CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kikao cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kilichomalizika jana jijini Dar es Salaam, hakikujadili uanachama wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kama ilivyoamuliwa na Mahakama Kuu.
Badala yake, chama hicho kiliendelea kumjadili Zitto katika masuala mengine yasiyohusiana na uanachama wake.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, jana Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika, alisema kuwa amri ya mahakama inazuia kujadili uanachama wa Zitto, lakini haijazuia kujadili mambo mengine yasiyohusiana na uanachama wake.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alikuwa akitoa ufafanuzi kwa gazeti hili ambalo juzi liliripoti kimakosa kwamba, licha ya mahakama kuzuia kujadili uanachama wa Zitto, CC ya CHADEMA itaendelea kujadili uanachama wa mbunge huyo ambaye hivi karibuni alisimamishwa uongozi kwa madai ya kukisaliti chama.
“Taarifa yenu ya jana haikuwa sahihi na imepotosha umma, kwamba tutaendelea kujadili uanachama wa Zitto wakati mahakama imezuia. Hatuwezi kuendelea kujadili uanachama wake kwani kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa mahakama na kuidharau,” alisisitiza Mnyika.
Zuio la Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam limetokana na ombi la Zitto aliyekimbilia mahakamani kuomba CC ya CHADEMA izuiliwe kujadili uanachama wake.
Kutokana na ombi hilo, Mahakama Kuu imekubali kwa muda kusitisha uamuzi wa CC ya CHADEMA kujadili uanachama wa Zitto hadi itakapotoa uamuzi Jumatatu ijayo.
Hata hivyo, CC ya CHADEMA imeruhusiwa kuendelea na kuwajadili wanachama wengine wawili; Dk. Kitilla Mkumbo na Samson Mwigamba, ambao nao walivuliwa uongozi kwa madai ya kukisaliti chama hicho.
Katika maombi yake katika kesi hiyo inayovuta hisia za wengi iliyopewa namba 1 ya mwaka 2014, Zitto anayetetewa na wakili Albert Msando, anaiomba Mahakama Kuu kuwazuia washitakiwa kwa pamoja na Kamati Kuu ya CHADEMA na chama au chombo chochote kwa makusudi, kujadili au kuamua suala la uanachama wake.
Maombi mengine ni kutaka apatiwe nakala ya uamuzi wa Kamati Kuu iliyoketi hivi karibuni na kumvua uanachama ili aweze kukata rufaa kwa Baraza la Uongozi la CHADEMA.
Katika ombi jingine, Zitto anaiomba mahakama iwazuie washitakiwa kuingilia kati wajibu na majukumu yake ikiwemo ya ubunge wa Kigoma Kaskazini.
Katika kesi hiyo, mshitakiwa wa kwanza ni Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa CHADEMA.
Sijawahi kujuta kuwa mwanaCHADEMA, ninaimani na na KK japo wamechelewa kuchukua hatua. swala la MASALIA lilijitokeza tokea miaka minne iliyopita na KK ilikuwa kimya. Hongera kwa uongozi mzima wa CHADEMA.
ReplyDelete