Saturday, December 7, 2013

Tume huru kura ya maoni yawagawa wabunge upinzani, CCM

Suala la kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi katika zoezi la kupiga kura ya maoni ya Katiba mpya limezua mjadala mkali, wakati bunge lilipokaa kama kamati kujadili kifungu kwa kifungu cha Muswada wa Sheria ya Maoni ya Katiba, 2013 kwa lengo la kuupitisha.

Wakati wabunge wengi wa upinzani wakitaka kipengele cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) katika Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni, 2013, kirekebishwe na badala yake iwapo Tume huru kusimamia kura hiyo, wabunge wa CCM na serikali waliunga mkono NEC na ZEC kufanya kazi hiyo.

Alikuwa Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema), ambaye aliwasilisha hoja ya kupinga pendekezo la NEC na ZEC kusimamia uchaguzi wa kura ya maoni ya Katiba mpya.

Alisema kwa kuwa hakuna kuaminiana katika suala la usimamizi wa uchaguzi na kwa vile NEC iliwahi kunukuliwa kuwa haina uhuru katika kufanya kazi zake, ni vema kama ikaanzishwa tume huru kusimamia zoezi la kura ya maoni.

Mapema Spika Anne Makinda alimtaka Wenje kuwashawishi wabunge kwa hoja kitu gani ambacho siyo huru kwa NEC na tume hiyo iundwe namna gani.
Akijibu Wenje alisema, “NEC yenyewe siyo huru na tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa siyo huru.

Akimuunga mkono Wenje, Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji, (CUF), alisema, “matatizo yetu makubwa yanatokana na Tume hizi za uchaguzi.

“Katika kusikilizana hata nyinyi (CCM) mkubali maoni ya wachache (upinzani), tume hizi siyo huru, wajumbe wake wanafuata matakwa ya waliowachagua,” alisema.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema ingawa Waziri Mkuu amezungumzia suala la kuaminiana katika mchakato huu wa kuandika Katiba mpya, suala la msingi hapa ni kujenga kuaminiana kwa pande zote.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba, (CCM), alisema, “hoja hapa ni kuaminiana, kama wapo wasioiamini tume, basi wao ndiyo wasioamini…nakubaliana na serikali kuwa tume hii iwapo,” alisema. 

No comments:

Post a Comment