Friday, December 6, 2013

Mbowe,Lissu,Mnyika,Marando kuwasha moto kongamano Bavicha

Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema (Bavicha) limeandaa kongamano kubwa kuadhimisha miaka 52 ya uhuru wa Tanganyika, litakalohudhuriwa na viongozi waandamizi watano wa chama hicho.

Viongozi hao, ambao wataongozwa na Mwenyekiti, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Wengine ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, Mabere Marando, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, pamoja na Dk. Kamilius Kasala, ambaye ni bingwa wa masuala ya uchumi. 

Katibu Mkuu wa Bavicha, Deogratius Munishi, alisema jana kuwa kongamano hilo litawahusisha vijana wa Chadema wa majimbo ya Dar es Salaam , wanafunzi wa vyuo vikuu vya jijini humo, ambao ni wanachama wa chama hicho.

Alisema msingi mkuu wa kongamano hilo ni kutoa tathmini halisi ya hali ya Taifa kwa kipindi cha miaka 52 na mwelekeo mbadala kutoka chama mbadala. 

Munishi alisema mgeni rasmi katika kongamano hilo atakuwa ni Mbowe, ambaye atatumia maadhimisho hayo kuzungumza na vijana juu ya mustakabali wa nchi, hususan masuala muhimu yanayolikabili Taifa kwa sasa.

Alisema pia kwa mara nyingine tena, kuanzia leo hadi keshokutwa, Bavicha itakuwa mwenyeji wa mkutano wa vijana wa vyama vya kidemokrasia kwa Ukanda wa Afrika Mashariki. Munishi alisema mkutano huo utafanyika jijini Dar es Salaam na utajumuisha vijana 40 kutoka mataifa wanachama wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia barani Afrika (Dua) kwa ukanda huo.

Alisema pia utawahusisha wageni maalumu kutoka nchini Ghana na wabunge kutoka Uingereza na utafunguliwa na Mbowe.

1 comment:

  1. naitakia mema CHADEMA ifike mbali migogoro ni sehemu ya mafanikio na ukomavu wa chama viongoz washikamane hakika tutafika mbali hata kuongoza nchi .

    ReplyDelete