneze ya Tanganyika? Walikuwa wapi wakati masuala yote yanayotishia kabisa Muungano yanazidi kukomaa?” alisema Mbowe.
Aliongeza kuwa haiwezekani kutumia muda mwingi na gharama kubwa ya fedha kuandaa katiba hiyo halafu  watu wengine wakaichakachua, na kwamba hata kama  katiba hiyo itakataliwa, haiwezekani kuendelea kutumika ile ya zamani inayotumika sasa, bali  ni lazima itaipasa serikali kuangalia utaratibu mwingine wa kuhakikisha katiba mpya inapatikana.
“Wazo la kurudi katika katiba ya zamani halipo kabisa, kama Serikali ya CCM inajidanganya kwamba watachakachua katiba inayoandaliwa sasa halafu tukarudi kutumia ile ya zamani, hiyo haipo na itawagharimu,” alisisitiza.
Kadhalika Mbowe alisema kuwa watazunguka nchi nzima kuwahamasisha Watanzania kususia zoezi la upigaji kura ya maoni ya katiba endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itashindwa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura.
Alisema kupiga kura ni haki ya msingi ya Watanzania, na kwamba hadi sasa zaidi ya Watanzania milioni tano na laki tatu hawana uwezo wa kupiga kura kwa sababu hawana shahada ya kupigia kura.

No comments:

Post a Comment