Saturday, December 7, 2013

TAARIFA SAHIHI YA CHADEMA MKOA WA SINGIDA JUU YA TAMKO BATILI LILILOTOLEWA TAREHE 03/12/203 NA ALIYEKUWA MWENYEKITI WA CHADEMA MKOA SINGIDA NDG. WILFRED NOEL KITUNDU KWENDA KWA VYOMBO VYA HABARI. TAREHE 6/12/2013

Ndugu waandishi wa habari, wanachama na viongozi wa CHADEMA,

Baraza la uongozi mkoa wa Singida lilipata taarifa za kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa Ndg WILFRED NOEL KITUNDU kutoka kwenye mitandao ya kijamii kama vile Jamiiforum, kutoka kwa waandishi wa habari waliopewa taarifa hata kabla ya uongozi wa chama kupata taarifa kutoka kwa mhusika. Mara baada ya kupata taarifa hizo na kuzipitia kwa kina, tumeona ni vyema na haki kuwapa taarifa sahihi juu ya upotoshaji uliofanywa na ndg.WILFRED NOEL KITUNDU.

Baada ya baraza la uongozi kukaa kikao cha dharura tarehe 4/12/2013 siku moja baada ya ndg WILFRED NOEL KITUNDU kujiuzulu umejadili na kujiridhisha kuwa tuhuma zilizotolewa na bwana huyu ni za UONGO, UZUSHI, UPOTOSHAJI USIYOMITHILIKA. Hivyo hatuwezi kuzifumbia macho bali tumeamua tutoe taarifa sahihi ili kuweka kumbukumbu sawa sawa.

Ndugu waandishi wa habari, wanachama na viongozi wa CHADEMA, katika kupitia barua yake ya kutangaza kujiuzulu uongozi tumebaini makosa yafuatayo ambayo ni MATUMIZI MABAYA YA LUGHA kama ifuatavyo:-

1.“….chama kinabaka na kudhalilisha demokrasia…” katika hili tunaomba muelewe kuwa CHADEMA haijawahi na haitawahi kutenda kosa hilo la ubakaji na udhalilishaji wa demokrasia kama alivyodai huyu bwana kwani kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na jina lenyewe la chama kama linavyojipambanua kwenye katiba ya 2006 CHAMA CHA “……DEMOKRASIA…..? ili kuhakikisha hata yeye anafuata neno hilo ndiyo maana leo hii ameamua kujiuzulu kwa shinikizo la hofu ya kuvuliwa uongozi.
2.“…upuuzi huu uliofanywa na kamati kuu……” tunaomba ieleweke hapa kuwa kamati kuu ni chombo halali cha kikatiba alichoshiriki yeye mwenyewe kukiuunda akiwa mjumbe halali wa vikao vilivyoandika katiba hii. Hivyo laana hii ya upuu itamrudia yeye kwani na yeye mwenyewe alishiriki kuunda chombo hiki. Kwa kifupi yeye amekuwa ni mzigo mkubwa kwa kushindwa kuisimamia katiba ya chama na ndiyo maana kaondoka kwa aibu kubwa kwani hatukutegemea mwenyekiti wa mkoa wenye majimbo 8 na kata 124 aondoke na apigwe picha na vyombo vya habari peke yake.
3. “……..kufumbia macho ujinga wa  kamati kuu….” Hapa napo kuna walakini kwani mwanademokrasia wa kweli kama anavyojiita hawezi kukimbilia mafichoni ndipo atoe tamko kama alivyofanya yeye kwani kama alikuwa anafikiri yuko sahihi angetumia ofisi ya chama na kuita kikao halali ambalo ni baraza lake la uongozi na wanachama wake ndipo atoe tamko lake. Hakuna ujinga unaoweza kuungwa mkono na mtu mmoja kama anavyouaminisha umma. Hapa ni lazima watanzania wahoji udemokrasia wake wa kweli upo wapi? Na hii yote ni kutokana na ujinga wakutokujua maana sahihi ya neno “DEMOKRASIA.”  Kwa ufupi huu ni ukibaraka tu.

Ndugu waandishi wa habari, wanachama na viongozi wa CHADEMA, kwa kuwa aliyeyasema hayo alikuwa kiongozi ambaye hatuna shaka na uelewa wake wa katiba, kanuni, itifaki na maadili ya chama hiki ambacho sasa yeye amebaki kuwa mwanachama wake wa kawaida na tayari matumizi ya lugha yanaonyesha kuwa yanaangukia kwenye ibara ya 10.0, 10.3 (4) …kujiepusha na upinzani dhidi ya chama na wagombea wake na makundi ya majungu ya kuwagonganisha viongozi na wanachama haswa wakati wa chaguzi za kichama ama za kiserikali…” anastahili kuvuliwa uanachama wake. Hivyo apime mwenyewe.
Vile vile amevunja katiba ya chama sura ya tano ibara za 5.1, 5.1.4, 5.1.5 kwa hiyo hastahili kuendelea kuwa mwanachama wa Chadema chama ambacho kinabaka demokrasia.

Ndugu waandishi wa habari, wanachama na viongozi wa CHADEMA, pia kwenye taarifa yake aliyodai ni ya chama mkoa wa Singida ina mapungufu makubwa ambayo tunaona hakuyaandika mwenyewe bali aliandikiwa kwani maudhui yake hayaonyeshi kama kweli yeye alikuwa mwenyekiti wa mkoa. Katika taarifa hiyo umeudanganya umma kwani madai aliyoyatoa ni ya UONGO ULIOVUKA MIPAKA.

Alidai kuwa yeye amejitolea kwa hali na mali kwa kujinyima na kuipunja familia yake ili ajenge chama mkoani Singida. Ni jambo la kusikitisha tunapoona hata wazee wanasema uongo kwa kiwango hiki. Ili kuweka kumbukumbu sawa, CHADEMA mkoa wa Singida tunasema haya yafuatayo:-

1.Mzee WILFRED NOEL KITUNDU hakuwahi kushiriki hata siku moja kufanya mkutano wowote akiwa kama mwanachama na akiwa kama mwenyekiti wa mkoa kwenye jimbo la Singida Mashariki lenye vijiji 49.
2.Hakuwahi kushiriki hata siku moja kwenye kampeni za kugombea ubunge za Mh. Tundu Lissu. Kwa hiyo si kweli kwamba ameleta mafanikio ya kupata wabunge 3 mkoani kwake.
3.Vile vile yeye mwenyewe ni mtuhumiwa aliyeharibu mchakato wa kwanza wa ubunge wa  viti maalumu na hili analijua vizuri sana na kutokana na uharamia anaoujua yeye ndiyo maana uongozi wa juu uliamua kumteu Dr Kitila Mkumbo kutengeneza utaratibu wa kuwapata wabunge wa viti maalumu. Kwahiyo wabunge hawa wa viti maalumu siyo zao lake.

OFISI YA CHADEMA
Ndugu waandishi wa habari, wanachama na viongozi wa CHADEMA, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amedai kuwa tangu mwaka 1992 hadi 2011 chama kimekuwa kikitumia nyumba yake kama ofisi ya chama. Jambo hili si la kweli kwani kumbukumbu zetu zinatunyesha kama ifuatavyo:-

1.Mwaka 1992 hadi 2000 ofisi ya CHADEMA ilitolewa na Mzee KALALU ambaye kwa sasa ni marehemu. Wakiti huo mzee Wilfred Kitundu alikuwa Mwenyekiti.

2.Mwaka 2000 hadi 2004 ofisi ya chama aliitoa mwanachama wetu alimaarufu MAMA VERO. Kwa kipindi hiki chote yeye hakuwa mwenyekiti wa chama bali mwenyekiti alikuwa ndugu NATANIEL MPANYA. Kwa hiyo sikweli kwamba yeye amekuwa mwenyekiti toka 1992-2013.

3.2000 aliondolewa kwenye uongozi kutokana na kudharau kikao cha uongozi mkoa hivyo aliondolewa kwenye uenyekiti kabla ya kuomba kugombea tena mwaka 2004.

4.2004 aliomba kugombea uenyekiti akapitishwa bila kupingwa kwani hakuwa na mpinzani na mwaka 2009 akagombea tena ambapo muda wake ulipaswa kuisha mwaka 2014 mwaka kesho. Kwahiyo kuanzia mwaka 2004 – 2011 ndipo ofisi ilihamia kwenye chumba cha sebule yake.

Kwahiyo si kweli kwamba yeye amekuwa ndiye mwenyekiti tangu 1992 – 2013 kama alivyosema kwenye taarifa yake.

Endelea.....Click Read More


MADAI YA HISTORIA YA USALITI KWENYE CHAMA.
Mzee huyu anataka umma uamini kuwa Dr. AMANI KABURU hakuwa msaliti. Ili kujua uongo wa mzee huyu tuwakumbushe baada ya Dr. Kaburu kufukuzwa chama ilikuwaje.
  1. Nani asiyejua kuwa baada ya Kaburu kufukuzwa CHADEMA alipewa ubunge wa Afrika MAshariki kupitia CCM? Je, ni kweli huyu hakuwa msaliti? Majibu mnayo.
  2. Nani asiyejua kuwa Dr. Kaburu ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma? Hili i halihitaji maelezo marefu.
  3. CHACHA WANGWE mzee huyu anafahamu vizuri kuwa yeye ni miongoni mwa wajumbe wa kamati kuu ya wakati huo iliyomvua ungozi CHACHA WANGWE mwaka 2007. yeye kama mjumbe wa kamati kuu iliyokaa na kuuaminisha umma kuwa WANGWE ni msaliti na akajenga hoja ya kumuondoa madarakani sasa leo anaiona kamati kuu ni ya kupuuzi na maamzi yake ni kipuuzi na kijinga???
Kwa hiyo udanganyifu wa namna hii hauwezi kufumbiwa macho kwani wanaoathirika ni watanzania wanaopenda kuona wanaongozwa na viongozi wa kweli na wenye nia ya dhati juu ya maslahi mapana ya chama chao na taifa kwa ujumla.

HOJA YA UKANDA.
Ndugu waandishi wa habari, wanachama na viongozi wa CHADEMA, kwanza tungependa mfahamu kuwa hoja hii imeshajibiwa sana na viongozi wetu wa sehemu zingine na hata viongozi wakuu wa chama kitaifa lakini kwa kuwa mzee huyu ameizungumzia kwenye taarifa yake ni vyema kuijibu.
 Katika kuhakikisha chama hiki hakimuonei mtu yeyote msaliti ndani ya chama,ndiyo maana Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Arusha amevuliwa uenyekiti ni wa Arusha. Juzi tu mwenyekiti wa Babati amevuliwa uongozi kwa usaliti huo huo ni kutoka kanda ya Kaskazini. Sisi tunasema badala ya watu kutumia vivuli vya demokrasia ya kweli kupotosha umma ni vyema wakatafakari pia kuwa kuna watu wenye uwezo wa kutafakari zaidi yao. Vile vile tunatoa wito kwa watanzania na wanachama wote kupuuza kauli hizi za ukanda au udini kwani zinawabagua watanzania na kutengeneza fitina na chuki ambazo mwisho wake ni mbaya sana.

WAVAMIZI NDANI YA CHADEMA.
Ndugu waandishi wa habari, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Katika hoja hii mzee huyu amesema uongo wa kiwango cha hali ya juu na ambao umevuka mipaka ya uongo. Amewataja watu kuwa wanavuruga chama na wengine hawajawahi kufanya hata mkutano mmoja wa kujenga chama mkoani mwake. Tunasema mtu ukizeeka na akili zinazeeka tu.

Usahihi katika jambo hili, kwanza kabisa tunapenda mfahamu kuwa CHADEMA kipo kwa ajili ya watanzania wote wanaopenda na kukubaliana na sera za chama juu ya mstakabali w taifa lao la baadaye. Hivyo ni haki ya kila raia wa Taaanzania kujiunga na Chadema ili mradi halazimishwi kujiunga nacho. Vile vile lengo la mtu yeyote anayejiunga na chama ni kuongeza mtandao na nguvu ya kujenga chama kwa uwezo wake kwa kumjibu ya katiba na misingi yake. Hivyo hawa anaowaita wavamizi wachama ni bora zaidi kuliko yeye kwani michango yao inaonekana kwenye chamba ambacho yeye amekuwa mwenyekiti na mwanachama kwa miaka 20 sasa lakini mchango wake ni wa mashaka.

Mfano amewataja Mh GODBLESS LEMA (MB), Mh MCH.PETER MSIGWA (MB) Mh. TUNDU LISSU (MB) na wengine hawa wote kwa muda mfupi waliojiunga Chadema wameonyesha mafanikio makubwa kuliko yeye aliyekaa zaidi ya miaka 20 kwenye chama.

Tunapenda tutoe ufafanuzi kwa kutaja mifano michache ya michango yao katika chama ya baadhi ya watu hawa anaowaita WAVAMIZI.

Mh GODBLESS LEMA ameshiriki kujenga chama mkoani Singida kwa kufanya mikutano ya hadhara maeneo yafuatayo:-
  1. Jimbo la Singida Mjini stendi ya zamani.
  2. Jimbo la Singida Kaskazini kata za MSANGE, NGAMU, ILONGERO
Je, Mzee Wilfred Kitundu amewahi kufanya wapi mkutano hata mmoja wa hadhara wa kujenga chama?

Mh TUNDU LISSU.

Ndugu waandishi wa habari, wanachama na viongozi wa CHADEMA, kuhusu Tundu Lissu, mzee huyu amedai kuwa Kamanda Lissu hakuwahi kufanya mkutano hata mmoja wa kujenga chama mkoani Singida zaidi ya Jimbo lake la Singida Mashariki. Huu ni uongo na pengine nia yake ni kutaka kuuaminisha umma kuwa kamanda Lissu hana mchango wowote wa kujenga CHADEMA mkoani Singida. Hapa tuna wasi wasi na taarifa hii aliyoitoa hakuiandika yeye maana aliyoyaandika hayajui.

Labda kwa faida ya wanachadema na watanzania kwa ujumla tunapenda kutoa mifano michache tu juu ya ushiriki wa Kamanda Tundu Lissu kujenga chama kabla na baada ya kuwa Mbunge.

1. Mh Lissu alianza kazi ya ujenzi wa chama mkoani Singida tarehe 4,January 2008 katika jimbo la SINGIDA KUSINI likiwa na jumla ya kata 26 na vijiji 104 kabla ya kugawanywa na kupata majimbo ya
(i)                 SINGIDA MASHARIKI
(ii)               SINGIDA MAGHARIBI

2.Kabla ya kuwa mbunge alifanya kazi ya ujenzi wa chama kwenye JIMBO LA SINGIDA KASKAZUNI kwenye vijiji vifuatavyo:-

i.                    KINYETO
ii.                  MKIMII
iii.                NTUNDUU
iv.                MINYAA
v.                  MWANYONYE
vi.                KINYAGIGI
vii.              MERIYA
viii.            MIPILO
ix.                MSANGE
x.                  NGAMU
xi.                MPIPITI
xii.              MTINKO
xiii.            MATUMBO
xiv.            ILONGERO.
xv.              MAKURO

3.Mh Lissu amejenga chama JIMBO LA IRAMBA MASHARIKI kata ya IGUGUNO
4.Mh Lissu amejenga chama JIMBO LA SINGIDA MJINI na nyinyi ni mashahidi.
5.Mh Lissu amejenga chama JIMBO LA MANYONI MASHARIKI.
6.Mh Lissu amejenga chama JIMBO LA MANYONI MAGHARIBI.
Swali la kujiuliza ni kuwa TUNA AKINA TUNDU LISSU WANGAPI?

Tunasema huu ni uongo na unafiki mkubwa. Yeye akiwa kama mwenyekiti aje hadharani aseme amewahi kufanya mkutano wapi wa hadhara japo wa tawi tu. Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa yeye amekuwa ni kikwazo kikubwa tu cha ukuaji wa chama mkoani Singida kwa kuzuia kuchukua maamzi ambayo yangekisaidia chama chetu kwani kama anawatu wasiyoweza kufanyakazi ya ujenzi wa chama angewachukulia hatua na hawakustahili hata kupitishwa kuwania ubunge.

Hatukatai kuwa Mh Zitto amefika Singida na kuhutubia mikutano ila si kwa kiwango mzee Wilfred Kitundu anataka umma uamini kuwa Mh. ZITTO KABWE ndiye amekuwa anajenga chama mkoani singida badala ya Mh Tundu Lissu. Tunapenda umma ufahamu kuwa Mh Zitto kafanya mikutano kwenye maeneo yafuatayo

1.            2011 Mh Zitto alikuja kumnadi mgombea udiwani kwenye uchaguzi mdogo akitokea IGUNGA kwenye kampeni za uchaguzi mdogo za ubunge.
2.            Tarehe 4, June 2011 Mh Zitto alifanya mkutano wa hadhara stendi ya zamani.
3.            Alifanya Mkutano kata ya SHELUI jimbo la Iramba Magharibi akiwa na Dr Kitila Mkumbo mwezi April 2013 kabla ya uanza kwa bunge la bajeti.

MSIMAMO WA CHADEMA MKOANI SINGIDA.
Ndugu waandishi wa habari, wanachama na viongozi wa CHADEMA, kuhusu msimamo anaodai kuwa ni wa chama mkoa wa Singida ni upotoshaji mkubwa sana kwani hauna mantiki yoyote ile na hauna baraka za chama.

Kupitia taarifa hii uongozi wa CHADEMA mkoa wa Singida unakanusha vikali kuhusu msimamo alioutoa kwani hakuwa na mamlaka kutoa msimamo huo kwa sababu zifuatazo.

  1. Yeye alitoa barua ya kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti hivyo kutokana na adhima yake hiyo, hana haki, vigezo vya kutoa msimamo alioutoa. Hivy ni batili na ni msimamo wake binafsi.
  2. Hakukuwa na kikao chochote cha chama kilichokaa kuweka msimamo huo. Hivyo tunawaomba wanachama na watanzania wote kutokuupa umuhimu wowote.
  3. Kuhusu ziara ya Katibu mkuu. Hakuna kikao kilichozuia ziara hiyo. Hivyo ziara ya katibu mkuu iko pale pale tarehe 23/12/2013 – 24/12/2013.
  4. Uongozi wa CHADEMA mkoa wa Singida unaendelea kuheshimu maamzi halali yaliyotolewa na kamati kuu ya Chadema kwani yalitolewa na kikao halali kikatiba.

Kwa hiyo tunatoa wito kwa wakazi wa Singida hususani wanachama na watanzania wanaoishi kata ya SHELUI utakapofanyikia mkutano wa hadhara kuwa wajiandae kikamilifu kupokea ugeni huo.

MAAZIMIO
  1. Tunamtaka mzee Kitundu awaombe radhi mara moja wajumbe wa kamati kuu kwa kuona maamzi yao waliyoyatoa kuwa ni ya kipuuzi na ya kijinga.
  2. Awaombe radhi wote aliowataja kwa majina kwenye taarifa yake batili.
  3. Uombe radhi uongozi pamoja na wanachama wa Chadema mkoani Singida kwa kuwasingizia na kuwawekea maneno ya uongo vinywani mwao.

Mwisho
 Tunawakaribisha wanachama wapya kwenye chama ili tuendelee kukijenga mkoani hapa hatimaye tuweze kulikomboa taifa hili kutoka kwenye makucha ya mafisadi wa rasilimali za nchi.

……………………………………………………………………...
SHABAN LYIMO, KAIMU MWENYEKITI WA MKOA.

……………………………………………………
PATRICK MSUTA, KATIBU WA CHADEMA MKOA. 

No comments:

Post a Comment